Menu

Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. 2 Huyo mwanzo

Wednesday, February 25, 2015

UCHUMI WA UFALME WA MBIINGUN

UCHUMI WA UFALME WA MBIINGUN


Mama mmoja aliyekuwa na watoto sita (lakini alikuwa hajaolewa), alipelekwa na mwenzake kwa Askofu wa dhehebu lao ili wapate msaada kwa kuwa walikuwa na maisha ya shida sana. Yule mama pamoja na watoto wake sita walikuwa wanakaa katika nyumba ya makaratasi, na hawakuwa na chakula cha kutosha.
Askofu alimuuliza yule mama amewapateje wale watoto wote sita na huku alikuwa hajaolewa.
Yule mama akajibu akasema; "Mtoto wa kwanza nilimpata kwa kuwa nilikuwa nataka mtoto, niliona nazeeka bila ya kuolewa nikaona nizae mtoto, Lakini mtoto wa pili nilimpata wakati nilipokuwa natafuta chakula cha mtoto wa kwanza. Mtoto wa tatu nilimpata nilipokuwa natafuta chakula cha watoto wawili niliokuwa nao. Na hali hii imeendelea mpaka sasa nina watoto sita – na sijui nitaendelea na hali hii mpaka lini".
Ni wazi kabisa si mapenzi ya Mungu huyu mama aishi maisha ya namna hiyo. Vikwazo vya uchumi ambavyo vilimzunguka yule mama na watoto wake vilitoka kwa ibilisi.
"Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa ……."(Hosea 4:6). Maneno haya yaliyosemwa na Mungu kwa kinywa cha Nabii Hosea yana ukweli ndani yake hata hivi leo. Watu wengi sana siku hizi wanaangamizwa, wanadhulumiwa, wanahuzunishwa na maisha kwa sababu tu wamekosa kuyajua maarifa ya Mungu yaliyomo katika Neno lake.
Wakati fulani nilikuwa nafundisha katika semina moja juu ya uhusiano wa maendeleo ya mtu na Wokovu, na wakati wa kipindi cha majadiliano Mchungaji mmoja akatueleza habari iliyotufikirisha sana.


Akasema ya kuwa katika kanisa alilokuwa analihudumia miaka ya nyuma aliwahi kufuatwa na mama mmoja wa usharika huo ambaye alikisema ya kuwa yeye alikuwa mmoja wa wakina mama thelathini ambao hawashiriki chakula cha Bwana kwa kuwa walikuwa wanaishi hapo mjini kwa njia za umalaya. Ombi lao kwa mchungaji wao lilikuwa ni kwamba akiweza kuwasaidia kupata kazi za halali waache umalaya. Wao wametafuta kazi bila ya mafanikio, na wanafanya umalaya si kwa sababu wanapenda, bali kwa kuwa hawakuwa na njia nyingine ya kupatia fedha.
Ni jambo la kumshukuru Mungu, ya kuwa mchungaji yule aliweza kuwatafutia kazi wale wakina mama wote katika kiwanda kimoja, na maisha yao yakabadilika wakaacha umalaya, na kuishi maisha ya kikristo yenye ushuhuda.
Ni watu wangapi ambo wanaishi maisha yao kinyume na maadili ya kikristo ili kupata fedha za kuwasaidia kila siku? – Ni wazi kuwa ni wengi. Je! hawawezi wakapata riziki yao bila kudhulumu au kuiba au kudanganya au kuzini? – Ni wazi kuwa wanaweza. Sasa, ni kwa nini wanaishi kwa jinsi hiyo?
Jambo ambalo watu wanahitaji kujua ni kuwa baba wa uongo yaani shetani amewadanganya kwenye mawazo ya kuwa hakuna njia nyingine ya halali ya kupatia fedha isipokuwa hizo. Na shetani anausimamia uongo huo ili uonekane kuwa ni kweli kwa kuwawekea watu hasa wakristo vikwazo vigumu vya kiuchumi.
Unaweza ukawa unajiuliza vikwazo hivyo ni vipi? Vikwazo hivi vinatofautiana katika watu mbalimbali na mahali mbalimbali. Kuna watu wengine wataona hakuna mradi wa halali wanaoufanya unaofanikiwa. Mwingine miradi yake inafanikiwa, lakini fedha yote inaishia kutafutia matibabu ya magonjwa yaliyomo ndani ya nyumba yake ambayo hayaishi.
Mwingine anapata magari mengi, lakini hayaishi kupata pancha na kuharibika au kuanguka. Mara nyingi utawasikia watu wa jinsi hii wanasema wana mkosi. Kwa kweli si mkosi bali vikwazo vya kiuchumi toka kwa shetani ili ushindwe maisha na UANZE KUTAFUTA MAISHA MAZURI KWA NJIA ZILIZO KINYUME NA MAADILI YA KIKRISTO YALIYO MATAKATIFU.

Jambo ambalo wakristo wengi hawalifahamu
 Mimi na mke wangu miaka ya mwanzo tulipookoka hasa mwaka 1984 na 1985 tulikumbana na vikwazo vigumu sana vya kiuchumi. Tuliona jinsi maisha yalivyokuwa yanarudi nyuma – fedha tuliishiwa, chakula tuliishiwa, nguo tuliishiwa, vitu ndani vilianza kuharibika na hatukuwa na fedha za kuvitengenezea. Tulijaribu kulima bustani za mboga, hazikufanikiwa. Tulijaribu kupika chapati za kuuza, hazikununuliwa zikaharibika tukazitupa.
Kwa kifupi tuliona maisha ya wokovu kuwa ni magumu, ya shida na ya kimaskini sana. Tulishindwa hata namna ya kuwasaidia ndugu zetu vizuri. Hali hii ilitutia uchungu sana. Watu hawakufahamu ya kuwa hali hii ilikuwa inatunyima amani ya kweli ya wokovu – kwa kuwa tulijitahidi kuwachangamkia wote ili kuficha mapambano tuliyokuwa nayo kimaisha.
Ilikuwa ni vigumu sana kuishi maisha ya ushuhuda mzuri wa kikristo katikati ya mahitaji makubwa kama hayo tuliyokuwa nayo.
Tulijua kuwa Zaburi 23:1 inasema, "Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu". Lakini tulikuwa tumepungukiwa na vitu vingi vya lazima katika maisha. Hatukufahamu kwa nini sisi kama kondoo wa Kristo tulikuwa tumepungukiwa namna hiyo!
Tulikuwa tunasoma lakini tunashindwa kumwelewa Mtume Paulo alipokuwa anasema katika Wafilipi 4:12 kuwa; "najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yo yote, na katika mambo yo yote, nimefundishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa".
Tuliona ya kuwa Mtume Paulo aliweza kuwa na amani na ushindi katika hali yo yote aliyokuwa nayo – hata katika upungufu. Sisi tulikosa amani tulipokuwa tumepungukiwa! Na hili jambo lilitusumbua sana.
Tulikuwa tunafurahi tunaposoma mstari kama ufuatao; " …..vyote ni vyenu …. Vile vilivyopo sasa, au vile vitakavyokuwapo; vyote ni vyenu, nanyi ni wa Kristo, na Kristo ni wa Mungu"(Wakorintho 3:21,22). Tulikuwa tunafurahi kwa kuwa maneno haya yanatupa uhalali wa kumiliki vitu vilivyo vya Mungu. Kwa mfano Hagai 2:8 inasema "Fedha ni mali yangu, na dhahabu ni mali yangu, asema Bwana wa Majeshi." Pia, Zaburi 24:1 inasema "Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana …" Lakini jambo lililotusumbua ni kwamba ingawa mistari hiyo ilitupa umilikaji juu ya fedha, dhahabu na vyote viijazavyo nchi ili tuvitumie – SISI HATUKUWA NAVYO WALA HATUKUJUA TUTAVIPATAJE!
Tulifahamu ya kuwa ni mapenzi ya Mungu tufanikiwe katika mahitaji ya kiroho na mahitaji ya mavazi, chakula, na malazi; soma kitabu cha 3 Yohana 1:2. Kwa hiyo tulikuwa na hamu kubwa ya kufanikiwa.
Tulitamani sana kuona maneno ya Wafilipi 4:19 yanatimia kwetu – nayo yanasema hivi;
"Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu".Hali hii ilitufanya tuingie katika maombi mazito, ili kumuuliza Mungu njia na namna ya kuondokana na hali tuliyokuwa nayo.
Mambo makubwa matatu yafuatayo, Roho wa Mungu alituambia kuwa ni chanzo cha matatizo yaliyokuwa yanatukabili: Alituambia yafuatayo:
Kuwa, ingawa tumezaliwa mara ya pili na kuingizwa katika ufalme wa Mungu – tulikuwa bado tunategemea utaratibu wa uchumi wa duniani badala ya kutumia na kutegemea utaratibu wa uchumi wa mbinguni;
Kuwa, tulikuwa tunapenda kupokea bila ya kuwa watoaji, na pia tulitaka kuvuna tusichokipanda. Roho Mtakatifu aliuliza swali, Je! unaweza kwenda kwenye bustani yako kuchuma nyanya huku ukijua kuwa hujawahi kupanda nyanya? Ni wazi kuwa jibu lilikuwa ni hapana.
Kuwa, hatujafahamu ya kuwa adui yetu ibilisi ndiye chanzo cha mahangaiko na mafadhaiko yaliyoambatana na kupungukiwa mahitaji katika maisha. Na pia tulikuwa hatutumii silaha tulizopewa ili kuzivunja kazi za ibilisi katika maisha yetu.
Baada ya kupokea majibu hayo kutoka kwa Mungu, tulitubu na kuomba msamaha. Tuliendelea kumwomba Mungu atufundishe na atuongoze katika kuishi maisha ya kutumia na kutegemea utaratibu wa uchumi wa ufalme wa mbinguni.
Mafundisho tuliyoyapata yalituondoa katika mahangaiko ya kupungukiwa na kutuingiza katika furaha na amani ya mafanikio NDANI YA KRISTO.
Ndiyo maana tumechukua hatua hii chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu kukushirikisha baadhi ya mafundisho hayo ili ikiwa umo katika hali ya mahangaiko ya kupungukiwa na mahitaji muhimu ya maisha upate msaada wa kuondokana nayo.
Kumbuka ni mapenzi ya Mungu ndani ya Kristo kuwa ufanikiwe na uishi maisha ya ushindi katika maeneo yote ya maisha yako na katika siku zote utakazoishi juu ya nchi.

