Menu

Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. 2 Huyo mwanzo

Monday, March 23, 2015

ASKOFU KAKOBE AZIDI KULITETEA NENO LA MUNGU

ASKOFU KAKOBE AZIDI KULITETEA NENO LA MUNGU


Askofu mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zakaria Kakobe hivi karibuni aliongea maneno makali kwa watumishi wa Mungu yaliyopelekea baadhi ya watu (kanisa) kujihoji kuhusu maisha yao na wakati huo huo wengi ikiwemo watumishi wa Mungu kukemea hali ya Askofu huyo kuhukumu bila kuwajua wahusika maisha yao binafsi na Mungu.

Askofu Kakobe alimwakia Rose Muhando kwa wazi  na kusema “Leo sikwepeshi…wanaume wanatikisa viuno Rose Muhando, hiyo ni team ya kwenda motoni, hakuna Mungu humo ndani….watu wanaoenda mbinguni hawako hivyo Rose Muhando rudi msalabani kama hujazaliwa mara ya pili zaliwa leo.Unatikisa viuno…..viuno unaleta kanisani,viuno peleka bar Rose Muhando kila mahali stage show, stage show, vitu hivi havikuwepo assemblies, vitu hivi havikuwepo kwa wapentekoste, nani atainuka mchungaji kukemea, kila mtu anajifanya ameokoka lakini huoni wokovu ule ”

Aliendelea kuwashukia wanasiasa maarufu kama Nape Nnauye, Mh. Mwakyembe, Mh. Lazaro Nyarandu na Paul Makonda na kuwataka  wajipime, warudi msalabani na kuzaliwa mara ya pili. Aliendelea zaidi na kusema “Mimi hapa sihitaji mtu, Waziri ukija hapa, Raisi ukija hapa utanisaidia nini, Raisi huwezi kunipa hela mimi.. mimi ndio nitakupa, mimi sihitaji hela ya mtu, Mungu aliyeniita ana fedha na dhahabu vyote ni mali yake, sihitaji hela ya mwanasiasa, sihitaji hela ya waziri…wakija kuleta harambee zao hapa watajisifu, tutashindwa kuwapiga kama hivi ninavyowapiga, lakini sasahivi ninakupiga Nape, nakupiga Makonda, Nakupiga Mangula, siangalii sura ya mtu hapa….Injili iko pale pale.Hakuishia hapo alimshukia mtumishi wa Mungu TB Joshua na kusema “Na tunaona mlolongo wa watu sasahivi wanajifichaficha wanaenda kwa TB Joshua, kwenye mchanganyo, TB Joshua hata haubiri kuhusu kuzaliwa mara ya pili, anazungumza vitu vya ajabu ajabu na miujiza feki, watu wanajazana hapo kama Mwigulu NchembaMpaka sasa hakuna Mchungaji aliyemjibu Askofu Zakaria Kakobe.

Tuesday, March 3, 2015

KARAMA ZA ROHO MTAKATIFU - SEHEMU YA PILI

KARAMA ZA ROHO MTAKATIFU - SEHEMU YA PILI

I Wakorintho 14:12; ''Vivyo hivyo na ninyi kwa kuwa mnatamani sana kuwa watu wenye karama za roho, takeni kwamba mzidi sana kuwa nazo ili kulijenga kanisa''.

UTENDAJI KAZI WA KARAMA.
Mambo muhimu (ya msingi) kufahamu ili karama ziweze kufanya kazi. Mambo hayo ni:-
1.) kubali kuwa karama za Roho zinaweza kufanya kazi kwako pia. I Wakorintho 12:4.11; ''Basi pana tofauti za karama bali Roho ni yeye yule, lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye''. Roho Mtakatifu ndani ya mtu anazo karama zote bali anamgawia kila mtu kama apendavyo yeye. Rumi 12:3-6; inasema ''kwa maana kwa neema niliyopewa na mwambia kila mtu aliyeko kwenu asinie makuu kupita ilivyo mpasa kunia ..........., basi kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbali ..............''.




2.) Uwe na hamu (haja) kubwa ya msaada wa Mungu. I Wakorintho:1,12; ''ufuateni upendo na kutaka sana karama za rohoni, lakini zaidi kwamba mpate kuhutubu, vivyo hivyo na ninyi kwa kuwa mnatamani sana kuwa watu wenye karama za roho, takeni kwamba mzidi sana kuwa nazo ili kulijenga kanisa''.
Angalizo: karama siku zote zina mvuto.
3.) Tembea katika wito (nafasi) yako. Warumi 12:6, ''......... kwa kadri ya neema tuliyopewa...'', yaani wito (kiwango) ulichopewa. Ndani ya wito kuwa nafasi ambayo Mungu amekupa. Kuna ngazi, kuna mahali na muda unaotakiwa kuufanyia huo wito. Galatia 2:6-7 ''......walipokwisha kujua neema niliyopewa........ walinipa mimi mkono wa kuume wa shirika''.
Mfano: kuna tofauti ya karama ya unabii na huduma ya unabii, yaani kila mtu aliyeokoka anaweza kutoa unabii bali si kila mtu ana karama ya unabii.
4.) karama kutenda kazi vizuri ndani ya mtu inategemea kiwango cha Imani alichonacho. Rumi 12:6; ''basi kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbali ........ ikiwa unabii tutoe unabii kwa kadri ya imani''. Sio zaidi ya hapo. Rumi 10:17; ''imani chanzo chake ni kusikia na kusikia huja kwa neno la kristo'' yaani kiwango cha imani ulichonacho hakiwezi kuzidi hapo. Imani huja tu kwa neno la Kristo. Biblia haituruhusu kutembea kwenye karama zaidi ya imani tuliyo nayo.
Angalizo: kufahamu neno la Kristo kwa wingi ni muhimu. Tembea katika karama za roho kwa kadri ya imani.

Jambo la nne linaendelea:
Karama zitumike kwa kadri ya Imani yaani utendaji kazi wa karama za Roho Mtakatifu ndani ya mtu utategemea kiwango cha neno la kristo kilichoko ndani yake. Hii ni kwa sababu Mungu alikusudia kuwa karama katikati ya kanisa zifanye kazi kwa ufanisi na usalama ili kulijenga kanisa.
Mfano: Mungu hakuweka unabii ili uongoze kanisa; ila ni kwa ajili ya kuthibitisha neno ambalo Mungu amekwisha kulisema ndani ya mtu.
Kwa sababu karama si zako ni za Roho Mtakatifu, kama huna neno la kutosha ndani yako karama inaweza ikaletwa ndani yako ukaikataa.
I Wakorintho 12:8 ''maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa apendavyo Roho yeye yule''. I Petro 4:10; ''kila mmoja kwa kadri alivyoipokea karama, itumieni kwa kuhudumiana....''. Kuna kupewa na kupokea- karama. Unaweza kukataa kwa kutokuja au hofu n.k.
5.) Jifunze jinsi Roho anavyowasiliana na roho yako, nafsi yako na mwili wako. I Wakorintho 3:16; ''hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?'' Mtu ni roho anayo nafsi na anaishi katika mwili. Roho Mtakatifu pia yuko ndani ya mwili. Hesabu 30:2 ''Mtu atakapo mwekea Bwana nadhiri, ....... Asitangue neno lake; atafanya sawasawa na hayo yote yamtokayo kinywani mwake''. Unaposema maneno yanafunga nafsi yako. Mwili unatawaliwa na nafsi, nafsi kazi yake ni kutafsiri kile ambacho mwili unasema ili roho ielewe na kile ambacho roho inasema ili mwili uelewe. Kwa hiyo nafsi inasaidiwa pale, unaposoma neno ili iweze kutafsiri mambo ya rohoni sawasawa na neno. Marko 2:5-8, ''naye Yesu, alipoiona imani yao, ........ wakifikiri mioyoni mwao ..... Yesu akafahamu rohoni mwake kwamba wanafikiri hivyo nafsini mwao .....''. Galatia 6:17; ''tangu sasa mtu asinitaabishe kwa maana ninachukua mwilini mwangu chapa zake Yesu.

6.) Ujazo wa Roho Mtakatifu. Sio wa siku moja ambao unatosheleza. I Petro 4:9-11 ''mkaribishane ninyi kwa ninyi, pasipo kunung'unika, kila mmoja kwa kadri alivyoipokea karama,........... mtu akihudumu na ahudumu kwa nguvu anazojaliwa na Mungu, .......''. yaani kila wakati kuna nguvu fresh, mtu asihudumu kwa nguvu alizojaliwa bali anazojaliwa kila wakati na Mungu. Hivyo tunahitaji kurudi kwa Mungu kila wakati kujazwa nguvu za Roho Mtakatifu.
Kuna kiwango cha nguvu za Roho Mtakatifu ndani ya mtu ambacho hakiwezi (kwa kuwa ni kidogo) kusukuma karama fulani ili ziweze kuhudumu au kufanya kazi; ndio maana tunahitaji kujazwa kila wakati.

KARAMA ZA ROHO MTAKATIFU - SEHEMU YA NNE

KARAMA ZA ROHO MTAKATIFU - SEHEMU YA NNE

Karama ya unabii
I Wakorintho 12:4,10 ''Basi pana tofauti za karama bali Roho ni yeye yule. na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii, na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha.
I Wakorintho 14:12; inasema ''.......takeni kwamba mzidi sana kuwa nazo ili kulijenga kanisa''.
Mambo ya msingi kuhusu huduma ya Nabii na karama ya unabii:-
1. kuna tofauti kati ya huduma ya nabii na karama ya unabii.
Efeso 4:11 ''Naye alitoa wengine kuwa Mitume; na wengine kuwa manabii....''. Hapa anazungumza habari ya nabii (ofisi) ya nabii. Huduma ni ofisi na karama ni vitendea kazi katika ofisi.


Kazi za nabii (kama huduma)


kufundisha mafundisho ya msingi / ya kuweka msingi wa kiroho ndani yako. Efeso 2:19-20 inasema, ''Basi tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji, ........mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni''. Hii haimaanishi kwamba kila nabii amepewa kufundisha.


Nabii pia anaweza kupewa kufanya kazi ya kubomoa na kuharibu kazi za shetani na kupanda pando la Mungu ndani ya mioyo ya watu, kama kuna mahali panahitajika kufanya hivyo. Tunaweza kusoma haya katika kitabu cha Yeremia 1:4,5,10; inasema '' .....kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa ............. Ili kung'oa na kubomoa na kuharibu na kuangamiza; ili kujenga na kupanda''.


Kazi nyingine ni kuonya. Tunaweza kuona haya katika kitabu cha Ezekieli 2:3-5; ''akaniambia mwanadamu, nakutuma kwa wana wa Israel, kwa mataifa wanaoasi, walioniasi mimi wao na baba zao wamekosa juu yangu.....''


Kazi nyingine ni mwonaji. I Samweli 9:9 ''(Hapo zamani katika Israel, mtu alipokwenda kuuliza neno kwa Mungu, husema hivi, Haya! Twende kwa mwonaji; maana mtu aitwaye sasa Nabii hapo zamani aliitwa mwonaji)''.


Kutabiri (kusema mambo yajayo). Yeremia 23:21; inasema ''mimi sikuwatuma manabii hao, lakini walikwenda mbio; sikusema nao, lakini walitabiri.

Kazi ya karama ya unabii. (kama kitendea kazi):
Ni kujenga, kufariji, kutia moyo na kujirunza, pia huthibitisha kile ambacho Mungu amekwisha kusema na wewe. Katika kitabu cha I Wakorintho 14:3,4,24,25,31; tunasoma ''Bali yeye ahutubuye, asema na watu maneno ya kuwajenga, na kuwafariji, na kuwatia moyo. Yeye anenaye kwa lugha hujijenga nafsi yake; bali ahutubuye hulijenga kanisa. Lakini wote wakihutubu, kisha akaingia mtu asiyeamini, au mjinga, abainishwa na wote, ahukumiwa na wote; siri za moyo wake huwa wazi, na hivyo atamwabudu Mungu, akianguka kifudi-fudi, na kukiri ya kuwa Mungu yu kati yenu bila shaka. Kwa maana ninyi nyote mwaweza kuhutubu mmoja mmoja, ili wote wapate kujifunza, na wote wafarijiwe''.

