Kwa neema ya Mungu, leo tunaichambua Biblia tukiwa katika Jengo letu jipya la Kanisa. Ni furaha iliyoje! Tunaendelea tena leo, kujifunza Kitabu cha YOHANA katika Biblia zetu. Leo, tunajifunza YOHANA 8:1-24. Kichwa cha somo letu la leo, ni “KUSHITAKIWA NA DHAMIRI”, hata hivyo, kuna mengi zaidi ya kujifunza katika vipengele tisa:-
(1)WALIKWENDA KILA MTU NYUMBANI KWAKE (MST. 1);
(2)YESU, KIELELEZO KATIKA KUWAHI KANISANI (MST. 2);
(3)UZINZI KOSA KUU (MST. 3-5);
(4)ASIYE NA DHAMBI AWE WA KWANZA KUTUPA JIWE (MST. 5-8);
(5)KUSHITAKIWA NA DHAMIRI (MST. 9);
(6)JINSI YA KUKWEPA HUKUMU (MST. 10-11);
(7)MIMI NDIMI NURU YA ULIMWENGU (MST. 12-15);
(8)MNGALINIJUA MIMI, MNGALIMJUA NA BABA YANGU (MST. 16-20);
(9)NINYI NI WA CHINI MIMI NI WA JUU (MST. 21-24).
(1) WALIKWENDA KILA MTU NYUMBANI KWAKE (MST. 1)
Kabla ya kwenda kila mtu nyumbani kwake, watu hawa walikuwa katika mafundisho hekaluni. Yesu mwenyewe akiwafundisha (YOHANA 1:14). Hapa tunajifunza kwamba Jengo la Kanisa si mahali pa kukaa kama hatuna chumba cha kupanga au ikiwa tumefukuzwa na wazazi wetu au waume zetu. Ikiwa haya yametupata, hatuna budi kuwasiliana na viongozi wetu wa Makanisa ya Nyumbani ili utafutwe uwezekano wa sisi kukaa na kaka zetu au dada zetu katika Kristo, majumbani mwao na siyo kuhamia Kanisani. Nyumba ya Bwana, haina budi kuheshimiwa. Baada ya mafundisho hekaluni, hatuna budi kwenda kila mtu nyumbani kwake. Jambo jingine tunalojifunza hapa ni jinsi Yesu alivyokwenda Mlima wa Mizeituni kuomba ili ajiweke tayari kwa mafundisho yaliyokuwa yanaendelea kesho yake (MST. 2). Mwalimu yeyote wa neno la Mungu, vivyo hivyo inampasa kuomba na kujiandaa vema akiwa peke yake na Mungu wake ili aone matokeo makubwa katika mafundisho yake. Itakuwa vigumu kwetu walimu wa neno au wahubiri, kuona matokeo makubwa ya mafundisho yetu ikiwa tutapenda kuwa sawa na wale tunaowafundisha na kwenda nyumbani tu badala ya kwenda Mlima wa Mizeituni. Mhubiri yeyote hawezi kuwa na mafanikio makubwa ikiwa hatakuwa radhi kujitenga na watu na maisha yake yote akawa Mlima wa Mizeituni.
(2) YESU, KIELELEZO KATIKA KUWAHI KANISANI (MST. 2)
Mapema asubuhi, Yesu aliwahi hekaluni. Hata watu wengine walipomwendea walimkuta yeye amekwisha kufika. Ikiwa sisi ni Wakristo, inatupasa kufuata kielelezo chake Yesu Kristo (YOHANA 13:15). Kuchelewa Kanisani na kukuta ibada imekwisha anza, siyo kufuata kielelezo cha Yesu Kristo. Kuwahi Kanisani kabla ibada haijaanza, kuinaonyesha jinsi tunavyomheshimu Mungu wetu kuliko vyote vingine. Wengi wetu tunawahi katika vituo vya mabasi katika muda tuliopangiwa lakini hatufanyi hivyo katika kuwahi Kanisani. Kipi ni bora; kuachwa na basi au kuachwa na Yesu? Yesu hutuacha ikiwa hatuzingatii kuwahi ibadani. Tukiwahi tuketi na kuomba kimyakimya, tukimwomba Mungu aseme nasi na kulibariki Kanisa lote, na kamwe tusisanze mazungumzo ya kawaida ndani au nje ya jengo la Kanisa. “Watu wote wakamwendea“, ni fundisho kwetu. Jana yake tu walikuwa wakimsikiliza, na asubuhi yake tena wako Kanisani. Hii ndiyo siri ya ushindi kwetu, kuhudhuria kila ibada, na siyo kuja Jumapili tu, au Jumatatu tu.