Mwenye haki ataishi kwa imani
 Nabii Habakuki aliishi katika kipindi kilichokuwa kigumu sana kiuchumi. Hali hii iliwafanya watu wengi kuingia katika dhuluma, udanganyifu na mambo mengine maovu ili tu waweze kuishi.
Lakini kilichoumiza moyo wa Nabii Habakuki ni kuona kuwa kulikuwa na watu wachache ambao hawakufuata mambo maovu – lakini waliishi maisha magumu na kuonewa na matajiri wa wakati huo. Hali hii ilimfanya Nabii Habakuki aingie katika maombi ya kumlalamikia Mungu, huku akihitaji kujua mpango wa Mungu juu ya watu waliosimama upande wake. Soma kitabu cha Habakuki sura ya 1 na 2.
Kati ya jibu ambalo Mungu alimpa Nabii Habakuki juu ya maisha ya watu wake katikati ya hali ngumu ya uchumi ni maneno haya;
"….mwenye haki ataishi kwa imani yake" (Habakuki 2:4)
Huu ndio uliokuwa mpango wake kwa watu wake wakati ule ili uwasaidie kuishi katikati ya dhuluma na maovu yanayotokana na hali ngumu ya uchumi.
Katika siku hizi za mwisho, kumetabiriwa kutokea tena hali ngumu ya uchumi inayoambatana na dhuluma pamoja na maovu mbalimbali. Mungu amekwisha andaa mpango mzuri kwa ajili ya wote watakaoipokea na kuikiri injili ya Kristo inayookoa. Na mpango huu ni sawa na ule aliopewa Nabii Habakuki.
Kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, Mtume Paulo alisema maneno muhimu yafuatayo:
" Kwa maana siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia. Kwa maana haki ya Mungu inadhihirishwa ndani yake, toka imani hata imani; kama ilivyoandikwa , MWENYE HAKI ATAISHI KWA IMANI" (Warumi 1:16-17). Huu ndio mpango wa Mungu kwa watu wote wanoipokea Injili ya Kristo na kuokolewa. Katikati ya dhuluma,wizi, uasherati na maovu mbalimbali yanayoambatana na hali ngumu ya uchumi iliyopo sasa na ile itakayotokea miaka si mingi iliyo mbele yetu kuanzia sasa – Mungu anawataka watu waishi kwa kufuata mpango wake – WAISHI KWA IMANI.
Kuishi kwa Imani ndiyo utaratibu wa uchumi wa mbinguni ambao kila mkristo anatakiwa kuufuata akitaka kuishi maisha ya mafanikio na matakatifu katikati ya hali ngumu ya uchumi – badala ya kujikuta amewezwa na masumbufu ya maisha haya.
Inasikitisha kuona kuwa wakristo wengi wameyatafsiri na kuyatumia vibaya maneno haya "kuishi kwa Imani". Na kwa ajili hiyo mpango wa Mungu uliomo ndani ya maneno haya haujaeleweka na wengi.
Wakristo wengine wanafikiri kuishi kwa imani ni kuacha kazi wanazozifanya na kuanza kuishi maisha ya omba omba na ya kubahatisha. Wamesahau kuwa biblia inasema mtu asipofanya kazi asile – soma 2Wathesalonike 3:6 – 12.
Ingawa kuna wakristo ambao wamelifanya neno hili "kuishi kwa Imani" lisieleweke vizuri; hali hii haiwezi wala haitaweza kubadilisha mpango wa Mungu uliomo ndani yake.
Mawazo yetu siyo mawazo ya Mungu; njia zetu si njia za Mungu; na mipango yetu si mipango ya Mungu. Hakuna njia ya mkato kwa mkristo safi ya kufanikiwa katika maisha, isipokuwa ni kwa kuishi ndani ya mpango wa Mungu uliofunuliwa katika Kristo Yesu.
"Mwenye haki ataishi kwa imani" maana yake nini? "Mwenye haki" maana yake Mkristo, au Mtakatifu, au Mwongofu, au Mteule, au Aliyeokoka. Kwa hiyo tunaweza kusema Mkristo ataishi kwa imani.
Pia tunasoma katika Waebrania 11:1 ya kuwa:"Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana"
Tena imeandikwa katika Warumi 10:17 ya kuwa;"Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo".
Tena imeandikwa katika Yakobo 2:26 ya kuwa;"Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa".
Kwa mistari hiyo michache na mingine mingi iliyomo katika Biblia inatusaidia kujua ya kuwa "Mwenye haki ataishi kwa imani"maana yake kila mkristo anatakiwa kuishi kwa kuwa mtendaji wa Neno la Kristo na siyo msikiaji tu – kila wakati na katika kila eneo la maisha yake.
Roho Mtakatifu alipokuwa anatufundisha haya mimi na mke wangu, tulijua hakika ya kuwa tunatakiwa kutumia muda mwingi kulisoma na kulitafakari Neno la Kristo, ili tuweze kulitenda Neno hilo katika maisha haya. Tulianza kusoma Neno la Mungu na vitabu mbalimbali vilivyoandikwa na watumishi wa Mungu na bado tunaendelea kufanya hivi hata leo, na tumeona mabadiliko makubwa katika maisha yetu – maana mahangaiko tuliyokuwa nayo yametoweka kwa jina la Yesu Kristo! Sasa tunaishi katika maisha ya ushindi na amani ndani yake Kristo.
Tatizo ambalo mtu analipata anapookoka, ni namna ya kuishi katika maisha mapya ya wokovu (2Wakorintho 5:17)
Biblia inatuambia ya kuwa sisi ni raia wa nyumbani mwake Mungu (Waefeso 2:19). Pia inatuambia kuwa sisi si wa ulimwengu huu (Yohana 17:14). Kwa hiyo maisha yetu hayatakiwi kuongozwa na utaratibu wa hapa duniani.
Kuna tofauti kati ya utaratibu wa uchumi wa duniani na utaratibu wa uchumi wa ufalme wa mbinguni. Ingawa sisi tulio wake Kristo tumo humu ulimwenguni hatutakiwi kuishi kwa kutegemea utaratibu wa uchumi wa dunia hii unaoyumba, bali tutegemee utaratibu wa uchumi wa ufalme wa mbinguni – usioyumba wala kubadilikabadilika kwa kuwa umejengwa juu ya mwamba imara – Neno la Kristo.
Wakristo wengi kwa kutokujua hili wamejikuta wakipata shida ya kutaka kuwatumikia mabwana wawili – yaani Mungu na Mali ambapo Yesu Kristo alikwishasema haiwezekani. Matokeo yake ni kupoteza ushuhuda wa kikristo na kuishi maisha ya mahangaiko.
Kutegemea utaratibu wa uchumi wa dunia hii kuna shida sana kwa kuwa uchumi huo ukiyumba kidogo, na wewe unayumba kimaisha. Lakini ukiutegemea utaratibu wa uchumi wa ufalme wa mbinguni huwezi kuyumba wakati uchumi wa dunia ukiyumba – kwa kuwa tumaini lako halimo mikononi mwa dunia na wanadamu – bali ndani ya Kristo Yesu ambaye ni mwamba imara usiotikisika.

Mwl. Mwakasege

Tuesday, February 24, 2015

UWEZA WA JINA LA YESU

UWEZA WA JINA LA YESU

Mtume Paulo anasema katika Waraka wake kwa Wakolosai sura ya tatu na mstari wa kumi na saba kuwa; “Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika JINA LA BWANA YESU, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye.”

Hii ina maana ya kuwa, tukila tule katika Jina la Yesu Kristo. Tukilala tulale katika Jina la Yesu Kristo. Tukizungumza tuzungumze katika jina la Yesu Kristo. Tukiimba tuimbe katika jina la Yesu Kristo. Tukitembea tutembee katika jina la Yesu Kristo. Tukisafiri tusafiri katika jina la Yesu Kristo. Tukilima shambani tulime katika jina la Yesu Kristo; na kadhalika.

Kwa nini tunatakiwa tufanye mambo yote katika jina la Yesu Kristo? Jina hili la Yesu Kristo lina sehemu gani katika maisha yetu ya kila siku?

Kama tunatakiwa kufanya mambo yote katika jina la Yesu Kristo, kwa nini hatufanyi hivyo?