2. manabii wapo hata leo ila nafasi zao ni tofauti na za wale wa agano la kale.
Efeso 4:11,14; ''naye alitoa wengine kuwa mitume na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamisisha watakatifu; hata kazi ya huduma itendeke hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa Imani na kumfahamu sana mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu............. Ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja tukizifuata njia za udanganyifu''.
Pia katika kitabu cha Matendo ya Mitume 13:1; tunasoma ''....... Palikuwako manabii na waalimu .....''. hii inaonyesha kuwa manabii wapo hata leo.
Tofauti iko hivi: kwamba manabii hapo zamani (katika agano la kale) walikuwa viongozi wakiongoza watu, yaani walipewa kuongoza watu, lakini katika agano jipya huduma ya nabii ipo ndani ya Kanisa na nabii hakupewa kuongoza kanisa- kila mmoja wakati huu amepewa Roho Mtakatifu ambaye anamwongoza. Hivyo nabii anayesema kwa mausia ya Mungu ni yule anayesema sawasawa na neno la Mungu.

Kanisa linajengwa juu ya misingi miwili ambayo ni:
a. Yesu Kristo
b. Mafundisho ya mitume na manabii ambao wanafundisha mafundisho ya msingi ambayo yanamfanya mtu awe mkristo. (foundation series). Ukisoma kitabu cha Waebrania 6:1; inasema ''kwa sababu hiyo, tukiacha kuyanena mafundishao ya kwanza ya Kristo; tukaze mwendo ili tuufikilie utimilifu; tusiweke msingi tena wa kuzitubia kazi zisizo na uhai, na wa kuwa na Imani kwa Mungu na wa mafundisho ya mabatizo, na kuwekea mikono, na kufufuliwa wafu na hukumu ya milele''.

Manabii wa sasa wanatofauti na akina Paulo na akina Petro ambapo hao wa zamani walipewa mafundisho ya msingi na hawa wa sasa wanapewa wito (hekima au special revelation) wanaposoma Biblia wanafungua siri za mafundisho ya msingi, ambayo akina Paulo walifundisha, na kutufunulia sisi.

Mambo ya msingi kuhusu huduma ya Nabii na karama ya Unabii, inaendelea........'
I Wakorintho 12:4,10
3. Karama ya Unabii (kinachosemwa na Nabii) lazima kipimwe.
Kwa nini kupima?


Si wote wametumwa na Mungu.
Ukisoma kitabu cha Yeremia 23:21,22; anasema ''mimi sikuwatuma manabii hao, lakini walikwenda mbio; sikusema nao lakini walitabiri. Lakini kama wangalisimama katika baraza yangu, ndipo wangaliwasikizisha watu wangu maneno yangu, na kuwageuza waziache njia zao mbaya,.....''. Maana yake ni manabii wa kweli ila tatizo ni kwamba walienda pasipo kutumwa, hawakukaa barazani pa Mungu na kusikiliza kile ambacho Mungu alitaka kisemwe.


Kuna manabii wa uongo waliojiingiza katika makundi ya Mungu.
Ukisoma Mathayo 7:15; anasema ''Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali.


Kuna manabii wa uongo ambao wanafanya kazi kwa kutumia Ishara na miujiza, ili kuwavuta watu wawafuate lakini Mungu hakuwatuma. Ukisoma Mathayo 24:24,25 ''kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa Ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini hata waliowateule. Tazama nimekwisha kuwaonya mbele''.


Kwa sababu ya matumizi yasiyo na utaratibu wa ki-Mungu juu ya huduma ya Nabii na karama ya unabii.
I Wakorintho 14:29,33,39,40; ''Na manabii wanene wawili, au watatu, na wengine wapambanue. Kwa maana Mungu si Mungu wa machafuko, bali wa amani, vile-vile kama ilivyo katika makanisa yote ya watakatifu. Kwa ajili ya hayo ndugu, takeni sana kuhutubu wala msizuie kunena kwa lugha. Lakini mambo yote na yatendeke kwa uzuri na utaratibu''.


Ni agizo.
Ukisoma I Yohana 4:1; anasema '' Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani''. Pia katika kitabu cha 2 Petro 1:20,21; ''mkijua neno hili kwanza, ya kwamba hakuna unabii katika maandiko upatao kufasiriwa kama apendavyo mtu fulani tu. Maana unabii haukutolewa popote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu''.

Unapimaje?
Katika kupima kwa ajili yako wewe kutoa karama ya Unabii au kwa kusikia kutoka mtu mwingine, jiulize maswali yafuatayo:-
a. Je roho inayokutumia kutoa unabii inakutawala au unaitawala? Ukisoma kitabu cha I Wakorintho 14:32,33 anasema ''Na roho za manabii huwatii manabii....'' Roho Mtakatifu hakuleta karama zake zikufanye mtumwa. Ukiona hali hii kaa kwenye maombi tena.
b. Je hayo yaliyosemwa kwa njia ya unabii ni sawasawa na neno? Ukisoma Warumi 12:6 inasema; ''......tutoe unabii kwa kadri ya imani''. Maana yake kwa kadri ya kiwango cha neno ulichonacho ndani yako. Pia kitabu cha Hesabu 22:18; inasema ''.....siwezi kupita mpaka wa neno la Bwana, alilosema ndani yangu Mungu wangu, kulipunguza au kuliongeza.
c. Je unapotumika katika unabii au kama nabii unajionaje ndani yako? Unaona kama hiyo karama ni kipimo cha kiroho kwamba uko mbali sana? Kitabu cha I Wakorintho 13:9 '' kwa maana tunafahamu kwa sehemu na tunafanya unabii kwa sehemu''. Maana yake hakuna mtu ambaye anajua kila kitu hivyo ni muhimu kuwa mnyenyekevu na kuwa tayari kujifunza kwa wengine.
Pia katika kitabu cha I Petro 4:9-10; inasema ''........ kila mmoja kwa kadri alivyoipokea karama, itumieni kwa kuhudumiana; kama mawakili wema wa neema mbalimbali za Mungu''. Maana yake uwe tayari kupokea karama ambayo inatenda kazi ndani ya mtu mwingine. Vile-vile kitabu cha I Wakorintho 13:2; anasema '' tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, ..... kama sina upendo si kitu mimi''.
d. Je Kristo anainuliwa au la? Kitabu cha Kumbukumbu la torati 13:1-4. ''kukizuka katikati yako nabii au mwotaji wa ndoto... akisema, na tuifuate miungu mingine ya nabii yule ............ tembeeni kwa kumfuata Bwana, Mungu wenu, ........''. Kuna hatari pale ambapo karama zinafanya kazi halafu utukufu wanapewa watu badala ya kumwinua Yesu.
e. Je unabii / kilichosemwa na nabii au unabii ulioletwa kwako unakuweka huru au la? Maana palipo Roho wa Bwana hapo ndipo penye uhuru.
f. Je unabii huo unatimia au la? Ukisoma Kumbukumbu la Torati 18:20-22 anasema ''Lakini nabii atakayenena neno kwa kujikinai kwa jina langu, ambalo sikumwagiza kulinena, au takayenena katika jina la miungu mingine, nabii yule atakufa...... atakaponena nabii kwa jina la Bwana, lisifuate jambo lile wala kutimia, hilo ndilo neno asilolinena Bwana;.........''.
g. Je tabia za hao manabii zikoje? Ukisoma Mathayo 7:15-23; anasema '' ........mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri.......... Ndiposa kwa matunda yao mtawatambua..............''
Mara nyingi tunda huwa linachukua muda kutokea lakini baada ya muda huo litatokea tu.
h. Je huo ujumbe aliotoa nabii unajenga au unabomoa? Ukisoma I Wakorintho 14:3-5,31 '' Bali yeye ahutubuye, asema na watu maneno ya kuwajenga, na kuwafariji, na kuwatia moyo........... bali ahutubuye hulijenga kanisa ............ kwa maana ninyi nyote mwaweza kuhutubu mmoja mmoja, ili wote wapate kujifunza, na wote wafarijiwe''.

