Vichwa vya Habari

KUNA SIRI GANI KWENYE KUSIFU NA KUABUDU


Sifa Na Kuabudu 

Yule mwanamke akamwambia [Yesu], ‘Bwana, naona ya kuwa u nabii. Baba zetu waliabudu katika mlima huu, nanyi husema ya kwamba huko Yerusalemu ni mahali patupasapo kuabudia.’ Yesu akamwambia, ‘Mama, unisadiki. Saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu wala kule Yerusalemu. … Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana, Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. Mungu ni Roho, nao
wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli’ (Yohana 4:19-24).
Maneno hayo kutoka kinywa cha Yesu yanaweka msingi wa sisi kuelewa juu ya mambo muhimu sana katika kuabudu. Yeye alizungumzia juu ya “waabuduo halisi” na kueleza sifa zao. Hii huonyeha kwamba wapo watu wanaoabudu, lakini si waabuduji wa kweli. Wanaweza kudhani kwamba wanamwabudu Mungu lakini ukweli si hivyo maana hawatimizi masharti Yake.
Yesu alitangaza alama za waabuduji wa kweli – wao huabudu “katika roho na kweli.” Basi, kinyume chake ni kwamba, waabuduji wasio wa kweli ni wale wenye kuabudu “katika mwili na uongo. Kimwili, waabuduji wasio wa kweli wanawea kufanya matendo yote ya kuabudu, lakini ni maonyesho tu maana hayatoki katika moyo unaompenda Mungu.
Ibada ya kweli kwa Mungu inatoka katika moyo unaompenda Mungu tu. Basi, kuabudu si kitu tunachofanya wakati tunapokutanika kanisani, bali ni kitu tunachofanya kila dakika ya maisha yetu, tunapotii amri za Kristo. Inashangaza kwamba yule mwanamke aliyekuwa anazungumza na Yesu alikuwa ameolewa mara tano, na wakati huo alikuwa anaishi na mwanamume, na bado alitaka kuhojiana na Yesu kuhusu mahali panapofaa kumwabudu Mungu! Yeye ni mfano wa watu wengi sana wenye dini, wanaohudhuria ibada huku wakiishi maisha yao kila siku katika kumwasi Mungu. Hao si waabuduji wa kweli.
Wakati fulani Yesu aliwakemea Mafarisayo na waandishi kwa sababu ya ibada yao ya uongo, isiyotoka moyoni.
Enyi wanafiki! Ni vema alivyotabiri Isaya kwa habari zenu, akisema, ‘Watu hawa huniheshimu kwa midomo; ila mioyo yao iko mbali nami. Nao waniabudu bure, wakifundisha mafundisho yaliyo maagizo ya wanadamu’ (Mathayo 15:7-9. Maneno mepesi kukazia).
Ingawa Wayahudi na Wasamaria katika siku za Yesu walitilia mkazo sana kuhusu mahali pa watu kuabudia, Yesu alisema kwamba mahali hapakuwa na maana sana. Cha muhimu ni hali ya moyo wa kila mtu, na jinsi anavyomheshimu Mungu. Hayo ndiyo yanaamua jinsi ibada yake ilivyo.
“Ibada” nyingi katika makanisa siku hizi ni taratibu tu zilizokufa, zinazotendwa na waabuduji waliokufa pia. Watu wanarudia maneno ya mtu mwingine kuhusu Mungu, bila hata kuyafikiri, wanapoimba “nyimbo za kuabudu.” Kuabudu kwao ni bure, maana maisha yao yanaonyesha kilicho halisi katika mioyo yao.
Mungu angetamani hata kuambiwa “Nakupenda” rahisi tu itokayo moyoni kutoka kwa mtoto wake mmoja mtiifu, kuliko kuvumilia kelele zisizotoka moyoni za maelfu ya Wakristo wa Jumapili asubuhi, wakiimba “Jinsi Wewe Ulivyo Mkuu.”

Kuabudu Katika Roho

Kuna wanaosema kwamba kuabudu “katika Roho” ni kuomba na kuimba kwa lugha zingine. Hiyo ni tafsiri ngumu kukubali, ukitazama maneno ya Yesu. Yeye alsiema kwamba “saa inakuja, na sasa ipo, ambayo waabuduji wa kweli watamwabudu Baba katika roho na kweli,” kuonyesha kwamba tayari walikuwepo watu waliotimiza masharti ya kuabudu “katika Roho” alipotoa tamko hilo. Ni kweli kwamba hakuna yeyote aliyenena kwa lugha mpaka Siku ya Pentekoste. Basi, aaminiye yeyote, awe ananena kwa lugha au hapana, anaweza kumwabudu Mungu katika roho na kweli. Kuomba na kuimba kwa lugha zingine hakika huwa ni msaada kwa mwabuduji katika kuabudu kwake, lakini hata kunena kwa lugha kunaweza kuwa utaratibu usiotoka moyoni.
Picha ya kusisimua kuhusu ibada ya kanisa la kwanza inapatikmana katika Matendo 13:1, 2.
Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli. Basi hawa walipokuwa wakimfanya Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, ‘Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia’ (Maneno mepesi kukazia).
Ona fungu hili linavyosema: “walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada.” Basi tunajifunza hapo kwamba ibada ya kweli humhudumia Bwana. Ila, ni hivyo wakati Bwana anapokuwa ndiyo lengo la upendo wetu.