Ukitafakari maagizo tuliyopewa katika biblia utaona ya kuwa, maisha yetu yote yanalitegemea jina hili la Yesu Kristo.

Kama mambo yetu yote yanatakiwa yafanyike kwa jina la Yesu, basi ni muhimu tujifunze zaidi na zaidi kila siku juu ya jina hili la ajabu.

Ni maombi yangu kwa Mungu Baba, katika jina la Yesu Kristo ya kuwa maneno yaliyomo katika somo hili yatachochea kwa upya kiu iliyomo ndani yako ya kutaka kufahamu zaidi siri iliyomo ndani ya jina la Yesu Kristo.

Wiki ya Kwanza: Jina la Yesu Kristo - Mojawapo ya Funguo za Ufalme wa Mbinguni
Wiki ya Pili: Tafakari juu ya Jina la Yesu Kristo
Wiki ya Tatu: Yesu Kristo - Jina la Mwana wa Mungu
Wiki ya Nne: Mamlaka ya Jina la Yesu
Wiki ya Tano: Omba kwa Jina la Yesu Kristo
Wiki ya Sita: Umuhimu wa kuweka imani yako katika Jina la Yesu Kristo

Sunday, February 22, 2015

UWEZA WA NENO LA MUNGU/THE POWER OF THE WORD OF GOD


UWEZA WA NENO LA MUNGU/power of word of God

Karibuni wapendwa tajadiliane na kushilikishana maneno ya Mungu, pia kupeana tarifa mbalimbali za kiroho, pia kuombeana ili tuweze kuishinda dunia hii chafu na kuingia mbinguni yaliko Makazi sahihi na ya milele.
hakuna mtu anayebanwa uhuru ni wako hubiri kadri uwezavyo, omba ushuri, au ombea wanzako .
kwa wachungaji au mtu nayetaka kuweka mahubiri yake kwenye eneo hili na akapata tatizo kama la kushindwa kuweka ujumbe wake... asisite kuwasiliana nami kwa kupitia email hii. embackgrace@hotmail.com



  UMUHIMU WA KUJUA NENO LA MUNGU
Na Mwinjilisti Simon Mkanza

Upo umuhimu wa kujua neno la Mungu katika maisha ya Mkristo halisi.
 
Biblia  inatuambia Yesu Kristo ndiye Neno la Mungu. Kwa maneno mengine Yesu ndiye Neno ambalo Mkristo anapaswa kuwa nalo (Yohana 1:1).

Kwa kusema hivyo kuna  umuhimu wa kumjua Yesu na kumshika, kwa maana yeye ndiye Neno la Mungu. Katika Biblia mtume Petro anasema mbele za Yesu kwamba, twende kwa nani na wewe ndio mwenye maneno ya uzima? Petro alijua upo umuhimu wa kumjua Yesu kama Neno maana ndani ya Neno kuna uzima
Biblia inasema neno la Kristo likae kwa wingi ndani yetu (Wakolosai 3:16).
Kwa nini basi neno la Kristo likae kwa wingi ndani yetu? Ni kwa sababu lina mambo yafuatayo ambayo ni muhimu katika maisha yetu ya Ukristo. Mambo hayo ni…
A) Neno la Mungu li Hai
B) Neno la Mungu lina nguvu (Mwanzo 1:6).
C) Neno la Mungu lina ukali kuliko upanga
D) Neno la Mungu linachoma hata kuzigawanya nafsi, roho viungo na mafuta yaliyomo ndani yake
E) Neno la Mungu li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo


KWA NINI NENO LA MUNGU LI HAI?
Neno la Mungu li hai kwa sababu  Mungu mwenyewe analithibitisha kwamba li hai maana 
a) Linafanya mabadiliko (Isaya 55:10-11).
b) Linatupa kushinda dhambi (Zaburi 119:11).
c) Neno la Mungu  li hai kwa sababu linatupa mafanikio katik mwili. Petro anasema ”kwa neno lako tunatupa nyavu zetu.“  Hapa tunaona kuwa Neno la Mungu  pekee yake ndilo linaloweza kuleta majibu katika maisha yetu (Luka 5:3-6).


Uhai wa Neno la Mungu kwa mtu ndio unaoleta kushinda dhambi. Nao wakamshinda kwa neno la ushuhuda wao (Ufunuo 12:11).

Daudi aligundua au kwa maneno mengine alifahamu umuhimu wa neno la Mungu katika maisha, kama vile mtume Paulo anavyosema na Wakolosai kwa habari ya neno la Kristo kwamba likae kwa wingi ndani ya mioyo yetu

Neno la Mungu lina nguvu na ndio maana  tunamshinda  shetani kwa neno la Mungu.
Yesu kama kielelezo yeye mwenyewe ni neno ndani ya neno anamshinda shetani (Luka 4:1-12). 


Katika mistari hiyo tunaona Yesu anamwambia  shetani  ”imeandikwa“   Shetani nae anageuza usemi nae anamwambia Yesu ”imeandikwa kwamba atakuagizia malaika usije ukajikwaa mguu wako.“ Kwa kuwaYesu neno la Mungu limo ndani yake hamwambii tena shetani imeandikwa ila anamwambia imenenwa. Kwa maneno mengine tukiwa na neno la Yesu ndani yetu hatuwezi kuyumbishwa. Kwanini? Kwa sababu tumeshaona jinsi ambavyo shetani  anajaribu kutumia neno la Mungu   kwa kusema ”imeandikwa.“  Na ni kweli imeandikwa ananukuu kutoka kitabu cha Zaburi 91 :1-12. Hata kama shetani ananukuu maandiko haina sababu  yamimi kushindwa na shetani  maana Yesu tayari alikwisha mshinda. Yesu kumshinda shetani ina nipelekea mimi kusoma neno la Mungu kwa bidii sana. Kwa mfano, ni kweli kabisa imeandikwa mtakula vitu vya kufisha havitawadhuru lakini je, ninywe sumu sitakufa kwa sababu imeandikwa? Hapana, ukinywa hakika utakufa. Shetani hutumia mandiko kuwafunga wasiojua neno la KristoYesu. 

Katika Biblia tunasoma pia kwamba ”imeandikwa“ Wanandoa MKE na MUME wasinyimane. Kwa kutojua neno vijana wa kiume na wa kike wamedanganywa. Si hao tu hata walioko kwenye ndoa wametegwa kwa andiko hilo. Neno linasema katika Mithali 6:32 ”Aziniye na mwanamke hana akili kabisa“ na Mwanamke vivyo hivyo akizini na mwanaume hana akili kabisa. Watu wamepata hasara ya mambo mengi kwa kutojua neno la Mungu. Ili tuweze kumshinda shetani  ni lazima  neno la Yesu liwe ndani  yetu ndiposa tutamshinda shetani. Ayubu kwa neno la Mungu alishinda. (Ayubu 19:25-27, Waefeso 6:17).

Nataka nikwambie neno la Mungu ni msaada katika maisha yetu maana hutupa  majibu ya maisha yetu. Katika Luka 5:3-6 tunasoma jinsi Petro na wenzake walivyopata samaki wengi kwa kutii neno la Kristo. Kumbuka pia juu ya yule akida, alimwambia Yesu ”...sema neno tu na mtumwa wangu atapona“ (Luka 7:2-10). Yesu akisema neno lazima mabadiliko yatokee. 

Neno la Mungu lina ukali kuliko upanga. Kwa nini neno la Mungu  lina ukali kuliko upanga? Upanga unaweza kukukata na usipone. Lakini neno linakata na kuponya. Kwa neno hili wafalme wanatubu. Yona alitumia neno la Mungu likawa kali watu wakatubu. (Yona 3:1-10; Matendo ya Mitume 8:18-24).

Neno la Mungu linachoma hata kuzigawa nafsi na roho na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake (Matendo 7:51-54, Yohana 4:16 -18, 27-29). Mwanamke akaambiwa mambo yake; Neno likachambua kila tabia..

Neno la Mungu li jepesi kutambua mawazo na makusudi ya moyo.
Yesu kama Neno la Mungu anajua mambo ambayo watu wanawaza ndani ya mioyo yao (Luka 5:17-24, 6:6-8 ; Mathayo 16:1-4)Yapo makusudi ya moyo ambayo ni ya siri sana kwa mwanadamu lakini nataka nikuambie neno la  Mungu ni jepesi kutambua makusudi ya moyo. 


Mtume Petro aliyependa kujua neno la Mungu, naye pia Mungu alimjalia neema ya kuyajua makusudi ya moyo wa mwanadamu (Matendo 5:1-11). Elisha aliyajua makusudi ya moyo wa mfalme ya kuwatenda Israeli kwa siri ila Mungu alimpa neema ya kuyajua mawazo ya mfalme (2 Wafalme 6:8-12). 

Hili ni jambo la msingi katika maisha ya Mkristo yaani kulijua neno la Mungu. Neno la Mungu  tukiwa nalo na likitenda kazi ndani yetu lazima tufanikiwe (Yoshua 1:8) .

