Vichwa vya Habari

TUSIHUKUMU BALI TUONYANE KWA UPOLE


  • Sote tu mashahidi wa changamoto na utata wa matumizi ya kiimani kuhusu misamiati ya maneno ya UPAKO na FEDHA za MADHABAHUNI. Ufunuo uliomo kwenye ujumbe wa leo unatusaidia kutafakari kwamba, changamoto hizi sio ngeni kibiblia kwa kuwa zilijitokeza kanisani tangu karne ya kwanza. Hebu tusome maandiko ambayo ndio ushahidi wa chimbuko la ujumbe wa leo:

    Utangulizi

    "Hata Simoni alipoona ya kuwa watu wanapewa Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono ya mitume, akataka kuwapa fedha akisema,  Nipeni na mimi uwezo huu, ili kila mtu nitakayemweka mikono yangu, apokee Roho Mtakatifu.  Lakini Petro akamwambia, Fedha yako na ipotelee mbali pamoja nawe, kwa kuwa umedhania ya kuwa karama ya Mungu yapatikana kwa mali..."(Mdo. 8:18-20)

    Kabla ya ufafanuzi natamani tujihoji na kutafakari maswali ya ufahamu yafuatayo: Kwanini Simoni aliutamani upako wa Petro kiasi cha kutaka kuununua kwa fedha? Ni watumishi wangapi hivi leo wenye ujasiri wa kukataa kupokea fedha ya Simoni madhabahuni? Ni watumishi wangapi hivi leo wenye ujasiri wa kumkemea Simoni anayedai kununua karama za Mungu (upako) kwa fedha madhabahuni ? Watumishi wangapi leo ambao sio tu kwamba wanapokea "Fedha ya Simoni madhabahuni", bali wao wenyewe ndio vinara wa "kutoza malipo ya upako madhabahuni"? 

    Hivi nini kingetokea, kama kweli Petro angeamua kuchukua "fedha ya Simoni madhabahuni"?
    a) Je! Roho Mtakatifu angekubaliana na tendo la "kuuzwa na kutumika na Simoni" kwenye huduma yake mpya aliyoinunua kwa Petro?
    b) Kama jibu ni hapana, Je huduma ya Petro ingepata madhara gani kwa tendo la kupokea fedha ya Simoni?
    c) Nini kingetokea kwa Simoni baada ya kuwekewa mikono na Petro ili apokee "upako wa kununua"?

    Maswali haya sio ya kufanyia mjadala bali ya kutusaidia kutafakari kwa kina na kwa makini kuhusu kisa cha ujumbe wa leo


    Kwanini Simoni alitamani
    kununua upako wa Petro?

    Simoni alikuwa Mkristo mchanga sana. Tukumbuke ya kwamba historia yake huko nyuma alikuwa mtu maarufu sana, na aliyekuwa akipata fedha nyingi kwa shughuli za uchawi/uganga wa tunguri. Mara ghafla Simoni alikuta amepoteza vyote, umaarufu na kipato! Hali hii ilimfanya kuwa uchungu na kinyongo moyoni!. Ndiyo maana Petro wakati akimkemea alimwambia "Kwa maana nakuona u katika uchungu kama nyongo, na tena u katika kifungo cha uovu" (Mdo.8:23)



    Kwa hiyo Simoni alipomwona Petro akiwekea mikono watu wanajazwa Roho, kwa "mtazamo wake wa zamani wa ki-uganga" alidhani anaweza kuununua kwa fedha "upako wa Petro" ili apate kuanzisha "biashara mbadala" ya ile ya "uganga wa tunguri".

    Pengine alidhani kwa njia hii angerudisha umaarufu wake alioupoteza na kupata fedha kwani uzoefu wa kutoza fedha huo tayari alikuwa nao! Najua kila mtumishi anaweza kuwa na mafunuo tofuati kuhusiana na kisa hiki! Nia ya ujumbe wangu ni kuthibisha kuwepo kwa dalili za kufanyia biashara karama za Mungu katika huduma.

    Kujibu maswali ya ni "watumishi wangapi wana ujasiri wa kukataa fedha ya akina Simoni na hata ujasiri wa kuwakemea madhabahuni?" Naomba kukiri kwamba pamoja na changamoto hii ya "biashara za upako madhabahuni" hata siku za leo bado wangalipo watumishi waaminifu katika utumishi wa Kristo!

    Lakini kuna mithali isemayo "Kwenye msafara wa mamba kenge nao wamo" Wasiwasi wangu kwa mithali hii ni vipi ikiwa "katika msafara huo idadi ya kenge itazidi kuongezeka kiasi cha kupita idadi ya mamba?" Huu utakuwa sio "msafara wa mamba" tena, bali ni "msafara wa kenge"! Hii ndiyo changamoto inayowakabili watumishi waaminifu wa Kristo. Tumeanza kuzidiwa kwa nguvu ya wingi wa "wajasiriamali wa upako" mfano wa akina Simoni katika huduma za kikanisa

    Nini kingelitokea kama Petro
    angechukua fedha ya Simoni

    Tukija kwenye majibu ya swali nyeti lisemalo "Nini kingetokea kama Petro angepokea fedha ya Simoni ya kununua upako madhabahuni?" Kwanza kabisa, kwa mtazamo wangu naona Petro mwenyewe angepoteza upako wake "orijino"! Angepoteza ushirika wake na Roho Mtakatifu.

    Hata kama Petro bado angesalia na "title" yake ya "Mtume" lakini upako wa kitume ungemtoka na akaingiliwa na "roho nyingine"! Na kwa nafasi yake aliyokuwa nayo katika Kanisa, huenda "Serikali ya mbinguni" ingemstaafisha kwa manufaa ya ufalme wa Aliye Hai! 

    Pili, kwa upande wa Simoni huenda siku hiyo ndiyo angekuwa amepata leseni ya kurejea kwenye uganga wake ila sasa ukiwa umeboreshwa kwa "upako bandia wa kusingizia ya kuwa ni Roho Mtakatifu" kwa kuwekewa mikono na Petro. Yale maroho ya zamani yangemrudia mara saba na uharibifu wake wa mwisho ungezidi wa mwanzo!

    Kwa kuhitimisha ujumbe huu napenda kujibu swali la mwongozo ambalo ni "Hatua gani zifanyike kukinusuru kizazi hiki na hatari ya ukengeufu wa maadili ya utumishi wa Kristo?"

    1. Dhambi itendwayo hadharani ikemewe hadharani!

    Hatupaswi kukemea watu hadharani kwa kutaja majina yao au majina ya taasisi zao. Lakini tuna uhuru wa kuzikemea hadharani hizi roho kwa kuanisha ukengeufu wake kwa mujibu wa Biblia kama vile ambavyo nimejaribu kuwasilisha ujumbe huu!

    "Wale wadumuo kutenda dhambi uwakemee mbele ya wote, ili na wengine waogope"(1.Tim.5:20)

    2. Kuna hitaji kubwa la kuhimiza walio waaminifu kujitakasa kwa kujitenga na waliokengeuka

    Kumbe kujitenga na wasiokuwa na imani sahihi, ni "kujitakasa" na kufanyika "chombo cha kupata heshima" 

    "Basi ikiwa mtu amejitakasa kwa kujitenga na hao, atakuwa chombo cha kupata heshima, kilichosafishwa, kimfaacho Bwana. kimetengenezwa kwa kila kazi njema." (2.Tim.2:21)


    3. Ianzishwe midahalo ya kujadili imani zenye utata

    Inahitajika midahalo ya nguvu na Makini itakayojadili waziwazi kwa hekima kuhusu "imani zenye utata" ili jamii ya waamini na wasioamini wote wajue ukweli uko wapi, na kazi kwao iwe ni kufanya maamuzi

    Tafsiri ya msamiati wa neno hili midahalo lina maana ya "..majadiliano baina ya watu wengi juu ya jambo moja maalum"! Siungi mkono mabishano yenye mashindano ya kibinafsi ya nani bora dhidi ya mwingine. Lazima ziwepo hadidu za rejea (ToRs) za kuendesha mijadala hii.

    "Lakini baadhi ya watu wa sinagogi lililoitwa sinagogi la Mahuru, na la Wakrene, na la Waiskanderia, na la wale wa Kilikia na Asia, wakaondoka na kujadiliana na Stefano; lakini hawakuweza kushindana na hiyo hekima na huyo Roho aliyesema naye" (Mdo.6:9-10
     - See more at: http://www.gospelkitaa.co.tz/2015/06/hoja-upako-wa-kununua-kwa-fedha.html#sthash.kyirBGim.dpuf

NENO NI UZIMA Designed by 5gear Copyright © 2014-2015

Theme images by Jason Morrow. Powered by Blogger.