insi Ya Kuongozwa Na Roho Mtakatifu
Injili ya Yohana ina idadi kubwa tu ya ahadi za Yesu kuhusu nafasi ya Roho Mtakatifu katika maisha ya waaminio. Hebu tusome baadhi yake.
Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele. Ndiye Roho wa kweli, ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui. Bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu (Yohana 14:16, 17).
Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote na kuwakumbusha yote niliyowaambia (Yohana 14:26).
Lakini mimi nawaambia iliyo kweli – yawafaa ninyi mimi niondoke. Kwa maana, mimi nisipo-ondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu, bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu. … Hata bado nikali ninayo mengi ya kuwaambia, lakini hamwezi kuyastahimili hivi sasa. Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote. Kwa maana, hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake. Yeye atanitukuza mimi, kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari. Na yote aliyo nayo Baba ni yangu, kwa hiyo nalisema ya kwamba atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasheni habari (Yohana 16:7; 12 – 15).
Yesu aliwaahidi wanafunzi Wake kwamba Roho Mtakatifu angekaa ndani yao. Pia angewasaidia, angewafundisha, angewaongoza na kuwaonyesha mambo yajayo. Sisi kama wanafunzi wa Kristo siku hizi tusidhani kwamba Roho Mtakatifu atafanya pungufu ya hayo.
Cha kushangaza ni kwamba, Yesu aliwaambia wanafunzi Wake kuwa ni kwa faida yao Yeye aondoke, la sivyo Roho Mtakatifu asingekuja! Hiyo ilionyesha kwao kwamba ushirika wao na Roho Mtakatifu ungekuwa wa karibu na wa ndani sana, sawa na jinsi ambavyo ingekuwa kama Yesu angekuwepo nao katika mwili wakati wote. Vinginevyo, isingekuwa faida kwao kuwa na Roho Mtakatifu badala ya kuwa na Yesu. Kwa njia ya Roho Mtakatifu, Yesu siku zote yuko pamoja nasi, na ndani yetu. Sasa – tumtazamie Roho Mtakatifu kutuongoza kwa njia gani?
Jina Lake tu – Roho Mtakatifu – linaonyesha kwamba nafasi Yake ya msingi katika kutuongoza itakuwa ni kuelekea kwenye utakatifu na kumtii Mungu. Basi, kila kitu kinachohusiana na utakatifu na kutimiz amapenzi ya Mungu hapa duniani kiko katika maongozi ya Roho Mtakatifu. Yeye atatuongoza kutii amri zote za jumla za Kristo, pamoja na zile moja moja za kipekee, zinazohusu mwito maalum sana ambao Mungu ametuitia. Hivyo, ukitaka kuongozwa na Roho kwa habari ya huduma yako maalum, lazima pia uongozwe na Roho Mtakatifu katika utakatifu kwa ujumla. Huwezi kupata kimoja bila kingine. Watumishi wengi sana wanataka kuongozwa na Roho Mtakatifu katika matendo ya huduma kuu na miujiza, lakini hawataki kushughulikia yale mambo “madogo” kuhusu utakatifu wa jumla. Hilo ni kosa kubwa. Je, Yesu aliwaongozaje wanafunzi Wake? Kimsingi ni kwa kuwapa wao mafundisho ya jumla kuhusu utakatifu. Maongozi Yake maalum kwa habari za majukumu yao kihuduma hayakuwa mara kwa mara. Ndivyo ilivyo na Roho Mtakatifu, anayekaa ndani yetu. Basi, ukitaka kuongozwa na Roho, lazima kwanza kabisa ufuate maongozi Yake juu ya kuwa mtakatifu.
Mtume Paulo aliandika hivi: “Kwa kuwa wote wanao-ongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu” (Warumi 8:14). Kuongozwa kwetu na Roho ndiyo alama kwamba tu miongoni mwa watoto wa Mungu. Hivyo, watoto wote wa Mungu wanaongozwa na Roho. Ni juu yetu sasa kama watu wenye uamuzi kutii maongozi ya Roho.
