Vichwa vya Habari

TAMBUA NGUVU ZA ROHO MTAKATIFU ( THE POWER OF THE HOLY SPIRIT) MWL.CHRISTOPHER MWAKASEGE

na mwl christopher mwakasege

 Je! Umewahi kujiuliza kwa nini wakati mwingine nguvu za Mungu zinakushukia kwa uwingi halafu baada ya muda zinapungua au zinaondoka – unabaki hali kama vile hujawahi kushukiwa hata siku moja? Inawezakana umewahi kujiuliza swali hili na inawezekana hujawahi kujiuliza. Na pia inawezekana hali hii tunayoiuliza hapa juu haijawahi kukutokea. Kumbuka kuwa nguvu za Mungu zinaweza kupungua ndani yako – kwa sababu mbalimbali – ambazo ni pamoja na kutozitumia kwa kiwango kilichokusudiwa. Unakumbuka Yesu alipoulilia mji wa Yerusalemu? Alisema; “Laiti ungalijua, hata wewe, katika siku hii, yapasayo amani!” (Luka 19:42). Alichokuwa anataka wajue ni kwamba ndani yake kulikuwa na nguvu au upako wa Roho Mtakatifu uletao amani. Lakini tunaona wazi ya kuwa Yerusalemu hawakutumia upako huu na amani ya Mungu ikaondoka pia. Tatizo la Yerusalemu lilikuwa ni kwa sababu hakutambua majira ya ‘kujiliwa’ kwake. Kwa lugha nyingine Yerusalemu ‘ulijiliwa’ au ulitembelewa na nguvu za Mungu ziletazo amani – lakini hawakutambua! Na kwa sababu hawakutambua hilo, kwa hiyo hata nguvu za Mungu hawakuzitambua wala kuzitumia. – Kilichotokea ni kwamba nguvu hizo (1Wakorintho 1:18,24) ziliondoka wasiweze kuzitumia.

Tunaona pia katika Yohana 1:11 ya kuwa “ Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea.” Yesu anaweza kuja kwako. Nguvu zake (ambazo ndizo nguvu za Roho Mtakatifu) zinaweza kuja kwako – usipozipokea itakuwa vigumu kuzitumia kwa kiwango kinachotakiwa. Maana katika mstari unaofuata wa 12, Yohana anaendelea kusema hivi: “ Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika …..” Ili uweze kuzipokea na kuzitumia nguvu za Mungu ipasavyo ni vizuri ujue Mungu amezituma nguvu zake kwetu kwa ajili ya nini. Zipo sababu nyingi katika biblia, lakini sisi tunataka tukupe angalau chache wakati huu ili ziwe changamoto kwako.

Sababu ya Kwanza: TUWE MASHAHIDI WAKE
Ili tuonekane na kujulikana ya kuwa sisi tu wanafunzi wa Yesu – tunachohitajika kufanya ni kupendana (Yohana 13:35). Huu ni upendo ambao watu wasiomjua huyu Mungu wetu  wanatakiwa wauone kwetu. Wakiona tunavyopendana, basi watajua ya kuwa sisi tu wanafunzi wa Yesu. Unapofanya sala ya toba na kumkaribisha Yesu katika maisha yako – unaokoka. Unaweza ukawa umeokoka lakini usiwe ‘mwanafunzi’ wa Kristo – kwa tafsiri ya Yesu juu ya nani ni mwanafunzi wake. Ikiwa umeokoka na huonyeshi upendo wa Kristo kwa waliookoka wenzako unapoteza hadhi ya kuwa mwanafunzi wa Kristo. Inapofika hali ya kuwa ‘shahidi’ inabidi upokee nguvu za Roho Mtakatifu. Yesu alisema katika kitabu cha Matendo ya Mitume 1:8 ya kuwa: “ Lakini mtapokea nguvu,; akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi” Kazi ya shahidi ni kusimama upande wa anayeshitaki au anayeshitakiwa kumtetea huyo ambaye ameamua kuwa shahidi upande wake – akisema na kwa kuonyesha vithibitisho ili kusisitiza kuwa anachokitetea ndicho sahihi. Katika mazingira ya Bwana Yesu, sisi tunakuwa mashahidi kwa kusema na kuonyesha au kuthibisha kwa vitendo ya kuwa yote ambayo Yesu Kristo amesema na yamefanyika juu yake ndivyo yalivyo, na ndiyo kweli inayotakiwa kufuatwa na kila anayemtafuta Mungu wa kweli. Nguvu za Roho Mtakatifu zinatufanya tuweze kusimama katika nafasi ya kuwa mashahidi wa Kristo.

