Vichwa vya Habari

UCHUMI WA UFALME WA MBIINGUN

UCHUMI WA UFALME WA MBIINGUN


Mama mmoja aliyekuwa na watoto sita (lakini alikuwa hajaolewa), alipelekwa na mwenzake kwa Askofu wa dhehebu lao ili wapate msaada kwa kuwa walikuwa na maisha ya shida sana. Yule mama pamoja na watoto wake sita walikuwa wanakaa katika nyumba ya makaratasi, na hawakuwa na chakula cha kutosha.
Askofu alimuuliza yule mama amewapateje wale watoto wote sita na huku alikuwa hajaolewa.
Yule mama akajibu akasema; "Mtoto wa kwanza nilimpata kwa kuwa nilikuwa nataka mtoto, niliona nazeeka bila ya kuolewa nikaona nizae mtoto, Lakini mtoto wa pili nilimpata wakati nilipokuwa natafuta chakula cha mtoto wa kwanza. Mtoto wa tatu nilimpata nilipokuwa natafuta chakula cha watoto wawili niliokuwa nao. Na hali hii imeendelea mpaka sasa nina watoto sita – na sijui nitaendelea na hali hii mpaka lini".
Ni wazi kabisa si mapenzi ya Mungu huyu mama aishi maisha ya namna hiyo. Vikwazo vya uchumi ambavyo vilimzunguka yule mama na watoto wake vilitoka kwa ibilisi.
"Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa ……."(Hosea 4:6). Maneno haya yaliyosemwa na Mungu kwa kinywa cha Nabii Hosea yana ukweli ndani yake hata hivi leo. Watu wengi sana siku hizi wanaangamizwa, wanadhulumiwa, wanahuzunishwa na maisha kwa sababu tu wamekosa kuyajua maarifa ya Mungu yaliyomo katika Neno lake.
Wakati fulani nilikuwa nafundisha katika semina moja juu ya uhusiano wa maendeleo ya mtu na Wokovu, na wakati wa kipindi cha majadiliano Mchungaji mmoja akatueleza habari iliyotufikirisha sana.


Akasema ya kuwa katika kanisa alilokuwa analihudumia miaka ya nyuma aliwahi kufuatwa na mama mmoja wa usharika huo ambaye alikisema ya kuwa yeye alikuwa mmoja wa wakina mama thelathini ambao hawashiriki chakula cha Bwana kwa kuwa walikuwa wanaishi hapo mjini kwa njia za umalaya. Ombi lao kwa mchungaji wao lilikuwa ni kwamba akiweza kuwasaidia kupata kazi za halali waache umalaya. Wao wametafuta kazi bila ya mafanikio, na wanafanya umalaya si kwa sababu wanapenda, bali kwa kuwa hawakuwa na njia nyingine ya kupatia fedha.
Ni jambo la kumshukuru Mungu, ya kuwa mchungaji yule aliweza kuwatafutia kazi wale wakina mama wote katika kiwanda kimoja, na maisha yao yakabadilika wakaacha umalaya, na kuishi maisha ya kikristo yenye ushuhuda.
Ni watu wangapi ambo wanaishi maisha yao kinyume na maadili ya kikristo ili kupata fedha za kuwasaidia kila siku? – Ni wazi kuwa ni wengi. Je! hawawezi wakapata riziki yao bila kudhulumu au kuiba au kudanganya au kuzini? – Ni wazi kuwa wanaweza. Sasa, ni kwa nini wanaishi kwa jinsi hiyo?
Jambo ambalo watu wanahitaji kujua ni kuwa baba wa uongo yaani shetani amewadanganya kwenye mawazo ya kuwa hakuna njia nyingine ya halali ya kupatia fedha isipokuwa hizo. Na shetani anausimamia uongo huo ili uonekane kuwa ni kweli kwa kuwawekea watu hasa wakristo vikwazo vigumu vya kiuchumi.
Unaweza ukawa unajiuliza vikwazo hivyo ni vipi? Vikwazo hivi vinatofautiana katika watu mbalimbali na mahali mbalimbali. Kuna watu wengine wataona hakuna mradi wa halali wanaoufanya unaofanikiwa. Mwingine miradi yake inafanikiwa, lakini fedha yote inaishia kutafutia matibabu ya magonjwa yaliyomo ndani ya nyumba yake ambayo hayaishi.
Mwingine anapata magari mengi, lakini hayaishi kupata pancha na kuharibika au kuanguka. Mara nyingi utawasikia watu wa jinsi hii wanasema wana mkosi. Kwa kweli si mkosi bali vikwazo vya kiuchumi toka kwa shetani ili ushindwe maisha na UANZE KUTAFUTA MAISHA MAZURI KWA NJIA ZILIZO KINYUME NA MAADILI YA KIKRISTO YALIYO MATAKATIFU.