Je unahitaji kuwa na imani katika neno la Mungu? Basi, ni neno la Mungu peke yake ambalo laweza kuumba imani, maana pasipo neno la Mungu hakuna imani (Waebrania 11:3 ; Warumi10:17). Ili uwe mwanafunzi wa Yesu ni lazima ulijue neno la Mungu na kulishika.(Yohana 8:31 ; Luka 2:19). Kama neno halimo ndani yetu tunayoyafanya yanakuwa hayana Mungu, hata twaweza kusalitiana. Mtu anayelitamani neno la Yesu  huling’ang’ania na kulitenda maana kwake ni nguvu. (1Wakorintho 1:18). Si kwamba Neno la Mungu ni nguvu tu: bali huleta faida (Mathayo 13:23).

Watu wengi tunapotea kwa kutokujua uwezo (nguvu) iliyomo katika neno la Mungu (Mathayo 22:29).

Yesu anasema, mtu anayelitenda neno la Mungu na kulishika huyo amepanda mbegu ambayo itazaa sana, maana ndani ya moyo wake imo mbegu ambayo ni neno la Mungu la uponyaji na mafanikio, msamaha, utu wema na mengi yanayofanana na hayo.

Yapaswa maisha yetu yawe yenye neno (mbegu) la  Mungu ili tuweze kuzaa mambo mazuri.
 

Wokovu wetu unaimarika kwenye neno la Mungu. Hilo neno la Mungu tunalipata wapi? Isaya 34:16. Upo umuhimu wa kuyachunguza maandiko ili kujua Mungu anasema nini (Matendo 17.10-11).  Je, tangu ulipowekwa msingi wa wokovu, neno limo ndani? (Hagai 2:18-19). Kila kitu kinaweza kupita lakini sio neno la Mungu (Isaya 40:8, Mathayo 24:35).
  
Ili neno litende kazi katika kinywa chako unapolitamka na kuamini ni lazima iwepo nguvu ya Roho Mtakatifu. Bila hii nguvu hamna kitakacho endelea. Utasema umeamini lakini hakutakuwa na matokeo. Mungu mwenyewe alipotamka neno liliambatana na nguvu ya Roho Mtakatifu (Mwanzo1:2-3).

**************** 

Kama una swali kuhusu somo hili nitumie barua pepe (ceymera@yahoo.co.uk)
au nipigie simu: +255 784 475622;  +255 786 477021

Mungu akubariki


BIBLIA NI NENO LA MUNGU LILILO HAI

Katika Biblia Yako SomaZaburi 119: 9-11,105;
Waebrania 4:12;  Marko 4:21-29.

Mstari Wa KukaririKila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema           (2Tim 3:16, 17).
Baadaye Zungumzieni Jambo HiliJe, unaamini kuwa Neno la Mungu ndilo lenye mamlaka yote katika maisha?
Jambo La Kufanya Kabla Hatujakutana TenaJitahidi kutenga muda maalum kila siku kwa ajili ya kutulia na kutafakari. Tekeleza mpango wa kusoma Biblia. Andaa alama saba za kuweka katika Biblia yako pale unapoachia kusoma ili uweze kupapata kirahisi utakapoendelea kupasoma tena wiki inayofuata.
Kazi Ya Kuandika Ya StashahadaKutoka katika 2Fal 22:8-13 na 2Fal 23:1-32 andika mageuzi yote aliyoyafanya mfalme Yosia baada ya kulisikia neno la Mungu.
Tafakari Andiko HiliMathayo 7:24-27

Tumia Dakika Moja Kuubadilisha Ulimwengu
Ombea taifa la Ujerumani.
Idadi ya watu: 80,000,000. Idadi ya Wakristo ni 75%
Ujerumani Mashariki maskini na Ujerumani Magharibi tajiri sasa zimeungana. Makanisa ya zamani yanapoteza watu. Uamsho unatakiwa haraka

1. Biblia Ni Neno La Mungu
Kwa kila mwamini neno la Mungu ni la kipekee na la thamani kubwa. Kwa karne nyingi zilizopita watu wengi wametoa maisha yao katika kuhifadhi kweli ya neno la Mungu kwa ajili yetu ili tupate kusoma. Kwa kuzingatia thamani kubwa ya neno la Mungu, na andiko kutoka Mk 4:21, swali ni hili, ‘Biblia iko wapi katika maisha yako?’ 

Je, imefichwa mbali;
Au imewekwa mahali pa juu ili ipate kumulika kila eneo la maisha yako?
2. Baraka Katika Neno La Mungu
Neno lake li hai, linanena nawe na kutenda kazi ndani yako (Ebr 4:12,13).
Neno lake ni kioo kinachokufanya ujione ulivyo kadiri unavyoendelea kulisoma. Neno lake kamwe halitakufanya ujidanganye mwenyewe, wala kuficha ukweli (Yak 1:22-24) (Mk 4:22).
Neno lake litakuandaa kikamilifu ili uwe, na ufanye kile Mungu anachotaka (2 Tim 3:15-17).

Kuanzia ulipokuwa mtoto hadi sasa umeyajua Maandiko Matakatifu yanayoweza kukupa hekima unayoihitaji kwa ajili ya kupata wokovu kwa imani katika Kristo Yesu. Maandiko yote yana pumzi ya Mungu nayanafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki, ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.

Inasemekana, na ndivyo ilivyo, kwamba Biblia ni Mwana wa Mungu katika maandishi, kwa sababu Yesu anaitwa ni Neno, na vilevile anaitwa Kweli (Yn 1:1).
Je, Unataka Kufanikiwa Na Kustawi?Basi fanya yale Yoshua aliyoagizwa kufanya (Yos 1:8). Na kama unataka kustawi kwa kila kitu zingatia Zab 1:1-3.
3. Je, Unaposoma Unasikia?
Je, umewahi kugundua kuwa unaposoma neno la Mungu ‘unasikia’ kwa ndani na si kwa masikio ya nje? Hiyo ni sauti ya Mungu. Yapasa tuwe makini na kile tunachosikia kwa sababu kwa kipimo kilekile tunachotumia, ndicho tutakachopimiwa (Mk 4:24).
4. Je, Unalitumiaje Neno La Mungu?

Unalitumia hilo neno kufanya upya moyo wako (Rum 10:17).
Unalitumia hilo neno kufanya upya mawazo yako Rum 12:2).
Unalitumia hilo neno kufanya upya maneno yako (Rum 10:10) (Mit 18:2).
Ulitumie hilo neno kufanya upya matendo yako (Yn 14:15).
Ulitumie hilo neno kuimarisha ushindi wako. Shetani hakuwa na usemi Yesu aliposema, ‘Imeandikwa’! (Mt 4:1-11)-zingatia mistari ya 4,7 na 10.
Litumie Neno Kuhuisha Maombi YakoWaamini wa kwanza mara kwa mara walinukuu maandiko ili yawaongoze katika maombi, na Mungu alijibu haraka (Mdo 4:23-31). Iwapo utaomba kwa kutumia neno la Mungu, yafuatayo yataanza kutokea:
Kwanza, unapanda mbegu ya neno.
Kisha kwa uvumilivu katika kuliomba neno, na saburi, huja masuke. Na kwa kadiri unavyoendelea kuwa na imani kwa Mungu na katika neno lake, huja ngano pevu, nafaka kukomaa na hatimaye mavuno.
(Mk 4:14, 26-29) (Isa 55:10, 11) (Mwa 8:22).
Ni Muhimu Kuwapa Wengine Neno La MunguNi muhimu kwa sababu ye yote mwenye neno la Mungu anaweza kuokolewa na kupewa zaidi, mathalani: uponyaji, uhuru, uongozi, baraka na ustawi, kwa kuliamini. Lakini mtu asiye na hilo neno la Mungu ili kuliamini na kulifanyia kazi, hana baraka yo yote katika hizo zilizotajwa, na atapoteza hata hicho alichonacho, yaani maisha yake na nafsi yake milele (Mk 4:25).
5. Unapataje Kulisikia Neno?
Mungu amefanya iwe rahisi sana kuisikia sauti yake. Wewe kaa peke yako na Yeye, na kisha fungua Biblia yako. Kiri udhaifu wako na omba kujifunza kwa msaada wa Roho Mtakatifu. Chukua muda kutafakari yale uliyosoma na kusikia, kwa sababu kwa njia hiyo utashangaa kuona jinsi Mungu atakavyozungumza na wewe na kujibu maswali yako.
Nikiwa mwamini mpya sikuyajua mambo haya.  Nilihudhuria kwenye kusanyiko la maombi na kimyakimya niliomba kwa ajili ya kazi yangu, nikamwombea mke wangu na watoto kwa sababu ya matatizo yote tuliyokuwa nayo. Baada ya muda mfupi nilihisi msukumo wa kuichukua Biblia yangu na ikafunguka yenyewe katika Zaburi ya 128. Na nilipoanza kusoma Mungu alinistusha na baadaye akanipooza  kwa neno lake akiuambia moyo wangu:

“Wamebarikiwa wote wamchao Bwana na kutembea katika njia zake.
Utakula matunda ya kazi yako, baraka na kustawi vitakuwa vyako.
Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao, na wanao kama matawi ya mtende mezani pako”.
Naliliamini neno la Mungu na leo hii, baada ya miaka kadhaa kupita naweza kuona jinsi Mungu alivyoitunza ahadi yake kwa kuibariki familia yangu na kazi yangu.
6. Namna Ya Kufurahia Usomaji Wa Biblia
Watu wengi huanza na kitabu cha Mwanzo na baadaye huacha wanapokutana na sehemu ngumu katika Agano la Kale ambazo hawazielewi. Sisi sote tunapenda kula vyakula mbalimbali siku kwa siku, na hivyo ndivyo ilivyo hata kwa chakula cha kiroho. Jaribu kufuata mpangilio ufuatao nawe utapata mlo tofauti kila siku. Kila siku soma Zaburi za kuabudu na Mithali kwa ajili ya kupata hekima.

Jumatatu
Hadithi za watu mashuhuri na za historia ya Biblia. Anza na kitabu cha Mwanzo na kuendelea hadi kitabu cha Esta.
Jumanne
Taarifa za watu waliomjua Yesu vizuri. Anza na injili ya Mathayo  na kuendelea hadi ya Luka.
Jumatano
Tembea katika vilima na mabonde ya ushairi. Anza na kitabu cha Ayubu  hadi Wimbo Ulio Bora.
Alhamisi
Nyaraka za upendo kutoka kwa Yohana. Anza na injili yake, ikifuatiwa na nyaraka zake, na kuishia na Ufunuo wake.
Ijumaa
Unabii wa Biblia. Anza na Isaya na kuendelea hadi Malaki; utastaajabu.
Jumamosi
Nyaraka kutoka kwa watu mashuhuri wa Mungu. Anza na Warumi, endelea hadi Petro na Yuda.
Jumapili
Tembelea makanisa yaliyo hai na misheni zilizoko mstari wa mbele kwa kusoma kitabu cha Matendo ya Mitume.
Kwa Kumalizia Omba Kwa Ajili Ya Watu Wa Ulimwengu Huu Ambao Bado Hawajafikiwa Na Injili, Ukiwataja Kwa Majina
  

UWEZA WA JINA LA YESU

Mtume Paulo anasema katika Waraka wake kwa Wakolosai sura ya tatu na mstari wa kumi na saba kuwa; “Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika JINA LA BWANA YESU, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye.”
            Hii ina maana ya kuwa, tukila tule katika Jina la Yesu Kristo. Tukilala tulale katika Jina la Yesu Kristo. Tukizungumza tuzungumze katika jina la Yesu Kristo. Tukiimba tuimbe katika jina la Yesu Kristo. Tukitembea tutembee katika jina la Yesu Kristo. Tukisafiri tusafiri katika jina la Yesu Kristo. Tukilima shambani tulime katika jina la Yesu Kristo; na kadhalika.
            Kwa nini tunatakiwa tufanye mambo yote katika jina la Yesu Kristo? Jina hili la Yesu Kristo lina sehemu gani katika maisha yetu ya kila siku?
Kama tunatakiwa kufanya mambo yote katika jina la Yesu Kristo, kwa nini hatufanyi hivyo?
Ukitafakari maagizo tuliyopewa katika biblia utaona ya kuwa, maisha yetu yote yanalitegemea jina hili la Yesu Kristo.
Kama mambo yetu yote yanatakiwa yafanyike kwa jina la Yesu, basi ni muhimu tujifunze zaidi na zaidi kila siku juu ya jina hili la ajabu.
Ni maombi yangu kwa Mungu Baba, katika jina la Yesu Kristo ya kuwa maneno yaliyomo katika somo hili yatachochea kwa upya kiu iliyomo ndani yako ya kutaka kufahamu zaidi siri iliyomo ndani ya jina la Yesu Kristo.

Sunday, February 15, 2015

Jinsi shetani/satan/ibilisi Anavyozuia Maombi Yako


Jinsi shetani/satan/ibilisi Anavyozuia Maombi Yako


Ndugu msomaji wa blog hii, kati ya makala au masomo ambayo nimeyaandika humu, hili ni somo na ushuhuda mmojawapo wenye nguvu sana ambao, kila mwana wa Mungu atakayeusoma, atapata msukumo wa rohoni usio wa kawaida. Haya ni mafunuo yenye nguvu mno ambayo, hakika yatakuinua kwa kiwango cha juu sana nawe utamshukuru Mungu. Nilipouona ushuhuda huu kwenye mtandao, moyo wangu ulianza kuwaka niweze kuutafsiri harakaharaka na kuuweka kwenye blog hii ili yamkini uweze kuwafikia wapendwa wengi iwezekanavyo.



Huu ni ushuhuda ulioandikwa na Mchungaji John Mulinde wa Uganda kutokana na kile alichosikia kutoka kwa mhusika mwenyewe. Mhusika huyo, mchungaji hajamtaja, lakini alikuwa ni kijana ambaye alimtumikia shetani tangu angali tumboni mwa mama yake. Baadaye, kwa neema ya Bwana kijana huyo aliokolewa, ndipo akaanza kueleza siri hizi za ufalme wa giza na ufalme wa nuru.


Mamilioni ya Wakristo duaniani tunamwomba Mungu wetu kwa ajili ya mahitaji mbalimbali tuliyonayo. Lakini liko swali moja kubwa linalojirudiarudia ndani ya mioyo yetu karibu kila siku. Tunajiuliza, “Nimeomba sana na kwa muda mrefu. Mbona Mungu hajibu...?” Tunabaki bila majibu, tunavunjika moyo, na tunaanza kudhani labda sisi ni wenye dhambi sana ndio maana hatujibiwi.


Ukiifahamu siri iliyomo kwenye ushuhuda huu, utatiwa nguvu sana za rohoni; maana maarifa ndiyo yanayotufanya tuwe na nguvu za Mungu. Tunaenenda kiimani kwa kadiri ya kiwango cha maarifa au ufahamu uliomo ndani yetu. Tukijua sana, tunaweza sana; tukijua kidogo, tunaweza kidogo.


Karibu ujipatie maarifa ambayo Bwana wetu ameruhusu yatufikie. Nami na hakika utamfurahia Bwana kwa kukupigisha hatua nyingine ya imani. Utafanya vema kama ukiweza kuwapatia na wengine somo hili la muhimu sana kwa ajili ya mwili wa Kristo.


******************

Yafuatayo ni maelezo ya Mchungaji John Mulinde:
Napenda nikushirikishe ushuhuda wa kijana mmoja ambaye aliokoka; kijana ambaye alikuwa akimtumikia ibilisi. Na mtu yule alipotoa ushuhuda wake, ulinitia changamoto kubwa sana. Sikutaka kuamini. Ilinibidi nifunge kwa muda wa siku kumi mbele za Bwana, huku nikimuuliza, "Bwana, hivi mambo haya ni kweli?" Na ilikuwa ni katika wakati huo ndipo Bwana alipoanza kunifundisha kile kinachotokea kwenye ulimwengu wa roho pale tunapoomba.

Kijana huyu alizaliwa baada ya wazazi wake kuwa wamejiweka wakfu wao wenyewe kwa lusifa. Wakati bado akiwa tumboni, walifanya matambiko mengi na kumweka wakfu awe mtumishi wa lusifa. Alipozaliwa na kufikisha miaka minne, tayari alianza kutumia nguvu zake za kiroho. Hata wazazi wake walianza kumwogopa! Akiwa na miaka sita, baba yake alimkabidhi kwa wachawi ili akapatiwe mafunzo. Na akiwa na miaka kumi, alikuwa akifanya mambo makubwa katika ufalme wa ibilisi. Alikuwa akiogopwa hata na wachawi wa kawaida.

Alikuwa bado ni kijana mdogo, lakini mambo aliyokuwa anafanya yalikuwa ni mabaya mno. Alikua hadi kufikia miaka ya ishirini akiwa na damu nyingi ya watu mikononi mwake. Aliua watu kila alipotaka. Alikuwa na uwezo wa kutoka nje ya mwili wake kupitia taamuli ya kinjozi (transcendental meditation), yaani kitendo cha kutuliza mawazo na mwili kama wafanyayo Wahindukatika yoga. Tazama mfano HAPA. Katika huko kutaamuli, angeweza hata kunyanyuka kimwili kutoka ardhini pale alipokaa na kuelea hewani (levitate). Tazama mfano HAPA. Wakati mwingine aliweza kutoka nje ya mwili; akauacha mwili wake na kwenda nje huko na kule kufanya mambo mbalimbali (astro-travelling).  Na kijana huyu alitumiwa na shetani kuharibu makanisa mengi; na kuwaharibu wachungaji wengi.

Siku moja, alipangiwa kwenda kuharibu kanisa moja ambalo lilikuwa na maombi ya kutosha. Kulitokea na migawanyiko mingi kanisani na kuchanganyikiwa kwingi. Alianza kufanya kazi kwenye kanisa hili; lakini mchungaji wa kanisa lile aliitisha mfungo wa kanisa zima. Kanisa lilipoanza kufunga, watu walitubu sana na kufanya mapatano mengi. Na watu wakawa kitu kimoja, na wakaanza kuomba kwa ajili ya kazi ya Bwana katikati yao. Na wakaendelea kufanya maombezi na kumlilia Mungu ili awarehemu na kuingilia kati maishani mwao. Na kadiri siku zilivyoendelea, bwana huyu alikuwa akija tena na tena akiwa na mapepo kinyume na kanisa hili. Lakini lilitoka neno la kinabii likiwaambia Wakristo wasimame pamoja na kufanya vita dhidi ya nguvu za giza ambazo zilikuwa zinashambulia kanisa lile.

Siku moja, kijana huyu aliuacha tena mwili wake chumbani kwake na akatoka nje. Aliongoza jeshi kubwa la mapepo moja kwa moja hadi kwenye kanisa lile ili kwenda kufanya vita vya kiroho.

