Vichwa vya Habari

KARAMA ZA ROHO MTAKATIFU - SEHEMU YA TANO

KARAMA ZA ROHO MTAKATIFU - SEHEMU YA TANO

Karama ya masaidiano.
I Wakorintho 12:28; inasema '' Na Mungu ameweka wengine katika kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, na tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano na maongozi na aina za lugha''.

Kuna huduma ya masaidiano na karama ya masaidiano. Karama ya masaidiano inafanya kazi kwa karibu sana na karama ya neno la maarifa ili upate kujua kuna mahali panahitaji msaada. Pia inafanya kazi kwa karibu sana na karama ya neno la hekima kujua ni msaada gani unatakiwa, vilevile inafanya kazi kwa karibu sana na karama ya Imani kwa sababu mahali pengine unahitaji kufanya vitu kwa imani pasipo kuona ishara ya nje.




Tumekwisha kujifunza kwamba kazi ya karama za Roho Mtakatifu ni kulijenga kanisa kwa hiyo kazi ya karama ya masaidiano pia ni kulijenga kanisa.

Maeneo manne ya kukusaidia kuifahamu zaidi karama ya masaidiano.

1. Inasaidia viungo vingine vifanye kazi yake katika kulijenga kanisa. Efeso 4:15-16; '' lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo. Katika yeye mwili wote ukiungamanishwa na kushikanishwa kwa msaada wa kila kiungo, kwa kadri ya utendaji wa kila sehemu moja moja, huukuza mwili upate kujijenga wenyewe katika upendo''. Maana yake kila kiungo katika kanisa kina kazi yake. Karama ya masaidiano huwa haionekani kwa nje lakini ni karama ya muhimu sana.

2. Inamsaidia mtu avuke kipindi chake cha mahangaiko asije akaacha kazi ya kulijenga kanisa. Matendo ya Mitume 9:1-19; anaeleza habari za Sauli (Paulo) akielekea Dameski. Katika mstari wa 8-9 anasema '' Sauli akainuka katika nchi, na macho yake yalipofumbuka hakuona kitu; wakamshika mkono wakamleta mpaka Dameski. Akawa siku tatu haoni; hali wala hanywi. Basi palikuwapo Dameski mwanafunzi ........''
Hapa tunaona Paulo (Sauli) alikuwa katika mahangaiko ndio maanahakula wala kunywa kwa siku tatu.
Anania aliwekewa mzingo wa kwenda kumsaidia Paulo katika mahangaiko hayo na tunasoma kwamba baada ya kumsaidi aliondoka. Hii inatokea mara nyingi sana pale ambapo watu wanapata mahangaiko ya wito na hapa ndipo karama ya masaidiano inahitajika.

3. Inamsaidia mtu mwingine afanikiwe katika wito alioitiwa na Mungu. Yohana 19:38-42; ''Hata baada ya hayo Yusufu wa Arimathaya, naye ni mwanafunzi wa Yesu (lakini kwa siri kwa hofu ya wayahudi) alimwomba pilato fuhusa ili auondoe mwili wa Bwana Yesu. Na pilato akampa ruhusa...........''.
Hapa tunaona wanafunzi wa Yesu, baada ya Yesu kufa, hawakuonekana kumsaidia Yesu kwenda kuuhifadhi mwili wake. Lakini msaada wa aina ya pekee ulitolewa na watu wengine ambao hawakuwa wanafunzi wa karibu sana na Bwana Yesu wakati wa maisha yake. Hii ni karama ya masaidiano ilishuka ndani yao kwa ajili ya kukamilisha wito wa Bwana Yesu.
Mfano: katika eneo kama hili ndipo watu wengine wanapewa mzigo kwa ajili ya utoaji (very specific giving) ili kusaidia kazi ya Mungu isilale, na hii inafanyika bila kujadiliana na yule anayesaidiwa. Hii inatokea hata kwa waombaji ambao wakati mwingine Roho Mtakatifu anaweka mzigo ndani yao ili kuombea tukio (event) fulani tu.


4. Inamsaidia mtu mwingine akubalike katika wito wake. Ukisoma Matendo ya Mitume 9:26-29; anazungumza habari za Sauli alipofika Yerusalemu, tunasoma kwamba alijaribu kujiunga na wanafunzi lakini walimwogopa. Lakini Barnaba, ambaye aliinuliwa na Mungu ili kusaidia, alimtwaa akampeleka kwa mitume na kumtambulisha.

Karama ya aina za lugha
Ili karama zifanye kazi kwa haraka weka ndani yako kiu ya kuona Yesu anatukuzwa. Mambo muhimu kuhusu karama ya aina za lugha:-
a. Hizi lugha zinazosemwa ni za aina gani? Ukisoma I Wakorintho 13:1; anasema '' nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao''. Maana yake Roho Mtakatifu anaweza akakuletea lugha ya wanadamu lakini siyo ile ambayo umejifunza. Na pia anaweza akakuletea lugha za Malaika.
b. kuna tofauti ya kunena kwa lugha kwa kila aaminiye na kunena kwa lugha kama karama. I Wakorintho 12:29,30 anasema ''Je wote ni Mitume? Wote ni manabii? Wote ni waalimu? Wote wanatenda miujiza? Wote wana karama za kuponya wagonjwa? Wote wanena kwa lugha? Wote wafasiri?''
Maana yake si kila mtu anapewa kufanya haya yote yaliyotajwa, si kila mtu hii karama ya kunena kwa lugha, inatokea kwake kila wakati, ila ni pale ambapo Mungu anaona panahitajika karama hiyo.
Mfano: karama hii inaweza kukusaidia pale ambapo hufahamu lugha fulani na unahitajika kupeleka ujumbe kwa lugha hiyo.
Kwa upande mwingine kuna kuna kunena kwa lugha kama ishara. Marko 16:17; '' na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watesema kwa lugha mpya''. Hapa anazungumza kunena kwa lugha kwa kila aaminiye na sio karama.
I Wakorintho 14:5; anasema ''nami nataka ninyi nyote mnene kwa lugha .......''. Maana yake kunena kwa lugha kama ishara kwa kila aaminiye na siyo karama kwa sababu anenaye kwa lugha anahuisha nafsi yake.

No comments:

Post a Comment

NENO NI UZIMA Designed by 5gear Copyright © 2014-2015

Theme images by Jason Morrow. Powered by Blogger.