Vichwa vya Habari

KUZALIWA UPYA/UBATIZO


Sura Ya Kumi
Kuzaliwa Upya 

Watu wanapotubu na kumwamini Bwana Yesu Kristo, wana”zaliwa mara ya pili”. Nini hasa maana ya kuzaliwa mara ya pili? Sura hii itatazama jambo hili.
Ili kuweza kuelewa maana ya kuzaliwa mara ya pili, inasaidia sana kuanza kwa kuelewa asili ya wanadamu. Maandiko yanatuambia kwamba sisi si viumbe wa kimwili tu, bali wa kiroho pia. Kwa mfano: Paulo aliandika hivi:
Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa. Nafsi zenu na roho zenu na miili yenu mhifadhiwe mwe kamili, bila lawama, hadi wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo (1Wathes. 5:23, maneno mepesi kukazia).
Kama Paulo alivyoonyesha, tunaweza kujihesabu kuwa viumbe wenye sehemu tatu: roho, nafsi na mwili. Maandiko hayafafanui sana hizo sehemu tatu, kwa hiyo, tunajitahidi sana kuzitofautisha kwa ufahamu wetu wa maneno yenyewe. Mara nyingi tunasema hivi: Mwili wetu ni umbo tulilo nalo – nyama, mifupa, damu na kadhalika. Nafsi yetu ni ufahamu wetu na uwezo wetu wa kujisikia – akili yetu. Roho yetu bila shaka ni ile hali yetu ya kiroho, au kama mtume Petro anavyoeleza, “utu wa ndani uliofichika” (1Petro 3:4, TLR).
Kwa sababu roho haionekani kwa macho ya kimwili, watu wasio-okoka wanakana kuwepo kwake. Lakini Biblia iko wazi kabisa kwamba wote sisi ni viumbe wa kiroho. Maandiko yanatuambia kwamba mtu anapokufa, ni mwili wake tu ndiyo unakoma kufanya kazi, lakini roho yake na nafsi vinaendelea kama kawaida. Wakati wa kufa, hivyo viwili vinatoka katika mwili (kwa pamoja) ili kwenda kuhukumiwa mbele za Mungu (ona Wabrania 9:27). Baada ya hukumu, vinakwenda mbinguni au jehanamu. Mwisho wa yote, kila roho na nafsi ya mtu itaungana na mwili wake wakati wa ufufuo.

Roho Ya Mwanadamu Ikifafanuliwa Zaidi

Katika 1Petro 3:4, Petro anazungumza juu ya roho kama “utu wa moyoni usioonekana” kuonyesha kwamba roho ni mtu. Paulo pia alizungumza juu ya roho kama “mtu wa ndani” kuonyesha imani yake kwamba roho ya mwanadamu si nguvu fulani au wazo tu, bali ni mtu. Anasema hivi:
Kwa hiyo hatulegei, bali, ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu wa ndaniunafanywa upya siku kwa siku (2Wakor. 4:16, maneno mepesi kukazia).
“Utu wa nje” bila shaka ni maelezo kuhusu mwili, na “utu wa ndani” ni maelezo kuhusu roho. Ni hivi: Japo mwili unazeeka, roho inafanywa upya kila siku.
Ona tena kwamba Paulo anataja mwili na roho kama watu. Basi, unapofikiria roho yako, usifikiri wingu fulani la kiroho. Ni afadhali ufikiri kuhusu mtu mwenye umbo linalofanana na lako. Kama mwili wako umezeeka, usidhani na roho yako imezeeka pia. Jaribu kufikiri jinsi ulivyokuwa ujanani mwako, kwa sababu, roho yako haijazeeka – iko kama ulivyokuwa ukiwa kijana! Inafanywa upya siku kwa siku.
Roho yako ndiyo sehemu yako inayozaliwa mara ya pili (kama umemwamini Bwana Yesu). Roho yako inaungana na Roho wa Mungu (ona 1Wakor. 6:17), na Yeye ndiye anayekuongoza unapomfuata Yesu (ona Warumi 10:14).
Biblia inafundisha kwamba Mungu pia ni roho (ona Yohana 4:24), na hata malaika, na mapepo pia. Wote wana maumbo na wote wapo katika ulimwengu wa roho. Ila, ulimwengu wa roho hauwezi kutambuliwa kwa hisia zetu za kimwili. Kujaribu kuwasiliana na ulimwengu wa roho kwa hisia zetu za kimwili ni sawa na kujaribu kushika mawimbi ya redio kwa mikono yetu. Hatuwezi kutambua kwa hisia zetu za kimwili kwamba mawimbi ya redio yanapita katika chumba, lakini hiyo haithibitishi kwamba hakuna mawimbi ya redio. Njia pekee ya kuyapata hayo mawili ni kuifungulia redio.
Hayo pia ni kweli kwa habari ya ulimwengu wa kiroho. Kwa kuwa ulimwengu wa kiroho hauwezi kutambuliwa na hisia za kimwili haimaanishi kwamba haupo. Upo, na watu wakijua au wasijue, ni sehemu ya ulimwengu wa kiroho kwa sababu ni viumbe wa kiroho. Ama wanahusiana na Mungu kiroho (kama wamezaliwa mara ya pili), au wanahusiana na Shetani kiroho (kama hawajatubu). Kuna watua mbao wamejifunza jinsi ya kuwasiliana na ulimwengu wa kiroho kwa njia ya roho zao, lakini wao wanawasiliana na ufalme wa Shetani – ufalme wa giza.