Jambo ambalo wakristo wengi hawalifahamu
 Mimi na mke wangu miaka ya mwanzo tulipookoka hasa mwaka 1984 na 1985 tulikumbana na vikwazo vigumu sana vya kiuchumi. Tuliona jinsi maisha yalivyokuwa yanarudi nyuma – fedha tuliishiwa, chakula tuliishiwa, nguo tuliishiwa, vitu ndani vilianza kuharibika na hatukuwa na fedha za kuvitengenezea. Tulijaribu kulima bustani za mboga, hazikufanikiwa. Tulijaribu kupika chapati za kuuza, hazikununuliwa zikaharibika tukazitupa.
Kwa kifupi tuliona maisha ya wokovu kuwa ni magumu, ya shida na ya kimaskini sana. Tulishindwa hata namna ya kuwasaidia ndugu zetu vizuri. Hali hii ilitutia uchungu sana. Watu hawakufahamu ya kuwa hali hii ilikuwa inatunyima amani ya kweli ya wokovu – kwa kuwa tulijitahidi kuwachangamkia wote ili kuficha mapambano tuliyokuwa nayo kimaisha.
Ilikuwa ni vigumu sana kuishi maisha ya ushuhuda mzuri wa kikristo katikati ya mahitaji makubwa kama hayo tuliyokuwa nayo.
Tulijua kuwa Zaburi 23:1 inasema, "Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu". Lakini tulikuwa tumepungukiwa na vitu vingi vya lazima katika maisha. Hatukufahamu kwa nini sisi kama kondoo wa Kristo tulikuwa tumepungukiwa namna hiyo!
Tulikuwa tunasoma lakini tunashindwa kumwelewa Mtume Paulo alipokuwa anasema katika Wafilipi 4:12 kuwa; "najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yo yote, na katika mambo yo yote, nimefundishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa".
Tuliona ya kuwa Mtume Paulo aliweza kuwa na amani na ushindi katika hali yo yote aliyokuwa nayo – hata katika upungufu. Sisi tulikosa amani tulipokuwa tumepungukiwa! Na hili jambo lilitusumbua sana.
Tulikuwa tunafurahi tunaposoma mstari kama ufuatao; " …..vyote ni vyenu …. Vile vilivyopo sasa, au vile vitakavyokuwapo; vyote ni vyenu, nanyi ni wa Kristo, na Kristo ni wa Mungu"(Wakorintho 3:21,22). Tulikuwa tunafurahi kwa kuwa maneno haya yanatupa uhalali wa kumiliki vitu vilivyo vya Mungu. Kwa mfano Hagai 2:8 inasema "Fedha ni mali yangu, na dhahabu ni mali yangu, asema Bwana wa Majeshi." Pia, Zaburi 24:1 inasema "Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana …" Lakini jambo lililotusumbua ni kwamba ingawa mistari hiyo ilitupa umilikaji juu ya fedha, dhahabu na vyote viijazavyo nchi ili tuvitumie – SISI HATUKUWA NAVYO WALA HATUKUJUA TUTAVIPATAJE!
Tulifahamu ya kuwa ni mapenzi ya Mungu tufanikiwe katika mahitaji ya kiroho na mahitaji ya mavazi, chakula, na malazi; soma kitabu cha 3 Yohana 1:2. Kwa hiyo tulikuwa na hamu kubwa ya kufanikiwa.
Tulitamani sana kuona maneno ya Wafilipi 4:19 yanatimia kwetu – nayo yanasema hivi;
"Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu".Hali hii ilitufanya tuingie katika maombi mazito, ili kumuuliza Mungu njia na namna ya kuondokana na hali tuliyokuwa nayo.
Mambo makubwa matatu yafuatayo, Roho wa Mungu alituambia kuwa ni chanzo cha matatizo yaliyokuwa yanatukabili: Alituambia yafuatayo:
Kuwa, ingawa tumezaliwa mara ya pili na kuingizwa katika ufalme wa Mungu – tulikuwa bado tunategemea utaratibu wa uchumi wa duniani badala ya kutumia na kutegemea utaratibu wa uchumi wa mbinguni;
Kuwa, tulikuwa tunapenda kupokea bila ya kuwa watoaji, na pia tulitaka kuvuna tusichokipanda. Roho Mtakatifu aliuliza swali, Je! unaweza kwenda kwenye bustani yako kuchuma nyanya huku ukijua kuwa hujawahi kupanda nyanya? Ni wazi kuwa jibu lilikuwa ni hapana.
Kuwa, hatujafahamu ya kuwa adui yetu ibilisi ndiye chanzo cha mahangaiko na mafadhaiko yaliyoambatana na kupungukiwa mahitaji katika maisha. Na pia tulikuwa hatutumii silaha tulizopewa ili kuzivunja kazi za ibilisi katika maisha yetu.
Baada ya kupokea majibu hayo kutoka kwa Mungu, tulitubu na kuomba msamaha. Tuliendelea kumwomba Mungu atufundishe na atuongoze katika kuishi maisha ya kutumia na kutegemea utaratibu wa uchumi wa ufalme wa mbinguni.
Mafundisho tuliyoyapata yalituondoa katika mahangaiko ya kupungukiwa na kutuingiza katika furaha na amani ya mafanikio NDANI YA KRISTO.
Ndiyo maana tumechukua hatua hii chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu kukushirikisha baadhi ya mafundisho hayo ili ikiwa umo katika hali ya mahangaiko ya kupungukiwa na mahitaji muhimu ya maisha upate msaada wa kuondokana nayo.
Kumbuka ni mapenzi ya Mungu ndani ya Kristo kuwa ufanikiwe na uishi maisha ya ushindi katika maeneo yote ya maisha yako na katika siku zote utakazoishi juu ya nchi.