Njia Za Kuabudu

Kitabu cha Zaburi ambacho tunaweza kusema ni kitabu cha nyimbo cha Israeli, kinatushauri kumwabudu Mungu katika njia nyingi tofauti tofauti. Kwa mfano: Katika Zaburi ya 32 tunasoma hivi:
Pigeni vigelegele vya furaha; ninyi nyote mlio wanyofu wa moyo (Zaburi 32:11b. Maneno mepesikukazia).
Japo kuabudu kimya, kwa utaratibu na heshima kuna nafasi yake, pia kuna nafasi ya kupiga kelele za shangwe.
Mpigieni Bwana vigelegele, enyi wenye haki, kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo. Mshukuruni BWANA kwa kinubi, kwa kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa. Mwimbieni wimbo mpya, pigeni kwa ustadi kwa sauti ya shangwe (Zaburi 33:1-3. Maneno mepesi kukazia).
Tunapaswa kumwimbia Bwana katika kuabudu, lakini kuimba kwetu kuwa kwa furaha, ambalo ni onyesho lingine la nje kuhusu undani wa moyo wa mtu. Pia tunaweza kuimba kwa furaha tukitumia vyombo mbalimbali vya muziki. Ila, katika mikutano mingi ya kanisa, vyombo vya muziki vinakuwa na sauti ya juu kiasi cha kwamba vinafunika kabisa sauti ya uumbaji. Ni vizuri vipunguzwe sauti au vizimwe. Ukisoma zaburi, tatizo hilo halikuwepo!
Ndivyo nitakavyokubariki maadamu ni hai. Kwa jina Lako nitaiinua mikono yangu (Zaburi 63:4. Maneno mepesi kukazia).
Tunaweza kuinua mikono yetu juu kwa Mungu kama ishara ya kujitolea Kwake na kumheshimu.
Mpigie Mungu kelele za shangwe nchi yote; imbeni utukufu wa jina lake; tukuzeni sifa zake.Mwambieni Mungu, ‘Matendo Yako yatisha kama nini! Kwa ajili ya wingi wa nguvu zako, adui zako watakuja kunyenyekea mbele zako. Nchi yote itakusujudia na kukuimbia, naam, italiimbia jina lako’ (Zaburi 66:1-4. Maneno mepesi kukazia).
Tunatakiwa kumwambia Bwana jinsi alivyo mkuu na kumsifu kwa jinsi alivyo wa ajabu. Zaburi ni mahali pazuri sana pa kupa ta maneno yafaayo ya kumsifu Mungu. Tunahitaji kwenda zaidi ya kurudia rudia maneno haya: “Nakusifu, Bwana!” Kuna mengi sana ya kumwambia.
Njooni tuabudu, tusujudu, tupige magoti mbele za BWANA aliyetuumba (Zaburi 95:6).
Hata jinsi tulivyo ni onyesho la ibada: iwe ni kusimama, kupiga magoti au kusujudu.
Watauwa na waushangilie utukufu, waimbe kwa sauti kuu vitandani mwao (Zaburi 149:5. Maneno mepesi kukazia).
Si lazima tuwe tumesimama au kupiga magoti ili kuabudu – tunaweza hata kuwa tumelala kitandani.
Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru, nyuani mwake kwa kusifu. Mshukuruni, lihimidini jina lake (Zaburi 100:4. Maneno mepesi kukazia).
Hakika, kushukuru kuwe sehemu ya kuabudu kwetu.
Na walisifu jina lake kwa kucheza (Zaburi 149:3. Maneno mepesi kukazia).
Tunaweza hata kumsifu Bwana kwa kucheza. Lakini kucheza kwenyewe kusiwe kwa kimwili, kwenye kuamsha ashiki, au kwa ajili ya kustarehesha watu.
Msifuni kwa mvumo wa baragumu; msifuni kwa kinanda na kinubi. Msifuni kwa matari na kucheza; msifuni kwa zeze na filimbi. Msifuni kwa matoazi yaliayo; msifuni kwa matoazi yavumayo sana. Kila mwenye pumzi na amsifu BWANA. Haleluya (Zaburi 150:3-6).
Mungu ashukuriwe kwa walio na vipawa vya muziki. Vipawa vyao vinaweza kutumika kumtukuza Mungu kama watavipiga kwa moyo wa upendo.