Pamoja na hayo, hakuna Mkristo anayehitaji kufundishwa jinsi ya kuongozwa na Roho Mtakatifu, kwa sababu Roho Mtakatifu anamwongoza kila Mkristo tayari. Ila, kwa upande wa pili, Shetani anajaribu kupotosha watoto wa Mungu, nasi bado tuna ile asili ya kale ya mwili ndani yetu, yenye kutuongoza kinyume na mapenzi ya Mungu. Hivyo, waamini wanahitaji kujifunza jinsi ya kutambua maongozi ya Roho na yale mengine. Hizo ni hatua kuelekea ukomavu. Lakini kweli ya msingi ni hii: Siku zote Roho atatuongoza kulingana na Neno la Mungu lililoandikwa, Naye atatuongoza siku zote kufanya kilicho sawa na chenye kumpendeza Mungu, na kitakachomletea Mungu utukufu (ona Yohana 16:14).
Sauti Ya Roho Mtakatifu
Ingawa Maandiko yanatuambia kwamba Roho Mtakatifu wakati mwingine anaweza kutuongoza kwa njia za kushangaza kama vile maono, unabii au sauti inayosikika ya Mungu, njia ya kawaida kabisa anayowasiliana nasi ni kuweka “dhana” ndani ya roho zetu. Yaani – kama Roho Mtakatifu anataka tufanye kitu fulani, “atatuvuta” ndani ya roho zetu – nasi tutajisikia “kuongozwa” kuelekea upande fulani au kufuata mwelekeo fulani.
Tunaweza kuita sauti ya roho zetu “dhamiri” yetu. Wakristo wote wanajua jinsi dhamiri yao inavyosema. Tunapojaribiwa kutenda dhambi, si kwamba tunasikia sauti ndani yetu inayosema, “Usikubali jaribu hilo.” Badala yake, tunajisikia kitu ndani yetu kikipinga jaribu hilo. Na tukikubaliana na jaribu, baada ya kutenda dhambi, hatusikii sauti ikisema, “Umetenda dhambi! Umetenda dhambi!” Tunahisi tu hukumu ndani yetu ambayo wakati huo inatuongoza kutubu na kuungama dhambi yetu.
Kwa hali hiyo hiyo, Roho Mtakatifu atatufundisha na kutuongoza katika kweli za jumla na ufahamu. Atatufundisha kwa kutupa mafunuo ya ghafula (yenye kukubaliana na Biblia kila mara) ndani yetu. Mafunuo hayo yanaweza kuhitaji dakika kumi kumweleza mtu, lakini huja kwa nukta chache tu kwa njia ya Roho Mtakatifu.
Vivyo hivyo, Roho Mtakatifu atatuongoza katika maswala ya huduma. Lazima tufanye juhudi za makusudi kuwa wasikivu kwa maongozi yale ya ndani na dhana, na tutajifunza polepole (kwa kujaribu na kukosea) kumfuata Roho kwa habari ya mambo yanayohusu huduma. Tunajikuta tukifanya makosa kwa habari ya mapenzi ya Mungu tunaporuhusu akili zetu (mawazo yetu sahihi au ya makosa) kufika kwenye nafasi ya mioyo yetu (mahali ambapo Roho anatuongoza).
Jinsi Roho Alivyomwongoza Yesu
Yesu aliongozwa na Roho Mtakatifu kwa dhana za ndani. Kwa mfano: Injili ya Marko inaeleza kilichotokea mara tu baada ya Yesu kubatizwa na Roho Mtakatifu, baada ya kubatizwa Kwake na Yohana.
Mara Roho akamtoa aende nyikani (Marko 1:12. Maneno mepesi kukazia).