Sasa, ufuatao ni ushuhuda wake.

Roho yake ilikuwa inapaa hewani juu ya kanisa lile na kujaribu kulishambulia, lakini kulikuwa na kifuniko cha nuru juu ya kanisa hilo. Wakati waliendelea na mapambano, ghafla, kulikuja jeshi la malaika ambalo liliwashambulia na kukawa na mapambano makali pale hewani. Hatimaye, mapepo yalikimbia, lakini yeye alikamatwa na wale malaika.  

Ndiyo, alikamatwa na malaika! Alijiona akiwa ameshikiliwa na malaika sita. Na wakamleta kwa kumpitisha kwenye paa hadi kwenye madhabahu ya kanisa. Akawa yuko pale huku watu wanaendelea kuomba. Walikuwa wamezama kwenye maombi, wakifanya vita vya kiroho; wakifunga na kuvunja, na kutupa nje. Mchungaji alikuwa kwenye madhabahu akiongoza maombi hayo na vita. Roho wa Bwana akaongea na mchungaji, akisema, "Nira imevunjika, na mhusika yuko hapa mbele yako. Msaidie kwa kumfungua."

Mchungaji alipofungua macho yake, alimwona yule kijana akiwa ameanguka pale hajitambui. Mwili wake ulikuwa pamoja naye! Kijana yule anasema kuwa haelewi ni kwa vipi mwili wake uliungana naye; maana alikuwa ameuacha nyumbani. Lakini ndio alikuwa pale; hajui ni kwa vipi aliingia, isipokuwa tu malaika walimpitishia kwenye paa.



Sasa, mambo haya ni magumu kuamini, lakini mchungaji alinyamazisha kanisa na kuwaambia kile ambacho Bwana alimwambia. Kisha akamwuliza yule kijana, "Wewe ni nani?" Kijana yule alikuwa anatetemeka wakati mapepo yalipoanza kumtoka.

Kwa hiyo, waliomba kwa ajili ya kufunguliwa kwake, na hatimaye baadaye alianza kusema ushuhuda wake. Hivi sasa kijana huyu ameshaingia kwa Bwana na ni mwinjilisti, akihubiri Injili. Anatumiwa sana na Bwana kuwaweka huru watu wengine.    

Usiku mmoja, mimi (John Mulinde) nilienda kwenye chakula cha usiku mahali fulani. Sababu hasa ya kwenda pale ni kwa vile kuna mtu alinieleza habari za huyo kijana; na nilikuwa na shauku kubwa sana ya kumwona, na kuona kama kweli hadithi yake ina ukweli wowote. Kwa hiyo, nilipofika, nilikaa mezani. Na jioni ile, kijana huyu alipewa nafasi ya kutoa ushuhuda wake. Alizungumza juu ya mambo mengi sana. Mara nyingine alilia kutokana na mambo aliyoyafanya. Alipomaliza kusema, alitoa ombi.

Kulikuwako na wachungaji wengi pale kwenye ukumbi. Alisema, "Ninawaomba ninyi, wachungaji. Tafadhalini, wafundisheni watu namna ya kuomba.”  Watu ambao hawaombi, wanaweza kuchukuliwa na chochote, katika chochote na ibilisi; na ziko hata njia za adui za kutumia maisha yao na maombi yao. Adui anajua hata namna ya kutumia kwa faida yake maombi ya watu wasiojua kuomba. "Wafundisheni watu namna ya kutumia silaha za kiroho ambazo Mungu amezitoa."

Kisha alieleza jinsi ambavyo alikuwa akiongoza mapambano kwenye anga. Alikuwa akienda pamoja na maajenti wengine wa shetani na mapepo mengi hadi angani. Ilikuwa kama zamu. Inabidi kwenda kutekeleza zamu yako. Kwa hiyo, ni mara nyingi tu alikuwa na muda wa kwenda kwenye anga ili kufanya vita. Na akasema kuwa kule angani, kwenye ulimwengu wa roho, kama anga limefunikwa na blangeti la giza, blangeti hilo linakuwa ni nene sana; na ni kama jiwe. Na linakuwa limefunika eneo lote. Na mapepo haya yanaweza kwenda juu yake na chini yake. Na yakiwa huko, yanaweza kuathiri matukio yanayoendelea duniani. 

Pale mapepo wachafu pamoja na maajenti wa shetani wa kibinadamu wanapomaliza zamu yao, wanashuka duniani kwenye maeneo ya kimaagano, iwe ni kwenye maji au ardhini, ili kuweza kurejesha upya nguvu zao, maana zinakuwa zimepungua kutokana na kufanya kazi angani wakati wa zamu yao. Na wanarejeshaje nguvu zao? Ni kupitia kafara ambazo watu wanatoa kwenye madhabahu hizi. Kafara zinaweza kuwa ni uchawi wa wazi, damu za aina zote, ikiwa ni pamoja na utoaji mimba, vita, na utoaji wa kafara za wanadamu na wanyama. Zinaweza pia kuwa ni kafara za uzinzi, pale ambapo watu wanafanya uzinzi na uashetati wa kila aina. Na matendo haya maovu yanaleta nguvu kwenye ulimwengu wa giza. Na ziko aina nyingi za kafara.  

Kijana huyo alisema kuwa, maajenti wa shetani wanapokuwa juu kwenye anga, na Wakristo wakaanza kuomba hapa duniani, maombi ya Wakristo huonekana kwa namna tatu. Maombi yote huonekana kama moshi ambao unapaa kuelekea mbinguni.

Baadhi ya maombi huonekana kama moshi, na yanaenda juu kiasi na kupotelea hewani. Maombi ya aina hii hutoka kwa watu ambao wana dhambi maishani mwao na hawako tayari kushughulika nazo. Maombi yao ni dhaifu sana, kiasi kwamba yanapeperushwa na kupotelea angani.

nyingine ya maombi nayo ni kama moshi ambao unainuka juu hadi unapofikia kwenye ule mwamba, lakini hayana nguvu ya kupenya mwamba huo. Kwa kawaida, hawa ni watu ambao hujaribu kujitakasa, lakini hawana imani juu ya kile ambacho wanakifanya pale wanapoomba, yaani wanaomba lakini moyoni hawana ujasiri kwamba kile wanachokiomba watakipokea. Mara nyingi huwa wanapuuzia mambo mengine ya muhimu yanayotakiwa wakati mtu anapoomba. 

Aina ya tatu ya maombi ni kama moshi ambao umejaa moto. Yanapokuwa yanapaa, yanakuwa ni ya moto sana kiasi kwamba yanapoufikia ule mwamba, unaanza kuyeyuka kama nta. Yanapenya mwamba huo na kuendelea hadi juu.

Mara nyingi watu wanapoanza kuomba, maombi yao huonekana kama aina ya kwanza ya maombi. Lakini kadiri wanavyoendelea kuzama, yanageuka na kuwa ya aina ya pili. Na wakiendelea zaidi, ghafla yanalipuka moto. Na maombi hayo yanakuwa yana nguvu sana kiasi kwamba yanapenya kabisa ule mwamba.

Mara nyingi maajenti wa uovu hubaini kwamba kuna maombi yanabadilika na kuelekea kwenye kuwa moto. Kisha huwasiliana na viumbe vingine vilivyoko duniani na kuwaambia, "Mvurugieni mtu huyo maombi! Mfanyeni aache kuomba! Mwondoeni kwenye maombi!"

Mara nyingi Wakristo hushindwa na mbinu hizi. Wanakuwa wanaomba kwa nguvu; wanatubu; wanaruhusu Neno kukagua nafsi zao; imani inaanza kujengeka. Maombi yao yanaanza kuwa na shabaha zaidi. Kisha ibilisi anaona kuwa maombi yao yanaanza kukusanya nguvu. Ndipo vurugu zinaanza ili kuharibu maombi hayo. Mara simu inalia. Wakati mwingine, katikati ya maombi ambapo mtu alikuwa amezama kabisa, , simu inaweza kulia na unawaza kuwa, ngoja niende nikaipokee kisha nitarudi kuendelea na maombi.  

Mbinu zingine za kuvuruga maombi nazo zinaweza kutumika; hata kama ni kukugusa mwili wako na kuleta maumivu mahali fulani. Hata pia kukufanya ujisikie njaa ambapo utajisikia kwenda jikoni kutengeneza japo chakula kidogo. Ilimradi tu wakiweza kukufanya utoke mahali pale, wanakuwa wameshakushinda. Wachungaji, ni lazima muwafundishe watu jinsi ya kuomba. Tengeni muda, si tu kwa ajili ya maombi ya juujuu. Mara moja kwa siku, Wakristo wanatakiwa kuwa na muda wa kujielekeza kwa moyo wote kwa Mungu, bila kuwapo kwa kitu chochote cha kuwaharibia umakini wao. 

Na kama watu waking’ang’ana kabisa kwa njia hii ya maombi na kuruhusu kupata mwongozo wa kiroho, kisha wakawa wanaendelea na kuendelea, lazima kitu kitatokea rohoni. Moto utalipuka na kugusa ule mwamba na kuuyeyusha! Kuyeyuka kunapoanza, ni moto sana kiasi kwamba hakuna pepo ambaye anaweza kustahimili. Wala hakuna roho ya mwanadamu inayoweza kustahimili pia. Wote wanakimbia.

Kama mtu atajitoa kuomba kwa bidii na kwa kumaanisha namna hiyo, hatimaye kutafuata kufunguka kwa ulimwengu wa roho. Na mara hili linapotokea, matatizo yote haya katika maombi yanafikia mwisho! [Yaani ule ugumu na ule uzito unakwishilia mbali!] Yule ambaye anakuwa anaomba duniani anakuwa sasa anajisikia kuwa maombi ni kitu kilaini kabisa, cha kuburudisha, na chenye nguvu.

Na nimegundua kuwa wakati huo, huwa tunapoteza kabisa hisia za muda na mambo mengine. Si kwamba tunakosa mpangilio; la hasha! Mungu anakuwa anashughulika na muda wetu. Lakini inakuwa ni kama unaachilia kila kitu, na unaunganishwa moja kwa moja na Mungu. Maombi yako yanapopenya, kunakuwa hakuna kizuizi tena kuanzia hapo; na mtu anayeomba anaweza kuendelea kwa muda mrefu kama apendavyo. Hakuna kabisa kizuizi. 

Na mara anapomaliza kuomba, lile tundu linabakia wazi.

Kijana huyu pia alisema kuwa, watu wa namna hii wanapomaliza kuomba na kuondoka mahali hapo, lile tundu linakuwa linaondoka pamoja nao. Wanakuwa hawaenendi tena chini ya lile blangeti la jiwe. Wanakuwa wanaenenda chini ya mbingu zilizo wazi. Na akasema kwamba, katika hali hiyo, ibilisi hawezi kufanya kile anachokitaka kwao. Na uwepo wa Mungu unakuwa kama nguzo kutoka mbinguni ikiwa iko juu ya maisha yao. Wanalindwa; na kunakuwa na nguvu kubwa sana ndani ya hiyo nguzo kiasi kwamba kadiri wanavyotembea huku na kule, uwepo huo unakuwa unagusa hata watu wengine. Nguzo hiyo inakuwa inatambua kile ambacho adui amefanya kwa watu wengine. Na pale watakatifu hao wanapozungumza na watu wengine, na wale watu wakawa wamesimama nao, wanaingia ndani ya nguzo hiyo. Na mradi tu wakiwa ndani ya ile nguzo, vifungo vyote vya adui vinadhoofika.  

Kwa hiyo, watu hawa wenye mpenyo huu wa kiroho wanapowashuhudia wenye dhambi habari za Yesu Kristo, upinzani wa wenye dhambi unakuwa wa chini. Ni rahisi kuwaleta wenye dhambi kwa Kristo. Wanapoomba kwa ajili ya wagonjwa, au kwa ajili ya mambo mengine, maombi yao yanakuwa na nguvu sana.

Na kama kuna sehemu ambako maombi ya namna hii huombwa mara kwa mara, uwepo wa Mungu unakuja mahali pale na hauondoki. Hivyo, hata watu wasiomjua Mungu wanapokuja kwenye sehemu kama hizo, ghafla vifungo vyao vinakatika.

Na kama atatokea mtu wa kusema nao kwa uvumilivu na kwa upendo, wanaweza kugeuka haraka sana; si kwa nguvu au kwa uwezo, bali ni kwa Roho wa Mungu, ambaye anakuwa yuko pale. Na kama hakuna mtu atakayewajali watu hawa, wanakuja kwenye uwepo wake na kujisikia hatia, wanaanza kujadili kama wakubali au la. Pale watakapoondoka, vifungo vinakuwa na nguvu zaidi kwao. Na ibilisi anajihadi kwa kila njia kutowaruhusu kurudi tena kwenye sehemu kama hizo.

Je, shetani anakaa kimya tu baada ya mtu kupata mpenyo?

Kijana huyu alisema kuwa, ibilisi anawachukia sana watu wa namna hiyo, yaani wale waliopata mpenyo wa maombi.

Sasa unaweza kupiga picha, sote tulikuwa tumekaa chini tunamwangalia kijana huyu akieleza ushuhuda wake. Alikuwa anatueleza mambo ambayo yeye mwenyewe alikuwa akiyafanya na aliyoyashuhudia kwa macho yake. Alitueleza kile ambacho walifanya kwa watu ambao walipata mpenyo katika maombi. Alisema kuwa waliwaweka akilini sana watu kama hao. Kisha waliwafuatilia sana na kujifunza kuhusu wao ili kuwajua vizuri. Walitafuta kila kitu kuwahusu. Hivyo, walifahamu udhaifu wao wote, na ikitokea mtu akawashinda kwenye maombi na kupenya, wanawasiliana na wengine kwenye ulimwengu wa giza na kusema, "Mumlenge mtu huyu kwenye eneo hili na hili. Udhaifu wake uko hapa na hapa."

Kwa kuwa mtu wa aina hii anapotoka nje ya kifuniko cha maombi, roho ya maombi inakuwa juu yake, uwepo wa Mungu upo juu yake, roho yake inakuwa iko juu, na furaha ya Bwana ndiyo nguvu zake; anapokuwa anaenda, adui anajaribu kila njia kuleta yale mambo ambayo yatamvuruga ili asielekeze macho yake kwa Bwana.

Kama, kwa mfano, imeshajulikana kuwa udhaifu wake uko kwenye eneo la hasira, basi adui atasababisha watu watende mambo ambayo yatamfanya akasirike. Na kama hayuko makini kumsikiliza Roho Mtakatifu, na akaingiwa na hasira, basi ataondoa macho yake kwa Bwana. Na anapokuwa na hasira hivyo, ghadhabu zinamjaa. Baadaye anapokuja kujirudi, anakuwa anataka kutupilia mbali hali hiyo na kuendelea na furaha ya Bwana, lakini anajikuta hajisikii tena ile furaha kama mwanzo. Anajitahidi kujisikia vizuri tena; lakini haiwezekani tena. Kwa nini? Alipojiachilia kwenye kishawishi cha hasira, mapepo walifanya bidii zote katika muda huo kufunga lile tundu kule juu. Na mara waliporudishia lile jiwe, uwepo wa Bwana unakuwa umekatika, yaani ile nguzo iliyokuwa inatokea mbinguni na kumfunika inakuwa haimfikii tena!

Mtu huyo hataacha kuwa mwana wa Mungu. Lakini ule upako wa ziada uliokuwa unaandamana naye maishani; ule uwepo uliokuwa ukitenda mambo bila yeye kutumia nguvu zozote, unakuwa umekatika! Maana pepo wachafu wanatafuta uliko udhaifu wako. 

Kama udhaifu wa mtu ni kwenye masuala ya mapenzi, adui ataandaa watu, matukio, na mambo ambayo yatainua hisia za mtu huyo za tamaa ya kimapenzi. Na kama mtu huyo atazikubalia hizo tamaa na kufungua akili yake kuyapokea mambo hayo, na kuyalea nafsini mwake, pale anapomaliza kila kitu na kutaka kurejea tena kwenye hali ya upako ili asonge mbele, anakuta kwamba ule uwepo haupo tena. Labda unasema, “Hii si vizuri kabisa.” Kumbuka tu Biblia inasemaje, " Tena ipokeeni chapeo ya wokovu. Vaeni dirii ya haki." Mara nyingi hatuoni haja ya silaha hizi za kivita. Lakini kumbuka Yesu alivyotuambia juu ya namna ya kuomba "Usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu."

Kila mara unapopata mpenyo katika maombi, unapofika mwisho, kumbuka kuwa wewe bado ni kiumbe mwanadamu aliye dhaifu. Kumbuka kuwa haujakamilishwa bado. Mwombe Bwana, useme, "Bwana, nimefurahia wasaa huu wa maombi, lakini nitakapotoka nje kwenye dunia, usiniongoze kwenye majaribu. Usiruhusu niangukie kwenye mtego wa ibilisi. Najua kuwa adui anatega mitego kule nje. Sijui ni mitego ya namna gani. Na ninajua kuwa bado mimi ni dhaifu katika baadhi ya maeneo. Kama nikiingia kwenye hali fulanifulani, nitaanguka. Unilinde, Bwana. Unapoona ninaelekea kule ambako kuna mitego niliyotegewa, nifanye nielekee upande mwingine. Uingilie kati, Ee, Bwana. Usiche niende tu kwa nguvu zangu na uwezo wangu. Niokoe na yule mwovu.”

Mungu anaweza kufanya hivyo. Lakini, kama kuna kitu kibaya kitatokea, ambacho kitakufanya uondoe macho yako kwa Kristo, wewe sema tu, “Asante Yesu.” Ndiyo sababu Mtume Paulo aliandika, “Mshukuruni Mungu kwa kila jambo.” Baadhi ya mambo si mazuri. Yanaumiza, na tunashangaa kwa nini Mungu anayaruhusu yatufikie. Lakini kama tu tungejua kwa njia hiyo anatuokoa na mambo yapi, tungemshukuru. Tukijifunza kumwamini Bwana, tutamshukuru kwa kila jambo.

Yule kijana aliendelea kusema kuwa, unapopata mpenyo katika maombi, majibu yako ni lazima yatakuja. Alisema kuwa jibu mara zote huja, lakini mara nyingi, huwa halifiki kwa mtu aliyeliomba. Kwa nini? Ni kwa sababu ya mapambano yaliyoko kwenye anga. Pia, majibu yanaweza kuzuiliwa iwapo viumbe waovu wa rohoni watafanikiwa kurejesha ule mwamba na kuziba tundu ambalo mwombaji alifanikiwa kulitoboa kwa njia ya maombi yake. 