Miili Ya Milele

Tukiwa katika mada hii, hebu nitaje kitu kuhusu miili yetu. Ingawa hatimaye itakufa, hali yetu ya kufa kimwili si tendo la mwisho. Iko siku ambapo Mungu Mwenyewe atafufua kila mwili wa mwanadamu uliokufa. Yesu alisema hivi:
Msishangae kwa hili, maana saa inakuja, ambayo wote waliomo makaburini wataisikia sauti Yake, nao watatoka. Waliofanya matendo mema, watafufuliwa ufufuo wa uzima, na wale waliofanya matendo maovu, watafufuliwa ufufuo wa kuhukumiwa (Yohana 5:28, 29, TLR).
Mtume Yohana aliandika katika kitabu cha Ufunuo kwamba kufufuliwa kwa miili ya wasio haki kutatokea miaka elfu moja baada ya kufufuliwa kwa miili ya wenye haki.
Nao [yaani, watakatifu waliouawa wakati wa dhiki] wakawa hai, wakatawala pamoja na Kristo miaka elfu. Na hao wafu waliosalia hawakuwa hai, hata itimie ile miaka elfu. Huo ndio ufufuo wa kwanza.[1] Heri na mtakatifu ni yeye aliye na sehemu katika ufufuo wa kwanza … watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, nao watatawala pamoja naye hiyo miaka elfu (Ufunuo 20:4b-6).
Biblia pia inatuambia kwamba wakati Yesu atakaporudi kulichukua kanisa, miili yote ya watakatifu itafufuliwa na kuunganishwa na roho zao, watakapokuwa wanarudi kutoka mbinguni na Yesu, kuja duniani. Tunasoma hivi:
Maana, ikiwa twaamini ya kwamba Yesu alikufa akafufuka, vivyo hivyo na hao waliolala katika Yesu, Mungu atawaleta pamoja naye. Kwa kuwa twawaambieni haya kwa neno la Bwana, kwamba, sisi tulio hai, tutakaosalia hata wakati wa kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia wao waliokwisha kulala mauti. Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko … nao waliokufa katika Kristo [yaani, miili yao] watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu ili tumlaki Bwana hewani, na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele (1Wathes. 4:14-17).
Mungu alimwumba mwanadamu wa kwanza kutoka katika mavumbi ya nchi, kwa hiyo, haitakuwa shida Kwake kuchukua mabaki au sehemu za mwili wa kila mmoja na kuumba tena miili binafsi kutoka katika vifaa vile vile.
Kwa habari ya kufufuka kwa miili yetu, Paulo aliandika hivi:
Kadhalika na kiyama ya watu. Hupandwa katika uharibifu; hufufuliwa katika kutokuharibika. Hupandwa katika aibu, hufufuliwa katika fahari. Hupandwa katika udhaifu; hufufuliwa katika nguvu. Hupandwa mwili wa asili; hufufuliwa mwili wa roho. … Ndugu zangu, nisemayo ni haya: Nyama na damu haziwezi kuurithi ufalme wa Mungu, wala uharibifu kurithi kutokuharibika. Angalieni, nawaambia ninyi siri – hatutalala sote [yaani, kufa], lakini sote tutabadilika, kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho. Maana parapanda Italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika. Maana sharti huu uharibikao uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa uvae kutokufa (1Wakor. 15:42-44a, 50-53).
Ona kwamba sifa kubwa ya miili yetu mipya ni kwamba itakuwa haifi na isiyoharibika. Haitazeeka, haitapata magonjwa, wala haitakufa! Miili yetu mipya itakuwa kama ule mwili mpya ambao Yesu alipokea baada ya kufufuka Kwake.
Kwa maama sisi wenyeji wetu uko mbinguni. Kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo; atakayeubadili mwili wetu wa unyonge upate kufanana na mwili wake wa utukufu,kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote viwe chini yake (Wafilipi 3:20, 21, maneno mepesi kukazia).
Hata mtume Yohana anathibitisha kweli hii ya kupendeza sana, hivi:
Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa. Lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa tutafanana naye, kwa maana tutamwona kama alivyo (1Yohana 3:2, maneno mepesi kukazia).
Japo hili ni gumu kwa akili zetu kuelewa kabisa, tunaweza kuliamini na kufurahia yaliyo mbele![2]