Yesu hakusikia sauti au kuona maono yaliyomwongoza kwenda nyikani – alitolewa (au alisukumwa) aende. Ndivyo Roho Mtakatifu anavyotuongoza sisi kwa kawaida. Tutajisikia kuvutwa, kuongozwa, kushawishika ndani yetu kufanya kitu fulani.
Yesu alipomwambia yule mtu aliyepooza, aliyetelemshwa na wenzake kupitia darini kwamba dhambi zake zimesamehewa, Yesu alijua kwamba waandishi waliokuwepo walifikiri anakufuru. Alijuaje mawazo yao? Tunasoma hivi katika Injili ya Marko:
Mara Yesu, akifahamu rohoni mwake kwamba wanafikiri hivyo nafsini mwao, akawaambia, Mbona mnafikiri hivi mioyoni mwenu? (Marko 2:8. Maneno mepesi kukazia).
Yesu alitambua (au kufahamu) rohoni Mwake walichokuwa wanafikiria. Kama tutakuwa wasikivu ndani ya roho zetu, sisi pia tunaweza kujua jinsi ya kuwajibu wale wanaopinga kazi ya Mungu.
Uongozi Wa Roho Katika Huduma Ya Paulo
Baada ya kutumika katika huduma kwa miaka kama ishirini hivi, mtume Paulo alikuwa amejifunza vizuri jinsi ya kufuata maongozi ya Roho Mtakatifu. Roho alimwonyesha “mambo yajayo” kuhusiana na huduma kwa kiwango fulani. Kwa mfano: Wakati Paulo alipokuwa anamalizia huduma yake kule Efeso, alipewa mtazamo wa mwelekeo wa maisha yake na huduma, kwa kipindi cha miaka mitatu iliyokuwa mbele yake.
Mambo hayo yalipokwisha kumalizika, Paulo akaazimu rohoni mwake, akiisha kupita katika Makedonia na Akaya, aende Yerusalemu, akisema, Baada ya kuwako huko, yanipasa kuuona na Rumi pia (Matendo 19:21).
Ona kwamba Paulo hakukusudia mwelekeo huo katika akili zake bali katika roho yake. Hiyo inaonyesha kwamba Roho Mtakatifu alikuwa anamwongoza rohoni mwake aende Makedonia kwanza na Akaya (katika Ugiriki siku hizi), kisha aende Yerusalemu, na hatimaye aende Rumi. Na hivyo ndivyo alivyofanya. Kama Biblia yako ina ramani ya safari ya utume ya tatu ya Paulo na safari yake kwenda Rumi, unawea kufuatilia mwendo wake kutoka Efeso (alikopangia safari yake katika roho yake) kupitia Makedonia na Akaya, mpaka Yerusalemu, na miaka kadhaa baadaye, akafika Rumi.
Paulo alisafiri kuptia Makedonia na Akaya, kisha akarudi nyuma na kupita Makedonia tena, akizunguka pwani ya Bahari ya Uyunani. Kisha, alisafiri pwani ya Bahari ya Uyunani katika Asia Ndogo. Katika safari hiyo alisimama mjini Mileto, akawaita wazee wa kanisa la Efeso, akawaaga kwa kusema hivi:
Basi sasa angalieni, nashika njia kwenda Yerusalemu hali nimefungwa rohoni, nisiyajue mambo yatakayonikuta huko; isipokuwa Roho Mtakatifu mji kwa mji hunishuhudia akisema ya kwamba vifungo na dhiki vyaningoja (Matendo 20:22, 23. Maneno mepesi kukazia).
Paulo alisema alikuwa “amefungwa rohoni”. Maana yake ni kwamba alikuwa na msukumo rohoni mwake uliokuwa unamwongoza kwenda Yerusalemu. Hakuwa na picha kamili juu ya kitakachotokea atakapofika Yerusalemu, lakini alisema kwamba katika kila mji aliosimama akisafiri, Roho Mtakatifu alishuhudia kwamba vifungo na mateso vinamsubiri huko Yerusalemu. Je, Roho Mtakatifu “alishuhudiaje” kuhusu vifungo na mateso hayo yaliyokuwa yanamngojea Yerusalemu?
