Vichwa vya Habari

UTAINUA MISINGI YA VIZAZI VINGI ISAYA 58:12


NAMNA YA KUSIKIA NA KUIELEWA SAUTI YA MUNGU ILI IKUSAIDE KATIKA KUFANYA MAAMUZI (Sehemu ya tatu)

August 20, 2015
4Na: Patrick Sanga
Mada – Njia anazotumia Mungu kusema na mwanadamu (Sehemu ya kwanza)
Katika sehemu ya kwanza na ya pili ya ujumbe huu naliandika mambo muhimu ya kujua kwanza kuhusu sauti ya Mungu. Ili kusoma sehemu hiyo bonyeza link hii https://sanga.wordpress.com/2015/04/08/namna-ya-kusikia-na-kuielewa-sauti-ya-mungu-ili-ikusaidie-katika-kufanya-maamuzi-sehemu-ya-2/ Katika sehemu hii ya tatu na ya kwanza kwa mada hii nitaendelea na somo hili kwa kuanza kunagalia njia ambazo Mungu hutumia kusema na wanadamu, naam sasa fuatana nami tuendelee;
Katika Yohana 5:30 imeandikwa ‘Mimi siwezi kufanya neno mwenyewe; kama NISIKIAVYO ndivyo nihukumuvyo; na hukumu yangu ni ya haki, kwa sababu siyatafuti mapenzi yangu mimi, bali mapenzi yake aliyenipeleka’. Andiko hili linatuonyesha utaratibu au nidhamu aliyokuwa nayo Yesu katika kutekeleza kusudi la kuletwa kwake hapa duniani.
Yesu anatueleza wazi kwamba katika utumishi wake, hakutafuta kutekeleza mapenzi yake, bali kadri ALIVYOSIKIA kutoka kwa baba yake ndivyo alivyotenda. Ushuhuda huu wa Yesu unatufanya tujue kwamba, kumbesauti ya Mungu ina umuhimu wa kipekee katika kutusaidia kufanya maamuzi mbalimbali yanayotukabili kila siku.
Sauti ya Mungu ni nini? – sauti ya Mungu si tu maneno yanayotoka kwenye kinywa chake kama wengi wanavyofahamu bali ni UJUMBE ambao Mungu analeta kwenye maisha yako kwa NJIA mbalimbali ili kukuondoa kwenye matakwa/makusudi yako na hivyo kukusaidia kuyatenda mapenzi yake makamilifu.
Zifuatazo ni baadhi ya njia muhimu ambazo Mungu hutumia katika kusema, kufikisha ujumbe au kufanya mawasiliano na mwanadamu;
  • Kupitia neno lake
Neno la Mungu ndio msingi mkuu wa Mungu kusema na mwanadamu. Hata njia nyingine ambazo Mungu atatumia kusema na wanadamu ni dhahiri kwamba ujumbe wake lazima uendane na neno lake na si vinginevyo.
Katika 2Timotheo 3:16-17 imeandikwa ‘Kila andiko lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema’.
1
Neno la Mungu ndiyo sauti kuu ya Mungu duniani kwa wanadamu na hivyo kuwa na ufahamu wa kutosha wa neno la Mungu ni lazima kwa mwamini anayetaka kuisikia sauti ya Mungu iliyoko ndani ya neno lake. Kadri mwamini anavyokuwa na neno la kutosha ndani yake, ndivyo anavyojiweka kwenye mazingira sahihi ya kusikia na kuelewa sauti ya Mungu kwenye kila eneo la maisha yako na hivyo kuwa kwenye nafasi bora ya kufanya maamuzi.
  • Kupitia ndoto
Katika Hesabu 12:6 imeandikwa ‘Kisha akawaambia, Sikizeni basi maneno yangu; Akiwapo nabii kati yenu, Mimi, BWANA, nitajifunua kwake katika maono, NITASEMA NAYE KATIKA NDOTO’. Ndiyo, Mungu husema kupitia ndoto, kwa kuwa ndoto ni lugha ya picha tena rahisi ya mawasiliano kwa yeye kufikisha ujumbe wake na hivyo kumsaidia mtu aelewe mpango wake (Mungu) kwenye maisha yake na hivyo kufanya maamuzi muafaka.