Anayosema Yesu Kuhusu Kuzaliwa Upya

Kuna wakati fulani ambao Yesu alizungumza na kiongozi Myahudi aliyeitwa Nikodemu juu ya umuhimu wa kuzaliwa upya kwa roho ya mwanadamu, kwa tendo la Roho Mtakatifu.
Yesu akajibu, akamwambia [Nikodemu], ‘Amin amin nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu.’ Nikodemu akamwambia, ‘Awezaje mtu kuzaliwa akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa?’ Yesu akajibu, ‘Amin amin nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho hawezi kuuingia ufalme wa Mungu. Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili, na kilichozaliwa kwa Roho ni roho. Usistaajabu kwa kuwa nimekwambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili’ (Yohana 3:3-7).
Mwanzoni, Nikodemu alidhani kwamba Yesu anazungumzia kuzaliwa kimwili mara ya pili alipomwambia kwamba lazima mtu azaliwe tena ili kuingia ufalme wa mbinguni. Yesu akaweka wazi kwamba alikuza anazungumza juu ya kuzaliwa upya kiroho. Yaani, roho ya mtu lazima izaliwe tena.
Sababu ya kuhitaji kuzaliwa upya kiroho ni kwamba, roho zetu zimeathiriwa na asili ovu ya dhambi. Hiyo asili ya dhambi mara nyingi inatajw akatika Biblia kwamba ni kifo. Ili tuweze kuelewa, tutaitaja asili hiyo ovu kwamba ni kifo cha kiroho ili tutofautishe kati yake na kifo cha kimwili (ambacho ni wakati mwili wa kawaida unapokoma kufanya kazi).

Kifo Cha Kiroho Kinafafanuliwa

Paulo anaeleza maana ya kufa kiroho katika Waefeso 2:1-3. Anasema hivi:
Nanyi mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zenu, ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi. Zamani sisi sote nasi tulienenda kati yao katika tamaa za miili yetu, tulipoyatimiza mapenzi ya mwili na ya nia, tukawa kwa tabia yetu watoto wa hasira kama na hao wengine (maneno mepesi kukazia).
Bila shaka Paulo alikuwa hazungumzii kifo cha kimwili kwa sababu alikuwa anawaandikia watu waliokuwa hai kimwili. Lakini akasema, hapo zamani walikuwa “wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zao.” Dhambi hufungua mlango wa kifo cha kiroho (tazama Warumi 5:12). Kuwa wafu kiroho maana yake ni kuwa na asili ya dhambi rohoni mwako. Ona maneno ya Paulo kwamba, “kwa tabia” wakawa watoto wa hasira.
Tena, kufa kiroho maana yake kuwa na asili ya Shetani katika roho yako kwa namna fulani. Paulo alisema kwamba wale wote waliokufa kiroho wana roho ya “mkuu wa uwezo wa anga” ikitenda kazi ndani yao. Huyo “mkuu wa uwezo wa anga” ni Shetani (tazama Waefeso 6:12), na roho yake inatenda kazi ndani yao wote ambao hawajaokoka.
Yesu aliwaambia hivi Wayahudi waliokuwa hawajazaliwa mara ya pili:
Ninyi ni wa baba yenu Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo, wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo husema yaliyo yake mwenyewe, kwa sababu yeye ni mwongo na baba wa huo (Yohana 8:44).
Kwa upande wa kiroho, wale ambao hawajazaliwa tena si tu kwamba wana asili ya Shetani katika roho zao, bali Shetani ni baba yao wa kiroho pia. Basi, ni kawaida kwao kutenda kama shetani. Wao ni wauaji na waongo.
Si kwamba watu wote ambao hawajaokoka wamefanya mauaji, bali ni kwamba wanahamasishwa na chuki ile ile kama ya wauaji, nao wangeweza kuua kama wangefanikiwa. Kuhalalishwa utoaji mimba katika nchi nyingi ni uthibitisho wa kweli hiyo. Watu ambao hawajaokoka wataua hata watoto wao wenyewe, ambao bado hawajzaliwa!
Hii ndiyo sababu mtu lazima azaliwe tena kiroho. Inapotokea hivyo, hiyo asili ya dhambi na kishetani huondolewa katika roho yake, na nafasi yake huchukuliwa na asili ya Mungu takatifu. Roho Mtakatifu wa Mungu huja na kukaa ndani ya roho yake. Hawi “mfu kiroho” tena, bali anafanywa “hai kiroho”. Roho yake haiwi imekufa tena bali inakuwa hai kwa Mungu. Badala ya kuwa mtoto wa kiroho wa Shetani, anakuwa mtoto wa kiroho wa Mungu.