Sababu ya Pili: Kushinda Dhambi
Ndiyo! Kushinda dhambi. Unaweza kuishinda dhambi. Katika Mwanzo 4:7 tunaambiwa inatupasa au ni lazima tuishinde dhambi. Mungu hawezi kusema tuishinde dhambi kama hakuna mbinu ya sisi kuishinda dhambi. Pia, katika Warumi tunaambiwa ya kuwa dhambi haitatutawala. Lakini ni lazima tujue ya kuwa hakuna mwanadamu yeyote anayeweza kuishinda dhambi kwa nguvu zake mwenyewe. Kila mtu lazima ajue kuzitumainia nguvu za Mungu tunazozipata katika Roho Mtakatifu kwa sababu ya Kristo kufa msalabani kwa ajili yetu. Ndiyo maana imeandikwa hivi katika 1 Wakorintho 1:18,23,24: “ Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookokolewa ni nguvu ya Mungu …… sisi tunamhubiri Kristo, aliyesulibiwa; kwa Wayahudi ni kikwazo, na kwa Wayunani ni upuzi; bali kwao waitwao, Wayahudi kwa Wayunani, ni Kristo, nguvu ya Mungu, na hekima ya Mungu.” Hiki ndicho kinachotokea unapookoka; Kristo anaingia ndani yako kwa uwezo wa Roho Mtakatifu- anakuwa nguvu ya Mungu inayokuwezesha kushinda dhambi. Kwa hiyo kama iko dhambi inayokusumbua – tubu, halafu omba Mungu akuongezee nguvu za Roho wake ili upate kushinda dhambi.

Sababu ya Tatu: Kuwa Tajiri
Jambo mojawapo lililotokea kwa mwanadamu dhambi ilipoingia ni kuishi maisha ya umaskini na kupungukiwa. Dhambi pia iliweka matabaka ya matajiri na maskini. Toka mwanzo na hata sasa na siku zote Mungu hapendi watu wake wawe maskini (kwa jinsi ya mwili) Katika 2 Wakorintho 8:9 tunasoma ya kuwa: “ Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake” Kwa hiyo ni mapenzi ya Mungu tuwe matajiri. Njia ambayo Mungu anatumia kutuwezesha tuwe matajiri ni kwa kutupa nguvu zake. Kwa maana imeandikwa katika kitabu cha Kumbukumbu ya Torati 8:18 ya kuwa: “Bali utamkumbuka Bwana, Mungu wako maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri, ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo” Tunasoma hapa ya kuwa tunaweza kuomba tupate msaada wa nguvu za Mungu ili tupate utajiri halali ndani ya Kristo.

Sababu ya Nne: Kushinda hila za shetani
Tunasoma katika kitabu cha Waefeso 6:10,11 ya kuwa: “Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za shetani” Haitoshi kupokea nguvu za Roho Mtakatifu bila kuwa hodari katika kuzitumia ili upate “kuweza kuzipinga hila za shetani” Ili uwe hodari katika mchezo fulani lazima ufanye mazoezi ya kutosha ili kujifunza mbinu za kukusaidia kushinda upinzani katika mashindano. Pia, katika mambo ya rohoni ni vivyo hivyo. Ili uwe hodari katika uweza wa nguvu za Mungu – haitoshi tu kuzipokea kwa kujazwa Roho Mtakatifu. Bali ni muhimu kufanya ‘mazoezi’ sawa na neno la Mungu ili uwe hodari. Hii ndiyo maana unaweza ukajawa nguvu za Mungu na bado shetani akakushinda na hila zake. Kwa nini? Kwa sababu hujazwa hodari katika kuzitumia. Hii ni sawa na mtu kuwa na silaha yenye nguvu vitani lakini kwa sababu hajui kuitumia ipasavyo anajikuta ameshindwa vita! Nguvu za Roho Mtakatifu zipo pia kwa ajili ya kutusaidia kumshinda shetani na hila zake dhidi ya maisha yetu. Lakini ni muhimu tujue kuzitumia sawa na neno la Mungu – tuwe hodari katika uweza wa nguvu zake. La sivyo tutakuwa tunashindwa na shetani wakati tunazo nguvu za kumshinda ndani yetu.

