Vichwa vya Habari

BARAKA.


Leo tutakuwa tunaangalia maana ya neno BARAKA. Watu wengi tumezoea kulitumia,  limezoeleka, limekuwa  neno la kawaida, na rahisi  kulitamka. Mtu ukimfanyia chochote, kikubwa au kidogo, utasikia ‘Mungu akubariki‘!.  Sielewi kama huwa tunaelewa kile tunachomaanisha, na pia sielewi kama huwa tunaelewa kile wale wanaotuambia huwa wanamaanisha..
Sasa tuanze somo hili kwa maandiko katika Mwanzo 12:1-3, yasemayo:
“Bwana akamwambia Abram, toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha, nami nitakufanya wewe kuwa Taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako, nawe uwe baraka, nami nitawabariki, naye akulaaniye nitamlaani, na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa“.
Mungu alimwambia Abram, [wakati hajawa Ibrahim] mambo mengi mno, na kama angekuwa hana bidii katika mambo ya Mungu, basi nadhani angeishia kusikia sauti ya Mungu tu, halafu hakuna matokeo yoyote ambayo yangetokea.
Isaya 1:19-20, “Kama mkikubali na kutii, mtakula mema ya nchi, bali kama mkikataa na kuasi mtaangamizwa kwa upanga, maana kinywa cha Bwana kimenena haya”
Mstari huu ni muhimu sana, una maelekezo muhimu sana hata kuweza kufikia kile kinachoitwa Baraka: anasema kama tutakubali, halafu tutii.  Ndugu mpendwa,  hakuna anayemkataa Mungu muumba wake, labda kichaa;  labda mpumbavu ndiye husema hakuna Mungu. Lakini kila mtu anakubali, kwenye mikutano wanakubali.  Wahubiri wanapomaliza kuhubiri huuliza wangapi wanamkubali Bwana Yesu  katika maisha yao, karibu uwanja wote, wanakubali, hata kama hawainui mikono, lakini mioyoni huwa kuna sauti inasema ‘lakini ni kweli’, hiyo wanakubali. Tatizo liko wapi? . . . KUTII! Hapo ndipo penye matatizo, na wala shetani hahangaiki kukuzuia usikubali, hilo anasema wewe kubali tu, tena pengine hata hatujui pale tunapoambiwa BWANA asifiwe, tunasema, “Amina!”. Maana yake “Amina” ni “iwe hivyo”. Kwa hiyo kukuacha ukubali hilo ni sawa, lakini tatizo ni hatakubali UMTII   MUNGU.
Ibrahim pamoja na maneno mazuri aliyoambiwa na Mungu wake, ilikuwa lazima afanye kazi ya ziada kupokea kile alichokuwa amekisema Bwana.
Ebr 6:13-15, ” Kwa maana Mungu alipompa Ibrahim ahadi, kwa sababu alikuwa hana mkubwa kuliko yeye mwenyewe wa kumwapa, aliapa kwa nafsi yake, akisema, Hakika yangu kubariki nitakubariki, na kuongeza nitakuongeza. Na kwa hivyo kwa kuvumilia akaipata ile ahadi“.
Tumeona Mungu akimsemea Ibrahim  mambo mazito, kama vile ambavyo Mungu amesema mambo mazito kwa ajili yetu, maana wote walio katika Kristo ni warithi wazirithio ahadi za Ibrahim. Wengi wetu tunazifahamu ahadi zilizoko kwenye Neno lake, wengi huzikariri katika kuomba, nyingi tu nzuri nzuri, hata zingine huwafanya watu ambao hawajaokoka waamue kuokoka ili wazipate.
Mpendwa, naomba unipe masikio yako;  Hapo juu tumeona neno zito kuwa Mungu aliapa kwa nafsi yake. Hii ina maana hawezi kusema uongo kama neno lisemavyo mahali fulani, kuwa Mungu si mtu aseme uongo, wala si mwanadamu ajute. Kujuta ni tabia ya watu;  tena ni tabia  ya watu kusema uongo, ndio maana tunatakiwa tuishi rohoni, tuache tabia za kiutu za ubinadamu.