Pia katika Ayubu 33:14 imeandikwa ‘Kwa kuwa Mungu hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali. Katika ndoto, katika maono ya usiku, Usingizi mzito uwajiliapo watu, Katika usingizi kitandani’. Hapa Biblia inatueleza kwamba kumbe ndani ya ndoto kuna sauti na hivyo mtu anaweza kuisikia sauti ya Mungu kupitia ndoto, ingawa si ndoto zote huambatana na sauti. Ndoto huja pale mtu anapokuwa amelala usingizi na hili lina maana, mtu anahitaji muda na mazingira bora ya kulala ili Mungu aweze kusema naye kwa njia hii. Ndoto inaweza kuja kwa mfano wa hadithi au tukio lenye kisa au uzoefu fulani ndani yake.
2
Endapo, katika ndoto ambayo ni ya kutoka kwa Mungu, ukiona unaongea, maana yake Mungu anakuonyesha nini cha kusema, kufanya au kuomba punde utakapoamka. Kuomba baada ya kuamka au kushtuka ni LAZIMA ili kuhakikisha zile za kutoka kwa Mungu zinatimia na zile za kutoka kwa Shetani zinazuiliwa.Jambo la msingi ni lazima mtu ajifunze kutafsiri ndoto anayoiota kama sauti ya Mungu kwa kuwa ndani ya ndoto kuna ujumbe. Kuwa na ufahamu wa kutosha wa neno la Mungu ndio msingi muhimu wa kuelewa na kufasiri ndoto unazoota. Rejea mifano ifuatayo ndani ya Biblia ili kuelewa zaidi njia hii.
Mungu anasema na Abramu kuhusu uzao wake (Mwanzo 15:12), Mungu anasema na Sulemani juu ya mambo mbalimbali (1Wafalme 3:5-13), Mungu anamonya Abimeleki kuhusu mke wa Abramu (Mwanzo 20:1-7), Mungu anamuonya Yusufu, asimwache Mariam (Matahyo 1:20), Mungu anasema na Yusufu kuhusu ulinzi wa Yesu dhidi ya hila za Herode (Mathayo 2:13).
  • Kupitia watumishi wa Mungu au viongozi wa kiroho   
Katika kuzungumza na wanadamu, Mungu amejiwekea pia utaratibu wa kutumia watumishi wake mbalimbali ikiwa ni pamoja wachungaji, manabii, walimu, manabii na mitume au kwa lugha ya ujumla viongozi wa kiroho. Mungu anatumia watu hawa kwa sababu (a) utaratibu aliojiwekea kama nilivyosema awali (b) kutokana na nafasi zao katika mwili wa Kristo na (c) watu wengi hawako tayari kulipa gharama ya kutafuta kuisikia na kuelewa sauti ya Mungu.
3
Watumishi wamewekwa maalum na Mungu kwa ajili yetu ili watusaidie kuelewa mapezi yake kwenye maisha yetu na hivyo kufanya maamuzi sahihi kwa kila hatua. Katika Luka 16:29 imeandikwa ‘wanao Musa na manabii wawasikilize wao’. Naam kwa lugha nyingine Musa na manabii (watumishi) ndiyo sauti ya Mungu kwao.
Hata hivyo ni lazima watu wawe na tahadhari kwamba watumishi wanaolengwa hapa ni wale walioitwa na Mungu kweli, yaani watumishi wa kweli (nuru) na si wa uongo (giza). Tafadhali rejea maandiko yafutayo kwa ufahamu zaidi (1Samweli 2:27, 1Samweli 9:9).
Mungu akubariki kwa kufuatilia mfululizo huu. Katika sehemu ya nne, nitaendelea kuandika njia nyingine ambazo Mungu hutumia kusema na wanadamu. Somo litaendelea….
Utukufu na heshima vina wewe Yesu, wastahili BWANA wangu.


ROHO YA HEKIMA NA UFUNUO

May 2, 2015
1Na: Patrick Sanga
Salaam katika jina lake BWANA Yesu
Katika Waefeso 1:17 Biblia inasema ‘Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi ROHO YA HEKIMA NA YA UFUNUO KATIKA KUMJUA YEYE’. Hili moja ya maombi muhimu ambayo Mtume Paulo alifanya kwa jili ya Kanisa la Efeso. Kila nisomapo mstari huu nimekuwa nikijuliza sana ni kwa nini Mtume Paulo aliomba maombi haya kwa kanisa hili?.
Katika kutafakari na kuendelea kujifunza niligundua kwamba kulikuwa na sababu kubwa tatu ambazo zilimpelekea Mtume Paulo kuwaombea jambo hili, na kutokana na umuhimu wake hata kwa kanisa la sasa ndiyo maana nimeona ni vema nikaliandika hapa ili na wewe msomaji uweze kujifunza.
Zifuatazo ni sababu kadhaa zilizompelekea Mtume Paulo aliombee kanisa la Efeso roho ya hekima na ufunuo na kwa sababu hiyo zinatusaidia kujua umuhimu wake kwa kanisa la sasa pia;
Ili waweze kumjua Mungu zaidi (Waefeso 1:17)
Waefeso 1:11 ‘Na ndani yake sisi nasi tulifanywa urithi, huku tukichaguliwa tangu awali sawasawa na kusudi lake yeye, ambaye hufanya mambo yote kwa shauri la mapenzi yake’.
4
Kazi ya roho ya ufunuo ni kumfunua Mungu kwa kiwango ambacho bado hujakiona wala kukizoea ili kuboresha uhusiano wako na Mungu na kukufanya umaanishe katika kumpenda. Ndiyo, lengo ni kumfunua Mungu kwako, kutoka kwenye kona tofauti tofauti ili umjue zaidi ili hali kazi ya roho ya hekima ni kukupa ufahamu (maarifa), werevu na busara katika kufanya maamuzi sahihi kuhusu uhusiano wako na Mungu na maisha yako kwa ujumla. Katika ufunuo kuna mambo ambayo Mungu atayaleta kwako na yanahitaji hekima katika kuyafasiri, kuyanena na kutenda.
Naam bado hatumjui Mungu kwa kiwango kitupasacho kumjua na ndio maana tunahitaji roho ya ufunuo. Roho ya ufunuo inamuongoza mtu kujenga mahusaino binafsi na Mungu wake tokana na ufunuo aliopata.  Roho hii inatuleta kwenye ufahamu muhimu kuhusu ulimwengu wa roho na kwamba ni lazima tuanze kuishi maisha katika ulimwengu wa roho kuliko vile tunavyoishi katika ulimwengu wa mwili ili kumjua Mungu zaidi.
Ili kujua mambo ambayo Mungu amewaandalia (1Wakorinto 2:9-10)
Katika fungu hilo Biblia inasema hivi ‘Lakini, kama ilivyoandikwa, MAMBO AMBAYO JICHO HALIKUYAONA WALA SIKIO HALIKUYASIKIA, (Wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu,) Mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao. LAKINI MUNGU AMETUFUNULIA SISI KWA ROHO. Maana Roho huchunguza yote, hata MAFUMBO ya Mungu’. Pia katika Waefeso 1:18 imeandikwa ‘MACHO YA MIOYO YENU YATIWE NURU MJUE tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo’
5
Mungu anataka watu wake wajue kwamba yeye anayo mawazo (Yeremia 29:11), mbalimbali ambayo amewaandalia watoto wake. Mawazo hayo yameunganishwa na kusudi la kuwepo kwao hapa duniani na hawana budi kuyajua, kuyapata na kuyatenda. Naam ili wafikie hapo sharti juu yao na ndani yao, wawe na roho ya hekima na ufunuo.
Kumbuka katika kila nyanja ya maisha iwe kazi, uchumi, biashara, familia, huduma, ndoa nk, yapo mambo ambayo ameyaandaa na anataka uyajue. Naam ni jukumu lako kuendelea kujenga na kuboresha mahusaino yako na Roho Mtakatifu yawe mazuri daima.
Ili kuujenga mwili wa Kristo ipasavyo
Katika 1Wakorinto 12:7 Biblia inasema ‘Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana’.  Ukiendelea Katika 1Wakorinto 12:20 imeandikwa ‘Na jicho haliwezi kuuambia mkono, sina haja na wewe; wala tena kichwa hakiwezi kuaimbia miguu; sina haja na ninyi’ na ule mstari wa 25 unasema ‘Ili kusiwe na faraka katika mwili, BALI VIUNGO VITUNZANE KILA KIUNGO NA MWENZIWE(1Wakorinto 12:25).
Hivyo roho ya ufunuo inatoa ufunuo ili kufaidiana, lengo ikiwa ni kuusaidia mwili wa Kristo kuimarika zaidi. Naam kumbuka ufunuo huu ni kwa sehemu kwa lengo la kulijenga kanisa, mwili wa Kristo. Katika 1Wakorinto 12:11 imeandikwa ‘Lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye’. Na tena Mtume Paulo anamalizia kwa kusema ‘Basi ninyi mmekuwa mwili wa Kristo, na viungo kila kimoja peke yake’ (1Wakorinto 12:27).
Naam hakuna mtu anayepewa karama zote, kila mmoja anapewa kwa SEHEMU kama KIUNGO ili kwa kushirikiana, MWILI wa Kristo ujengwe vema. Naam kila kiuingo lazima kihakikishe kina kuwa na ufanisi unaotakiwa, si kwa ajii yake, bali kuhakikisha mwili wa Kristo unajengwa ipasavyo, kupitia ufunuo/uwepo wa kile kiungo.
Kanisa lazima lifike mahali pa kuwa na uelewa kamili juu ya mwili wa Kristo unavyopaswa kutenda kazi kupitia ufunuo wa Roho Mtakatifu kwa kuwa ‘Mungu amevitia viungo kila kimoja katika mwili kama alivyotaka (1Wakorinto 12:18). Naam kila mshirika unayemuona NI KIUNGO CHA MWILI WA KRISTO KUPITA KARAMA, VIPAWA NA HUDUMA ALIZOPEWA kwa lengo la kuujenga mwili wa Kristo.  Roho ya hekima ikuongoze kutenda na kujua kwamba karama, huduma na vipawa ulivyonavyo ni kwa ajili ya kuujenga mwili wa kristo.
Naam hatupaswi kumdharau mtu yoyote kutokana na hali yake ya nje kwa jinsi ya kibinadamu maana yeye ni kiungo kinachostahili heshima zaidi (1 Wakorinto 12:22) Kazi ya Mchungaji na viongozi wa kanisa ni kufuatilia ili kujua Mungu ameweka/ametoa/amefunua kitu gani (karama/vipawa/huduma) juu ya wale wanaowaongoza ili kuviendeleza kwa lengo la kuujenga mwili wa Kristo.
3
Hivyo tokana na umuhimu wa roho ya hekima na ufunuo juu ya kanisa la Mungu na kwa mtu mmoja mmoja ni vizuri tukachukua au ukachukua hatua ya kuanza kumomba Mungu akujalie roho ya hekima na ufunuo wewe binafsi, familia yako, jamaa zako na kanisa kwa ujumla ili manufaa yake yawe dhahiri katika mwili wa Kristo ulimwenguni kote.
Roho ya hekima na ufunuo na iwe nanyi
Utukufu na heshima vina wewe Yesu, wastahili BWANA!

MAMBO YA KUMSAIDIA KIJANA ALIYEOKOKA AISHI MAISHA YENYE USHUHUDA MZURI

April 16, 2015
AuthorsNa: Patrick S. Sanga

Mtume Paulo katika waraka wake kwa Timotheo anamwambia hivi, ‘Mtu awaye yote ASIUDHARAU ujana wako, bali uwe KIELELEZO kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi.JITUNZE nafsi yako, na mafundisho yako. DUMU katika mambo hayo; maana kwa kufanya hivyo UTAJIOKOA NAFSI YAKO NA WALE WAKUSIKIAO PIA’ (1Timotheo 4:12 & 14).
Sentensi hizi zinatuonyesha kwamba kijana yeyote ambaye amefanya uamuzi wa kuokoka, kwa hakika amefanya maamuzi ambayo yanamtaka amaanishe katika kumfuata kwake Yesu au kuuishi wakovu wake. Pamoja na kumpa Yesu maisha yake ni lazima kijana afanye maamuzi ya kuishi maisha ya kudumu kumpendeza Mungu kwa kuzikubali gharama zinazohusiana na wokovu aliouchagua na si kuishi maisha yenye kupelekea jina la BWANA kutukanwa kama ilivyo kwa baadhi ya vijana wengi leo.
Ukisoma mstari huu wa 1Timotheo 4:14 kwenye toleo la kiingereza la ESV unasema ‘Keep a close watch on yourself and on the teaching. Persist in this, for by so doing you will save both yourself and your hearers’.Kwa mujibu wa dictionary ya kigiriki na kiebrania neno ‘save’ lina maana ya kuweka huru (deliver), kulinda (protect), kuponya (heal), kutunza (preserve), kuokoa (save). Jambo muhimu ambalo Mtume Paulo alikuwa akilisisitiza hapa ni hili; jambo muhimu si tu kumpokea Yesu kama Bwana na mwokozi wako, bali kila mwamini ana kazi kubwa ya kufanya iliKUULINDA NA KUUTUNZA WOKOVU WAKE.
Moja ya changamoto kubwa sana ambazo zinawakabili vijana wengi waliokoka leo ni kuipenda dunia. Kuipenda dunia kumekuwa tanzi kwa vijana wengi na kwa sababu ya kuipenda dunia; (a) Mahusiano ya vijana wengi na Mungu wao yameharibika (b) Maisha ya vijana wengi yamekosa uelekeo (c) Kutokana na uovu wao jina la Bwana Yesu limekuwa likitukanwa.
4
Katika kile kitabu cha 1Yohana 2:16 ni dhahiri kwamba dunia imejaaTAMAA YA MWILI, TAMAA YA MACHO NA KISHA KIBURI CHA UZIMA. Tamaa ina nguvu ya kuvuta pamoja na kudanganya, naam inamuingiza mtu kwenye jaribu. Hii ina maana tamaa ni mlango, naam mlango huu unapaswa kufungwa mapema usikupoteze. Hebu tujifunze kutokana na anguko la mfalme Daudi na mke wa Bathssheba (Samweli 11:1-2). Tunaona anguko la Daudi lilisaabishwa na kumpa Ibilisi nafasi kwa kutokwenda vitani. Mkristo akipoa katika kuvipiga vita vya kiroho inakuwa rahisi kwake kuanguka dhambini             (Yakobo 1:14-15), naamkumbuka kwamba siku zote tamaa inalenga kumfurahisha mtu binafsi (self-pleasing) bila kujali matokeo yake.
Hivyo katika nyakati tulizonazo sasa suala la kuipenda dunia ni lazima litafutiwe ufumbuzi wa kudumu miongoni mwa vijana wetu. Ujumbe huu mfupi unalenga kueleza kwa namna gani kuipenda dunia kumekuwa tanzi kwa vijana na nini vijana wafanye ili kuikabili na kuishinda changamoto husika.
Pia katika waraka 2Timotheo 2:15 Mtume Paulo anaendelea kumwambia kijana Timotheo ‘Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu,mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli’.
Pengine kila mmoja wetu atafakari maisha yake kwa kuhusianisha na maelekezo ya Paulo kwa Timotheo. Naomba jiulize na kujijibu kwa uaminifu kwamba mosi, je, ujana wako wako unaheshimika au unadharauliwa? Pili, je, kwa waamini wenzako umekuwa kielelezo cha kweli kwa habari ya imani, upendo, usafi, usemi na mwenendo au la?
DSCF0028
Binafsi  nimekuwa nikijiuliza ni kwa namna gani kijana atahakikisha kwamba(a) Ujana wake haudharauliwi (b) Anakuwa kielelezo kwa waamini wenzake (c) Anathibitisha kwamba kweli amekubaliwa na Mungu. Naam katika kusoma na kutafakari neno la Mungu nimejifunza kwamba zifuatazo ni njia ambazo zitatusaidia sisi vijana wa leo kuifikia kweli hii ya neno la Mungu.
  • Kijana adumu katika kuomba na kusoma (kutafakari + kulitenda) neno la Mungu
Katika Zaburi 119:9 & 11 Biblia inasema ‘Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii AKILIFUATA neno lako’. Pia kwenye ule mstari wa 11 inasema ‘moyoni mwangu nimeliweka neno lako, NISIJE NIKAKUTENDA DHAMBI’.
Naam katika Mathayo 26:41 imeandikwa ‘Kesheni, mwombe, MSIJEmkaingia majaribuni; roho I radhi, lakini mwili ni dhaifu’. Yohana 17:17 inasema ‘uwatakase kwa ile kweli ;neno lako ndiyo kweli. Mambo haya mawili yanapaswa kwenda kwa pamoja nakijana akidumu katika kuomba na kusoma neno la Mungu ushindi ni lazima.
  • Kijana asimpe Ibilisi nafasi.
Kijana anapaswa kujiuepusha na mazingira yenye kumfanya aiepende na kuifuatisha namna ya dunia hii. Katika kitabu cha 1Wakorinto 6:12 imeandikwa ‘Vitu vyote ni halali kwangu, lakini si vyote VIFAAVYO; vitu vyote ni halali kwangu, lakini mimi sitatiwa chini ya UWEZO wa kitu chochote’.  Ni vizuri ukahakikisha kwamba ufahamu wako hautawaliwi na mambo yasiyo ya msingi (non-essentials of life) – Je ufahamu wako umetawaliwa ni nini?
Hii ndiyo sababu iliyomfanya Paulo awaambie Waefeso ‘Wala msimpe Ibilisi nafasi’ (Waefeso 4:27) na pia awaambie Warumi “Bali mvaeni Bwana Yesu Kristo, wala msiuangalie mwili hata kuwasha tamaa zake’. Toleo la KJV linasema ‘But put ye on the Lord Jesus Christ, andMAKE NOT PROVISION for the flesh, to fulfill the lusts thereof’.  Na toleo la ESV linasema ‘But put on the Lord Jesus Christ, AND MAKE NO PROVISION FOR THE FLESH, TO GRATIFY ITS DESIRES’ (Warumi 13:14).  Je hivi leo ni kwa namna gani vijana wanaungalia mwili na kumpa Ibilisi nafasi? – Mitandao ya kijamii, kuangalia na kusoma vitu vichafu, hasira, mawazo, mazingira.
Mfano wa Vijana
  • Kijana azikimbie tamaa za ujanani
Katika 2Timotheo 2:22 imeandikwa ‘LAKINI ZIKIMBIE TAMAA ZA UJANANI; ukafuate haki, na imani, na upendo, na amani, pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi’. Kijana anawezaje kuzikimbia tama za ujanani? Hebu tuangalie mfano wa Yusufu. Ushindi wa Yusufu dhidi ya mke wa Uria (Mwanzo 39:2-9). Hii ni habari ya kijana Yusufu ambaye alikuwa msimamizi mkuu wa mali za Potifa.
Pamoja na ushawishi aliokutana nao Yusufu alijibu kwamba ‘Nifanyeje ubaya huu mkubwa nikamkose Mungu?’ Mwanzo 39:12 inasema ‘huyo mwanamke akamshika nguo zake, akisema, Lala nami. Yusufu akaiacha nguo yake mkononi mwake akakimbia akatoka nje. Ili kuzikimbia tamaa za ujanani kijana anapswa (a) ajiepushe na mazingira/marafiki wabaya (Mithali 1:10 & 1Wakorinto 15:33) (b) Ajitenge na uovu (Mithali 16:17, Zaburi 1:1).
Ni muhimu ukakumbuka kwamba hukupewa mwili kwa ajili ya zinaa maana miili yenu ni ni viungo vya Kristo na tena hekalu la Roho Mtakatifu (1 Wakorinto 6:15 & 19), tena yeye aliyeungwa na Bwana ni roho moja naye (1 Wakorinto 6:17) maana tena imeandikwa ‘Lakini mwili si kwa zinaa, bali ni kwa Bwana, naye Bwana ni kwa mwili’ (1Wakorinto 6:13b). Tena imeandikwa ‘Lakini uasherati USITAJWE kwenu kamwe, wala uchafu wowote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu’   (Waefeso 5:3).
  • Kijana ajifunze kuenenda kwa roho na si kwa mwili
Katika wagalatia 5:16 imeandikwa ‘Basi nasema ENENDENI KWA ROHO, wala HAMTATIMIZA kamwe TAMAA ZA MWILI. Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayoyataka’.
Je kuenenda kwa Roho ndio kukoje?
Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, ATAWAONGOZA awatie kwenye kweli yote (Yohana 16:13) na pia imeandikwa ‘kwa kuwa woteWANAOONGOZWA na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu’ (Warumi 8:14). Kuenenda kwa Roho ina maana ya kuishi kwa kufuata utaratibu/uongozi wa Roho Mtakatifu kwenye maisha yako (Warumi 8:2).
Naam kadri unavyokuwa mtiifu kufuata utaratibu wake ndivyo unavyokuwa mbali na sheria ya dhambi na mauti ambayo ni mwili.Kumbuka imeandikwa ‘kwa maana wale waufuatao mwili huyafikiri mambo ya mwili; bali wale waiufuatao roho huyafikiri mambo ya roho. Kwa kuwa nia mwili ni mauti bali nia ya roho ni uzima na amani (Warumi 8:5-6) na pia Wafilipi 4:8.
2
Naam imeandikwa ‘Kila mmoja wenu ajue KUUWEZA MWILI wake katika utakatifu na heshima; si katika hali ya tamaa mbaya, kama mataifa wasiomjua Mungu. Maana Mungu HAKUTUITIA UCHAFU, bali tuwe katika utakaso’ (1Thesalonike 4:4-5, 7). Ni jambo la ajabu sana kwamba kwamba tumepewa fursa ya kuiweza miili yetu. Ndio tunapaswa kuuweza mwili kwa maana ya kuudhibiti kwa kuuongoza na kuufanya ufuate nia ya roho.
Kijana mwenzangu kama umechagua kumpa Yesu maisha yako kwa njia ya wokovu,  nakusihi na kukushauri zingatia haya ili kuwa na maisha yenye kielelezo na ushuhuda mzuri maana imeandikwa  ‘Kwa maana wale waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua Bwana na Mwokozi Yesu Kristo, kama wakinaswa tena na kushindwa, hali yao ya mwisho imekuwa mbaya kuliko ile ya kwanza. Maana ingekuwa heri kwao kama wasingaliijua njia ya haki, kuliko kuijua, kisha kuiacha ile amri takatifu waliyopewa’ (2Petro 2:20-21).
Neema ya Kristo iwe nanyi, na tuzidi kuombeana.
Utukufu na heshima vina wewe Yesu, wastahili BWANA.

NAMNA YA KUSIKIA NA KUIELEWA SAUTI YA MUNGU ILI IKUSAIDIE KATIKA KUFANYA MAAMUZI (Sehemu ya 2)

April 8, 2015
Na: Patrick Sanga
1
Mada: Mambo mhumu kujua kuhusu sauti ya Mungu
Katika sehemu ya kwanza ya ujumbe huu niliandika kuhusu mambo matatu ambayo ni kujenga mahusiano na Roho Mtakatifu, kuongeza ufahamu wako kuhusu alama za mawasilano na tatu ujue namna ya kutofautisha sauti ya Mungu na isiyo ya Mungu. Ili kusoma sehemu ya kwanza bonyeza link hii  https://sanga.wordpress.com/2015/04/02/namna-ya-kusikia-na-kuielewa-sauti-ya-mungu-ili-ikusaide-katika-kufanya-maamuzi-sehemu-ya-1/ Sasa fuatana nami tuendelee na mabo mengine muhimu kujua:
  • Vifahamu vikwazo vinavyopelekea kutokusikia sauti ya Mungu
Biblia imeainisha vikwazo kadhaa vyenye kupelekea mtu kutokuisika sauti ya Mungu. Vikwazo hivyo ni pamoja na moja kutenda dhambi au kuishi maisha ya dhambi (Isaya 59: 1-2), pili kukosa uaminifu (Hesabu 12:7-8, 1 Samweli 2:35). Biblia katika Isaya 59: 1-2 inasema ‘Lakini maovu yenu, yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia’ Pia katika Hesabu 12:7-8 imeandikwa ‘Sivyo ilivyo kwa mtumshi wangu, Musa; Yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote; Kwake nitanena mdomo kwa mdomo, Maana, waziwazi wala si mafumbo.
2
  • Ongeza ufahamu wako kuhusu njia anazotumia Mungu kuzungumza
Ni dhahiri kwamba zipo njia mbalimbali ambazo Mungu hutumia kusema na wanadamu. Namna Mungu anavyosema na huyu sivyo atakavyosema namtu mwingine. Tofauti hizi zipo tegemeana na mahusainao yaliyopo kati ya Mtu na Mungu na pia ngazi ya kiroho aliyonayo mtu katika ulimwengu wa roho. Hivyo ni muhimu sana kuwa na uelewa wa hizi njia mbalimbali ili kuelewa mazingira yake na hivyo kutafuta kumsika Mungu kupitia njia hizo ili kudumisha mahusiano na mawasiliano yako na Mungu. Katika sehemu ya tatu ya somo hili nitaanza kufundisha njia husika hivyo naamini ufahamu wako utaongezeka.
  • Unahitaji kufahamu umuhimu wa Mungu kuzungumza/kusema nawe
5
Zipo sababu nyingi za Mungu kuzungumza na wanadamu laikini kubwa yenye kuzibeba zote ni ile iliyoandikwa katika Zaburi 32:8 kwamba‘Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama’. Ni muhimu ukakumbuka kwamba kwa mujibu wa Wayumi 8:28 umeitwa ili kulitumika kusudi la Mungu katika siku zako. Ili uweze kulitumika ipasavyo sharti akuongoze katika njia sahihi. Naam njia mojawapo ya kukuongoza na kukufundisha ni kwa yeye kusema na wewe.
Lengo lake katika kusema na wewe ni kukuongoza katika njia sahihi kwa kukuondoa kwenye makusudi ambayo yapo nje na mapenzi yake kwenye maisha yako maana imeandikwa ‘Kwa kuwa Mungu hunena mara moja, Naam hata mara ya pili ajapokuwa mtu hajali, ili amwondoe mtu katika makusudio yake, Na kumfichia mtu kiburi’ (Ayubu 33:14, 17).
  • Ongeza ufahamu wako kuhusu ulimwengu wa roho
Mambo yote yanayotokea katika ulimwengu wa mwili yameanzia katika uilimwengu wa roho, naam maamuzi ya kile ambacho hutokea katika ulimwengu wa mwili hufanyika katika ulimwengu wa roho. Zaidi hata mapambano (vita vya kiroho) yote aliyoanayo mwamini katika kulitumikia kusudi la Mungu hufanyika katika ulimwengu wa roho.
Hivyo kuwa na ufahamu wa ulimwengu wa roho hususani namna ya kuishi na  kuwasiliana katika ulimwengu huo ni muhimu sana kwa mwamini mwenye kutafuta kujua na kuisikia sauti/mawazo ya Mungu katika maisha yake kwa kuwa Mungu ni roho kama alivyo na Shetani pia. (Rejea 2 Wafalme 6:8-17 na Waefeso 6:10-12).
3
Mpenzi msomaji usiruhusu yale unayoyapitia au yale ambayo watu /mazingira yanasema juu yako yabadilishe au kuongoza maisha yako, bali tafuta kuijua na kuielewa sauti ya Mungu kwenye maisha yako. Na ndiyo maana somo hili limekuja ili kukusaidia kufika mahala ambapo utaweza kuyatenda mapenzi kamili ya Mungu kwenye maisha yako.
Baada ya kuwa tumeangalia mambo haya saba ambayo ni muhimu kujua kuhusiana na sauti ya Mungu, katika sehemu ya tatu nitaanza kuandika kuhusu njia mbalimbali ambazo Mungu hutumia kusema na wanadamu. Somo litaendelea….
Utukufu na heshima vina wewe Yesu, wastahili BWANA.

NAMNA YA KUSIKIA NA KUIELEWA SAUTI YA MUNGU ILI IKUSAIDE KATIKA KUFANYA MAAMUZI (Sehemu ya 1)

April 2, 2015
Na: Patrick Sanga
1
Salaam katika jina la Yesu Kristo na heri ya Pasaka mpenzi msomaji.
Je ni kweli Mungu anazungumza na mwanadamu hata sasa? Hili ni moja ya swali ambalo watu wengi wamekuwa wakijiuliza na kukosa majibu muafaka kwani baadhi yao hawaamini kwamba ni kawaida ya Mungu kuzungumza na wanadamu. Kama ilivyokuwa katika agano la kale, agano jipya, naam hata sasa, Mungu ni yeye yule jana na leo na hata milele. Hivyo ni kusudio la ujumbe huu kuongeza ufahamu wako ili uweze kujua ni kwa namna gani Mungu huzungumza na mwanadamu na kisha nini ufanye ili kumuelewa Mungu anapozungumza. Naam fuatana name sasa katika mfululizo huu…
Kwa nini Mungu azungumze/aseme na mwanadamu? – mtu anahitaji kusikia sauti ya Mungu ili; (a) aishi sawasawa na kusudi au mapenzi ya Mungu awapo hapa duniani      (b) kujenga na kudumisha mahusiano/mawasiliano mazuri kati yake na Mungu (c) kuona kama Mungu aonavyo na hivyo kutafsiri mambo ya rohoni kwa maneno ya rohoni (Rejea Zaburi 32:8, 1Samweli 3:1 na Isaya 55:8).
Mambo mhumu kujua kuhusu sauti ya Mungu
Yafuatayo ni baadhi ya mambo muhimu ya kukusaidia kuijua, kuisikia na kuielewa sauti ya Mungu, nawe hunabudi kuyafahamu na kuyatenda;
  • Jenga na kudumisha mahusiano mazuri na Roho Mtakatifu – Ni vizuri ukafahamu kwamba Roho Mtakatifu yupo duniani sasa akiliongoza kanisa katika kuyatenda mapenzi ya Mungu. Hivyo uwepo wa mahusiano mazuri kati yako na Roho Mtakatifu ndio ufunguo wa mawasilaino mazuri kati yako na Mungu. Biblia katika 1Wakorinto 2:10 inasema ‘Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu… vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu’. Andiko hili linatuonyesha nafasi ya Roho Mtakatifu katika kutusaidia kuisikia sauti ya Mungu. Hivyo jenga na kudumisha uhusiano wako na yeye, itakusaidia sana katika kiujua na kuisikia sauti ya Mungu.
Roho Mtakatifu
  • Ongeza ufahamu wa viashiria (signal) vya mawasiliano kati yako na Mungu                              Ufahamu wa viashiria (signal) za mawasiliano kati yako na Mungu ni wa lazima ili kusikia na kuielewa sauti ya Mungu. Zipo alama mbalimbali kwa kila mwamini ambazo Mungu hutumia katika kusema naye. Biblia katika 1Samweli 3:9 inasema   ‘… Enenda, kalale, itakauwa AKIKUITA, utasema, Nena, BWANA; kwa kuwa mtumishi wako anasikia…’ Jambo ninalotaka ulijue hapa ni kwamba Mungu ana njia nyingi za KUITA, naam anaweza kukuita kwa sauti itokayo kinywani pake au KWA NJIA KUKULETEA ALAMA/VIASHIRIA VYENYE KUKUFANYA UJUE MUNGU ANANIITA. Kama ilivyo kwa jinsi ya kibinadamu anayekuita si lazima aongee, anaweza kutumia alama za mikono au hata maandishi nk, kukuita. Katika kukuita kwa njia ya viashiria/alama Mungu anaweza kuleta nguvu/msisimuko/ubaridi/maumivu fulani kwenye sehemu ya mwili wako au huzuni moyoni mwako kama ishara/kiashiria cha uwepo wake juu yako na hivyo KUTAFUTA/KUTAKA USIKIVU WAKO ILI ASEME NAWE. Hivyo ni lazima uwe na ufahamu na utafute kujua kuhusu alama/namna ya kwako ambayo Mungu hutumia kutafuta usikivu wako.

  • Ni lazima ujue kutofautisha sauti ya Mungu na sauti nyingine                                                                           Hili ni muhimu sana kwako kulielewa ili usije ukaipuuza sauti ya Mungu kwa kudhani ni mawazo yako au ni ya Shetani au usije ukatekeleza jambo ukiamini kwamba Mungu amesema nawe kumbe Shetani ndiye alisema nawe. Katika             1 Samweli 3:7 imeandikwa ‘Basi Samweli alikuwa hamjui BWANA bado, na neno la BWANA lilikuwa bado halijafunuliwa kwake’. Andiko hili linatuonyesha makosa aliyofanya kijana Samweli katika kuielewa sauti ya Mungu akiichanganya na babu yake Kuhani Eli. Ni muhimu ukaelewa kwamba Mungu anaweza kusema na wewe hata kama uko katikati ya mkutano wa watu wenye kelele nyingi sana. Hii ni kwa sababu Mungu hatumii mdomo kusema nasi bali anatumia moyo wako kuzungumza. Moyo ndio kiungo muhimu cha mawasiliano kati ya mtu na Mungu.
2
Ukisoma katika Matendo ya Mitume 12:22 Biblia inasema ‘Watu wakapiga kelele, wakasema, Ni sauti ya Mungu, si sauti ya Mwanadamu’. Kauli hii ya watu ilikuja baada ya Mfalme Herode kuhutubia watu na kutoa maneno makuu. Watu waliamini kwamba ile ilikuwa sauti ya Mungu, kumbe sivyo na matokeo yake Herode alipigwa na Mungu akafa. Tahadhari, kuna wakati mtu/watu/watumishi wanaweza kunena mambo makubwa na watu wakadhani Mungu wa kweli anasema ndani yao, kumbe ni mungu wa dunia hii. Na ndio maana ni muhimu wewe binafsi uongeze ufahamu wako katika kuijua, kuisikia na kuielewa sauti ya Mungu, ili hata mwanadamu akinena unajua kwamba hili limetoka kwa Mungu wa kweli au vinginevyo.
Naam zipo sauti mbalimbali ambazo zote zinalenga kupambana/kuharibu kusudi la Mungu ndani ya mtu, zipo sauti za wanadamu (wazazi, walezi, mwenza wa ndoa, viongozi wa kiroho), ipo sauti ya Shetani kupitia majeshi ya pepo wabaya nk. Ni lazima mwanadamu amjue sana Mungu kiasi cha kuweza kutofautisha sauti hizi. Na namna pekee ya kutofautisha sauti hizi na ile ya Mungu ni kuwa na ufahamu mkubwa wa neno la Mungu kwani Mungu hawezi kukuagiza kutenda jambo lililo kinyume na neno lake.
Photo 3
Katika sehemu inayofuata nitakuonyesha mambo mengine kadhaa kujua na kuyaelewa kabla sijaanza sasa kuandika kuhusu njia ambazo Mungu hutumia kusema na wanadamu. Maombi yako ni muhimu sana.
Kwa mara nyingine heri ya Pasaka na amani ya Kristo iwe nawe. Tutaendelea na sehemu ya pili…
Utukufu na heshima vina wewe Yesu! Wastahili BWANA.

No comments:

Post a Comment

NENO NI UZIMA Designed by 5gear Copyright © 2014-2015

Theme images by Jason Morrow. Powered by Blogger.