Matengenezo Si Kuzaliwa Upya

Kwa sababu watu ambao hawajaokoka wamekufa kiroho, hawawezi kuokolewa kwa matengenezo, hata kama watajaribu kiasi gani. Watu ambao hawajaokoka wanahitaji asili mpya, si matendo mapya ya nje tu. Unaweza kumchukua nguruwe, ukamsafisha vizuri akawa safi, ukampulizia hata manukato na kumfungia tai ya rangi nzuri tu shingoni mwake, lakini mwisho wa siku ulicho nacho ni nguruwe aliyesafishwa tu! Bado asili yake ni ile ile. Na hautapita muda mrefu kabla hajaanza kunuka vibaya tena na kulala kwenye matope tena.
Ndivyo ilivyo kwa watu washika dini sana ambao hawajawahi kuzaliwa tena. Wanaweza kuwa wasafi kwa nje, lakini ndani ni wachafu tu kama kawaida. Yesu alisema hivi kwa watu washika dini wa siku Zake:
Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnasafisha nje ya kikombe na chano, na ndani yake vimejaa unyang’anyi na kutokuwa na kiasi. Ewe Farisayo kipofu! Safisha kwanza ndani ya kikombe, ili nje yake nayo ipate kuwa safi! Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mmefanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, nayo kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu na uchafu wote. Vivyo hivyo ninyi nanyi: Kwa nje mwaonekana na watu kuwa wenye haki, bali ndani mmejaa unafiki na maasi! (Mathayo 23:25-28).
Maneno ya Yesu ni maelezo sahihi kabisa ya washika dini wote ambao hawajawahi kuzaliwa upya kwa njia ya Roho Mtakatifu. Kuzaliwa upya huwasafisha watu ndani, si nje tu.

Nini Kinachotokea Kwa Nafsi Wakati Roho Inapozaliwa Upya?

Roho ya mtu inapozaliwa upya, nafsi yake hapo mwanzoni inabakia kama ilivyokuwa (ingawa kwa akili zake anakuwa amefanya uamuzi wa kumfuata Yesu). Ila, Mungu anatazamia kwamba tufanye kitu na nafsi zetu mara tunapokuwa watoto Wake. Nafsi zetu (au nia) zinapaswa kufanywa upya kwa Neno la Mungu ili tuweze kufikiri kama Mungu anavyofikiri. Kwa kufanywa upya nia zetu, badiliko la kudumu la nje linafanyika maishani mwetu, na kutufanya tuzidi kufanana na Yesu.
Wala msiifuatishe namna ya dunia hii, bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu (Warumi 12:2, manenomepesi kukazia).
Hata Yakobo naye aliandika kuhusu mfuatano huo wa mambo katika maisha ya mwamini, hivi:
Kwa hiyo wekeni mbali uchafu wote na ubaya uzidio, na kupokea kwa upole neno lile lililopandwa ndani, liwezalo kuziokoa nafsi zenu (Yakobo 1:21, TLR).
Ona kwamba Yakobo alikuwa anawaandikia Wakristo – watu ambao roho zao zilikuwa zimekwisha zaliwa upya. Ila, walihitaji nafsi zao kuokolewa, na hayo yangefanyika tu wakati anapopokea “neno lile lililopandwa ndani”. Hii ndiyo sababu waamini wapya wanatakiwa kufundishwa Neno la Mungu.