Biblia inasema IBRAHIM KWA KUVUMILIA AKAIPATA ILE AHADI.
Hapo napo pana matatizo.  Kwa kuvumilia nini? Hakuna kitu kizuri kinachovumiliwa, mtu akiniambia “vumilia tu unywe chai hii!”;  mara moja nitajua chai ina matatizo hii, mara ninajua haina sukari.
Sitaingia kwa ndani kukuambia kuwa alivumilia nini? Ebu fikiri hili: Wataalam wanasema tangu Mungu alipomwambia atampatia mtoto kutoka katika viuno vyake ilimchukua miaka 25. Je! Ni mangapi yalisemwa wakati huo wa kusubiri?   Watu walisema walivyoweza, kila aliyeweza kusema alisema, huwa nawaambia watu kuwa kusema hakuhitaji fedha za kununulia betri, wala kuweka umeme, hapana. Ni pale mtu anapokula chochote akashiba, inaweza kuwa mhogo, ugali, mhindi, n.k.
Ni ombi langu kwako; ebu vumilia, tulia mngojee Bwana aliyesema ni mwaminifu, kile alichokuambia atatimiza tu!
Mwanzo 22:15-18, “Malaika wa Bwana akamwita Ibrahim mara ya pili kutoka mbinguni, akasema, nimeapa kwa nafsi yangu asema Bwana, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee, katika kubariki, nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani, na mzao wako utamiliki mlango wa adui zao. Na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia, kwa sababu umeitii sauti yangu.”
Bwana hakumwambia kuwa “nitakubariki kwa kuwa unaisikiliza sauti yangu”, hakumwambia kwa kuwa “nimekuchagua tu ili nikubariki”, hakumwambia “kwa kuwa umeamua kuwa na dini kubwa ya pili, au ya tatu”….! Hakumwambia “kwa sababu umeomba usiku kucha”, “kwa kuwa unanena kwa lugha kama cherehani”. Hapana. Bali ni “Kwa kuwa UMETII SAUTI YANGU“.
Nimesema kuwa hapa kwenye Kutii ndipo penye matatizo makubwa.  Na Isaya amesema kama tukitii tutakula mema ya Nchi, hakusema “kukitafuta mema ya nchi kwa kuombewa tutayapata”, hakusema “tukiwekewa mikono tutapata mema ya nchi”, hapana. Bali ni “kama mkikubali na kutii“.
Nilipokuwa natafakari maana ya BARAKA, niliona kwa ndani zaidi kuwa Kubarikiwa ni:
“Kukubaliwa na Mungu”.  “Kuitikiwa na Mungu”. “Kushughulikiwa na Mungu”. “Kupiganiwa na Mungu”.  “Kutetewa na Mungu”.  “Ni kukingwa na Mungu”. “Kulindwa na Mungu”.  “Ni kulikuza jina Lako”.  “Ni kukufanya wewe mwenyewe uwe baraka”.
Wanaokubariki, utawafanya wabarikiwe. Wanaokulaani, yeye atawalaani. Kwa lugha nyingine vita si yako, ni yake. Wewe utakuwa sababu ya watu wengine kubarikiwa, kunzia kwa watoto wako, wajukuu zako, na majirani zako, hata Taifa lako pia.
Dan 4:10-12, “Njozi  za kichwa changu kitandani mwangu zilikuwa hivi, naliona na tazama, palikuwa na mti katikati ya nchi, urefu wake mkubwa sana, mti ule ukakua, ukawa na nguvu, urefu wake ulifika mpaka mbinguni, , na kuonekana kwake mpaka mwisho wa dunia, majani yake yalikuwa mazuri, na matunda yake mengi, na ndani yake chakula cha kuwatosha watu wote, wanyama wa kondeni walipata uvuli chini yake, na ndege wa angani walikaa katika matawi yake. Kila kitu chenye mwili kilipata chakula kwake.”