Mifano Mwili
Katika sura ya 21 ya Kitabu cha Matendo, tuna habari mbili zenye kujibu hilo swali. Mfano wa kwanza ni wakati Paulo alipofika katika mji wa Tiro, uliokuwa bandari katika Bahari ya Mediteranea.
Tukiisha kuwaona wanafunzi tukakaa huko siku saba, nao wakamwambia Paulo kwa uweza wa Roho, asipande kwenda Yerusalemu (Matendo 21:4).
Mstari huu umewafanya waandishi wengine wa vitabu vya kufafanua Biblia kusema kwamba Paulo aliacha kumtii Mungu kwa kuendelea na safari yake kwenda Yerusalemu. Lakini, kutokana na habari zaidi tupatazo katika kitabu cha Matendo, hatuwezi kusema hivyo. Hii itaonekana tunapoendelea kufuatilia kisa hiki.
Inaonekana kwamba wanafunzi wa Tiro walikuwa wasikivu, na walihisi kwamba dhiki ilikuwa inamsubiri Paulo huko Yerusalemu. Wakajaribu sana kumzuia asiende. Tafsiri moja ya Kiingereza ya Agano Jipya inatoa mwanga zaidi, maana mstari huo unasomeka hivi: “Kwa sababu ya dhana zilizotolea na Roho, walizidi kumwonya Paulo asikanyage Yerusalemu.”
Wale wanafunzi huko Tiro hawakufanikiwa, kwa sababu Paulo aliendelea na safari yake kwenda Yerusalemu, licha ya maonyo yote hayo.
Hii inatufundisha kwamba tunapaswa kuwa makini tusiongeze tafsiri yetu wenyewe kwa mafunuo tunayopokea katika roho zetu. Paulo alifahamu vizuri kabisa kwamba taabu ilikuwa inamsubiri huko Yerusalemu, lakini pia alijua kwamba ni mapenzi ya Mungu yeye kwenda huko. Kama Mungu atatufunulia kitu kwa Roho Mtakatifu, haimaanishi kwamba tunapaswa kukisema. Pia, tuwe makini tusije tukaongeza tafsiri yetu wenyewe katika yale ambayo Roho Mtakatifu amefunua.
Mapumziko Mafupi Kaisaria
Mji uliofuata katika safari ya Paulo kwenda Yerusalemu ni bandari ya Kaisaria.
Basi, tulipokuwa tukikaa huko siku nyingi, nabii mmoja jina lake Agabo akashuka kutoka Uyahudi. Alipotufikia, akautwaa mshipi wa Paulo, akajifunga miguu na mikono, akasema, Roho Mtakatifu asema hivi, Hivyo ndivyo Wayahudi wa Yerusalemu watakavyomfunga mtu mwenye mshipi huu, nao watamtia katika mikono ya watu wa Mataifa (Matendo 21:10, 11).
Hapo tena ni mfano mwingine wa Roho Mtakatifu akimshuhudia Paulo kwamba “vifungo na dhiki” vilikuwa vinamngojea Yerusalemu. Lakini, ona kwamba Agabo hakusema, “Kwa hiyo, Bwana asema hivi: Usiende Yerusalemu!” Hapana. Mungu alikuwa anamwongoza Paulo aende Yerusalemu, na kwa unabii wa Agabo alikuwa anamwandaa tu kwa ajili ya matatizo yaliyokuwa yanamsubiri huko. Pia, ona kwamba unabii wa Agabo ulithibitisha tu kitu ambacho Paulo alijua tayari katika roho yake, miezi mingi kabla. Hatupaswi kuongozwa na unabii kamwe. Kama unabii hauthibitishi tunachofahamu tayari, tusiufuate.