Mabaki Ya Asili Ya Kale

Baada ya kuzaliwa upya kwao, Wakristo wengi hugundua kwamba ni watu wenye asili mbili, na kujikuta wakikabiliana na kile kitu kinachoitwa na Paulo, vita kati ya “Roho na mwili”.
Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili, kwa maana hizi zi mepungana, hata hamwezi kufanya mnayotaka (Wagalatia 5:17).
Mabaki ya ile asili ya kale ya dhambi, yanaitwa “mwili” na Paulo. Hizo asili mbili ndani yetu huleta shauku tofauti, ambazo, kama watu watakubaliana nazo, husababisha matendo tofauti na mitindo tofauti ya maisha. Ona tofauti anayoweka Paulo kati ya “matendo ya mwili” na “tunda la Roho” katika fungu lifuatalo:
Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya: Uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo. Katika hayo nawaambia mapema, kama nilvyokwisha kuwaambia ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu. Lakini tunda la Roho ni: Upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi. Juu ya mambo kama hayo hakuna sheria (Wagalatia 5:19-23).
Bila shaka inawezekana kwa Wakristo kukubaliana na mwili, vinginevyo Paulo asingewaonya kwamba kuzoea kuufuata mwili kutawafanya wasiweze kuurithi ufalme wa Mungu. Katika barua yake kwa Warumi, Paulo aliandika pia juu ya hizo asili mbili za kila Mkristo, na akaonya tena juu ya matokeo hayo hayo, kama watu watakubaliana na mwili. Anasema hivi:
Na Kristo akiwa ndani yenu, mwili wenu umekufa kwa habari ya dhambi, bali roho yenu iko hai kwa habari ya haki. … Basi ndugu, kama ni hivyo, wote tunawajibika, si kwa mwili kwamba tuishi kwa kufuata mambo ya mwili. Kwa maana, mkiishi kwa kufuata mambo ya mwili mwataka kufa,bali mkiyafisha matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi. Kwa kuwa wote wanao-ongozwa na Roho wa Mungu ndio wana wa Mungu hao (Warumi 8:10, 12-14, TLR. Maneno mepesi kukazia).
Hilo ni onyo dhahiri kabisa kwa Wakristo kwamba, kuishi (yaani tabia ya kawaida, au mazoea) kulingana na mwili matokeoyake ni kifo. Bila shaka Paulo alikuwa anaonya juu ya kifo cha kiroho maana kila mtu hatimaye hufa kimwili – hata Wakristo wale wanao”yafisha matendo ya mwili”.
Mkristo anaweza kuangukia katika mojawapo ya dhambi ambazo Paulo aliorodhesha hapo kwa kitambo tu. Ila, mwamini anapofanya dhambi, atajisikia hukumu na pengine atatubu. Yeyote anayeungama dhambi yake na kumwomba Mungu amsamehe, atasafishwa (ona 1Yohana 1:9).
Mkristo anapotenda dhambi haimaansihi kwamba amevunja uhusiano wake na Mungu. Maana yake ni kwamba amevunja ushirika wake na Mungu. Yeye bado ni mtoto wa Mungu, lakini sasa ni mtoto asiyeti. Ikiwa mwamini hataungama dhambi yake na kutubu, anajiweka kwenye nafasi ya kuadhibiwa na Bwana.