Ebu  tuendelee kuona baraka maana yake nini, ambayo hailetwi kwa kutabiriwa tu, kisha tukae tukingojea maadamu watumishi wa Mungu wameshatutabiria, hata wangetuwekea mikono yote miwili, kisha waongeze na miguu yote miwili, kama hatutakuwa WAVUMILIVU,  na WATII, Nasema kwa ujasiri wote kuwa tutakuwa tunatwanga maji kwenye kinu!
Yakobo 5:7-11,  “Kwa hiyo ndugu vumilieni hata kuja kwake Bwana, Tazama mkulima hungoja mazao ya nchi, yaliyo ya thamani, huvumilia kwa ajili yake, hata yatakapopata mvua ya kwanza na ya  mwisho. Nanyi vumilieni, mthibitishe mioyo yenu, kwa maana kuja kwake Bwana kunakaribia. Ndugu msinung’unikiane, msije mkahukumiwa, angalieni, mwamuzi amesimama mbele ya milango. Ndugu watwaeni manabii walionena kwa jina la Bwana, wawe mfano wa kustahimili mabaya, na wa uvumilivu. Angalieni twawaita heri wao waliosubiri. Mmesikia habari ya subira yake  Ayubu, mmeuona mwisho wa Bwana ya kwamba Bwana ni mwingi wa rehema, mwenye huruma.”
Maandiko hayo yanaendelea kuonyesha wazi kuwa uvumilivu ni jambo la muhimu kabisa katika safari yetu ya kuelekea Mbinguni. Pale tunapokosa uvumilivu kuna jambo hutokea.Tunaposhindwa kumngojea Bwana huwa tunashawishika kutafuta na kushika njia nyingine. Hapo manung’uniko mengi na kulaumiana kwingi hutokea.
Wafilipi 2:12-13, “Basi wapendwa wangu kama vile mlivyotii siku zote, si wakati mimi nilipokuwapo tu, bali sasa zaidi sana mimi  nisipokuwapo, utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka. Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema”.
Bado neno linaendelea kukazia kuhusu utii, neno linasema “tutimize”. Kuna kitu tunatakiwa kutimiza. Bila hivyo hatuwezi kuziona ahadi za Mungu tulizoahidiwa, au tunazozisoma katika Biblia. Paulo anasema wakati alipokuwepo  pamoja nao, walitii, lakini sasa anasema asipokuwapo, wao watii zaidi na kutetemeka. Wako watu wanaomtii Mungu wakati Mchungaji wake yupo, wakati kiongozi wa kanisa yupo. Lakini mtu huyo akiwa peke yake, hakuna utii wowote anaouonyesha kwa Mungu. Kumbuka Yusuph alikuwa peke yake kule Misri, tena wakati mke wa Potifa alipomtaka hakuwepo mtu mwingine, ila yeye alikataa kabisa kumtenda Mungu dhambi!
Ndugu zangu Baraka tele tumeahidiwa na Mungu wetu, ama kwa unabii, ama kwa Neno lake, ni za kwetu kabisa,.Lakini zitakuwa za kwetu pale tutakapomtii Mungu wetu; Pale tutakapofanya kile Mungu anatutaka tufanye. Naomba Bwana atupatie roho ya utii, ili tuweze kumtii Mungu wetu.
Namalizia nikikutakia baraka tele, juu yako mwenyewe, juu ya watoto wako, juu ya majirani zako, kiwe chakula nyumbani mwako, cha kimwili na cha kiroho, cha kuwatosha watu wote walio pamoja na wewe.
Nitaendelea kukuombea mpaka baraka zilizotamkwa katika Biblia zikufikilie, pamoja na maombi yangu, lakini nawe umeona unachotakiwa kufanya:

NENO NI UZIMA Designed by 5gear Copyright © 2014-2015

Theme images by Jason Morrow. Powered by Blogger.