Mwenye haki ataishi kwa imani
 Nabii Habakuki aliishi katika kipindi kilichokuwa kigumu sana kiuchumi. Hali hii iliwafanya watu wengi kuingia katika dhuluma, udanganyifu na mambo mengine maovu ili tu waweze kuishi.
Lakini kilichoumiza moyo wa Nabii Habakuki ni kuona kuwa kulikuwa na watu wachache ambao hawakufuata mambo maovu – lakini waliishi maisha magumu na kuonewa na matajiri wa wakati huo. Hali hii ilimfanya Nabii Habakuki aingie katika maombi ya kumlalamikia Mungu, huku akihitaji kujua mpango wa Mungu juu ya watu waliosimama upande wake. Soma kitabu cha Habakuki sura ya 1 na 2.
Kati ya jibu ambalo Mungu alimpa Nabii Habakuki juu ya maisha ya watu wake katikati ya hali ngumu ya uchumi ni maneno haya;
"….mwenye haki ataishi kwa imani yake" (Habakuki 2:4)
Huu ndio uliokuwa mpango wake kwa watu wake wakati ule ili uwasaidie kuishi katikati ya dhuluma na maovu yanayotokana na hali ngumu ya uchumi.
Katika siku hizi za mwisho, kumetabiriwa kutokea tena hali ngumu ya uchumi inayoambatana na dhuluma pamoja na maovu mbalimbali. Mungu amekwisha andaa mpango mzuri kwa ajili ya wote watakaoipokea na kuikiri injili ya Kristo inayookoa. Na mpango huu ni sawa na ule aliopewa Nabii Habakuki.
Kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, Mtume Paulo alisema maneno muhimu yafuatayo:
" Kwa maana siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia. Kwa maana haki ya Mungu inadhihirishwa ndani yake, toka imani hata imani; kama ilivyoandikwa , MWENYE HAKI ATAISHI KWA IMANI" (Warumi 1:16-17). Huu ndio mpango wa Mungu kwa watu wote wanoipokea Injili ya Kristo na kuokolewa. Katikati ya dhuluma,wizi, uasherati na maovu mbalimbali yanayoambatana na hali ngumu ya uchumi iliyopo sasa na ile itakayotokea miaka si mingi iliyo mbele yetu kuanzia sasa – Mungu anawataka watu waishi kwa kufuata mpango wake – WAISHI KWA IMANI.
Kuishi kwa Imani ndiyo utaratibu wa uchumi wa mbinguni ambao kila mkristo anatakiwa kuufuata akitaka kuishi maisha ya mafanikio na matakatifu katikati ya hali ngumu ya uchumi – badala ya kujikuta amewezwa na masumbufu ya maisha haya.
Inasikitisha kuona kuwa wakristo wengi wameyatafsiri na kuyatumia vibaya maneno haya "kuishi kwa Imani". Na kwa ajili hiyo mpango wa Mungu uliomo ndani ya maneno haya haujaeleweka na wengi.
Wakristo wengine wanafikiri kuishi kwa imani ni kuacha kazi wanazozifanya na kuanza kuishi maisha ya omba omba na ya kubahatisha. Wamesahau kuwa biblia inasema mtu asipofanya kazi asile – soma 2Wathesalonike 3:6 – 12.
Ingawa kuna wakristo ambao wamelifanya neno hili "kuishi kwa Imani" lisieleweke vizuri; hali hii haiwezi wala haitaweza kubadilisha mpango wa Mungu uliomo ndani yake.
Mawazo yetu siyo mawazo ya Mungu; njia zetu si njia za Mungu; na mipango yetu si mipango ya Mungu. Hakuna njia ya mkato kwa mkristo safi ya kufanikiwa katika maisha, isipokuwa ni kwa kuishi ndani ya mpango wa Mungu uliofunuliwa katika Kristo Yesu.
