Vichwa vya Habari

UZIMA WA MILELEL KATIKA DAMU YA YESU MWL. CHRTOPHER & DIANA MWAKASEGE

MWL. CHRISTOPHER MWAKASEGE: UZIMA WA MILELE KATIKA DAMU YA YESU KRISTO.


Na Mwl. Christopher Mwakasege
Basi Yesu akawaambia, Amini, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kunywa damu yake, hamna Uzima ndani yenu. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao UZIMA WA MILELE; nami nitamfufua siku ya mwisho. Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli; na damu yangu ni kinywaji cha kweli. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi” (Yohana 6:53-57).
Mtu ambaye ameula mwili wa Kristo na kuinywa damu yake ile iliyomwagika msalabani, ni yule ambaye anakaa ndani ya Yesu Kristo, na Yesu Kristo anakaa ndani yake. Kwa maneno mengine amepokea uzima wa Mungu, ambao ni uzima wa milele.
Unapompokea Yesu Kristo moyoni mwako unapokea uzima wa milele; kwa kuwa, “Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu” (Yohana 1:4).
Inatupasa tukumbuke ya kuwa, kwa mtu mmoja Adamu, dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi.
Pia, inatupasa tukumbuke ya kuwa, “ikiwa kwa kukosa mtu mmoja mauti ilitawala kwa sababu ya yule mmoja, zaidi sana wao wapokeao wingi wa neema, na kile kipawa cha haki, watatawala katika UZIMA kwa yule mmoja, Yesu Kristo” (Warumi 5:17).
Dhambi inapoingia mahali inaleta mauti, magonjwa, uasi, ubishi, umaskini na kutokufanikiwa. Uzima wa milele unapoingia ndani ya mtu unaleta, – Uzima, uponyaji, amani, upendo, utajiri na kufanikiwa na baraka zingine za Mungu.
UZIMA WA MILELE NA UPONYAJI
Kabla sijampokea Yesu Kristo moyoni mwangu awe Bwana na Mwokozi wangu, nilisumbuliwa sana na magonjwa.
Nakumbuka nilikuwa nasumbuliwa na maumivu ya kichwa mara kwa mara. Nilipokwenda kupimwa hospitali kwa daktari, niliambiwa nina ugonjwa wa vidonda vya tumbo ‘Ulcers’ na pia ‘High blood pressure’.
Nilipewa dawa za kutumia, na pia niliambiwa nisile vyakula vya aina fulani maana vitaniongezea ugonjwa.
Niliyafuata masharti ya daktari, na nilipata nafuu kidogo. Lakini kitu cha kushangaza ni kwamba mara kwa mara magonjwa yalinirudia na kunisumbua sana – sikujua kitu cha kufanya. Baada ya miaka kadha neema ya Bwana ilifuniliwa moyoni mwangu, nikaokoka baada ya kutubu na kumpokea Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wangu. Mabadiliko yaliyotokea katika maisha yangu ni makubwa mno. Wakati huo nilikuwa sijajua ni kitu gani kimetokea – lakini nilijua kuwa ninaishi maisha mapya.
Nilishangaa kuona kuwa miezi kadhaa imepita bila kusumbuliwa na magonjwa. Kichwa hakikiniuma tena, moyo uliacha kwenda mbio tena vyakula vingine nilivyokatazwa nisile na daktari havikunidhuru nilipovila tena kama mwanzo. Nilijua hakika kuwa nimepona!
Wakati huo sikuweza kufahamu kitu kilichotokea hata nikapona mara moja namna hiyo. Lakini kwa kadri ambavyo Roho Mtakatifu alivyoendelea kunikuza katika wokovu nilikuja kufahamu ya kuwa MSAMAHA WA DHAMBI UNAONGOZANA NA UPONYAJI WA MWILI.
Kabla ya mwanadamu kutenda dhambi, hakukuwa na magonjwa. Dhambi ilipoingia ilileta na magonjwa pia. Sadaka ya uhai wa Yesu Kristo msalabani ilileta msamaha na ondoleo la dhambi na madhara yake yote ikiwa ni pamoja na MAGONJWA.
Unapompokea Yesu Kristo moyoni mwako kuwa Bwana na Mwokozi wako, unampokea MPONYAJI. Roho wa Uzima wa milele anayeingia kutawala maisha yako, ni Roho wa Uponyaji anayefukuza magonjwa yote ndani yako na kukupa afya.
Ndiyo maana imeandikwa hivi; “Hata kulipokuwa jioni, wakamletea (Yesu Kristo) wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake, akawaponya wote waliokuwa hawawezi, ili litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, na KUYACHUKUA MAGONJWA YETU” (Mathayo 8:16,17). Soma pia (Isaya 53:4,5)