Unabii wa Agapo unaweza kuangukia katika fungu la “maongozi yenye kusisimua” kwa sababu ulizidi dhana ya ndani ya roho ya Paulo. Wakati Mungu anaporuhusu “maongozi ya kusisimua” kama vile maono au kusikia sauti kabisa, ni kwa sababu anajua kwamba njia haitakuwa rahisi. Tutahitaji uhakikisho wa ziada unaoletwa na maongozi aina hiyo. Kwa habari ya Paulo ni kwamba, alikuwa anaelekea kwenye kupokea chupuchupu kuuawa na kundi la watu wenye hasira, na angekaa gerezani miaka kadhaa kabla hajasafiri kwenda Rumi kama mfungwa. Ila, kwa sababu ya maongozi hayo ya kusisimua aliyopata, aliweza kuwa na amani kamilifu kabisa katika hayo yote, kwa sababu alijua kwamba hatima yake ingekuwa nzuri.
Katika Minyororo, Katika Mapenzi Ya Mungu
Paulo alipofika Yerusalemu alikamatwa na kufungwa. Hapo tena alipokea maongozi ya kusisimua. Safari hii, ni maono ya Yesu Mwenyewe.
Usiku ule Bwana akasimama karibu naye [Paulo], akasema, Uwe na moyo mkuu; kwa sababu, kama ulivyonishuhudia habari zangu Yerusalemu, imekupasa kunishuhudia vivyo hivyo Rumi nako (Matendo 23:11).
Angalia kwamba Yesu hakusema hivi: “Unaona sasa Paulo! Unafanya nini hapa? Nilijaribu kukuonya usije Yerusalemu!” Yesu alithibitisha tu maongozi ambayo Paulo alikuwa ametambua rohoni mwake miezi kadhaa kabla. Paulo alikuwa katika mapenzi ya Mungu kabisa huko Yerusalemu, ili kushuhudia habari za Yesu. Hatimaye angemtangaza Kristo hata Rumi kwenyewe.
Tusisahau kwamba sehemu ya wito wa Paulo hasa ilikuwa kuwashuhudia Wayahudi na Mataifa, pamoja na wafalme pia (ona Matendo 9:15). Paulo alipokaa kifungoni huko Yerusalemu na baadaye Kaisaria, alipata nafasi ya kushuhudia mbele za Feliksi aliyekuwa Mkuu wa Mkoa, pamoja na Porkio Festo, na Mfalme Agripa, aliyekaribia “kushawishiwa” kumwamini Yesu (Matendo 26:28). Mwishowe, Paulo alipelekwa Rumi kushuhudia mbele za Nero, aliyekuwa mfalme wa dola ya Rumi.
Kuelekea Kwa Nero
Paulo alipokea tena maongozi ya Mungu kwa kusikiliza roho yake akiwa safarini kwenda Italia. Nahodha wa merikebu pamoja na kiongozi wa safari walipokuwa wanajaribu kuamua bandari ipi ya Krete watie nanga ili kusubiri majira ya baridi, Paulo alipata ufunuo.
Na wakati mwingi ulipokwisha kupita na safari ikiwa ina hatari sasa kwa sababu siku za kufunga zilikuwa zimekwisha kupita, Paulo akawaonya, akawaambia, Wanaume, naona kwamba safari hii itakuwa na madhara na hasara nyingi, si ya shehena na merikebu tu, ila na maisha yetu pia (Matendo 27:9, 10. Maneno mepesi kukazia).
Paulo alitambua mambo ambayo yangetokea. Bila shaka kutambua huko kulitokana na dhana iliyotolewa na Roho.