Vita Yenyewe

Kama umejikuta unatamani kufanya mambo unayojua ni makosa, basi umeanza kukabiliana na “tamaa ya mwili”. Bila shaka umegundua pia kwamba unapojaribiwa na mwili kufanya kisicho sawa, kuna kitu ndani yako kinachopinga majaribu hayo. Hicho ni “tamaa ya Roho”. Na kama unajua jinsi kujisikia hatia kunavyokupata ukikubaliana na majaribu, basi unaifahamu sauti ya roho yako, tunayoiita “dhamiri” yetu.
Mungu alijua vizuri sana kwamba tamaa zetu za mwili zingetujaribu tufanye makosa. Lakini, hiyo si sababu inayoturuhusu kukubaliana na tamaa za mwili. Bado Mungu anatutazamia tutende kwa utii na utakatifu, na tushinde asili ya mwili.
Lakini nasema hivi: Enendeni katika Roho, nanyi hamtazitimiza tamaa za mwili (Wagalatia 5:16, TLR).
Hakuna mbinu ya kiuchawi ya kushinda mwili. Paulo alisema tu kwamba “tuenende katika Roho” nasi “hatutatimiza tamaa za mwili” (Wagalatia 5:16). Hakuna Mkristo mwenye uwezo zaidi ya mwenzake katika jambo hili. Kutembea katika Roho ni uamuzi ambao kila mmoja wetu lazima aufanye, na kujitolea kwetu kwa Bwana kunaweza kupimwa kwa kiwango cha kutojitolea kwetu kwa tamaa za mwili.
Paulo akaandika hivi tena:
Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulubisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya, na tamaa zake (Wagalatia 5:24).
Ona anachosema Paulo: Wale walio wa Kristo wameusulubisha mwili (anatumia lugha ya wakati uliopita). Hayo yalitokea wakati tulipotubu na kumwamini Bwana Yesu Kristo. Hapo, tulisulubisha ile asili ya dhambi, tukaamua kumtii Mungu na kupingana na dhambi. Sasa, si swala la kusulubisha mwili tena, bali kudumisha kule kusulubiwa.
Si rahisi kuendelea kuusulubisha mwili, lakini ni kitu kinachowezekana. Kama tutatenda kulingana na kuongozwa kwa utu wa ndani badala ya kukubaliana na misukumo ya mwili, tutaonyesha maisha ya Kristo na kuenenda katika utakatifu mbele Zake.

Asili Ya Roho Zetu Zilizoumbwa Tena

Kuna neno moja lenye kueleza vizuri zaidi asili ya roho zetu zilizoumbwa tena. Neno hilo ni Kristo. Kwa njia ya Roho Mtakatifu ambaye ana asili ile ile ya Yesu, sisi ndani yetu tuna asili ya Yesu. Paulo aliandika hivi: “Si mimi ninayeishi tena, bali Kristo anaishi ndani yangu” (Wagalatia 2:20, TLR).
Kwa sababu tuna uwezo Wake na asili Yake ndani yetu, tunao uwezo wa ajabu sana wa kuishi kama Kristo. Hatuhitaji upendo zaidi, au uvumilivu, au kiasi – ndani yetu tunaye Mtu mwenye upendo sana, mwenye uvumilivu sana, mwenye kiasi sana – anakaa ndani yetu! Tunachohitaji kufanya ni kumruhusu Yeye kuishi kwa kututumia sisi.
Ila, wote tuna adui mmoja mkubwa ambaye anapambana na asili ya Yesu, akiizuia isijidhihirishe kupitia kwetu, naye ni mwili wetu. Ndiyo maana Paulo alisema lazima kuusulubisha mwili wetu. Ni wajibu wetu kufanya kitu juu ya mwili wetu, na ni kupoteza wakati kumwomba Mungu afanye chochote kuhusu mwili. Hata Paulo alikuwa na matatizo na asili yake ya kimwili, lakini aliwajibika na kuushinda. Anasema hivi:
Ninautesa mwili wangu na kuufanya mtumwa, ili, baada ya kuwahubiri wengine, mimi mwenyewe nisije nikakataliwa (1Wakor. 9:27, TLR).
Hata wewe itabidi kuufanya mwili wako kuwa mtumwa wa roho yako, kama unataka kuenenda kwa utakatifu mbele za Bwana. Na, inawezekana!

[1] Kwa sababu Yohana anasema huu ndiyo “ufufuo wa kwanza”, hayo yanatufanya tuamini kwamba hakuna ufufuo mwingine kabla ya huo. Na kwa sababu unatokea wakati wa kumalizika kwa kipindi cha dhiki ya dunia nzima wakati Yesu anaporudi, ni kinyume na lile wazo la kuwepo kwa unyakuo kabla ya dhiki, maana tunajua kwamba utakuwepo ufufuo wa wote wakati Yesu anapotoka mbinguni kulinyakua kanisa kulingana na 1Wathes. 4:13-17. Tutajifunza zaidi katika sura iliyoko mbele iitwayo UNYAKUO WA KANISA NA NYAKATI ZA MWISHO.
[2] Ukitaka kujifunza zaidi kuhusu mada ya ufufuo, tazama Danieli 12:1-2; Yohana 11:23-26; Matendo 24:14-15; 1Wakor. 15:1-57.

No comments:

Post a Comment

NENO NI UZIMA Designed by 5gear Copyright © 2014-2015

Theme images by Jason Morrow. Powered by Blogger.