Karama Za Roho Mtakatifu
Biblia imejaa mifano mingi tu ya watu – wanaume kwa wanawake – kupewa uwezo usio wa kawaida – wa kiMungu – na Roho Mtakatifu. Katika Agano Jipya, kuwezeshwa huko kusiko kwa kawaida kunaitwa “karama za Roho.” Ukweli ni kwamba ni zawadi kwa sababu haziwezi kufanyiwa kazi ndipo zipatikane. Ila, tusisahau kwamba Mungu huwainua wale anaoweza kuwaamini. Yesu alisema hivi, “Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia; na aliye dhalimu katika lililo dogo huwa dhalimu katika lililo kubwa pia” (Luka 16:10). Basi, tungetazamia kwamba karama za Roho zitatolewa kwa wale ambao wamethibitisha kuaminika kwao mbele za Mungu. Kujitoa kabisa na kukubali kuongozwa na Roho Mtakatifu pia ni muhimu, maana Mungu atawatumia watu aina hiyo kwa njia isiyo ya kawaida. Kwa upande mwingine, Mungu aliwahi kumtumia punda kutabiri. Kwa hiyo, anaweza kumtumia yeyote apendaye. Kama ingebidi kutusubiri mpaka tukamilike ndipo atutumie, asingemtumia yeyote kati yetu!
Katika Agano Jipya, karama za Roho zimeorodheshwa katika 1Wakorintho 12, nazo ni tisa katika ujumla wake, kama ifuatavyo:
Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima na mwingine neno la maarifa, apendavyo Roho yeye yule. Mwingine imani katika Roho yeye yule, na mwingine karama za kuponya katika Roho yule mmoja; na mwingine, matendo ya miujiza. Na mwingine unabii, na mwingine kupambanua roho. Mwingine aina za lugha, na mwingine tafsiri za lugha (1Wakor. 12:8-10).
Kujua jinsi ya kufafanua kila karama moja si kigezo cha kutumiwa na Mungu katika utendaji wake. Manabii wa Agano la Kale na makuhani na wafalme, pamoja na wahudumu katika kanisa la kwanza la Agano Jipya walitenda kazi kwa karama za Roho bila hata ya kujua jinsi ya kuzipanga au kuzifafanua. Lakini, kwa kuwa karama za Roho zimepangwa kwenye orodha kwa ajili yetu katika Agano Jipya, bila shaka Mungu anataka tuzielewe. Paulo aliandika hivi: “Basi ndugu zangu, kwa habari ya karama za Roho, sitaki mkose kufahamu” (1Wakor. 12:1).
Orodha Ya Zile Karama Tisa
Zile karama tisa za Roho zimepangwa katika mafungu mengine tena siku hizi, kama matatu hivi: (1) Za kuzungumza, ambazo ni: aina za lugha, tafsiri za lugha, na unabii. (2) Za ufunuo, ambazo ni: neno la hekima, neno la maarifa, na kupambanua roho. (3) Za nguvu, ambazo ni: matendo ya miujiza, imani maalum, na karama za kuponya. Karama tatu husema kitu; tatu hufunua kitu; na tatu hufanya kitu. Karama hizo zote zilidhirishwa na kufanya kazi katika kipindi cha agano la zamani, isipokuwa tu ile ya aina za lugha na tafsiri za lugha. Hizo mbili ni maalum kwa ajili ya agano la sasa.
Agano Jipya halitoi maelezo kuhusu matumizi sahihi ya hizo “karama za nguvu”, na kuna maelezo kidogo sana kuhusu matumizi sahihi ya “karama za ufunuo”. Ila, kuna mafundisho mengi tu kuhusu matumizi sahihi ya “karama za kusema” yatolewayo na Paulo, na pengine ni kwa sababu mbili.
Kwanza – karama za kusema ndizo zenye kudhihirishwa mara nyingi sana katika makusanyiko kanisani, na zile za ufunuo hudhihirishwa kidogo sana, na zile za nguvu si mara nyingi. Basi, ni sawa kuhitaji mafundisyho mengi juu ya karama ambazo zinadhihirishwa mara kwa mara katika makusanyiko ya kanisa.
Pili – karama za kusema zinaonekana kuhitaji sehemu kubwa ya ushirikiano wa mwanadamu. Basi, ndizo rahisi sana kutumiwa vibaya. Ni rahisi zaidi kuongeza kitu kwenye unabii na kwa njia hiyo kuuharibu, kuliko karama ya kuponya.
Kama Roho Apendavyo
Ni muhimu kutambua kwamba karama za Roho hutolewa kama Roho apendavyo, si kama mtu yeyote apendavyo. Biblia inaweka jambo hilo wazi kabisa, hivi:
Lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yakekama apendavyo yeye (1Wakor. 12:11. Maneno mepesi kukazia).
Mungu naye akishuhudu pamoja nao kwa ishara na ajabu na nguvu za namna nyingi, na kwa magawanyo ya Roho Mtakatifu, kama alivyopenda mwenyewe (Waebrania 2:4. Maneno mepesikukazia).