Kwa bahati mbaya, yule nahodha wa merikebu hakumsikiliza Paulo, naye alijaribu kufikia bandari nyingine. Matokeo ni kwamba merikebu ilinaswa katika dhoruba kali kwa majuma mawili. Hali ikawa hatari kiasi kwamba mabaharia wa ile merikebu walitupa mizigo yote siku ya pili, na siku ya tatu wakatupa mpaka vyombo vya merikebu. Baadaye, Paulo akapokea tena maongozi mengine. Tunasoma hivi:
Jua wala nyota hazikuonekana kwa muda wa siku nyingi, na tufani kuu ikatushika, basi tukakata tamaa ya kuokoka. Na walipokuwa wamekaa wakati mwingi bila kula chakula, Paulo akasimama katikati yao akasema, Wanaume, ilinipasa kunisikiliza mimi na kutokung’oa nanga huko Krete, na kupata madhara haya na hasara hii. Sasa nawapeni shauri, iweni na moyo mkuu, kwa maana hapana hata nafsi moja miongoni mwenu atakayepotea, ila merikebu tu. Kwa maana usiku huu wa leo malaika wa Mungu yule ambaye mimi ni wake, naye ndiye nimwabuduye, alisimama karibu nami akaniambia, Usiogope Paulo. Huna budi kusimama mbele ya Kaisari; tena tazama, Mungu amekupa watu wote wanaosafiri pamoja nawe. Basi wanaume, changamkeni; kwa sababu namwamini Mungu ya kwamba yatakuwa vile vile kama nilivyoambiwa. Lakini hatuna hudi kupwelewa katika kisiwa kimoja (Matendo 27:20-26).
Bila shaka sababu ya Mungu kumpa Paulo “maongozi ya kusisimua” ya ziada iko wazi, ukizingatia hali halisi. Baada ya tukio hili, Paulo angekabiliwa na kuvunjikiwa merikebu. Baadaye kidogo angeumwa na nyoka wa sumu (ona Matendo 27:41 hadi 28:5). Ni vizuri kuwa na malaika atakayekwambia kwamba mambo yote yatakuwa mazuri kabla hayajatokea!
Mawaidha Muhimu
Anza kutafuta rohoni mwako zile dhana na hisia ambazo ni maongozi ya Roho Mtakatifu. Pengine mwanzoni utakosea kidogo, ukidhani kwamba Roho Mtakatifu anakuongoza na kumbe sivyo, lakini hiyo ni kawaida. Usivunjike moyo; endelea tu.
Pia inakusaidia kupata muda wa utulivu mbele za Mungu, ukiomba kwa lugha na kusoma Biblia. Tuombapo kwa lugha, iombayo ni roho yetu, nasi kwa kawaida tunakuwa wasikivu wakati huo. Kwa kusoma na kutafakari Neno la Mungu, tunakuwa wasikivu zaidi kwa roho zetu kwa sababu Neno la Mungu ni chakula chetu cha kiroho.
Mungu anapokuongoza mwelekeo fulani, uongozi huo haupungui. Yaani, unapaswa kuendelea kuombea maamuzi fulani makubwa kwa kitambo, ili kuwa na uhakika kwamba ni Mungu ndiye anayekuongoza, wala si mawazo yako au hisia zako. Kama huna amani moyoni wakati unapoomba juu ya mwelekeo fulani, usielekee huko mpaka upate amani.
Ukipata maongozi ya kusisimua, vizuri, ila, usijaribu “kuamini” ili uone maono au usikie sauti. Mungu hajatuahidi kutuongoza hivyo (japo wakati mwingine Yeye hufanya hivyo kulingana na mapenzi Yake kama Mwenyezi). Ila, tunaweza kuamini wakati wote kwamba atatuongoza kwa ushuhuda wa kutoka ndani.
Mwisho: Usiongeze chochote katika yale ambayo Mungu anakwambia. Mungu anaweza kukufunulia huduma fulani ambayo amekuandalia kwa wakati ujao, lakini wewe unaweza kudhani kwamba wakati wa kutimia kwa hilo ni juma lijalo kumbe ni miaka mingi baadaye. Mimi najua hayo kwa uzoefu nilio nao. Usifikiri tu. Paulo alijua kidogo juu ya wakati wake wa baadaye. Hakujua yote, na ni kwa sababu Mungu hakufunua kila kitu. Mungu anataka tuendelee kutembea kwa imani wakati wote.