Sababu ya Tano: Kudumu katika maombi
Kila mtu aliyeokoka ndani yake anahamu ya kufanya maombi – kuzungumza na Mungu. Lakini karibu kila mtu anajua ya kuwa kila akiomba anatamani angeweza kuomba vizuri zaidi, kuliko anavyoomba wakati huo.
Jambo hili la kuwa na upungufu katika maombi lisikushangaze. Biblia inatuambia; “…. Hatujui kuomba jinsi itupasavyo ….” (Warumi 8:26). Kazi ya Roho Mtakatifu ni kutusaidia udhaifu huu tulionao wa kuomba – ili kwa nguvu zake tuweze kuomba utupasavyo, na pia tuweze kuwaombea “watakatifu kama apendavyo Mungu” (Warumi 8:27). uzuri wa maombi si tu kwamba ni sababu ya Mungu kutupa Roho wake ili kwa msaada wa nguvu zake tuweze kuomba itupasavyo; bali maombi pia ni njia au mlango wa nguvu za Mungu kuongezeka katika maisha yetu. Ndiyo maana mara nyingi ukikaa katika maombi muda mrefu zaidi – nguvu za Mungu zinaongezeka. Lengo la nguvu hizi kuongezeka ni ili uendelee kuomba kama impendezavyo Mungu hadi upate unachoomba. Kwa mfano, kama nguvu za Mungu ni kidogo ndani yako – hasa wakati umo taabuni au katika majaribu – ni rahisi sana ‘kuzimia’ au kukata tamaa. Imeandikwa hivi: “Ukizimia siku ya taabu, nguvu zako ni chache” (Mithali 24:10) “Bali vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana wataanguka, bali waowamngojeao Bwana watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia” (Isaya 40:30,31) Nguvu za Mungu ndani yako zitakusaidia usizimie wala usichoke wala usikate tamaa iwe ni wakati wa raha au wakati wa taabu. Ukiona unachoka au unakata tamaa maana yake una nguvu kidogo au zimepungua – kwa hiyo omba Mungu akuongezee nguvu zake ili usichoke wala kuzimia wala kukata tamaa.

Sababu ya Sita: Kuondoa woga
Mtume Paulo aliwahi kumwandikia Timotheo maneno muhimu sana ambayo yanasema na watu wengi hata sasa aliposema; “ Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi” (2 Timotheo 1:7) Timotheo asingeandikiwa maneno haya kama hakuwa mwoga! Inaonyesha alikuwa mwoga kuichochea ‘karama ya Mungu’ iliyokuwa ndani yake! (2 Timotheo 1:6) Kama alikuwa mwoga basi hali hii ilifanya utumishi wake ulegee. Hii inawezekana ilitokea kwa sababu aliona na kushuhudia mateso aliyopata Mtume Paulo alipochochea karama ya Mungu iliyokuwa ndani yake. Kwa kuogopa kuteswa na yeye kama Mtume Paulo, aliamua kuacha kuchochea karama ya Mungu iliyokuwa ndani yake. Ndiyo maana Mtume Paulo  alimhimiza aichochee hiyo karama “….maana Mungu hakutupa roho ya woga bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi” Kama unasikia woga wa kumtumikia Mungu kwa sababu moja au nyingine hauko peke yako. Dawa yake ni nguvu za Mungu ziongezeke ndani yake- na woga huo utaondoka! Timotheo alibanwa na woga. Lakini pia Yoshua alipokuwa anakabidhiwa wajibu wa kuongoza wana wa Israeli baada ya Musa kufa – alishikwa na woga! La sivyo Mungu asingemwambia awe na moyo wa ushujaa mara tatu! (Yoshua 1:6,7,9). Yeremia naye alipokuwa anapewa wajibu wa kumtumikia Mungu akiwa bado mtoto – aliingiwa na woga! Lakini Mungu akamwambia – “Usiogope” (Yeremia 1:4-10). Kwa hiyo kama unasikia woga katika kumtumikia Mungu – omba ili Mungu akupe nguvu zake zaidi ili ziondoe woga. Jambo hili liliwahi kumtokea Mtume Petro. Pamoja na kwamba alimpenda Yesu sana na kuahidi kuwa naye kila mahali – bado woga ulimwingia alipoulizwa kama alimjua Yesu wakati Yesu amekamatwa. Lakini  baada ya kujazwa nguvu za Roho Mtakatifu siku ya Pentekoste hatuoni tena woga ukijitokeza ndani yake – bali tunaona ujasiri mwingi.

