***JIFUNZE KWA EDOMU USIDANGANYWE NA KIBURI***
Obadia ni kitabu ufupi katika Agano la Kale, kina sura 1 na mistari 21 tu! Kinatangaza adhabu ya Mungu dhidi ya taifa la kale na lililosahaulika kwa muda la Edomu; na kumfanya Obadia kuwa mojawapo wa manabii watatu tu ambao walitamka hukumu juu ya mataifa mengine; wengine wakiwa ni Nahumu Habakuki. Lakini kuna zaidi ya hicho kwenye kitabu hiki. Wakati vitabu vingine vya kinabii vina kurasa zenye mistari ya hukumu juu ya Edomu na mataifa mengine, lengo kuu la Obadia japo wengi wetu inatuwia vigumu kulielewa ni ukweli kuhusu uhusiano wa ubinadamu na Mungu.
Ili kumwelewa vizuri Obadia, tunahitaji kurudi nyuma hadi katika kitabu cha Mwanzo. Tunaanzia kugusa Mwanzo 12:1-3 pale Mungu alipomuahidi Ibrahimu kuwa atawabariki watakao mbariki na kuwalaani watakao mlaani. Halafu Mwanzo 21:12; 26:24 pale baraka zilipohamishiwa kwa Isaka mwana wa Ibrahimu. Halafu Mwanzo 25: 23-26 pale baraka hizi zinapokuja kwa mmoja wa wana mapacha wa Isaka.
Katika Mwanzo sura ya 25, kuanzia na mstari wa 23, tunajifunza kwamba Rebeka mke wa Isaka alikuwa na ujauzito wa watoto mapacha. "Bwana akamwambia, “Mataifa mawili yamo tumboni mwako; makabila mawili yatakayozaliwa nawe, yatafarakana. Moja litakuwa lenye nguvu kuliko lingine; mkubwa atamtumikia mdogo.” Hapa Mungu alikuwa akimaanisha mapacha Yakobo na Esau. Esau alikuwa wa kwanza kuzaliwa, hivyo yeye alikuwa na haki juu ya urithi toka kwa baba yake. Lakini Yakobo akamdanganya ndugu yake na kumpatia haki ya kuzaliwa badala yake kwa bakuli la supu. Lakini ukifikiria utaona Esau hakufurahishwa na hili, hivyo alijenga chuki dhidi ya ndugu yake.
Baada ya muda kupita tunasoma kuwa Yakobo anaoa na kuwa na watoto kumi na moja. Siku usiku mmoja akiwa peke yake, alikutana na mtu, akapigana naye mwereka mpaka alfajiri. Mtu huyu alipomwambia Yakobo amwache aendezake, Yakobo akamwambia kwamba hawezi kumwacha mpaka ambariki! Katika hatua hiyo, mtu huyo alimbadilisha jina Yakobo... Jina lake sasa likawa Israeli. (Mwanzo 32:24-28)
Hapa sasa unaweza kupata kitu! Yakobo akawa Israel. Yakobo akaanzisha taifa la Israeli mara baada ya jina lake kubadilishwa; halafu akapata mwana mwingine – wakawa wana 12 ambao ni makabila 12 ya Israeli.
Tukimgeukia Esau tunajifunza nini? Esau alianzisha taifa la Edomu; na Edomu lilikuwa taifa la Wayahudi, kutoka kwa Ibrahimu. Na uchungu kati ya mataifa mawili hakuacha hata wakati Esau alipokufa. Katika 1 Samweli 14, Sauli anapigana vita dhidi ya Edomu. Katika 2 Samweli 8, Daudi alishinda vita dhidi ya Edomu. Katika 2 Wafalme 8 Edomu waliiasi Israeli. Isaya sura ya 34 alisema kuwa hukumu i juu ya Edomu. Yeremia katika sura ya 49 alisema kuwa Mungu ataleta msiba kwa Edomu. Ezekia katika sura ya 35 alisema kuwa Mungu ataiweka miji yao katika uharibifu. Malaki na Maombolezo pia vinataja uharibifu wa Edomu. Na sasa, Obadia.
Lakini tujiulize; kwa nini Mungu ailaani Edomu na si taifa jingine lolote? Je, nchi hii ya Esau imefanya nini hata istahili hukumu hiyo?
Obadia katika mstari huu hapa chini anatujibu swali hili;
Kiburi cha moyo wako kimekudanganya,
Wewe ukaaye katika pango za majabali,
Mwenye makao yako juu sana;
Asemaye moyoni, Ni nani atakayenishusha mimi? (Obadia 1:3)
Wewe ukaaye katika pango za majabali,
Mwenye makao yako juu sana;
Asemaye moyoni, Ni nani atakayenishusha mimi? (Obadia 1:3)
KIBURI NI TATIZO KUBWA LA EDOMU.
Kiburi ni chanzo cha maovu yote ya binadamu. Mithali 6:16 neno linasema; “Kuna vitu sita anavyovichukia Bwana; Naam, viko saba vilivyo chukizo kwake.” Kitu cha kwanza kabisa kwenye listi ni nini? “Macho ya kiburi” vingine vyote vinatokana na kiburi.
Kwa mwanadamu kiburi huja kwa aina mbalimbali. Katika kitabu cha Obadia tuonaona aina mbalimbali za viburi;
Aina mojawapo ya kiburi ni MAJIVUNO.
Asemaye moyoni, Ni nani atakayenishusha mimi?
Ujapopanda juu kama tai,
Ijapokuwa kioto chako kimewekwa kati ya nyota,
Nitakushusha kutoka huko; asema Bwana. (Obadia 1:3,4)
Ujapopanda juu kama tai,
Ijapokuwa kioto chako kimewekwa kati ya nyota,
Nitakushusha kutoka huko; asema Bwana. (Obadia 1:3,4)
Katika kujiona au kujivuna tunapata picha ya mtu ambaye anasema, "Hakuna mtu anaweza kunifanya chochote. Mipango yangu yote na kila kitu changu kiko sawa. Sihitaji msaada wa mtu yeyote. Nina uwezo wa kufanya chochote bila kumtegemea mtu”
Tabia hii ya kujiona na au kujivuna ni alama ya kiburi. Naye Bwana anasema kwamba " Ujapopanda juu kama tai, Ijapokuwa kioto chako kimewekwa kati ya nyota, Nitakushusha kutoka huko.”
Kibuli hutufanya tusione umuhimu wa uwepo wa Mungu. “Naweza kuendesha maisha yangu, kwa hekima yangu mwenyewe, kwa nguvu zangu mwenyewe, kwa uwezo wangu mwenyewe, kwa kipaji changu mwenyewe...Mungu wa nini?”
Kujiona kunaonekana kwa Mkristo ambaye anamuhitaji Mungu katika nyakati za hatari na hofu na shinikizo tu, na si katika nyakati nzuri. Ngoja nikupe story moja:
“Kuna jamaa alikuwa anaezeka paa la nyumba yake, kwa bahati mbaya akateleza na kuanzwa kuseleleka kuelekea ukingoni mwa paa. Huku akiteleza jamaa akawa anamwomba Mungu; Mungu nisaidie, Mungu nisaidie! Alipokaribia ukingoni mwa paa msumari ukadaka nguo yake; na kumfanya asiendelee kuteleza. Jamaa akamwambia Mungu; “Usijali Mungu nimeshajizuia nisianguke”
Wakristo tunapaswa kuelewa kwamba pale tunapoona kuna kitu chochote kwenye maisha yetu tumekipata au tunaweza kukifanya bila msaada wa Mungu; tunautukuza mwili na kujihusisha na kiburi cha Edomu. Hata kama wewe ni tajiri kwenye biashara zako, kiongozi kwenye jamii au jumuia yako, bosi ofisini au mtumishi kanisani; hakuna unachoweza kufanya bila kumtegemea Mungu.
Aina nyingine ya kiburi ni UDHALIMU;
“Kwa sababu ya udhalimualiotendwa ndugu yako Yakobo, Aibu itakufunika, nawe utakatiliwa mbali hata milele.” (Obadia 1:10)
Mtu anayempiga mkewe, anayemnyanyasa mwingine kijinsia, anayemnyanyasa mtoto, anayedhulumu mali za yatima, na wengine wanaofanya matendo yanayofanana na hayo, wanafanya udhalimu. Kiburi ni kiini cha ubinafsi na hupambana na kufanya udhalimu dhidi ya chochote au yeyote anayethubutu kutoa changamoto juu ya utawala wake mkuu katika maisha.
Aina nyingine ya kiburi ni KUTOJALI;
“Siku ile uliposimama upande, siku ile walipochukua mali zake, na watu wa kabila nyingine walipoingia katika malango yake, na kutupa kura juu ya Yerusalemu, wewe nawe ulikuwa kama mmoja wao.” (Obadia 1:11)
Kutojali ni kusimama na kutazama tu wakati mwingine akipata matatizo badala ya kumsaidia. Kutojali ni aina ya kiburi. Kutojali ni chanzo cha matatizo mengi katika ndoa na mahusiano. Kwenye migogoro mingi ya ndugu na wanandoa utasikia maneno kama; hanijali, ananipuuza, hanisikilizi, hapendi vitu ninavyovipenda na mengine yafananayo na hayo. Hayo yote yanaendana na kutojali ambayo ni sababu moja wapo ya Mungu kumchukia Esau. Wakristo hatupaswi kuwa watu tusiojali.
Aina nyingine ya kiburi ni MASIMANGO;
“Lakini usiitazame siku ya ndugu yako, siku ya mashaka yake, wala usisimange juu ya wana wa Yuda siku ya kuangamizwa kwao, wala usinene maneno ya kiburi katika siku ya shida yao” (Obadia 1:12)
Mungu anamhukumu Edomu kwa kusimanga na kubeza ambavyo vinatokana na kosa lake la kiburi. Watu wengi tunakiburi cha kubeza au kusimanga wenzetu wanapopata matatizo. Utasikia; “nilikwambia, nilijua tu, ndio ukome, umejitakia na mengineyo ambayo yote ni maneno ya yanadhihirisha tabia ya kubeza, kusimanga na kukejeri ambavyo hutokana na kiburi cha Edom. Tunayafanya au kuyasema haya pale wenzetu wanapopatwa na matatizo wakati sisi tuko salama, ila yanatokana na kiburi ambacho ni chukizo kwa Bwana.
Aina nyingine ya kiburi ni UNYONYAJI
“Wala usisimame penye njia panda, ili kuwakatilia mbali watu wake wakimbiao; wala usiwatoe watu wake waliosalia katika siku ya dhiki.” (Obadia 1:14)
Wakati Waisraeli walipotoka Misri na kutaka kupita katika nchi ya Edom; Waedomi waliwazuia. (Hesabu 20:14-21) Walipofikwa na majanga, Edomu alitumia nafasi hiyo kujifaidisha. Waedomi waliwateka, wakichukulia faida ukweli kwamba hawa walikuwa wakimbizi, na kutumia shida zao na mateso yao kwa faida yao wenyewe. Kuna mifano mingi ya hili katika maisha ya kila siku. Mmoja wapo ni kumshawishi mtu mwenye shida auze kitu chake kizuri ili ukinunue kwa bei ya chini au aweke rehani ili akishindwa kulipa umuongezee fedha kidogo uwe umekipata kwa bei rahisi. Mungu anachukia tunapoutumia udhaifu wa mwingine au bahati mbaya ya mwingine kwa faida yetu.
Hiyo ni baadhi tu ya mifano inayosababisha chuki ya Mungu kwa Edomu. Lakini mkubwa katika hiyo ni pale Obadia anaposema; “Kiburi cha moyo wako kimekudanganya” (Obadia 1:3)
Kiburi ni kibaya. Kinatudanganya, kinatutega, kutunasa na kutufanya tusijitambue hadi pale tunapopatwa na matatizo. Wakati mwingine tunaendelea kujivuna, kujisikia na kuamini mambo yetu yako sawa hata pale ambapo watu wengine wanaona tunaharibikiwa na kupotea. Pengine tunaambiwa kabisa lakini kiburi kinatufanya kushupaza shingo mpaka mambo yanakwenda mrama kabisa.
Unabii wa Obadia unalenga katika nguvu ya uharibifu wa kiburi. Unatukumbusha matokeo ya kuishi kwa namna binafsi ya kujiona wenyewe, ya kuzifuata hisia na tamaa zetu wenyewe bila kuzingatia athari zake kwa wale walio karibu nasi. Ingawa kiburi kimekuwa sehemu ya maisha na maanguko ya mwanadamu tangu janga la kuanguka katika Edeni, Obadia anatukumbusha kujiweka chini ya mamlaka ya Mungu, kuzitumi hamu zetu kwa makusudi yake, na kupata tumaini letu katika kuwa watu wake wakati wa wa kuhukumiwa na kufanywa upya vitu vyote utakapokuja.
No comments:
Post a Comment