Karama ya unabii inavyofanya kazi


Kusema chini ya upako. 2 Petro 1:20-22 anasema '' ..........., wakongozwa na Roho Mtakatifu


Ujumbe unaoambatana na Matendo. Matendo ya mitume 21:9-14; inasema ''..... alipotufikia akautwaa mshipi wa Paulo, akajifunga miguu na mikono, akasema, Roho Mtakatifu asema hivi, hivyo ndivyo wayahudi wa Yerusalemu watakavyomfunga mtu mwenye mshipi huu nao watamtia katika mikono...........''.


Unabii mwingine unatimia kwa maombi. Yakobo 5:17-18; anasema '' Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia pamoja na sisi, akaomba kwa bidii mvua isinye na mvua haikunya juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita. Akaomba tena, mbingu zikatoa mvua nayo nchi ikazaa matunda yake''.

KARAMA ZA ROHO MTAKATIFU - SEHEMU YA TATU

KARAMA ZA ROHO MTAKATIFU - SEHEMU YA TATU

Karama ya neno la Maarifa
I Wakorintho 12:4,8; ''Basi pana tofauti za karama bali Roho ni yeye yule. Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima, na mwingine neno la maarifa, apendavyo Roho yeye yule''.
Kama tulivyo jifunza huko nyuma kazi ya karama ni kulijenga kanisa.
Kazi ya karama ya neno la maarifa.

Kukupa habari ya mambo yaliyopo na/au yaliyopita ili kukurahisishia kufanya maamuzi na kutambua hila zilizojificha ili kukwamisha utumishi wako.


Wakati mwingine karama hii itakupa kujua maswali waliyonayo watu kabla hawajauliza au kujua mahitaji waliyonayo kabla hawajakwambia.
Njia nne ambazo karama ya neno la maarifa inafanya kazi:
i. kwa kutumia mawazo
ii. kwa kutumia ndoto
iii. kwa kutumia maono, maono yamegawanyika katika sehemu zifatazo:

maono ya ndani

maono ya wazi

maono yanayotokea wakati akili zako hazina matunda.(suspended)
iv. kwa kutumia njia ya kuweka mwilini mwako maumivu au hali aliyo nayo mtu mwenye kuhitaji.

Karama zinafanya kazi kwa kutegemeana/kushirikiana.
Mfano. Unaweza kupewa swali na jibu. Kulijua swali ni neno la maarifa na kujua jibu la swali hilo ni neno la hekima.

i. Njia ya kutumia MAWAZO / WAZO
Hii ndio njia kuu ambayo inatumika mara nyingi zaidi. Marko 2:6-8 inasema ''....... Mara (ghafla) Yesu akafahamu rohoni mwake kwamba wanafikiri hivyo nafsini mwao.....''. Maana yake ghafla wazo tofauti, na lile alilokuwa akiwaza saa hiyo lililetwa na Roho Mtakatifu ndani yake.
Ukisoma Luka 3:15-16; inasema ''..........Yohana alijibu akawaambia wote,............''. Yaani alijibu swali ambalo lililetwa ndani yake na Roho Mtakatifu; sio kwamba aliulizwa na mtu yeyote yule.
Luka 20:18-26; inasema ''..........wakamvizia-vizia, wakatuma wapelelezi waliojifanya kuwa watu wa haki, ili wamnase katika maneno yake, wapate kumtia katika enzi na mamlaka ya liwali. Wakamwuliza wakisema,................... Lakini yeye alitambua hila yao akawaambia ................ Wakastaajabia majibu yake, wakanyamaa''.

Mambo ya kukuwezesha kufanya kazi na njia hii ya mawazo:
a. Jizoeze kukabidhi roho yako, nafsi yako na mwili wako kila siku upya mbele za Mungu.
b. Omba maombi ya vitu vifuatavyo:

Usikivu (sensitivity)

Utulivu

Kufundishwa na Mungu namna ya kutembea katika hiyo karama.
Hii inasaidia kwa mfano, Mungu akisema jenga safina wakati sio msimu wa mvua. Yaani kutii sauti ya Mungu bila kuangalia dalili za nje.

Karama ya neno la hekima

I Wakorintho 12:4,8; inasema '' Basi pana tofauti za karama bali Roho ni yeye yule. Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima.......''.
I Wakorintho 14:12 '' ......takeni sana mzidi kuwa nazo ili kulijenga kanisa''.
Karama ya neno la maarifa na neno la hekima zinafanya kazi kwa karibu sana.

Kazi ya karama ya neno la hekima na inavyofanya kazi:
1. kukupa jibu la swali unaloulizwa lakini hasa swali lenye hila, mtego, ushindani au mashtaka ndani yake.
Luka 21:12-15 inasema ''lakini, kabla hayo yote hayajatokea watawakamata na kuwaudhi; watawapeleka mbele ya masinagogi........ basi kusudieni mioyoni mwenu, kutofikiri-fikiri kwanza, mtakavyojibu, kwa sababu mimi nitawapa kinywa na hekima ambayo watesi wenu wote hawataweza kushindana nayo wala kuipinga''.
Luka 20:19-26; ''...lakini yeye alitambua hila yao .....''
Marko 3:1-6; inasema ''..........akamwambia yule mtu mwenye mkono uliopooza simama katikati ..........nyosha mkono wako. Naye akaunyosha mkono wake ukawa mzima tena''.
Hapa tunaona neno la maarifa (kutambua hila ya wale waliotaka kumkamata) ilianza kufanya kazi, neno la hekima pia likafanya kazi baadaye pale Yesu alipomwambia yule mwenye kupooza ''simama katikati'' na tunasoma akaanza kuzungumza na wale watu.