Mwl Christopher Mwakasege atoa shuhuda juu ya kifo Fanuel Sedekia

Alisema Roho mtakatifu akwambiavyo omba hiyo haina MJADALA ni kuingia kwenye maombi mpaka upate unachokiomba kwa kuwa gharama ya kuingia kwenye maombi ili kupata ulichotakiwa kukipata ni ndogo kuliko gharama ya kukosa kile ulichoambiwa ukipate katika Maombi hayo.
Roho mtakatifu anapokupa mzigo wa kuombea jambo anakupa na muda ukizembea  muda huo ukipita kinakuwa ni kiporo, na kiporo kinaweza kikalika na kipo ambacho hakiliki.  .
“Tulipoenda Israel na Fanuel Sedekia kisha akaanza kuumwa madaktari waliniambia ubongo wake kwa asilimia tisini haufanyi kazi. Lakini walishangaa kwa nini kila mara niko pale Hospitali wakasema kwa nini usikae tu Hotelini kisha ukawa unapiga simu kuulizia hali ya Mgonjwa? Wao hawakujua kwa nini naenda pale kwa kuwa suala la kupiga simu tu sio tatizo ningeweza kurudi Arusha kisha nikawa napiga simu.
Suala hapa ni kuwa nilikuwa naenda kila mara kwa ajili ya kumfanyia maombi, nilikuwa nakaa kandokando ya Bahari ya Galilaya nafanya maombi juu ya Sedikia kwa masaa sita nikitoka hapo nasikia upako wa ajabu sana kIsha napanda Taxi kuelekea Hospitali. Nikifika Hospitali madactari na watu wa ICU walikuwa washanifahamu hivyo naenda moja kwa moja kwenye chumba cha nguo nabadili nguo kIsha naingia ICU alikolazwa.
Nikifika nambana Mungu kwa maswali Mengi namuuliza Sedekia, hivi unaongea nini na Yesu muda wote huo si urudi? na kisha namuuliza Yesu, hivi Yesu si unafahamu kuwa Sedekia anamke ukimchukua mkewe atamuachia nani? Kisha baada ya maneno hayo naweka mkono juu yake. Nilipokuwa nikiweka mkono juu yake ghafla upako wote unakuwa kama umenyonywa.
Baada ya hapo narudi hotelini naanza tena kumuuliza Mungu hivi Mungu kama basi husikii maombi yangu sikia maombi ya watanzania kwa kuwa saa hiyo nilijua watanzania wengi wanamuombea Sedekia.
Inafikia wakati nakata tamaa lakini ndani yangu najisemea Mwakasege haiwezekani jitie moyo kisha nabadili aina ya maombi, kwa kuwa nilikuwa na nguo zake pamoja na passport yake nikawa naviweka kati kisha nikawa naanza maombi ya Yeriko, nikawa niko hotelini usiku nazunguka nguo zake na paspot yake huku nikifanya maombi.
Taratibu Mungu akaanza kuniambia kuwa sedekia harudi, Kipidi hicho mimi na familia yangu tulikuwa tumepanga kwenda kupumzika nchini Uingereza wakati wa skukuu ya Chrismass,  na booking mpaka ya Hotel tulikuwa tumeshafanya, na watoto wote wako nyumbani wakijiuliza tunaendaje kupumzika wakati Sedekia anaumwa? Chrismass ikapita na mwaka mpya pia kisha Sedekia akafariki.
Baada ya kifo hicho sikuchoka nkarudi tena kwa Mungu nikamuuliza kwa nini Mungu umeamua kumchukua Sedekia mikononi mwangu? Mungu alinijibu vitu ambavyo siwezi kuvisema hapa.
Kila siku mimi ni mgeni katika maombi namhitaji ROHO anifundishe kwa upya kwa kuwa sijui vita gani ninakwenda kupambana nayo, Mungu anabaki kuwa Mungu kwa kuwa hufanya atakavyo”


NINI MAANA YA KUMPENDA BWANA?

Kumbukumbu la Torati 6:5 Nawe, mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote na Pia ile Mathayo 22:37 inasema Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote”. Hivyo basi kwa kutumia hiyo mistari miwili tunaona kwamba mtu anatakiwa kumpenda Bwana Mungu wake kwa;
Moyo wake wote, Roho yake yote, Nguvu zake zote, Na akili zake zote.
Lakini pia ukisoma kile kitabu cha 1 Yohana 5:3 Biblia inasema “Kwa maana huku ndiko kumpenda Mungu, kwamba, tuzishike amri zake, wala amri zake si nzito”. Hivyo basi kumpenda Mungu ni kuzishika amri zake. Sasa kuzishika amri za Mungu ni suala linalohitaji Moyo wako, roho yako, nguvu zako na akili zako vyote kwa pamoja vifanye kazi ya kumpenda Mungu kwa maana ya kuzishika amri zake.
*Kumpenda Bwana kwa moyo wako.
Kumpenda Bwana kwa moyo wako ni kwa kuutafakarisha moyo wako amri za Bwana kwa maana ya maagizo yake unayotakiwa kuyashika. Hii ni pamoja na kutumia muda wako siku zote kuliweka neno la kristo kwa wingi ndani yako kwa kulitafakari. Unapolitafakari neno la Bwana ndipo pia unapopata mawazo na njia za Mungu za kukufanikisha kimaisha. Zaburi 27:4.
*Kumpenda Bwana kwa roho yako.
Hapa unatakiwa kuitafakarisha roho yako neno la Bwana ambalo linazungumzia wakati ujao (future yako) ishibishe roho yako ahadi za Mungu ili imani yako iongezeke na uanze kuona mambo ya wakati ujao kana kwamba yapo halisi kwa wakati wa sasa. Hili litakusaidia kuishi kwa Imani, maana siku zote utakuwa unafanya yale yanayompendeza Mungu.
*Kumpenda Bwana kwa nguvu zako zote.
Nguvu ni uwezo alionao mtu katika kufanya kazi fulani. Sasa tumia nguvu zako zote za kimwili za kiufahamu, za kifedha nk katika kutekeleza yale yote ambayo neno la Mungu linakuagiza kila siku unapolitafakari kumbuka nimekuambia katika kulitafakari neno la Bwana utapata mawazo ya Bwana juu yako na ndani ya hayo mawazo kuna mipango na mikakati ya kuitekeleza.
*Kumpenda Bwana kwa akili zako zote.
Vile vile akili ni uwezo wa kiufahamu alionao mtu katika kufanya mambo. Hivyo basi wakati unatumia nguvu kutekeleza maagizo ya Bwana basi hakikisha unatekeleza kwa kutumia akili ili ufanye kitu sahihi, kwa wakati sahihi na kwa usahihi.