Kwa kuwa alichukua dhambi zetu, dhambi hizo zimeondolewa kwetu, na tumepokea utakatifu wake. Kwa kuwa alichukua magonjwa yetu, hakuna sababu ya sisi kuendelea kuumwa kwa kuwa tumepokea uponyaji wake. Ndiyo maana imeandikwa hivi;
Yeye mwenyewe (Yesu Kristo) alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti; ili tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na KWA KUPIGWA KWAKE MLIPONYWA” (1Petro 2:24).
Angalieni anasema, “ Kwa kupigwa kwake MLIPONYWA” na siyo ‘MTAPONYWA’. Ikiwa TULIPONYWA kwa hiyo sasa TUMEPONA!
Ndiyo maana watu wengi sana nimewasikia wakishuhudia ya kuwa magonjwa yaliyokuwa yanawasumbua kwa muda mrefu yamepona baada ya kumpokea Yesu Kristo mioyoni mwao na kuokoka.
Kuna mama mmoja alinishuhudia ya kuwa alisumbuliwa sana na majini kwa muda wa miaka kumi na mitatu. Alikwenda hospitali – hakupona. Alikwenda kwa waganga wa kienyeji – hakupona. Mwili wake ulidhoofu sana.
Siku moja neema ya Mungu ilimzukia aliamua kuokoka. Mhubiri aliposema watu wanaotaka kuokoka waje mbele, huyo mama naye alikwenda – akafanya sala ya toba na kumkaribisha Yesu Kristo moyoni mwake.
Mama huyo alinambia tangu wakati huo maumivu aliyokuwa nayo mwilini kwa miaka 13 yaliondoka. Mume wake na ndugu zake walishangaa sana. Tangu wakati huo aliookoka na kupona hadi alipokuwa ananisimulia ilikuwa imepita miaka minne, na bado alikuwa amepona na afya njema.
Kama wewe unayesoma haya unaumwa na hujaokoka, nakushauri utubu dhambi zako na umpokee Yesu Kristo moyoni mwako, na DAMU YAKE itakutakasa, na utapokea uponyaji unaouhitaji sasa. Kwa sababu imeandikwa, “ Akusamehe maovu yako yote, akuponya magonjwa yako yote” (Zaburi 103:3).
UZIMA WA MILELE NA MABADILIKO YA TABIA:
Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama! Yamekuwa mapya” (2Wakorintho 5:17)
Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi yaani, msamaha wa dhambi”.(Wakolosai 1:13,14).
Yesu Kristo alisema ukiula mwili wake na ukiinywa damu yake yeye anakaa ndani yako na wewe unakaa ndani yake – unapokea uzima wake au uzima wa milele.
Mtu akiwa ndani ya Kristo, anakuwa mtu mpya. Mtu anapokuwa ndani ya Kristo anabadilika tabia yake kwa kuwa amehamishwa toka katika nguvu za giza na tabia yake na kuingia katika ufalme wa Kristo na tabia ya Kikristo.
Mtu akiwa ndani ya Kristo anavua utu wake wa kale na kuvaa utu mpya – anavaa tabia mpya.
Wakati fulani nilikuwa mji fulani hapa nchini nikihubiri mkutano wa siku nane, asubuhi moja alikuja mzee mmoja kuniona katika hotel niliyokuwa ninakaa.
Yule mzee akasema; “ Unakumbuka jana ulipoita watu wanaotaka kuokoka waje mbele waombewe, kuna mtoto mmoja alikuwa wa kwanza kufika mbele”.
Ndiyo, nakumbuka”; Nikamjibu.
Yule mzee akaendelea kusema; “Yule mtoto ni wa kwangu, na tangu jana kumetokea mabadiliko makubwa mno ya tabia, nikaona heri nije nikushirikishe”.
Nikamuuliza, “Kumetokea mabadiliko gani?
Huyu mtoto wangu”; yule mzee alieleza; “Kabla ya jana alipoamua kuokoka, alikuwa si mtii, alikuwa hapendi usafi, alikuwa hawezi hata kutandika kitanda chake akiamka asubuhi. Hata tukimwambia afagie uwanja unaozunguka nyumba yetu alikuwa hasikii. Kweli, tumempiga fimbo mpaka tuliogopa tutamuumiza. Lakini kuanzia jana alipookoka (sisi tulifikiri anatania) tabia yake imebadilika kabisa. Amekuwa mtii, kazi anajituma kufanya, amekuwa msafi, hata wakati wa usiku, anachukua biblia na kusali yeye mwenyewe – maajabu haya”.
Yesu Kristo alisema ukiula mwili wake na kuinywa damu yake, yeye atakaa ndani yako na wewe utakaa ndani yake unapokea uzima wake wa milele unaokuvika tabia ya Uungu.
Haya ndiyo yaliyotokea kwa huyu mtoto mdogo wa umri wa miaka kumi na miwili. Huyu mtoto alipompokea Yesu Kristo na kuokoka – Kiroho aliula mwili wa Yesu na kuinywa damu yake – akapokea uzima wa milele, Yesu Kristo aliingia ndani ya mtoto, na mtoto akaingia ndani ya Yesu Kristo – yote yalifanyika kwa Uwezo wa Roho Mtakatifu.
Unadhani mtoto huyu alipata wapi ujasiri wa kufanya sala yeye mwenyewe, kitu ambacho alikuwa anaogopa kufanya kabla hajaokoka?
Jibu lake ni – Damu ya Yesu Kristo! Imeandikwa hivi; “Basi ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya Yesu…….” (Waebrania 10:19).
Niliwahi kukaribishwa katika mkoa mwingine kuhubiri katika Kanisa fulani, nakumbuka kuwa nilihubiri juu ya Bartimayo yule kipofu aliyeponywa na Yesu Kristo kule Yeriko. Nilipomaliza mahubiri nilikaribisha watu waje mbele wale wanaotaka kuokoka na kuombewa magonjwa.
Watu wengi waliokoka na pia kuponywa maradhi yaliyokuwa yanawasumbua.
Baada ya wiki moja kupita, alikuja mtu mmoja nyumbani kwangu tukasalimiana na nikamkaribisha aingie ndani. Alipokwisha kukaa kwenye kiti, akaniuliza akasema; “ Mlimpa kitu gani ndugu (alitaja jina lake) siku mlipokuja kuhubiri kanisani kwetu – maana mimi sikuwepo.
Nikamuuliza, “Kwani kumetokea nini?
Yule mgeni akasema; “Huyo ndugu alikuwa hawezi kunywa chai ya maziwa wala maziwa – akinywa maziwa alikuwa anaugua. Nilishangaa siku moja alifika nyumbani, nilipomkaribisha chai ya rangi alikataa, akasema sasa anakunywa chai ya maziwa bila shida yoyote.
Nilipomuuliza ameanza lini kunywa chai ya maziwa, akasema tangu baada ya maombi ya Jumapili pale Kanisani. Lakini pia, niliona tabia yake imebadilika. Alikuwa hachani nywele- sasa anachana. Alikuwa mlevi sana – sasa haonji tena pombe. Alikuwa mchafu, hajijali – nilishangaa kumwona amevaa nguo safi. Ni kitu gani mlimpa?
Nikamjibu nikasema; “ Sisi tulichokifanya ni kuhubiri habari za Yesu Kristo na uwezo wake. Ndugu yako alifungua moyo wake siku ile, akampokea Yesu Kristo moyoni mwake ili awe Bwana na Mwokozi wake akaokoka. Pia tukamuombea tatizo la ugonjwa alilokuwa nalo na Bwana akamponya”.
Ni jambo la kumsifu Mungu sana katika Kristo, kwa sababu baada ya huyo ndugu kuokoka, na maisha yake kubadilika – sasa hivi ana kazi nzuri ya kuajiriwa na pia, ni mhubiri wa injili. Jina la Bwana libarikiwe!
Huwezi ukampokea Yesu Kristo moyoni mwako na bado ukawa na tabia uliyokuwa nayo zamani. Unapompokea Yesu Kristo moyoni mwako – unapokea Uzima wa milele unaokupa tabia ya Uungu.
Yesu Kristo alisema hivi; “ Amini, amini, nawaambieni, msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake hamna Uzima ndani yenu…..Aulaye mwili wangu na kuinywa DAMU YANGU hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa pekee yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu. Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lolote…….Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa” (Yohana 6:53,56; Yohana 15:4,5,7)
Mtume Paulo alisema; “ Hata imekuwa, mtu akiwa NDANI YA KRISTO amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama! Yamekuwa mapya” (2Wakorintho 5:17).
Mtume Paulo alisema hivi katika waraka wake wa pili kwa watu wote, sura ya kwanza mstari wa tatu na wa nne; “Kwa kuwa uweza wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima wa utauwa, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe. Tena kwa hayo atumetukirimia ahadi kubwa mno, za THAMANI, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa WASHIRIKA WA TABIA YA UUNGU, mkiokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa”.

No comments:

Post a Comment

NENO NI UZIMA Designed by 5gear Copyright © 2014-2015

Theme images by Jason Morrow. Powered by Blogger.