"Mwenye haki ataishi kwa imani" maana yake nini? "Mwenye haki" maana yake Mkristo, au Mtakatifu, au Mwongofu, au Mteule, au Aliyeokoka. Kwa hiyo tunaweza kusema Mkristo ataishi kwa imani.
Pia tunasoma katika Waebrania 11:1 ya kuwa:"Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana"
Tena imeandikwa katika Warumi 10:17 ya kuwa;"Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo".
Tena imeandikwa katika Yakobo 2:26 ya kuwa;"Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa".
Kwa mistari hiyo michache na mingine mingi iliyomo katika Biblia inatusaidia kujua ya kuwa "Mwenye haki ataishi kwa imani"maana yake kila mkristo anatakiwa kuishi kwa kuwa mtendaji wa Neno la Kristo na siyo msikiaji tu – kila wakati na katika kila eneo la maisha yake.
Roho Mtakatifu alipokuwa anatufundisha haya mimi na mke wangu, tulijua hakika ya kuwa tunatakiwa kutumia muda mwingi kulisoma na kulitafakari Neno la Kristo, ili tuweze kulitenda Neno hilo katika maisha haya. Tulianza kusoma Neno la Mungu na vitabu mbalimbali vilivyoandikwa na watumishi wa Mungu na bado tunaendelea kufanya hivi hata leo, na tumeona mabadiliko makubwa katika maisha yetu – maana mahangaiko tuliyokuwa nayo yametoweka kwa jina la Yesu Kristo! Sasa tunaishi katika maisha ya ushindi na amani ndani yake Kristo.
Tatizo ambalo mtu analipata anapookoka, ni namna ya kuishi katika maisha mapya ya wokovu (2Wakorintho 5:17)
Biblia inatuambia ya kuwa sisi ni raia wa nyumbani mwake Mungu (Waefeso 2:19). Pia inatuambia kuwa sisi si wa ulimwengu huu (Yohana 17:14). Kwa hiyo maisha yetu hayatakiwi kuongozwa na utaratibu wa hapa duniani.
Kuna tofauti kati ya utaratibu wa uchumi wa duniani na utaratibu wa uchumi wa ufalme wa mbinguni. Ingawa sisi tulio wake Kristo tumo humu ulimwenguni hatutakiwi kuishi kwa kutegemea utaratibu wa uchumi wa dunia hii unaoyumba, bali tutegemee utaratibu wa uchumi wa ufalme wa mbinguni – usioyumba wala kubadilikabadilika kwa kuwa umejengwa juu ya mwamba imara – Neno la Kristo.
Wakristo wengi kwa kutokujua hili wamejikuta wakipata shida ya kutaka kuwatumikia mabwana wawili – yaani Mungu na Mali ambapo Yesu Kristo alikwishasema haiwezekani. Matokeo yake ni kupoteza ushuhuda wa kikristo na kuishi maisha ya mahangaiko.
Kutegemea utaratibu wa uchumi wa dunia hii kuna shida sana kwa kuwa uchumi huo ukiyumba kidogo, na wewe unayumba kimaisha. Lakini ukiutegemea utaratibu wa uchumi wa ufalme wa mbinguni huwezi kuyumba wakati uchumi wa dunia ukiyumba – kwa kuwa tumaini lako halimo mikononi mwa dunia na wanadamu – bali ndani ya Kristo Yesu ambaye ni mwamba imara usiotikisika.

Mwl. Mwakasege

No comments:

Post a Comment

NENO NI UZIMA Designed by 5gear Copyright © 2014-2015

Theme images by Jason Morrow. Powered by Blogger.