imani ihamishayo milima

MARKO 11: 20- 24.

20. Na asubuhi walipokuwa wakipita, waliuona ule mtini umenyauka toka shinani. 21. Haya ni matokeo ya Bwana Yesu kuulaani mtini usitoe matunda tena. Alisema neno tu juu ya huo mti, na kesho yake umenyauka! Petro akakumbuka habari yake,akamwambia, Rabbi, tazama mtini ulio ulaani umekauka. Mtini ulikuwa mlengwa wa imani itendayo kazi. Hapa Petro anaona jinsi Neno la Bwana Yesu lilivyokausha mtini ingawa bado haelewi kilicho tokea. Petro anachokumbuka ni Bwana Yesu kuulaani mtini, na kesho yake kukauka. 22. Yesu akajibu akawaambia, Mwaminini Mungu.
Hili ni Neno kubwa analosema Bwana Yesu. Wakati wanafunzi wanashangaa kukauka kwa mtini, wanaambiwa wa mwamini Mungu, kwani imani isiyomtegemea Mungu ni batili na butu. Kumwamini Mungu ni zaidi ya kumwamini kwa kukiri tu kwa kinywa, ni zaidi ya kuamini moyoni mwako. Imani hii anayoizungumzia Bwana Yesu hapa ni ile ya utendaji, yaani imani inayomfanya Mungu kutenda miujiza. Ni imani inayokufanya kuchukua hatua ukijua kwa hakika Mungu atafanya. Ukitaka kuhamisha milima katika maisha yako, ni lazima umwamini Mungu, na sio uwezo wako wala watu.
23. Amini nawaambia,Ye yote atakayeuambia mlima huu, Ngo’ka ukatupwe baharini wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia yatakuwa yake.  Maelezo haya ndio yenye siri ya ushindi kwa watoto wa Mungu. Bwana Yesu anatuonyesha sumu iuayo imani, yaani mashaka. Mashaka maana yake ni sawa na kumwambia Mungu kwa vitendo kwamba hauamini kuwa atafanya lile unalomwomba akufanyie. Unaweza kusema kwa mdomo na hata kufikiri kuwa moyoni mwako una mwamini Mungu, lakini kile utakachokifanya ndicho kitakachoonyesha kwa uhakika kama unamwamini Mungu au unaenenda kwa mashaka.
• Jambo la pili hapa ambalo ni la muhimu kuelewa ni kuwa anayehamisha milima katika maisha yako ni Mungu, hivyo katika imani yako unatakuwa kutambua kuwa Mungu atahamisha huu milima ulio mbele yangu ni kuamini kwa vitendo. Na hili hutendeka vipi? Kama nina milima katika maisha yangu, nikamwomba Mungu aihamishe, baada ya maombi hayo, nisiendelee tena kuishi au kuongea kama mtu ambaye bado anakabiliwa na milima, kwani tayari nilikwisha mwamini Mungu kuuondoa huo mlima, na hakika Mungu atauondoa!
24. Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali aminini ya kwamba mnayapokea nayo yatakuwa yenu. Hapa tunapewa uthibitisho wa uaminifu wa Mungu katika kujibu maombi yetu tukiamini kwa vitendo. Mashaka ni sumu ya imani kiasi kwamba imetunyima Baraka nyingi toka kwa Mungu. Angalia ahadi hiyo ya Mungu hapo juu, kwamba tukiomba lo lote na kujua kwamba anayetupatia ni Mungu, tutapokea. Mashaka hutuambia kuwa hilo haliwezekani, yaani kuna wakati Mungu atajibu na kuna wakati hatakujibu; kama hivyo ndivyo unavyojisikia wakati unamwomba Mungu ikatae roho hiyo kwani hayo ni mshaka.
Neno la mwisho kuhusu roho ya mashaka:  “Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima na aombe dua kwa Mungu awapaye wote kwa ukarimu, wala hakemei naye atapewa. Ila na aombe kwa imani, pasipo shaka yo yote, maana mwenye shaka ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo, na kupeperushwa huku na huku. Maana mtu kama Yule asidhani ya kuwa atapokea kitu kwa Bwana.” (Yakobo 1:5-7)