2. inakupa uwezo wa kutatua tatizo lililoko mbele yako.
Mathayo sura ya 1 na ya 2: Habari ya Yusufu na Mariamu. Katika sura hizi karama ya neno la maarifa na la hekima ilifanya kazi kwa kutumia ndoto. Si ndoto zote zinatoka kwa Mungu lakini kama ukiwa na neno la Mungu utatambua ndoto ya Mungu na isiyo ya Mungu.

3. kukupa uhuru wa kushirikiana na watu usiowajua kwa kazi ya Mungu.
Matendo ya mitume 10:1-20; Habari za Petro na Kornelio. Habari hii inaeleza jinsi Petro alivyoona maono wakati amezimia roho (akili zake zilikuwa hazina matunda).
Maono ya aina nyingine, kama tulivyokwishaona hapo nyuma ni ya wazi, ambapo akili zako zinaona na zinaelewa na bado unaweza kuona katika ulimwengu wa roho.
Aina nyingine ni maono ya ndani kwa mfano: unapoomba halafu ghafla ndani yako inakuja picha.
Sasa karama ya neno la maarifa na la hekima itakusaidia kukuwezesha kushirikiana na watu usiowajua.

4. inakurahisishia kuamua kwa haki katika nafasi ya uongozi Mungu aliyokupa au mahali unapohitajika kutoa maamuzi
I Wafalme 3:4-28; habari za mfalme Sulemani, jinsi alivyoomba hekima kwa Mungu na akapewa. Vilevile tunaona jinsi ambavyo aliweza kutoa uamuzi wa haki juu ya kesi ya wanawake wawili waliokuwa wakigombea mtoto. Uamuzi wa haki unahitaji msaada wa Mungu.

ZIJUE KARAMA ZA ROHO MTAKATIFU -SEHEMU YA KWANZA

ZIJUE KARAMA ZA ROHO MTAKATIFU -SEHEMU YA KWANZA

I Wakorintho 14:12. Inasema 'vivyo hivyo na ninyi, kwa kuwa mnatamani sana kuwa watu wenye karama za rohoni, takeni kwamba mzidi sana kuwa nazo ili kulijenga kanisa. Mungu hafanyi kitu bila kusudi, na kusudi la semina hii ni:-

· Kuna jambo Mungu anataka kufundisha katikati yetu ambalo litahusisha sana utendaji wa karama za Roho Mtakatifu.


· Kurahisisha ujenzi wa kanisa lake na kazi zake. Mfano, kuna urahisi wa kujenga kwa kutumia mashine za kujengea na kubeba matofali kuliko kutumia mkono, ni sawa na kufanya kazi ya Mungu kwa kutumia karama za Roho Mtakatifu.
I Wakorintho 12:4; anasema pana tofauti za karama bali Roho ni yeye yule. Karama si za mtu ni za Roho Mtakatifu na kazi yake ni kulijenga kanisa.

Yesu alisema katika kitabu cha Mathayo 16:18; ''nitalijenga kanisa langu wala milango ya kuzimu haitaliweza''. Karama zinatokea mahali kama apendavyo Roho. Katika kitabu cha Yohana 14:16, Yesu alizungumza habari za kutuletea msaidizi mwingine, yaani Roho atakapokuja atachukua nafasi ya Yesu katika kulijenga kanisa lake.
Roho Mtakatifu sio karama bali anazo karama, pia Roho Mtakatifu sio nguvu bali anazo nguvu. Tunda la Roho linapofunuliwa ndani ya mtu tabia ya Mungu hujitokeza kwake.

Katika kutafuta vitu vya Mungu, ili kufahamu karama za Roho Mtakatifu na kazi zake, kuna gharama. Mfano, kwenye ndege kuna first class, business class na third class. Ukitaka kupata huduma nzuri zaidi lazima uongeze pesa (gharama) ili upande business class au first class. Lakini dereva wa ndege (captain) ni yule yule. Vivyo hivyo katika maswala ya Mungu wako wanaokaa first, business au third class, lakini wote tunakwenda mbinguni. Hivyo tunahitaji kuingia gharama ili tukae first class ndani ya Yesu. Gharama hizo ni kama:-
i) kusoma neno la Mungu kwa bidii kwa kadri inavyowezekana ili neno hilo likae ndani yako kwa wingi, maan kujua karama za Roho Mtakatifu bila kuwa an maneno ya Mungu ni vigumu.
ii) Maombi n.k.

I Wakorintho 12:1 inasema 'basi ndugu zangu kwa habari ya karama za roho, sitaki mkose kufahamu'. Tunahitaji kuwa na hamu ya kuona kwamba karama za Roho Mtakatifu zinafanya kazi na zinafahamika. Hamu hiyo imepotea katika kanisa la Mungu na hivyo kufanya kazi ya ujenzi wa kanisa la Mungu kutofanyika kama Mungu anavyokusudia.

KARAMA ZA ROHO MTAKATIFU - SEHEMU YA TANO

KARAMA ZA ROHO MTAKATIFU - SEHEMU YA TANO

Karama ya masaidiano.
I Wakorintho 12:28; inasema '' Na Mungu ameweka wengine katika kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, na tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano na maongozi na aina za lugha''.

Kuna huduma ya masaidiano na karama ya masaidiano. Karama ya masaidiano inafanya kazi kwa karibu sana na karama ya neno la maarifa ili upate kujua kuna mahali panahitaji msaada. Pia inafanya kazi kwa karibu sana na karama ya neno la hekima kujua ni msaada gani unatakiwa, vilevile inafanya kazi kwa karibu sana na karama ya Imani kwa sababu mahali pengine unahitaji kufanya vitu kwa imani pasipo kuona ishara ya nje.




Tumekwisha kujifunza kwamba kazi ya karama za Roho Mtakatifu ni kulijenga kanisa kwa hiyo kazi ya karama ya masaidiano pia ni kulijenga kanisa.

Maeneo manne ya kukusaidia kuifahamu zaidi karama ya masaidiano.

1. Inasaidia viungo vingine vifanye kazi yake katika kulijenga kanisa. Efeso 4:15-16; '' lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo. Katika yeye mwili wote ukiungamanishwa na kushikanishwa kwa msaada wa kila kiungo, kwa kadri ya utendaji wa kila sehemu moja moja, huukuza mwili upate kujijenga wenyewe katika upendo''. Maana yake kila kiungo katika kanisa kina kazi yake. Karama ya masaidiano huwa haionekani kwa nje lakini ni karama ya muhimu sana.

2. Inamsaidia mtu avuke kipindi chake cha mahangaiko asije akaacha kazi ya kulijenga kanisa. Matendo ya Mitume 9:1-19; anaeleza habari za Sauli (Paulo) akielekea Dameski. Katika mstari wa 8-9 anasema '' Sauli akainuka katika nchi, na macho yake yalipofumbuka hakuona kitu; wakamshika mkono wakamleta mpaka Dameski. Akawa siku tatu haoni; hali wala hanywi. Basi palikuwapo Dameski mwanafunzi ........''
Hapa tunaona Paulo (Sauli) alikuwa katika mahangaiko ndio maanahakula wala kunywa kwa siku tatu.
Anania aliwekewa mzingo wa kwenda kumsaidia Paulo katika mahangaiko hayo na tunasoma kwamba baada ya kumsaidi aliondoka. Hii inatokea mara nyingi sana pale ambapo watu wanapata mahangaiko ya wito na hapa ndipo karama ya masaidiano inahitajika.

3. Inamsaidia mtu mwingine afanikiwe katika wito alioitiwa na Mungu. Yohana 19:38-42; ''Hata baada ya hayo Yusufu wa Arimathaya, naye ni mwanafunzi wa Yesu (lakini kwa siri kwa hofu ya wayahudi) alimwomba pilato fuhusa ili auondoe mwili wa Bwana Yesu. Na pilato akampa ruhusa...........''.
Hapa tunaona wanafunzi wa Yesu, baada ya Yesu kufa, hawakuonekana kumsaidia Yesu kwenda kuuhifadhi mwili wake. Lakini msaada wa aina ya pekee ulitolewa na watu wengine ambao hawakuwa wanafunzi wa karibu sana na Bwana Yesu wakati wa maisha yake. Hii ni karama ya masaidiano ilishuka ndani yao kwa ajili ya kukamilisha wito wa Bwana Yesu.
Mfano: katika eneo kama hili ndipo watu wengine wanapewa mzigo kwa ajili ya utoaji (very specific giving) ili kusaidia kazi ya Mungu isilale, na hii inafanyika bila kujadiliana na yule anayesaidiwa. Hii inatokea hata kwa waombaji ambao wakati mwingine Roho Mtakatifu anaweka mzigo ndani yao ili kuombea tukio (event) fulani tu.


4. Inamsaidia mtu mwingine akubalike katika wito wake. Ukisoma Matendo ya Mitume 9:26-29; anazungumza habari za Sauli alipofika Yerusalemu, tunasoma kwamba alijaribu kujiunga na wanafunzi lakini walimwogopa. Lakini Barnaba, ambaye aliinuliwa na Mungu ili kusaidia, alimtwaa akampeleka kwa mitume na kumtambulisha.

Karama ya aina za lugha
Ili karama zifanye kazi kwa haraka weka ndani yako kiu ya kuona Yesu anatukuzwa. Mambo muhimu kuhusu karama ya aina za lugha:-
a. Hizi lugha zinazosemwa ni za aina gani? Ukisoma I Wakorintho 13:1; anasema '' nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao''. Maana yake Roho Mtakatifu anaweza akakuletea lugha ya wanadamu lakini siyo ile ambayo umejifunza. Na pia anaweza akakuletea lugha za Malaika.
b. kuna tofauti ya kunena kwa lugha kwa kila aaminiye na kunena kwa lugha kama karama. I Wakorintho 12:29,30 anasema ''Je wote ni Mitume? Wote ni manabii? Wote ni waalimu? Wote wanatenda miujiza? Wote wana karama za kuponya wagonjwa? Wote wanena kwa lugha? Wote wafasiri?''
Maana yake si kila mtu anapewa kufanya haya yote yaliyotajwa, si kila mtu hii karama ya kunena kwa lugha, inatokea kwake kila wakati, ila ni pale ambapo Mungu anaona panahitajika karama hiyo.
Mfano: karama hii inaweza kukusaidia pale ambapo hufahamu lugha fulani na unahitajika kupeleka ujumbe kwa lugha hiyo.
Kwa upande mwingine kuna kuna kunena kwa lugha kama ishara. Marko 16:17; '' na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watesema kwa lugha mpya''. Hapa anazungumza kunena kwa lugha kwa kila aaminiye na sio karama.
I Wakorintho 14:5; anasema ''nami nataka ninyi nyote mnene kwa lugha .......''. Maana yake kunena kwa lugha kama ishara kwa kila aaminiye na siyo karama kwa sababu anenaye kwa lugha anahuisha nafsi yake.

UTAJIRI WAKE KRISTO USIOPIMIKA

UTAJIRI WAKE KRISTO USIOPIMIKA

" Mimi, niliye mdogo kuliko yeye aliye mdogo wa watakatifu wote, nalipewa neema hii ya kuwahubiri Mataifa UTAJIRI WAKE KRISTO USIOPIMIKA; na kuwaangaza watu wote wajue habari za madaraka ya siri hiyo, ambayo tangu zamani zote ilisitirika katika Mungu aliyeviumba vitu vyote, ili sasa, kwa njia ya Kanisa, hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi ijulikane na falme na mamlaka katika ulimwengu wa roho"(Waefeso 3:8 - 10).

" Na Mungu wangu atawajazeni KILA MNACHOHITAJI KWA KADIRI YA UTAJIRI WAKE KATIKA UTUKUFU,NDANI YA KRISTO YESU" (Wafilipi 4:9)

Kristo ana utajiri usiopimika. Na wote walio ndani yake ni warithi pamoja naye wa utajiri usiopimika. Kutokana na utajiri huo TUNAJAZWA KILA TUNACHOKIHITAJI. Mahitaji haya ni ya kiroho, kiakili


 na kimwili. Kwa hiyo hakuna sababu ya mkristo kuishi maisha ya kupungukiwa, ikiwa Kristo yuko ndani ya moyo wake pamoja na utajiri wake usiopimika. Au wewe una maoni tofauti juu ya hili?
Jambo la kujiuliza ni hili; kwa nini utajiri huu wa Kristo usiopimika hauonekani katika maisha ya wakristo wengi? Wakristo waishije katika ushuhuda wa wokovu ndani ya Kristo, wakati wanaishi katika ulimwengu wenye hali ngumu kiuchumi? Watumishi wa Mungu kwa mfano, wachungaji, wainjilisti na kadhalika, waishije katika kumtumikia Mungu vizuri bila kupoteza ushuhuda wao wakati wanaishi katika mazingira yenye maisha magumu kiuchumi?
Haya si maswali mepesi kuyajibu, lakini ni muhimu yatafutiwe ufumbuzi. Kabla hatujaanza kuyajibu napenda tusome Waefeso 4:11;

" Naye (Yesu Kristo) alitoa wengine kuwa mitume; na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti; na wengine kuwa wachungaji na Waalimu."
Ni kwa kusudi gani Bwana Yesu Kristo aliamua kuwaweka hawa katika kazi yake kanisani? Waefeso 4:12-16 inatupa maelezo:-
"Kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo, ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu. Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo. Katika yeye mwili wote ukiunganishwa na kushikanishwa kwa msaada wa kila kiungo, kwa kadri ya utendaji wa kila sehemu moja moja, huukuza mwili upate kujijenga wenyewe katika upendo"

Kwa kuisoma mistari hii tunapata kufahamu ya kuwa hawa waliotajwa ni watumishi wa Mungu katika Kristo. Na wana wajibu maalum waliopewa na Mungu. Pia ni muhimu kukumbuka kuwa si hao peke yao waliotumwa kazini na Kristo, lakini kila mkristo ana wajibu wa kufanya (Yohana 17:18; Warumi 12:4-8).
Naamini kabisa ya kuwa tukifahamu Mungu aliwatunzaje watumishi wake katika biblia, tutakuwa tumepata mwanga wa jinsi ambavyo anawatunza watumishi na watu wake hivi leo. Ni budi tukumbuke ya kuwa Yeye ni yule aliyekuwepo, aliyepo na atakayekuja (Ufunuo 4:8) na pia ni "Yeye yule jana na leo na hata milele" (Waebrania 13:8)
Baada ya kuisoma biblia kwa makini nimeona ya kuwa kuna njia nne ambazo Mungu amekuwa akizitumia kuwahudumia na kuwatunza watumishi wake na watu wake. Na naamini hata hivi leo anatumia njia hizi, kwa namna ambayo yeye mwenyewe amechagua.

Njia ya kwanza; Mshahara:
Njia mojawapo anayotumia ni kuwapa watu wake mishahara au ujira - kufuatana na kazi wanazozifanya.
"Ni askari gani aendaye vitani wakati wo wote kwa gharama zake mwenyewe? Ni nani apandaye mizabibu asiyekula katika matunda yake? Au ni nani achungaye kundi, asiyekunywa katika maziwa ya kundi? Je! Ninanena hayo kwa kibinadamu? Au torati nayo haisemi yayo hayo? Kwa maana katika torati ya Musa imeandikwa, usimfunge kinywa ng'ombe apurapo nafaka. Je! hapo Mungu aangalia mambo ya ng'ombe? Au yamkini anena hayo kwa ajili yetu? Naam, yaliandikwa kwa ajili yetu, kwa kuwa alimaye nafaka ni haki yake kulima kwa matumaini; naye apuraye nafaka ni haki yake kutumaini kupata sehemu yake."

Ikiwa sisi tuliwapandia ninyi vitu vya rohoni je! Ni Neno kubwa tukivuna vitu vyenu vya mwilini?
".......... Hamjui ya kuwa wale wazifanyao kazi za hekaluni hula katika vitu vya hekalu, na wale waihudumiao madhabahu huwa na fungu lao katika vitu vya madhabahu? Na Bwana vivyo hivyo ameamuru kwamba wale waihubirio injili wapate riziki kwa hiyo injili" (1 Wakorintho 9:7-14)
Kwa sababu unafanya kazi ya injili, Bwana ameamuru kwamba upate riziki yako katika injili. Watu wengine kwa kutokuelewa vizuri juu ya mistari hiyo tuliyoisoma, wameigeuza kazi ya kumtumikia Mungu kama mradi wa kupatia fedha za kumsaidia kuishi. Lakini kazi hiyo ni wito. Na kila wito una kusudi lake. Na kwa kuwa Mungu anafahamu kuwa utahitaji kuwa na mahitaji muhimu ya maisha, anakupa mshahara au ujira. Njia anazotumia kutoa mishahara au ujira ni nyingi, na anazitumia kama apendavyo yeye.
Na kwa wale walio na utaratibu wa kuwapa wachungaji kama mishahara, fedha hizo mara nyingi zinakuwa hazitoshi kukidhi mahitaji yao ya kila siku na familia zao. Na hii ndiyo hali halisi. Lakini jambo muhimu ni kwamba wanapewa mshahara.
Ukisoma kitabu cha Hesabu 18:8-15, 18 - 20 na Kumbukumbu la Torati 18:1-5 utaona ya kuwa kwa kadri wana wa Israeli walivyomtolea Mungu wao sadaka ndivyo na makuhani walivyoopokea ujira wao. Kwa maneno mengine ina maana ya kuwa, kama wangetoa sadaka kidogo, basi na makuhani wangepata ujira kidogo.
Na pia watumishi wa Kristo wanatakiwa watunzwe kwa chakula katika nyumba ambazo wanakwenda kuhudumu. " Akawaambia, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache; basi mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake. Enendeni, angalieni nawatuma kama wana kondoo katika ya mbwa-mwitu ..... Na nyumba yoyote mtakayoingia, semeni kwanza, Amani iwemo nyumbani humu ...... Basi, kaeni katika nyumba iyo hiyo, mkila na kunywa vya kwao; maana, mtenda kazi amestahili kupewa ujira wake ..... Na mji wowote mtakaouingia, wakiwakaribisha, vileni vyakula viwekwavyo mbele yenu" 
(Luka 10:1-8).

Njia ya Pili: Utoaji:
Njia nyingine ambayo watumishi wa Kristo na wakristo wanaweza kupokea vitu vya kuwasaidia katika maisha yao ni kwa njia ya utoaji.

Biblia inasema katika Luka 6:38;" Wapenzi watu vitu, nanyi mtapewa, kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwasukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpiamacho ndicho mtakachopimiwa".

Swali muhimu la kujiuliza ni kama mtu anaweza kutoa kama hana kitu cha kutoa. Ni wazi kwamba hataweza kutoa. Lakini mara nyingi hatakosa kitu cha kumtolea Mungu.
Na jambo hili Mungu anafahamu. Hata kule jangwani alipowaambia wana wa Israeli watoe kwa ajili ya ujenzi wa Hema ya kukutanikia; alijua kabisa kuwa alikuwa amewapa vitu hivyo kabla hawajatoka Misri. Kwa hiyo walitoa walizokuwa wamepewa na Mungu tayari. Na walipotoa, Bwana aliwabariki zaidi.
Kwa mkristo je! Anapotakiwa atoe ili apokee, atoe kitu gani alichopewa na Mungu? Wazo la kwanza linalonijia ni atoe fungu la kumi la mshahara wake kila mwezi kama yanenavyo maandiko. Soma Malaki 3:10.
Mkristo asipokuwa mwaminifu kumtolea Mungu ahadi yake ya fungu la kumi, anategemea kubarikiwa kwa njia gani? Na je! Ni vizuri kwa mchungaji kutokuwa mtoaji, wakati anawafundisha wakristo wawe watoaji?
Bora kutoa kuliko kupokea. Wengine wanasema bora kupokea kuliko kutoa. Lakini neno la Mungu linasema bora kutoa kuliko kupokea.
Tatizo la wakristo wengi katika utoaji huwa wanatoa bila ya kuwa na lengo maalum. Wengine wanatoa kwa kuwa wameambiwa watoe, lakini wao wenyewe hawana lengo maalum katika utoaji huo. Na kwa sababu hii hawaoni baraka zilizopo katika maisha ya utoaji.

Ukiangalia katika Biblia utaona ya kuwa kuna sababu kubwa zifuatazo:
(a) Tunatoa ili Mungu ashukuriwe ndani ya Kristo Yesu kwa utoaji huo (2Wakorintho 9:11 -12)
(b) Tunatoa ili injili ihubiriwe (1 Wakorintho 9:7-14)
(c) Tunatoa ili waliopungukiwa wapate riziki (2Wakorintho 9:12)
(d) Tunatoa ili Mungu amkemee shetani au yule anayeharibu matunda yetu ndani ya Kristo (Malaki 3:10-12)
(e) Tunatoa ili tupate zaidi (Malaki 3:10 - 13; Luka 6:38; 2 Wakorintho 9:6-11)
Unapotoa kitu chochote kwa Mungu kama sadaka, au zaka au dhabihu, uwe na malengo hayo ndani yako.
Wakristo wengi kwa mfano huwa wanatoa bila kutegemea kupokea. Mara nyingi huwa nawauliza wasikilizaji ninapofundisha juu ya jambo hili hivi; "Je! Ninyi huwa mnatoa fedha kama sadaka?"
Wanajibu; "Ndiyo'
Halafu nauliza tena; "Je! huwa mnawapa watu fedha ili ziwasaidie katika shida zao?"
Pia wanajibu "Ndiyo"
Halafu nawaambia tusome Luka 6:38 inayosema hivi:"Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; KIPIMO cha KUJAA na KUSHINDILIWA, na KUSUKWA -SUKWA hata KUMWAGIKA, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa".
Ikiwa umetoa fedha, Mungu kwa kutumia njia zake atakupa fedha nyingine kwa kipimo cha KUJAA na KUSHINDILIWA, na KUSUKWA-SUKWA hata KUMWAGIKA! Kwa nini Mungu akutajirishe? Ni ili malengo ya utoaji niliyoyasema yaendelee kutekelezwa!
Kwa hiyo uwe mtoaji, kwa maana kuna vitu ambavyo Mungu amekwishakupa tayari, hata kama ni vichache.

Njia ya tatu; Muujiza:
Muujiza ni tendo linalotokea tofauti na taratibu zinazofahamika na mwanadamu.
Je! unakumbuka jinsi Nabii Eliya alivyolishwa na Mungu kwa kumtumia kunguru? Na unakumbuka jinsi ambavyo Mungu alivyomlisha Nabii Eliya kwa kumtumia yule mama wa Serepta? Je! unakumbuka jinsi ambavyo Mungu alimlisha yule mama wa Serepta pamoja na mtoto wake kwa miujiza.
Na wana wa Israeli je! si nao walilishwa kwa mana jangwani?
Je!unadhani Mungu hawezi kuyafanya hayo tena? Au na wewe uko upande wa wale wasemao miujiza ilikoma walipokufa mitume?
Mimi naamini Mungu wetu hajabadilika na anaweza kufanya tena miujiza katika kuwalisha watumishi wake.
Lakini usije ukaacha kufanya kazi kwa kutaka kuusubiri muujiza wa Bwana. Hiyo haitakuwa sawa. Kwa sababu Mungu anazo njia nyingi za kuwatunza watu wake, muujiza ni njia mojawapo, na njia hii haitumii mara nyingi sana; na kumbuka ataitumia katika muda anaotaka na kwa mtu anayemtaka; kwa ajili ya utukufu wa jina lake.

Njia ya nne; Kazi za kuongeza kipato
Ni kweli kwamba mishahara ya watu haitoshi kukidhi mahitaji yao ya kila siku pamoja na familia zao.
Ukisoma katika 2Wathesalonike 3:6-12; Mtume Paulo anawaeleza Wathesalonike juu ya umuhimu wa kila mtu kufanya kazi. Na hata anaendelea kusema, "ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi , asile chakula. Na katika 1Wathesalonike 4:11 - 15 anazidi kukaza juu ya mtu kufanya kazi kwa mikono yake mwenyewe.
Naamini unafahamu ya kuwa ingawa watu walimhudumia Mtume Paulo kwa kumpa vitu vya kumsaida kimaisha; lakini yeye mwenyewe hakuwalemea bali alifanya kazi kwa mikono yake ili aongeze kipato chake.
Wachungaji na wakristo wengi wanajihusisha na miradi mbalimbali binafsi kwa ajili ya kuongeza kipato. Hili ni jambo zuri; lakini ni muhimu kuwa mwangalifu ili miradi hiyo au kazi unazofanya ili kuongeza kipato, hazitaharibu uhusiano wako na Mungu na kuzorotesha wito wako.

Mwl. C. Mwakasege