Kisha aliongea jambo ambalo kwa kweli lilitikisa imani yangu. Binafsi ilinibidi niingie kwenye mfungo wa siku kumi, ili kumwuliza Bwana kama hilo alilosema lilikuwa na ukweli wowote. Basi sikiliza haya: Kijana huyu alisema kuwa, kila Mkristo anaye malaika ambaye anamtumikia Mkristo huyo. Nasi tunafahamu kuwa Biblia inasema kuwa malaika ni roho wanaotutumikia. (Waebrania 1:14).  Alisema kuwa watu wanapoomba, majibu huletwa kwa mikono ya malaika. Malaika huleta majibu, kama ambavyo tunasoma kwenye kitabu cha Danieli. Kisha alisema jambo ambalo ni gumu sana. Alisema kwamba, kama yule anayeomba anafahamu silaha za kiroho na amejivika silaha hizo, majibu nayo huja kwa kupitia malaika ambaye, naye amejivika kikamilifu kwa silaha hizohizo.

Lakini, kama anayeomba hajali silaha za kiroho, basi malaika nao wanakuja bila silaha hizo. Wakristo ambao hawajali kile ambacho kinaingia mawazoni mwao; hawashindani kuangusha mawazo yasiyofaa; malaika wao huja bila chapeo. Silaha zozote utakazoacha kuzitilia maanani duniani, malaika anayekutumikia naye anakuwa hanazo. Kwa maneno mengine, silaha zetu za kiroho hazitulindi miili yetu, bali zinalinda vitu vile vya kiroho tunavyofanikiwa kuvipata kutoka kwa Bwana.

Malaika anapokuwa anakuja, mapepo wanamtazama na kumkagua na kubaini maeneo ambayo hajajifunika; na hayo ndiyo maeneo ambayo watashambulia. Kama hana chapeo kichwani, basi watashambulia kichwani. Kama hana dirii, watashambulia kifuani. Kama hana viatu, watajaribu kutengeneza moto ili kumwunguza miguuni.

Sasa, najua kuwa hili ni gumu kuamini; mimi narudia tu kile ambacho kijana huyu alisema. Kisha tulimwuliza, “Je, malaika wanaweza kuungua moto?” Na unajua alisema nini? Kumbuka kuwa huu ni ulimwengu wa roho. Hizi ni roho kwa roho zinapambana. Mapambano ni makali sana, na pale wanapomshinda malaika wa Mungu, jambo la kwanza wanalokimbilia ni lile jibu alilobeba; na wanalichukua hilo. Na hizi zinakuwa ni zawadi ambazo hutolewa kwa watu kupitia imani za siri, au uchawi.

Kumbuka kile ambacho Biblia inasema kupitia kitabu cha Yakobo. Vipawa vyote vyema hutoka kwa Mungu (Yakobo 1:17). Kwa hiyo, shetani anapata wapi vitu vizuri anavyowapatia watu? Baadhi ya watu ambao hawawezi kupata watoto, huenda kwa wachawi na waabudu shetani, na wanapata mimba! Mtoto anakuwa ametoka wapi? Je, shetani ni muumbaji? HAPANA! Anaiba kutoka kwa watu ambao hawaombi maombi yao hadi mwisho.

Katika Biblia, Yesu alisema, "Ombeni bila kukoma." Pia alisema, "atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani? " Je, Yesu atakukuta bado unangojea? Au utakata tamaa na kumwacha adui aibe kile ambacho umekuwa ukikiombea?

Na hawaridhiki tu na kuiba jibu la maombi. Wanataka pia kumweka malaika kifungoni. Na wanaanza kupambana naye. Wakati mwingine wanafanikiwa kumkamata na kumfunga malaika. Inapotokea hivyo, Mkristo anakuwa kama chakula chao duniani. Wanaweza kumfanyia chochote maana hana ulinzi tena kwenye ulimwengu wa roho.

Nilimwuliza kijana huyo, “Una maana kuwa malaika anaweza kushikiliwa katika ulimwengu wa giza?” Sasa alikuwa anaeleza uzoefu wake, na akasema, hawatamshikilia malaika kwa muda mrefu kwa sababu ya Wakristo wengine ambao wanaomba mahali pengine. Jeshi la ziada litatumwa, na malaika atakuwa huru. Na kama yule Mkristo anayehusika hajaomba hadi kwenye mpenyo, basi atabakia mateka. Ndipo shetani atatuma malaika wake na malaika wa nuru  kwa mtu huyu, na hapo ndipo uongo na udanganyifu unapotokea; maono ya uongo na unabii wa uongo. Uongozi wa uongo, na kufanya kila aina ya maamuzi mabaya. Na mara nyingi, mtu wa namna hii anaweza kupata mashambulizi na vifungo vya kila aina.

Niliondoka kwenye kile chakula cha jioni huku na mawazo mengi sana. Nikasema, “Bwana, sitaki hata kujaribu kuamini jambo hili.” Linaondoa ujasiri na usalama wangu wote! Nilipoenda kumlingana Bwana, ilikuwa ni kwa siku kumi; na Bwana alifanya mambo mawili. Kwanza, si tu kwamba alithibitisha mambo hayo niliyoyasikia kutoka kwa yule kijana, bali pia alifungua akili zangu zaidi ili kuona mambo mengine mengi zaidi ya yale ambayo niliyasikia. Pili, aliniongoza kuona kile ambacho tunatakiwa kukifanya wakati mambo haya yanapotokea ili tuweze kuwa washindi.

Alinipa mambo matatu:

Moja: namna ya kutumia silaha za vita vyetu vya kiroho. Biblia inaziita silaha za Mungu. Si silaha zetu. Tunapozitumia, tunamruhusu Mungu kupigana kwa niaba yetu.

Mbili: tambua uhusiano wa roho zinazotutumikia, yaani malaika, na maisha yetu ya kiroho. Na ni lazima kuwa makini sana na kile kinachotokea mioyoni mwetu; kama mwongozo wa kile ambacho kinatakiwa kutokea rohoni kutuhusu sisi.

Tatu: ni Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu hatakiwi kuja kama mtumishi wetu, kututumikia na kutuletea vitu mbalimbali. Hakimbiikimbii kwa Baba kumweleza kile ambacho tunataka. Hiyo ni kazi ya malaika. Lakini Yeye husimama pamoja nasi. Anafanya nini? Anatuongoza, anatufundisha, anatutangulia, anatusaidia kuomba inavyotakiwa. Na mambo haya yanapotokea kwenye ulimwengu wa roho, anatuambia. Wakati mwingine anakuamsha usiku na kukwambia, “Omba.” Wewe unasema, “Hapana! Muda wangu haujafika.” Na anasema, “Omba sasa!” Kwa nini inakuwa hivyo? Ni kwa sababu Yeye anaona kila kinachoendelea kwenye ulimwengu wa roho. Wakati mwingine anasema, “Kesho ni kufunga.” Wewe unasema, “Hapana, nitaanza Jumatatu!” 

Lakini kumbuka kuwa Yeye anaelewa kile kinachoendelea kwenye ulimwengu wa roho. Ni lazima tujifunze kuwa makini na Roho Mtakatifu. Anatuongoza kwenye njia za haki. Wapendwa, tuishie hapa. Labda wakati mwingine tutaongea jinsi ambavyo tunaweza kuomba hadi kupata mpenyo, maana sasa tunajua mapambano yaliyoko rohoni na jinsi ya kupenya; na namna tunavyoweza kudumu tukiwa na mpenyo tuliopata. Na mara tunapojifunza hili, linakuwa ni jambo la furaha sana. Tukumbuke tu jambo moja: vita si vyetu, bali ni vya Bwana! Haleluya!  

Hebu tusimame. Mwangalie mwenzio machoni na utafakari ni mara ngapi amekosa kile ambacho Mungu alikiandaa kwa ajili yake. Lakini shikaneni mikono kama inawezekana; watu wawili au watatu, kisha tu muambiane, “Hakuna haja ya kushindwa tena! Tunaweza kushinda! Iko nguvu ya kutosha kushinda! Yesu tayari ameshafanya kazi yote.” Muombeane ninyi kwa ninyi ili Bwana aweze kutusaidia kushinda. Hatutakiwi kushindwa. Iko neema ya kutosha; nguvu ya kutosha kuleta ushindi!

Asante Yesu.


**********************


Ndugu msomaji wa blog hii, somo hili ambalo ni muhimu sana kwa kila mwanadamu na mwili wa Kristo, nimeliweka pia kama E-Book, hivyo unaweza kulipakua na kulisoma tena na tena; na pia kuwagawia wengine. 


Unaweza pia kusoma ushuhuda huu kwa Kiingereza (pamoja na shuhuda zingine) 


Usikate tamaa. Simama imara katika imani. Unaweza kushinda. Bwana si dhalimu; anakupenda na amekuwa akijibu maombi yako siku zote. Je, Biblia si inasema kuwa KILA aombaye hupokea? (Mathayo 7:8). Na kwamba Mungu si mwanadamu hata aseme uongo (Hesabu 23:19).


Tumia mafunzo haya kusonga mbele katika wokovu na imani yako. Bwana Yesu akubariki sana.
source:Yesu ni njia blog