njia ya kweli na uzima

Kuna sauti nyingi zidanganyazo zikidai kuwa imani au dini yao ndiyo bora kuliko zingine na hata zingine kudai mtume wao ndiyo wa mwisho kuja duniani na anapashwa kufuatwa huyo, na kusababisha hata (wakristo jina) kupoteza muelekeo na kuona labda kuna ukweli ndani na kuiacha ile kweli.kwanza tujiulize je MUNGU baba wa yesu kristo aliyeumba mbingu na dunia anayosifa ipi?na sifa za hao miungu wengine bandia zikoje?sasa kwa nini mtu afikirie kuhusu Yesu huko juu, wakati Muhammad au Confucius (Mwana filosofia Fulani wa china), Buddha, au Charles Taze Russell, au Joseph Smith? Kwani hata hao si njia zote zinaelekea Mbinguni? Kwani si Dini zote ziko sawa? Ukweli ni kwamba Dini zote hazielekei Mbinguni kama jinsi ambavyo njia zote hazielekei kariakoo.
 Yohana 14:   1Yesu akawaambia, ``Msifadhaike mioyoni mwenu. Mwaminini Mungu, niaminini na mimi pia. 2Katika nyumba ya baba yangu mna nafasi nyingi. Kama sivyo, nisingeliwaambia kwamba nakwenda kuwaandalia makao. 3Na nikishawaandalia, nitarudi kuwachukua mkae pamoja nami; ili mahali nilipo, nanyi mpate kuwepo. 4Ninyi mnajua njia ya kufikia ninakokwenda.''5Tomaso akamwuliza, ``Bwana, hatujui unakokwenda; tutaijuaje njia?'' 6Yesu akawaambia, ``Mimi ndiye Njia na Kweli na Uzima; mtu hawezi kufika kwa Baba bila kupitia kwangu. 7Kama mngekuwa mnajua mimi ni nani, mngemfahamu na Baba yangu. Tangu sasa mnamfahamu Baba yangu na mmemwona.''
   8Filipo akamwambia Yesu, ``Bwana, tuonyeshe Baba yako nasi tutaridhika.'' 9 Yesu akamjibu, ``Filipo, imekuwaje hunifahamu baada ya mimi kuwa pamoja nanyi muda wote huu? Mtu ye yote ambaye ameniona mimi, amemwona Baba. Sasa inakuwaje unasema, `Tuonyeshe Baba'? 10Je, huamini ya kuwa mimi niko ndani ya Baba yangu, na Baba yangu yuko ndani yangu? Mambo ninayowaambia siyasemi kwa mamlaka yangu mwenyewe, bali yanatoka kwa Baba yangu ambaye anaishi ndani yangu, na ndiye anayetenda haya yote.
Yesu pekee huzungumza kwa mamlaka ya Mungu kwasababu Yesu peke yake alishinda mauti. Muhammad,Confucius (Mwana filosofia Fulani wa china), na wengineo wanaendelea kubadilika kuwa mavumbi makaburini mwao mpaka leo hii, lakini Yesu, kwa nguvu zake, alitoka kaburini siku ya tatu baada ya kufa juu ya msalaba wa warumi uliojaa dhiki. Ni Yesu  pekee mwenye uwezo juu ya mauti, anastahili usikivu wetu. Ni Yesu pekee astahiliye kusikizwa.

Ushahidi unaosimamia kufufuka kwa Yesu Kristo ni wa ushindi mkuu na haupingiki. Mwanzo, palikuwa na mashahidi zaidi ya mia tano waliokuwa wamefufuka kwa Kristo! Hao ni mashahidi wengi waliojionea kwa macho. Sauti mia tano haziwezi kupuuziwa. Pia kunalo jambo la kaburi lililokuwa tupu; maadui zake Yesu wangelikuwa wamesimamisha kwa njia ya rahisi habari zote za ufufuo kwa kuonyesha mwili wake , mwili uliooza kama ushahidi, lakini hawakuwa na mwili wowote wa kuonyesha! Kaburi lilikuwa tupu! Je, pengine mitume walikuwa wameuiba mwili? Ni vigumu. Kwa kuzuia uvumi huu usiokuwa wa kweli,kaburi lake Yesu lilikuwa limelindwa vilivyo na Askari waliokuwa wamejihami. Ukichunguza utaona marafiki wake wa karibu walikuwa wametoroka kwa uoga wa kukamatwa kwake na kusulubishwa, haingelikuwa rahisi kwa wavuvi waliokuwa wamevunjika moyo na kutishika, kupambana ana kwa ana na askari waliofunzwa,na wenye ujuzi. Ukweli wa mambo nikwamba ufufuo wa Yesu hauwezi kubatilishwa!

Tena, Yesu ndiye mwenye mamlaka juu ya mauti astahili kusikilizwa.Yesu alithibitisha nguvu zake juu ya mauti, kwahivyo, twahitaji kusikia kile asemacho. Yesu asema ndiye njia ya pekee ya uzimani (Yohana 14:6). Yeye si njia tu; Yeye si mmoja kati ya njia nyingi, lakini Yesu ndiye njia.

Na Yesu huyu asema hivi, “Njoni kwangu,ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo,nami nitawapumzisha’’ (Mathayo 11:28). Huu ni Ulimwengu mzito na maisha ni magumu. Wengi wetu tumefanyiwa madhambi, tumejeruhiwa, na tumetishika kivita. Ni kweli? Sasa, unataka nini? Uregesho ama dini tu? Mwokozi aishiye au Mmoja kati ya “Mitume’’ wengi waliokufa? Uhusiano wa maana au Kafara za utupu? Yesu si chaguo tu, Yeye ndiye chaguo!

Yesu ndiye “dini’’ ya kweli kama unatafuta msamaha (Matendo 10:43). Yesu ndiye “dini’’ ya kweli kama unatafuta uhusiano wa maana na Mungu (Yohana 10:10). Yesu ndiye “dini’’ ya kweli kama unatafuta uzima wa milele Mbinguni (Yohana 3:16). Weka imani yako kwa Yesu kama Mwokozi wako-hutajilaumu! Mwamini yeye kwa msamaha wa dhambi zako-hutaaibika.

Kama ungelitaka kuwa na Uhusiano  na Mungu,fuatisha Maombi haya. Kumbuka ya kwamba kwa kuomba Ombi hili au Ombi lengine lolote lile haiwezi kukuokoa. Ni kwa kumwamini Kristo pekee ndiko kutakuokoa toka dhambini. Ombi hili “Mungu, najua yakwamba nimefanya dhambi kinyume chako na ninastahili adhabu. Lakini Yesu Kristo akaichukua adhabu niliyostahili ili kwa kumwamini yeye nipate kusamehewa. Ninaziacha dhambi zangu kwa kumaanisha na ninaweka imani yangu kwako ili niokolewe. Ahsante kwa Neema yako ya ajabu na kwa msamaha-karama ya uzima wa milele! Amina!’

luka 17

11Yesu alipokuwa akienda Yerusalemu alipitia kati ya Samaria na Galilaya. 12Alipokuwa akikaribia kijiji kimoja, watu kumi waliokuwa na ukoma walikutana naye. 13Wakasimama mbali wakaita kwa nguvu, ``Yesu! Bwana! tuonee huruma!'' 14Alipowaona akawaambia, ``Nendeni mkajionyeshe kwa makuhani.'' Na walipokuwa wakienda, wakapona ukoma wao. 15 Mmoja wao alipoona kwamba amepona, akarudi kwa Yesu akimsifu Mungu kwa sauti kuu. 16Kwa heshima kubwa akajitupa miguuni kwa Yesu akamshukuru. Yeye alikuwa ni Msamaria .
   17Yesu akauliza, ``Hawakuponywa wote kumi? Wako wapi wale tisa wengine? 18Hakuna hata mmoja aliyekumbuka kurudi kumsifu Mungu isipokuwa huyu mgeni?'' 19Akamwambia, ``Inuka, uende; imani yako imekuponya.'' Ufalme Wa Mungu Utakavyokuja
   20Siku moja, Mafarisayo walipomwuliza Yesu Ufalme wa Mungu utakuja lini, aliwajibu hivi: ``Ufalme wa Mungu hauji kwa kuone kana, 21wala watu hawatasema, `Huu hapa' au `Ule kule' kwa maana Ufalme wa Mungu umo ndani yenu.''
   22Kisha akawaambia wanafunzi wake, ``Wakati utafika ambapo mtatamani kuiona siku yangu moja, mimi Mwana wa Adamu lakini hamtaiona. 23Watu watawaambia, `Yule pale' au, `Huyu hapa!' Msiwa kimbilie. 24Kwa maana kama umeme unavyomulika mbingu kutoka upande mmoja hadi mwingine, ndivyo itakavyokuwa siku ya kuja kwangu, mimi Mwana wa Adamu. 25 Lakini kwanza itanipasa nite seke sana na kukataliwa na watu wa kizazi hiki. 26Kama ilivyokuwa nyakati za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa siku ya kurudi kwangu, mimi Mwana wa Adamu. 27Wakati wa Nuhu watu walikuwa wakila, wakinywa, wakioa na kuolewa mpaka siku ile Nuhu alipoingia katika safina. Ndipo mafuriko yakaja yakawaangamiza wote. 28Hata nyakati za Lutu ilikuwa hivyo hivyo. Watu walikuwa wakila, waki nywa, wakifanya biashara, wakilima na kujenga. 29Lakini siku ile Lutu alipoondoka Sodoma, moto ulishuka kutoka mbinguni uka waangamiza wote.30Ndivyo itakavyokuwa siku ambapo mimi Mwana wa Adamu nitakapotokea kwa utukufu.
   31``Siku hiyo, mtu akiwa darini na vitu vyake vikiwa ndani, asiteremke kuvichukua. Hali kadhalika atakayekuwa shambani asirudi nyumbani kuchukua chochote. 32Kumbukeni yaliyompata mke wa Lutu! 33Mtu yeyote anayejaribu kusalimisha maisha yake atayapoteza; na ye yote atakayekuwa tayari kuyapoteza maisha yake atayaokoa. 34Nawaambia, usiku huo watu wawili watakuwa wamelala kitanda kimoja; mmoja atachukuliwa, mwingine ataachwa. 35 Wana wake wawili watakuwa wanatwanga pamoja; mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.'' [36Wanaume wawili watakuwa wanafanyakazi pamoja shambani; mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.] 37Wakamwuliza, ``Haya yatatokea wapi Bwana?'' Akawaambia, ``Pale ulipo mzoga, ndipo tai wanapokutanika.'' Mfano Wa Hakimu Dhalimu

je ni vyema?

MCHUNGAJI wa Kanisa la EAGT lillilopo Mtaa wa Ichenjezya, mjini Vwawa, wilayani Mbozi, Mbeya, Simon Kitwike (48), amehukumiwa kifungo cha miezi sita jela baada ya kukataa kuapa ili atoe ushahidi mahakamani.
Mchungaji huyo, alihukumiwa kifungo hicho na Hakimu Kajanja Nyasige wa Mahakama ya Wilaya ya Mbozi.
Kitwike, aliyevunjiwa nyumba yake mwishoni mwa mwaka jana na kuibiwa mali kadhaa , alifika mahakamani hapo, ili kutoa ushahidi wake, lakini alikataa kuapa kabla ya kutoa ushahidi wake akidai ni dhambi.
Hakimu Nyasige, alimwamuru asome kifungu katika Biblia kinachomtaka asiape mahakamani, ndipo mchungaji huyo alifungua Mathayo 5: 35 na kudai ndicho kinachompa msimamo huo.
Baada ya kusoma kifungu hicho, Hakimu Nyasige alimuuliza tena kama atakuwa tayari kuapa, ili atoe ushahidi, lakini mchungaji huyo aliendelea kubaki na msimamo wake wa kukataa kuapa.
Ndipo hakimu huyo alimsomea kifungu cha sheria na 198 (1) kama ilivyorekebishwa mwaka 2002 kinachokataza mtu kudharau mahakama na kuwa kuendelea kukataa kuapa ni kuvunja sheria na hivyo ametenda kosa la jinai.
Hata hivyo, Hakimu Nyasige aliendelea kumvumilia mchungaji huyo, ili abadili msimamo wake kwa kumwamuru kusoma Biblia hiyo tena Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi 13:1- 5, shahidi huyo alisoma kifungu hicho, lakini alipoulizwa kama amebadili msimamo wake alijibu kuwa hawezi kubadili msimamo wake.
Kutokana na hali hiyo, Hakimu Nyasige aalimtia hatiani kutokana na kumuamuru kwenda jela miezi sita na atatakiwa kufika mahakamani tena baada ya kumaliza kifungo  ili atoe ushahidi wake kwa kesi ya msingi.
Akizungumza na mara baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Mchungaji Mwandamizi wa kanisa hilo aliyejitambulisha kwa jina moja la Mwakasaka, alisema amesikitishwa na hukumu hiyo na kudai mchungaji wake alielewa vibaya vifungu vya Biblia vinavyozungumzia viapo.

NENO NI UZIMA Designed by 5gear Copyright © 2014-2015

Theme images by Jason Morrow. Powered by Blogger.