(3) UZINZI KOSA KUU (MST. 3-5)
Tangu mwanzoni kabisa, uzinzi limekuwa ni kosa kuu lililoambatana na adhabu kali (MWANZO 38:24; AYUBU 31:9-11; WALAWI 20:10; KUMBUKUMBU 17:5). Kulingana na waandishi wa historia, Wayahudi walimwadhibu mzinzi kwa kumvua nguo na kumwacha karibu sawa na uchi kisha walimfunga mikono nyuma kwa kamba, na kumtupa chini kutoka katika jukwaa la urefu wa futi 12, kisha wakamtupia mawe makubwa kifuani hadi alipokufa. Kwa mwanamke mzinzi, mawe hayo yalilengwa kwenye matiti yake. Maandiko yanasema, yeye aziniye na mwanamke HANA AKILI KABISA na hata akisamehewa dhambi, fedheha yake haifutiki (MITHALI 6:32-33). Hata leo uasherati au uzinzi haupaswi kamwe kutajwa kwa yeyote anayejiita Mkristo. Kufanya uasherati au uzinzi haupaswi kamwe kutajwa kwa yeyote anayejiita Mkristo. Kufanya uasherati au uzinzi humfanya mtu kuunga na kahaba na kujitoa katika mwili wa Kristo (1 WAKORINTHO 6:15-18; WAEFESO 5:3).
(4) ASIYE NA DHAMBI AWE WA KWANZA KUTUPA JIWE (MST. 5-8)
Mafarisayo na Waandishi walikuwa ni watu waliojikinai kwamba ni wenye haki. Hata hivyo, walikuwa ni makaburi yaliyopakwa chokaa (MATHAYO 23:27-28). Pamoja na wao kumleta mzinzi mble ya Yesu na kumshitaki, Yesu alitaka kwanza kila mmoja wao aangalie maisha yake kwanza kabla ya kuyaangalia ya wengine, na kutoa kwanza boriti iliyo ndani ya jicho lake mwenyewe, kabla ya kutazama kibanzi kilicho ndani ya jincho la mwingine (MATHAYO 7:3-4; WARUMI 2:21-22). Watu wengi leo wako kama Waandishi na Mafarisayo. Ni wepesi kuona makosa ya wenzao kabla ya kuona makosa ya kwao kwanza. Hatupaswi kuwa hivi. Tuendelee kutafakari mistari hii kwa makini. Yesu hapa aliambiwa “Nawe wasemaje?“ akiwa katika kujaribiwa ili wapate sababu ya kumshitaki. Kama angeamuru mwanamke yule apigwe kwa mawe, wangemshitaki kwamba amejitwalia mamlaka ya liwali (LUKA 20:20). Kama angeamuru aachiwe huru na kusema wasimpige kwa mawe (kama walivyotarajia), wangemshitaki kwamba yeye ni kinyume na desturi na sheria walizopewa na Musa (MATENDO 6:11-14). Alipopewa swala hili lenye mtego, aliinama BILA KUJIBU NENO. Katika kutulia kimya, ndipo Roho wa Mungu hutupa hekima ya jinsi ya kujibu maswali hayo (YAKOBO 1:19; ISAYA 52:12). Hatimaye aliandika kwa kidole chake katika nchi. Baadhi ya nakala za Kiyunani za maneno haya zinasomeka, “Enos hekastou auton tas hamartias“ kwa kumaanisha, “akaandika kwa kidole chake katika nchi dhambi za kila mmoja wao“. Kila mmoja akajiona naye ni mwenye dhambi.