Yawezekana mtu kutumiwa mara kwa mara katika karama fulani, lakini hakuna mwenye kumiliki karama yoyote. Kwa kuwa tu ulipata upako mara moja kufanya muujiza si ishara kwamba wewe waweza kufanya muujiza wakati wowote utakapo, wala si uhakikisho kwamba utatumiwa tena kufanya muujiza.
Tutajifunza kwa kifupi na kutazama mifano michache ya kiBiblia ya kila karama. Ila, kumbuka kwamba Mungu anaweza kudhihirisha neema Yake na nguvu Zake kwa njia nyingi zisizo na mipaka, hivyo si rahisi kufafanua hakika jinsi ambavyo kila karama itakavyofanya kazi kila mara. Tena, hakuna maelezo ya zile karama tisa za kiroho katika Maandiko – kuna majina yake tu. Hivyo, tunaweza tu kutazama Maandiko na kuona mifano itolewayo, kisha kujaribu kuamua kwamba kila moja iangukie wapi, na hatimaye kuzifafanua kwa tofauti zake zilizo dhahiri. Kwa kuwa zipo njia nyingi san asana ambazo Roho Mtakatifu anaweza kujifunua Mwenyewe kwa njia ya karama za kiroho, si busara kujaribu kubana sana mafafanuzi yetu. Kuna karma zingine ambazo ni kama muunganiko wa karama kadhaa. Paulo aliandika hivi kwa habari hiyo:
Basi, pana tofauti za karama, bali Roho ni yeye yule. Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule. Kisha pana tofauti za kutenda kazi [au matokeo], bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. Lakini, kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana (1Wakor. 12:4-7. Maneno mepesi kukazia).
Karama Za Nguvu
1) Karama za kuponya: Karama za kuponya bila shaka zinahusika na wagonjwa kupokea uponyaji. Mara nyingi zimefafanuliwa kwamba ni kuwezeshwa kusiko kawaida ili kuponya watu wagonjwa. Hakuna haja ya kuongezea hapo. Katika sura iliyopita tulitzama mfano mmoja wa karama ya kuponya ikidhihirishwa kwa Yesu wakati alipomponya mtu kiwete pale Birika la Betzata (ona Yohana 5:2-17).
Mungu alimtumia Elisha kumponya ukoma Naamani wa Shami, ambaye alikuwa mwabudu sanamu (ona 2Waf. 5:1-14). Kama tulviyojifunza wakati wa kutazama maneno ya Yesu katika Luka 4:27 kwa habari ya uponyaji wa Naamani, Elisha asingeweza kumponya mwenye ukoma yeyote wakati wowote aliotaka. Mara tu aliwezeshwa kwa njia isiyo ya kawaida kumshauri Naamani akajichovye mara saba katika Mto Yordani, na wakati Naamani alipotii, alitakaswa na ukoma wake.
Mungu alimtumia Petro kumponya yule kiwete pale kwenye mlango wa Hekalu ulioitwa Mzuri kwa njia ya karama ya kuponya (ona Matendo 3:1-10). Si kwamba yule kiwete aliponywa tu, bali ishara hiyo isiyo ya kawaida iliwavutia watu wengi wasikilize Injili kutoka kinywani kwa Petro, na kiasi cha watu elfu tano waliokoka na kuongezeka kanisani siku hiyo. Karama za kuponya mara nyingi hufanya kazi mbili: kuponya wagonjwa na kuwavutia watu ambao hawajaokoka, wamjie Kristo.
Wakati Petro alipokuwa anahubiri ujumbe wake kwa watu waliokusanyika siku hiyo, alisema hivi:
Enyi Waisraeli! Mbona mnastaajabia haya, au mbona mnatukazia macho sisi, kana kwamba tumemfanya huyu aende kwa nguvu zetu sisi au kwa utauwa wetu sisi? (Matendo 3:12).
Petro alitambua kwamba Mungu hakumtumia kumponya yule kiwete kwa sababu ya nguvu aina yoyote aliyokuwa nayo yeye, au kwa sababu ya jinsi alivyokuwa mtakatifu. Kumbuka kwamba Petro, miezi miwili tu kabla ya muujiza huo alikuwa amemkana Yesu akasema hamjui kabisa! Ukweli kwamba Mungu alimtumia Petro kwa miujiza kiasi hicho katika kurasa za kwanza za Matendo ya Mitume ukuze imani yetu na uhakika kwamba Mungu atatutumia sisi pia kama apendavyo.
Wakati Petro alipojaribu kueleza jinsi huyo mtu alivyoponywa, sidhani kama angesema ni “karama ya kuponya”. Kitu alichojua Petro ni kwamba yeye na Yohana walikuwa wanapita karibu na mtu kiwete, na ghafula akapata upako wa imani kwa ajili ya mtu huyo kuponywa. Basi, akamwamuru mtu huyo atembee katika jina la Yesu, akamshika mkono wake wa kuume na kumwinua. Yule kiwete akaanza “kutembea na kuruka ruka, na kumsifu Mungu.” Petro anafafanua kama ifuatavyo:
Na kwa imani katika jina lake, jina lake limetia nguvu mtu huyu mnayemwona na kumjua, na imani ile iliyo kwake yeye imempatia huyu uzima huu mkamilifu mbele yenu ninyi nyote (Matendo 3:16).
Inatakiwa imani maalum sana kumshika mtu kiwete kwa mkono na kumwinua, na kutazamia atatembea! Pamoja na hiyo karama ya kuponya, kulikuwepo pia na kutolewa kwa imani ili kuwezesha hilo kufanyika.
Kuna wanaodhani kwamba sababu ya karama hii kuwa “za” ni kwamba zipo karama mbalimbali zinazoponya aina mbalimbali za magonjwa. Wale ambao wametumika sana katika karama za kuponya wanagundua wkati mwingine kwamba magonjwa fulani huponywa zaidi katika huduma zao kuliko mengine. Kwa mfano: Mwinjilisti Filipo alionekana kuwa na mafanikio sana katika kuponya watu waliopooza na vilema (Matendo 8:7). Kuna baadhi ya wainjilisti wa karne za nyuma ambao, kwa mfano, wamefanikiwa sana kwa habari ya kuponywa vipofu au viziwi au wenye shida za moyo na kadhalika, kutegemeana na karama gani za kuponya zilizodhihirishwa kupitia kwao mara nyingi.
2) Karama ya imani na matendo ya miujiza: Karama ya imani na ya matendo ya miujiza ni kama zinafanana. Katika hizi mbili, mwenye kutumiwa hupokea ghafula imani kwa ajili ya yasiyowezekana. Tofauti kati ya hizo mbili mara nyingi hufafanuliwa kama ifuatavyo: Kuhusu karama ya imani, ni kwamba yule anayetiwa upako hupewa imani ili apokee muujiza kwa ajili yake mwenyewe, ila, kwa habari ya karama ya matendo ya miujiza ni kwamba, mhusika hupewa imani ili kutenda muujia kwa ajili ya mwingine.
Karama ya imani wakati mwingine huitwa “imani maalum” au ya kipekee kwa sababu ni kupewa imani inayozidi ya kawaida. Imani ya kawaida huja kwa kusikia ahadi ya Mungu, wakati ambapo imani maalum huja kwa toleo la ghafula la Roho Mtaka tifu. Wale ambao wamewahi kufahamu karama hii ya imani maalum hutaarifu kwamba mambo ambayo walikuwa wanayahesabu hayawezekani yanawezekana, na ukweli ni kwamba wanajikuta haiwezekani kuwa na shaka. Mambo ni hivyo hivyo kuhusu karama ya matendo ya miujiza.
Habari ya rafiki watatu wa Danieli – Shadraka, Meshaki na Abednego – ni mfano mzuri sana jinsi ambavyo “imani maalum” inavyofanya isiwezekane kuwa na shaka. Wakati walipotupwa katika tanuru la moto kwa kukataa kusujudia sanamu ya mfalme, wote walipewa karama hiyo ya imani maalum. Kweli – kukubali kuingia katika tanuru la moto mkali kulihitaji imani zaidi ya kawaida! Hebu tutazame imani waliyo-onyesha hao vijana watatu, mbele ya mfalme.
Ndipo Shadraka na Meshaki na Abednego wakajibu, wakamwambia mfalme, Ee Nebukadreza! Hamna haja kukujibu kat ika neno hili. Kama ni hivyo, Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto; naye atatuokoa na mkono wako, Ee mfalme. Bali kama si hivyo [yaani, kama hutatutupa katika tanuru hiyo ya moto], ujue ee mfalme ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu yako, wala kuisujudia hio sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha (Danieli 3:16-18. Maneno mepesi kukazia).
Ona kwamba karama ilikuwa inafanya kazi hata kabla hawajatupwa katika tanuru la moto. Hapakuwa na shaka katika akili zao kwamba Mungu angewakomboa.
Eliya alifanya kazi chini ya karama hiyo ya imani maalum wakati alipolishwa kila siku na kunguru, katika kipindi cha njaa ya miaka mitatu wakati wa utawala wa Mfalme mwovu, Ahabu (ona 2Waf. 17:1-6). Unahitaji imani ya ziada kumwamini Mungu kwamba atatumia ndege wakuletee chakula asubuhi na jioni. Ingawa Mungu hajatuahidi popote katika Neno Lake kwamba kunguru watatuletea chakula kila siku, tunaweza kutumia imani ya kawaida kumtegemea Mungu kwamba mahitaji yetu yatatoshelezwa – kwa sababu hiyo ni ahadi iliyopo (ona Mat hayo 6:25-34).
Matendo ya miujiza yalifanyika mara kwa mara katika huduma ya Musa. Karama hii ilikuwa kazini wakati alipogawa Bahari ya Shamu (ona Kutoka 14:13-31), na mapigo mbalimbali yalipoishukia nchi ya Misri.
Karama hii ilikuwepo katika huduma ya Yesu wakati alipowalisha watu elfu tano kwa kuongeza mikate michache na samaki (ona Mathayo 14:15-21).
Mfano mwingine wa karama hii ni wakati Paulo alipomfanya Elima mchawi kuwa kipofu kwa muda kwa sababu alikuwa anapingana na huduma yake pale kisiwani Kipro (ona Matendo 13:4-12).
Karama Za Ufunuo
1) Neno la maarifa na neno la hekima: Karama ya neno la maarifa mara nyingi hufafanuliwa kwamba ni kupewa kwa ghafula kufahamu habari fulani, ya wakati uliopita au uliopo. Mungu ambaye ana maarifa yote, wakati mwingine atatoa kiasi kidogo cha maarifa hayo. Pengine ndiyo sababu huitwa neno la maarifa. Neno ni sehemu ndogo ya sentensi, na neno la maarifa linaweza kuwa sehemu ndogo ya maarifa ya Mungu.
Neno la hekima ni sawa tu na neno la maarifa, ila mara nyingi hufafanuliwa kama uwezo wa ghafula usio wa kawaida, wa kujua matukio yajayo. Wazo la hekima mara nyingi huhusiana na kitu fulani cha baadaye. Hapa tena si kwamba tafsiri hizi ni kamilifu.
Hebu tutazame mfano wa Agano la Kale kuhusu neno la maarifa. Baada ya Elisha kumtakasa ukoma Naamani Mshami, Naamani alimpa Elisha fedha nyingi sana kama shukrani kwa kuponywa. Elisha alikataa zawadi hiyo, mtu yeyote asije akafkiri kwamba uponyaji wa Naamani ulinunuliwa badala ya kutolewa na Mungu kwa neema tu. Mtumishi wa Elisha aliyeitwa Gehazi, akaona nafasi ya kujipatia utajiri binafsi, naye kwa siri akapokea kiasi fulani cha malipo yaliyokusudiwa kumfikia Naamani. Baada ya Gehazi kuficha fedha yake aliyopata kwa udanganyifu, alisimama mbele ya Elisha. Tunasoma hivi:
Elisha akamwambia, Watoka wapi Gehazi? Akanena, Mtumwa wako hakuenda mahali. Akamwambia, Je! Moyo wangu haukwenda na wewe, hapo alipogeuka yule mtu katika gari ili akulaki? (2Waf. 5:25b, 26a).
Mungu ambaye alifahamu vizuri tendo baya la Gehazi, alimfunulia nabii Elisha kwa njia ya ajabu. Habari hii inaonyesha dhahiri ya kwamba Elisha “hakumiliki” karama ya neno la maarifa – yaani, hakujua kila kitu kuhusu kila mtu kila wakati. Kama ingekuwa hivyo, Gehazi asingeota ndoto kwamba angeweza kuficha dhambi yake. Elisha alifahamu vitu kwa njia isiyo ya kawaida wakati tu Mungu alipomfunulia vitu hivyo, mara kwa mara. Karama ilifanya kazi kama Roho alivyopenda.
Yesu alitumia karama hiyo wakati alipomwambia yule mwanamke pale kisimani Samaria kwamba alikuwa na wanaume watano (ona Yohana 4:17, 18).
Petro alitumia karama hii wakati alipojua kimuujiza kwamba Anania na Safira walikuwa wanadanganya kusanyiko kwamba walichokuwa wanatoa ndiyo bei kamili ya uwanja wao waliokuwa wameuuza karibuni (ona Matendo 5:1-11).
Kuhusiana na karama ya neno la hekima, inadhihirishwa mara kwa mara katika Agano la Kale kwa manabii wote. Kila walipotabiri tukio la wakati ujao, neno la hekima lilikuwa kazini. Yesu alipewa karama hii mara kwa mara pia. Alitabiri kuhusu kuharibiwa kwa mji wa Yerusalemu, kuhusu kusulubiwa Kwake, na matukio ambayo yangetokea duniani kabla ya kuja Kwake mara ya pili (ona Luka 17:22-36; 21:6-28).
Mtume Yohana alitumiwa katika karama hii wakati alipofunuliwa zile hukumu za Wakati wa Dhiki Kuu. Ametuandikia hayo yote katika Kitabu cha Ufunuo.
2) Karama ya kupambanua roho: Hii karama mara nyingi inafafanuliwa kuwa ni kuwezeshwa kwa njia isiyo ya kawaida, kuona au kutambua kitu kinachoendelea katika ulimwengu wa roho.
Maono katika akili au macho ya mwamini yanaweza kuwekwa katika fungu la kupambanua roho. Hii karama inaweza kumruhusu mwamini aone malaika, mapepo, au hata amwone Yesu Mwenyewe, kama ilvyotokea kwa Paulo mara kadha (ona Matendo 18:9, 10; 22:17-21; 23:11).
Wakati Elisha na mtumishi wake walipokuwa wanatafutwa na jeshi la Shamu, walijikuta wamenaswa katika mji wa Dotani. Mtumishi wa Elisha alitazama juu ya kuta za mji na baada ya kuona makundi ya askari yanajikusanya, alipata wasiwasi sana.
[Elisha] Akamjibu, Usiogope; maana walio pamoja nasi ni wengi kuliko wale walio pamoja nao. Elisha akaomba akasema, Ee BWANA! Nakusihi mfumbue macho yake, apate kuona. BWANA akamfumbua macho yule mtumishi; naye akaona na tazama, kile kilima kilikuwa kimejaa farasi na magari ya moto yaliyomzunguka Elisha pande zote (2Waf. 6:16, 17).
Je, ulifahamu kwamba malaika husafiri kwa farasi wa kiroho na magari ya kiroho? Siku moja utawaona mbinguni, lakini mtumishi wa Elisha alipewa uwezo wa kuwaona hapa duniani.
Kwa njia ya karama hii, aaminiye anaweza kumtambua pepo mchafu anayemtesa mtu fulani na kuwa na uwezo wa kutambua ni roho ya aina gani.
Pia, karama hii haiwezeshi kuona katika ulimwengu wa roho tu bali hata kupambanua kwa namna nyingine yoyote katika ulimwengu wa kiroho. Kwa mfano: inakuwezesha kusikia kitu kutoka katika ulimwengu wa kiroho, kama sauti ya Mungu Mwenyewe.
Mwisho – hii karama si “ya utambuzi” kama ambavyo wengine wanazoea kuiita. Watu wenye kudai kuwa nayo wakati mwingine hudhani kwamba wanaweza kutambua makusudi au nia za wengine, lakini si kweli. “Karama” wanayodai kuwa nayo ni sahihi ikielezwa kwamba ni “karama ya kukosoa na kuhukumu wengine.” Ukweli ni kwamba pengine hata wewe ulikuwa nayo kabla ya kuokoka, na sasa kwa kuwa umeokoka, Mungu anataka akuweke huru kutokana nayo moja kwa moja!
Karama Za Kusema
1) Karama ya unabii: Karama ya unabii ni uwezo usio wa kawaida kusema kwa uvuvio wa Mungu maneno kwa lugha ya msemaji. Kila mara inaweza kuanza kwa maneno yafuatayo: “Bwana asema hivi.
Karama hii si kuhubiri wala kufundisha. Mahubiri na mafundisho yaliyovuviwa yana kiwango fulani cha unabii kwa sababu hutokea kwa upako wa Roho Mtaka tifu, lakini si unabii halisi. Mara nyingi mhubiri mwenye upako au mwalimu atasema mambo kwa uvuvio wa papo kwa papo, ambayo hakupanga kuyasema, lakini huo si unabii japo anayosema yanaweza kuhesabika kuwa ya kinabii.
Karama ya unabii yenyewe hufanya kazi ya kujenga, kufariji na kutia moyo.
Bali yeye ahutubuye asema na watu maneno ya kuwajenga, na kuwafariji na kuwatia moyo (1Wakor. 14:3).
Hivyo basi, karama ya unabii peke yake haina ufunuo wowote. Yaani, haifunui chochote kuhusu wakati uliopita, uliopo au ujao, tofauti na neno la hekima au neno la maarifa. Kama tulivyo-ona mwanzoni, karama za Roho zinaweza kufanya kazi kwa kushirikiana. Basi, neno la hekima au neno la maarifa yanaweza kufikishwa yanakotakiwa kwa njia ya unabii.
Tunaposikia mtu akitoa unabii katika kusanyiko, wenye kueleza matukio ya wakati ujao, si kwamba tumesikia unabii tu, bali tunakuwa tumesikia neno la hekima likifikishwa kwetu kwa karama ya unabii. Ile karama ya unabii kama ilivyo itasikika kana kwamba ni mtu anasoma maneno ya kujenga kutoka kwenye Biblia, kama vile “Mwimarike katika Bwana na katika uwezo Wake,” au “Sitakuacha wala sitakupungukia.”
Kuna wanaoamini kwamba unabii wa Agano Jipya haupaswi kuwa na chochote ambacho ni “kinyume” maana hautatimiza masharti ya “kujenga, kufariji na kutia moyo”. Si kweli. Kuweka mipaka kuhusu atakachosema Mungu kwa watu Wake, na kumruhusu aseme yaliyo “mazuri” tu hata kama wanastahili kukemewa, ni kujitukuza juu ya Mungu. Yawezekana kukemea kukaangukia kwenye kufariji na kutia moyo.Utaona kwamba hata zile jumbe za Bwana Yesu kwa yale makanisa saba ya Asia katika Ufunuo wa Yohana zina maneno ya kukemea. Je, tuziache? Hapana!
2) Karama ya aina za lugha na tafsiri za lugha: Karama ya aina za lugha ni ule uwezo wa ghafula wa kusema lugha ambayo haijulikani na msemaji. Hii karama kwa kawaida inaambatana na ile ya tafsiri za lugha, ambayo ni kuwezeshwa ghafula kufasiri kilichosemwa katika lugha isiyojulikana.
Karama hii inaitwa tafsiri za lugha. Basi, tusitazamie tafsiri ya neno kwa neno ya jumbe zinazotolewa kwa lugha. Kwa maana hiyo, inawezekana kuwa na “ujumbe mfupi kwa lugha” na tafsiri ndefu, na hata kinyume chake.
Karama hii ya kutafsiri lugha inafanana sana na unabii kwa sababu yenyewe kama ilivyo haina ufunuo, na kwa kawaida huwa ni kwa ajili ya kujenga, kufariji na kutia moyo. Kulingana na 1Wakorintho 14:5, tunaweza kusema kwamba lugha na tafsiri ya lugha ni sawa na unabii, kwa sababu hii:
Maana yeye ahutubuye ni mkuu kuliko yeye anenaye kwa lugha, isipokuwa afasiri, ili kusudi kanisa lipate kujengwa.
Kama tulivyokwisha ona kabla, hakuna mafundisho katika Biblia kuhusu jinsi ya kufanya kazi na karama za nguvu. Yapo mafundisho kidogo kuhusu jinsi ya kutumia karama za ufunuo, ila, yapo mafundisho mengi sana sana kuhusu jinsi ya kufanya kazi na karama za kusema. Kwa kuwa kulikuwepo na hali ya kutoelewa katika kanisa la Korintho juu ya utendaji wa karama za kusema, Paulo alitumia karibu sura nzima ya kumi na nne ya Wakorintho wa Kwanza kushughulikia swala hilo.
Tatizo la kwanza lilihusu matumizi sahihi ya kunena kwa lugha zingine kwa sababu, kama ambavyo tumekwisha ona katika sura kuhusu ubatizo wa Roho Mtakatifu, kila aaminiye aliyebatizwa na Roho Mtakatifu ana uwezo wa kuomba katika lugha wakati wowote anaotaka. Wakorinto walikuwa wananena sana kwa lugha katika ibada zao za kanisani, lakini sehemu kubwa walifanya kinyume cha utaratibu.
Matumizi Mbalimbali Ya Lugha Nyingine
Ni muhimu sana sana kwamba tuelewe tofauti kati ya matumizi ya hadharani ya lugha, na matumizi ya binafsi. Ingawa kila mwamini aliyejazwa na Roho Mtakatifu aweza kunena kwa lugha wakati wowote, hiyo haimaanisha kwamba Mungu atamtumia katika karama ya aina za lugha, ifanyayo kazi hadharani au mbele za watu. Matumizi ya msingi ya kunena kwa lugha ni katika maisha ya maombi ya binafsi ya kila aaminiye. Ila, Wakorintho walikuwa wanakusanyika pamoja na kunena kwa lugha wote kwa mara moja, bila tafsiri yoyote, tena, bila yeyote kupata msaada au kujengwa (ona 1Wakor. 14:6-12, 16-19, 23, 26-28).
Njia moja ya kutofautisha kati ya matumizi ya lugha hadharani na binafsi ni kusema kwamba matumizi binafsi ni kuomba katika lugha, na matumizi hadharani ni kunena kwa lugha. Paulo anataja matumizi hayo mawili katika sura ya kumi na nne ya barua yake ya kwanza kwa Wakorintho. Tofauti zenyewe ni nini?
Tunapoomba katika lugha, roho zetu zinamwomba Mungu, au, zinasema na Mungu (ona 1Wakor. 14:2, 14). Lakini, wakati mtu anapopata upako ghafula na kupewa karama ya aina za lugha, ni ujumbe kutoka kwa Mungu kwenda kwa kusanyiko (ona 1Wakor. 14:5), nao hueleweka mara tafsiri inapotolewa.
Kulingana na Maandiko, tunaweza kuomba kwa lugha kama tupendavyo (ona 1Wakor. 14:15), lakini karama ya aina za lugha hufanya kazi kama Roho Mtakatifu apendavyo tu (ona 1Wakor. 12:11).
Kwa kawaida, karama ya aina za lugha ingeambatana na karama ya tafsiri za lugha. Ila, matumizi ya binafsi ya kuomba katika lugha hayana tafsiri. Paulo alisema kwamba wakati alipoomba kwa lugha akili yake ilikuwa haina matunda (1Wakor. 14:14).
Mtu binafsi anapoomba kwa lugha yeye tu ndiye anayejengwa (ona 1Wakor. 14:4), lakini karama ya aina za lugha inapofanya kazi pamoja na ile ya tafsiri za lugha, kanisa zima hujengwa (ona 1Wakor. 14:4b, 5).
Kila aaminiye anapaswa kuomba kwa lugha kila siku, kama sehemu ya ushirika wake na Bwana. Kitu kizuri kimojawapo kuhusu kuomba kwa lugha ni kwamba huna haja ya kutumia akili yako. Maana yake ni kwamba unaweza kuomba kwa lugha wakati akili zako zimesongwa na kazi yako au vitu vingine. Paulo aliwaambia hivi Wakorintho, “Namshukuru Mungu ya kuwa nanena kwa lugha zaidi ya ninyi nyote” (1Wakor. 14:18. Maneno mepesi kukazia). Bila shaka alitumia muda mwingi sana kunena kwa lugha mpaka akawazidi washirika wote wa Kanisa la Korintho!
Vile vile, Paulo aliandika kwamba tunapoomba kwa lugha, wakati mwingine “tunambariki Bwana” (1Wakor. 14:16, 17). Mara tatu “lugha ya maombi” ninayotumia ime-eleweka na mtu aliyekuwa hapo nikiomba. Mara zote tatu nilikuwa nanena Kijapani. Kuna wakati mmoja nilimwambia Bwana kwa Kijapani, “Wewe ni mzuri sana!” Wakati mwingine nilisema, “Asante sana.” Wakati mwingine nilisema, “Njoo upesi! Njoo upesi! Ninangojea!” Si ajabu hiyo? Sijawahi kujifunza Kijapani hata neno moja, lakini mara tatu nimewahi “kumbariki Bwana” katika lugha hiyo!
Maagizo Ya Paulo Kuhusu Kunena Kwa Lugha
Maagizo aliyotoa Paulo kwa kanisa la Korintho yalikuwa wazi kabisa, na ya kueleweka. Katika kila kusanyiko au mkutano, idadi ya watu walioruhusiwa kunena kwa lugha kwa sauti ni wawili au watatu. Tena, wasinene wote kwa wakati mmoja, bali wangojane na kunena kwa zamu (ona 1Wakor. 14:27).
Maana yake si kwamba ni “jumbe tatu tu za lugha” zinazoruhusiwa. Maana yake ni kwamba watu wasizidi watatu katika ibada, watakaonena jumbe kwa lugha. Inadhaniwa na wengine kwamba kama wangekuwepo watu zaidi ya watatu ambao wanatumiwa mara kwa mara katika karama hiyo ya aina za lugha, yeyote angeweza kujiachilia kwa Roho na kutoa “ujumbe katika lugha” ambao Roho Mtakatifu alitamani kuudhihirisha kanisani. Kama si hivyo, maagizo ya Paulo yangemwekea mipaka Roho Mtakatifu kwa kuweka mipaka ya idadi ya jumbe katika lugha ambazo zingeweza kudhihirishwa katika mkutano mmoja. Kama Roho Mtakatifu asingeweza kutoa karama zaidi ya tatu za aina za lugha katika kusanyiko, isingekuwepo haja ya Paulo kutoa maagizo aliyotoa.
Ni hivyo hivyo hata kwa habari ya tafsiri za lugha. Inadhaniwa kwamba mtu zaidi ya mmoja katika kusanyiko anaweza kujiachilia kwa Roho na kutoa tafsiri ya “ujumbe katika lugha”. Watu aina hiyo walihesabiwa kuwa “watafsiri” (ona 1Wakor. 14:28), maana wangetumiwa mara kwa mara katika karama hiyo ya kutafsiri lugha. Kama ndivyo, pengine ndicho Paulo alichomaanisha aliposema, “na mmoja afasiri” (1Wakor. 14:27). Pengine hakuwa anasema mtu mmoja afasiri jumbe zote katika lugha. Pengine alikuwa anaonya tu dhidi ya “tafsiri shindani” za ujumbe huo huo mmoja. Kama mfasiri mmoja angefasiri ujumbe wa lugha, basi mfasiri mwingine hakuruhusiwa kufasiri ujumbe ule ule, hata ingawa alidhani angeweza kutoa tafsiri bora zaidi.
Kwa ujumla ni kwamba kila kitu kilitakiwa kufanyika “vizuri na kwa utaratibu” katika makusanyiko au mikutano ya kanisa – sio mchanganyiko wa usemaji usio na mpango, wa ghafula, unaochanganya watu na wa mashindano. Tena, waainio wawe makini na kuwajali wasioamini wowote wanaoweza kuwepo katikati yao. Paulo aliandika hivi kuhusu hilo:
Haya! Ikiwa kanisa lote limekusanyika pamoja, na wote wanene kwa lugha kisha ikawa wameingia watu wajinga au wasioamini, je, hawatasema ya kwamba mna wazimu? (1Wakor. 14:23)
Hilo ndilo tatizo lililokuwepo Korintho – kila mtu alikuwa ananena kwa lugha kwa wakati mmoja, na mara nyingi hazikuwepo tafsiri.
Maagizo Kuhusu Karama Za Ufunuo
Paulo alitoa maagizo machache kuhusu “karama za ufunuo” kwa habari ya jinsi zinavyodhihirishwa katika manabii, kama ifuatavyo:
Na manabii wanene wawili au watatu, na wengine wapambanue. Lakini mwingine aliyeketi akifunuliwa neno, yule wa kwanza na anyamaze. Kwa maana ninyi nyote mwaweza kuhutubu mmoja mmoja ili wote wapate kujifunza, na wote wafarijiwe. Na roho za manabii huwatii manabii. Kwa maana Mungu si Mungu wa machafuko bali wa amani; vile vile kama ilivyo katika makanisa yote ya watakatifu (1Wakor. 14:29-33).
Kama ambavyo katika kanisa la Korintho walikuwepo washirika waliokuwa wanatumiwa mara kwa mara katika karama ya kufasiri lugha na wakajulikana kuwa “watafsiri”, walikuwepo pia wale waliokuwa wanatumiwa mara kwa mara katika karama za unabii na ufunuo, ambao walihesabiwa kuwa “manabii”. Hawakuwa manabii kwa maana ya wale wa Agano la Kale, au kama Agabo katika Agano Jipya (ona Matendo 11:28; 21:10). Wao huduma zao zingekuwa za kanisani kwao tu.
Ingawa wanaweza kuwepo zaidi ya manabii watatu wa namna hiyo katika kusanyiko la kanisa, hapo tena Paulo aliweka mipaka ya huduma ya kinabii kwamba, “ni wawili au watatu”. Hii inaonyesha kwamba wakati Roho alipokuwa anatoa karama za kiroho katika kusanyiko, mtu zaidi ya mmoja angeweza kujitoa ili kupokea karama hizo. Kama si hivyo, mashauri ya Paulo yangeishia kwa Roho Mtakatifu kutoa karama ambazo zisingefurahiwa na kusanyiko lote, maana aliweka mipaka ya idadi ya manabii waliokuwa na ruhusa ya kusema.
Kama wangekuwepo manabii zaidi ya watatu, wale wengine, japo wamezuiwa kusema, wangesaidia katika kupambanua (au kupima) yale yaliyokuwa yanasemwa. Hilipia lingeonyesha uwezo wao wa kutambua kile ambacho Roho alikuwa anakisema, nap engine maana yake ni kwamba wangekuwa wao wenyewe wamejitoa kwa Roho, ili watumiwe katika kmarama zile zile zilizokuwa zinadhihirishwa kupitia manabii wale wengine. La sivyo, wangepima unabii na mafunuo tu kwa njia ya jumla, kwa kuhakikisha kwamba yalikuwa yanakubaliana na mafunuo ambayo Mungu alikwisha toa tayari (kama katika Maandiko), kitu ambacho kingweza kufanywa na aaminiye yeyote aliyekomaa vizuri.
Paulo akasema kwamba hao manabii wote wangeweza kutabiri kwa zamu (ona 1Wakor. 14:31) na kwamba “roho za manabii huwatii manabii” (1Wakor. 14:32), kuonyesha kwamba kila nabii angeweza kujizuia asimwingilie mwingine kumkata kauli, hata wakati akipewa unabii au ufunuo kutoka kwa Roho ili kushirikisha kusanyiko lote. Hii inaonyesha kwamba Roho anaweza kutoa karama mbalimbali kwa manabii kadhaa kwa wakati mmoja katika kusanyiko, lakini kila nabii angeweza na anatakiwa kutawala wakati mafunuo yake au unabii wake utasemwa kwa kusanyiko.
Hiyo ni kweli pia kuhusu karama yoyote yakusema ambayo inaweza kudhihirishwa kupitia mwamini yeyote. Kama mtu akipokea ujumbe katika lugha au unabii toka kwa Bwana, anaweza kuuzuia mpaka wakati unaofaa katika kusanyiko. Ni kosa kuingilia unabii wa mtu mwingine na kumkata kauli au mafundisho, ili kutoa unabii wako.
Paulo aliposema, “Kwa maana ninyi nyote mwaweza kuhutubu mmoja mmoja” (1Wakor. 14:31), kumbuka kwamba alikuwa anasema kwa habari ya manabii waliopokea unabii. Kwa bahati mbaya, kuna watu wamepotosha maana ya maneno ya Paulo na kusema kwamba kila aaminiye anaweza kutabiri katika kilakusanyiko. Karama ya unabii hutolewa kama Roho apendavyo.
Siku hizi kanisa linahitaji msaada wa Roho Mtakatifu, na nguvu Zake, uwepo Wake na karama Zake. Paulo aliwapa waamini wa Korintho ushauri kwamba “takeni sana karama za rohoni, lakini zaidi kwamba mpate kuhutubu” (1Wakor. 14:1). Hii inaonyesha kwamba kiwango chetu cha kutamani au shauku huhusiana na jinsi karama za kiroho zinavyodhihirishwa, la sivyo Paulo asingetoa ushauri wa namna hiyo. Basi, mtumishi afanyaye watu kuwa wanafunzi, anayetamani kutumiwa na Mungu kwa ajili ya utukufu Wake, atatamani mno karama za kiroho, na kuwafundisha wanafunzi wake kufanya vivyo hivyo.