Nyimbo Za Kiroho

Mwimbieni BWANA wimbo mpya, kwa maana ametenda mambo ya ajabu (Zaburi 98:1a. Maneno mepesi kukazia).
Hakuna kosa lolote kuimba wimbo wa zamani, mpaka inapokuwa mazoea. Hapo ndipo tunahitaji wimbo mpya utokao mioyoni mwetu. Katika Agano Jipya, tunajifunza kwamba Roho Mtakatifu atatusaidia kutunga nyimbo mpya. Tunaambiwa hivi:
Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu (Wakolosai 3:16).
Tena msilewe kwa mvinyo ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho; mkisemezana kwa zaburi na tenzi na nyimbo za rohoni, huku mkiimba na kumshangilia Bwana mioyoni mwenu; na kumshukuru Mungu Baba siku zote kwa mambo yote, katika jina lake Bwana wetu Yesu Kristo (Waefeso 5:18-20).
Paulo aliandika kwamba tunapaswa kuwa tunaimbiana “zaburi, na tenzi na nyimbo za rohoni”. Basi, hizo tatu zina tofauti. Uchunguzi wa lugha ya Kiyunani hautoi msaada wowote, ila pengine “zaburi” maana yake ni kuimba zaburi kama zilivyo katika Biblia, pamoja na vyombo. Pengine “tenzi” ni nyimbo mbalimbali za shukrani zilizokuwa zimetungwa na waamini katika makanisa. “Nyimbo za rohoni” labda zilikuwa nyimbo za papo kwa papo kutoka kwa Roho Mtakatifu, ambazo ni sawa na ile karama ya unabii, ila, zenyewe ziliimbwa.
Kusifu na kuabudu vinapaswa kuwa sehemu ya maisha yetu ya kila siku – si kitu fulani tunachofanya wakati wa kukutanika kanisani. Mchana kutwa tunaweza kumhudumia Bwana na kufanikiwa kujisikia ushirika wa karibu na Yeye.

Sifa Ni Imani Ikitenda Kazi

Kusifu na kuabudu ni madhihirisho ya kawaida kabisa ya imani yetu kwa Mungu. Kama kweli tunaamini ahadi za Neno la Mungu, basi tutakuwa watu wenye furaha, waliojaa sifa kwa Mungu. Yoshua na Waisraeli walitakiwa kupiga kelele kwanza, ndipo kuta zikaanguka. Biblia inatushauri hivi: “Furahini katika Bwana sikuzote” (Wafilipi 4:4), na “Shukuruni kwa kila jambo” (1Wathes. 5:18a).
Mfano mmoja wa hali ya juu sana kuhusu nguvu za sifa unapatikana katika 2Nyakati sura ya 20, wakati taifa la Yuda lilipovamiwa na majeshi ya Moabu na Amoni. Akijibu maombi ya Mfalme Yehoshafati, Mungu aliwaagiza Israeli hivi:
Msiogope wala msifadhaike kwa ajili ya jeshi kubwa hili kwani vita si yenu bali ni ya Mungu. Kesho shukeni juu yao … Hamtahitaji kupigana vita, jipangeni, simameni, mkauone wokovu wa BWANA ulio pamoja nanyi, enyi Yuda na Yerusalemu (2Nyakati 20:15b – 17).
Kisa kinaendelea, hivi:
Wakaamka asubuhi na mapema, wakaenda nje katika jangwa la Tekoa; nao walipokuwa wakitoka, Yehoshafati akasimama akasema, ‘Nisikieni enyi Yuda nanyi wenyeji wa Yerusalemu; mwaminini BWANA Mungu wenu, ndivyo mtakavyothibitika; waaminini manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa.’ Naye alipokwisha kufanya shauri na watu, akawaweka wale watakaomwimbia BWANA, na kumsifu katika uzuri wa utakatifu, wakitoka mbele ya jeshi, na kusema, Mshukuruni BWANA; kwa maana fadhili zake ni za milele. Nao walipoanza kuimba na kusifu, BWANA akaweka waviziao juu ya wana wa Amoni, na Moabu, na wa mlima Seiri, waliokuja juu ya Yuda; nao wakapigwa. Kwani wana wa Amoni na wa Moabu waliwaondokea wenyeji wa mlima Seiri kuwaulia mbali na kuwaharibu; nao walipokwisha kuwakomesha hao wakaao Seiri, wakajitia kuharibu kila mtu mwenziwe. Hata Yuda walipofika mnara wa kulindia wa jangwani, wakalitazama hilo jeshi; nao angalia, walikuwa maiti walioanguka nchi, wala hapana aliyeokoka. Nao Yehoshafati na watu wake walipokuja kuchukua nyara zao, wakaona kati yao wingi wa mali, na mavazi, na johari za thamani, walivyojivulia, zaidi kuliko wawezavyo kuchukua; wakawa siku tatu katika kuteka nyara, maana zilikuwa nyingi sana (2Nyakati 20:20-25. Manenomepesi kukazia).
Sifa iliyojaa imani huleta kulindwa na husababisha utoaji wa Mungu!
Kwa maelezo zaidi kuhusu mada hiyo ya nguvu za sifa, ona Wafilipi 4:6-7 (sifa huleta amani), 2Nyakati 5:1-14 (sifa huleta uwepo wa Mungu), Matendo 13:1, 2 (sifa hudhihirisha makusudi na mipango ya Mungu), na Matendo 16:22-26 (sifa huleta kuhifadhiwa na Mungu, na kufunguliwa kutoka gerezani).

No comments:

Post a Comment

NENO NI UZIMA Designed by 5gear Copyright © 2014-2015

Theme images by Jason Morrow. Powered by Blogger.