(5) KUSHITAKIWA NA DHAMIRI (MST. 9)
Kila mwanadamu ndani ya nafsi yake, kuna kitu kinachoitwa dhamiri. Tunapofanya makosa au dhambi, dhamiri yetu hutushitaki mara baada ya kusikia neno linalofichua dhambi zetu (WARUMI 2:15; 1 TIMOTHEO 4:2). Dhamiri hii imewekwa na Mungu ili kutusaidia kutubu dhambi zetu mara tunaposhitakiwa na dhamiri. Mwelekeo wetu baada ya kushitakiwa na dhamiri, ni wa muhimu sana katika kutufanya tupate uzima au mauti. Waandishi na Mafarisayo hawa baada ya kushitakiwa na dhamiri zao walikuwa na mwelekeo mbaya – “walitoka mmoja mmoja“ na kumwacha Yesu. Hili lilikuwa kosa kubwa. Walipaswa kumsogelea Yesu zaidi na kutubu dhambi zao! Dhamiri zikitushitaki halafu tukawa tunapingana na dhamiri hiyo, mwisho dhamiri hiyo hufa na mauti kutusogelea. Vivyo hivyo ni muhimu kufahamu pia kuwa, dhamiri hufundishika. Kabla ya mafundisho mtu anaweza kushuhudiwa kwamba kufanya hili au lile siyo dhambi lakini baada ya kufundishwa hamiri ile humshuhudia kuwa ni dhambi kama ilivyokuwa kwa Mafarisayo hawa. Mwanamke mzinzi huyu, yaye hakutoweka, ingawa likuwa na nafasi ya kukimbia , bali alimkaribia Yesu na kutubu na akamwita Yesu “Bwana“ (MST. 11). Mwanamke huyu alibaki na Yesu peke yake. Siku inakuja kwa kila mmoja wetu na kila mmoja atabaki na Yesu peke yake katika hukumu! Dhambi zetu zitaandikwa kwetu kwa kidole kama wakati wa Belshaza (DANIELI 5:1-30).
(6) JINSI YA KUKWEPA HUKUMU (MST. 10-11)
Tunaweza kukwepa hukumu, kwa kutubu dhambi zetu, na kumaanisha moyoni kutokuzitenda tena, au siyo hukumu bado inatukalia (ISAYA 55:7; MITHALI 28:13). Kutubu dhambi kwa taratibu tu za kidini za kila wiki na halafu tunaendelea kuzitenda, namna hii siyo jinsi ya kukwepa hukumu.
(7) MIMI NDIMI NURU YA ULIMWENGU (MST. 12-15)
Jua moja hutoa nuru katika ulimwengu wote. Kwa jinsi hiyohiyo, Yesu anaitwa “JUA LA HAKI“(MALAKI 4:2). Mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni MMOJA Kristo Yesu, kama Jua lilivyo moja tu wakati wote (1 TIMOTHEO 2:5). Yesu kama Jua la Haki, ndiye pekee anayetuangazia njia. Tukimfuata Yesu kwa kulifuata Neno lake, tunaifuata nuru, hivyo hatuwezi kwenda gizani kamwe. Ushuhuda huu ni kweli, maana Yesu ndiye Kweli (YOHANA 14:6).
(8) MNGALINIJUA MIMI, MNGALIMJUA NA BABA YANGU (MST. 16-20)
Hatuwezi kudai kwamba tunamjua Mungu ikiwa hatumjui Yesu anayewaokoa watu wake na dhambi zao (MATHAYO 1:21). Ikiwa hatujamfanya Yesu kuwa Mwokozi wetu hatuna haki ya kumtaja Mungu kwamba ni Baba yetu aliye mbinguni. Kumkataa Yesu ni kumkataa Mungu Baba na kukosa uzima wa milele (YOHANA 3:36; LUKA 10:16; 1 YOHANA 5:11-12).
(9) NINYI NI WA CHINI MIMI NI WA JUU (MST. 21-24)
Sisi wanadamu ni wa chini Yesu ni wa juu. Alitoka juu na kuja kwetu chini, kisha akapaa kurudi huko juu. Ni yeye pekee wa kutueleza jinsi ya kufika mbinguni. Tusipomfuata tutakufa katika dhambi zetu na kuangamia. Wakati wote tukumbuke pia kwamba pamoja na elimu, karama, maarifa au utajiri tulionao SISI NI WA CHINI na Yesu NI WA JUU. Hakuna haja ya kujivuna. Pasipo yeye wa juu sisi wa chini hatuwezi kufanya neno lolote (YOHANA 15:5). Siku zote tukumbuke kutokujifumainia nafsi zetu bali tumtumainie yeye katika yote.
…………………………………………………………………………………………………………………………………..
Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni? Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14). Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27). Kinyonge ni kipi? Ni yule anayetenda dhambi. Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge! Je, wewe ni mtakatifu? Jibu ni la! Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13; YOHANA 14:6). Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii? Najua uko tayari. Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni; “Mungu Baba asante kwa ujumbe huu. Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi. Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha. Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo. Bwana Yesu niwezeshe. Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu. Amen”. Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni. Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu. MUNGU AKUBARIKI !!!
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .
Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe.