Vichwa vya Habari

MAPAMBANO DHIDI YA ADUi SHETANI



Mapambano dhidi ya adui shetani
Silaha za Mungu
Mkristo anapaswa kuvaa silaha zote za Mungu ili aweze kusimama na kumshinda adui katika moto wa aina yeyote atakaotaka kuuwasha, silaha hizi lazima kuizima mishale ya moto ya adui mwovu. Na hizi silaha za Mungu zavaliwa kwa njia ya maombi na kuishi maisha yetu ya kila siku kwa imani.
Bible inatuambia kwenye Waefeso 6:10-18 namna ya kuvaa silaha zote za Mungu.
Mstari wa 10: Hatimaye mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake.
Kuna vita ipo ikiendelea kati ya nuru na giza.Kazi ya giza ipo kukuharibu wewe kiumbe wa Mungu, lakini hazina nafasi endapo utajitoa na kumtii Mungu ipasavyo.
Mwenye nguvu ni Mungu wetu ambaye ni mtawala wa vitu vyote na anayeishi milele.
Mstari wa 11: Vaeni silaha zote za Mungu mpate kuweza kuzipinga hila za shetani.
Kwa kuvaa silaha za Mungu, haina maana kwamba tunavaa vile vitu kwenye miili yetu, vionekanavyo kwa macho kama wanavyovivaa askari wa JW waendapo vitani, kama ilivyokuwa vita vya Tanzania na Uganda miaka ya 80. Bali twapaswa kuzivaa kiroho, kwa kuzivaa kiroho ina maana kwamba tunamtii Mungu. Kwa njia hii ya kumtii Mungu wetu, twaweza kabisa kumshinda adui mwovu. Kwa kuzivaa silaha zote, ina maana kwamba kuvaa kila kifaa tunachoambiwa kuvaa mahali hapa, na sio kuvaa nusu. Kwa kufanya hivyo hatutaweza kumwogopa shetani, kwa maana tunaye Mungu tunayemtumikia. Kama mkristo, hakikisha kwamba hutafumwa ukiwa hujavaa silaha zote za Mungu.
Mstari wa 12: Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya (a) falme na (b) mamlaka, (c) juu ya wakuu wa giza hili, (d) juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.
Vita si kati yetu na wanadamu wenzetu hapana, yaani sio kati ya sisi kwa sisi, bali ni kati yetu sisi na adui mwovu shetani. Tunashindana na shetani pamoja na sheji lake zima na mapepo yote, yaani na ufalme wake wote. Hatuwezi kuwaona kwa kuwa wao ni roho hawana miili, ila kwa kweli wana nguvu na hujipanga kweli kweli. Wapo nje nje kutukamata na kutuharibu, ila kumbuka kwamba ukiwa ndani ya Yesu na kulitii neno lake, hawezi kukushinda Efeso 2:20-21. Yesu ni juu ya vitu vyote, na kama tukilijua hilo, basi nasi tupo pamoja naye Efeso 2:6.
Mstari wa 13: Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.
Shetani alishahukumiwa tayari, tena siku nyingi pale Bwana wetu Yesu Kristo alipolipa gharama ya dhambi zetu sisi wanadamu kwa kufa kwake kwa njia ya msalaba. Tusimame katika imani kwenye neno lake (Ebrania 2:14), shetani hana nguvu katika neno la Mungu na wala hawezi kulipinga.
Mstari wa 14-17: (Silaha sita) Basi simameni, hali mmejifunga
(a) Kweli viunoni
Tunafahamu ya kwamba Yesu ni kweli, na neno la Mungu ni kweli. Kwa hiyo sote tunapaswa kuliweka neno la Mungu na kulitunza ndani ya mioyo yetu. Hii inafanyika kwa kulisoma na kujifunza neno la Mungu. Kwa hiyo basi, tulitumie neno la Mungu katika maisha yetu ya kila siku ili tuweze kumshinda adui.
(b) Na kuvaa dirii ya haki kifuani,
Lazima tuishi maisha safi na yenye haki mbele za Mungu Baba yetu aliyetuweka duniani ili tumtumikie. Tusiishi maisha ya dhambi kama hao wote wasiomjua na kumfuata Yesu Kristo. Tutaweza kuishi maisha haya pale tu tutakapotambua kuwa Bwana wetu Yesu Kristo ni Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Kila amwaminiye Yesu Kristo, anakuwa amevalishwa haki mbele za Mungu (2Wakorintho 5:21). Na hii inatokea pale unapomkiri na kumkubali Yesu awe kiongozi wa maisha yako hapa duniani. Damu yake imekusafisha dhambi zako na haupo mbali na Mungu, umeunganishwa na Mungu Baba yake na baba yetu. Umefanywa mwenye haki mbele ya macho ya Mungu kwa njia ya upatanisho wa Bwana Yesu pale alipoziosha dhambii zako kwa damu yake. Tuendelee kuishi maisha matakatifu kwa kuikinga miili yetu ili isichafuliwe na takataka za shetani. Kwani miili yetu ni nyumba ya Mungu, iwe safi siku zote, ili asitukimbie maana hakai kwenye uchafu.
(c) V.15 Na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani;
Watahubiri namna gani kama wasipotumwa na kupelekwa. Ina heri miguu ile inayokwenda kulihubiri neno la amani na habari njema ya Bwana katikati ya watu (Warumi 10:15). Wakristo hatupaswi kuwa na aibu ya neno la Bwana wala tusilionee haya. Habari njema kuhusu neno la Kristo ndio njia pekee ya kuleta ukombozi na amani katikati ya watu. Tutembee katika mwanga siku zote 1Yohana 1:17. Kutembea katika mwanga ina maana tuzitii amri zote za Mungu na kuepukana na kila kitu ambacho hakipo katika mpango wake.
(d) V.16 Zaidi ya yote mkitiwa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto wa yule mwovu,
Askari anapokuwa amevaa ngao, anakuwa amekingwa na hiyo ngao (bullet proof) na wala hakuna mshale wa aina yeyote utakaomlenga. Vile vile kwa mkristo ni lazima kuvaa bullet proof ambayo ni imani katika Kristo (1 Yohana 5:4-5). Tunahitaji kuwa na imani ili kuishinda hofu kwa adui. Tukiwa na imani kwa Kristo, mishale ya adui ikija mbele yetu itagonga ngao hii ya imani na kudondoka chini pasipo kutudhuru.
Zingatia: Lazima kila wakati tukumbuke ya kwamba tunalindwa na Mungu pale tunapomwamini – tunapoliamini neno lake.
(e) V.17 Tena ipokeeni chepeo ya wokovu,
Chepeo ni lile kofia la chuma ambalo huitwa helmet huvaliwa na wale wajenzi au askari wakivikinga vichwa vyao visiumie endapo itatokea hatari ya aina yeyote ile. Kuvaa chepeo ni kuwa na hakika ya uzima wa milele. Tambua ya kwamba hatujaokolewa kwa kuwa tumefanya jema au zuri lolote, bali wokovu wetu ni ule halisi, tumeokolewa na Yesu (Efeso 2:8-9). Wokovu ni zawadi toka kwa Mungu kama tunaamini kwa imani (1 Yohana 5:12-13). Kama askari vitani amejeruhiwa kichwa chake pasipo kuvaa chepeo basi huyo atakuwa mahututi. Katika ulimwengu wa roho, shetani hujaribu kumdhuru mwanadamu kwenye nafsi yake, anafanya hivi kwa kutuwekea mawazo mabaya na ya uongo ndani ya nafsi zetu. Shetani huwaambia wakristo ya kwamba hawajaokoka, yaani hamna wokovu hapa duniani ni kudanganyana tu, kwani imekuwa ni mchezo siku hizi dini zimeanzishwa ili wachungaji kujipatia pesa. Ukimsikiliza, ujue kuwa umeacha kumtii Mungu na matokeo yake atakushinda.
(f) Na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu;
Ni lazima na muhimu kujua neno la Mungu lasema nini kuhusu maisha yetu hapa duniani ili tuweze kufika Mbinguni. Yesu alikuwa na umri wa miaka 30 pale alipoanza kuhubiri neno la Mungu, alihubiri na kuponya watu. Baada ya kubatizwa aliendelea kufanya hivi na alifunga siku 40 (yaani mchana 40 na usiku zilikuwa nazo 40). Katika kipindi hiki shetani alimjaribu sana. Je wafahamu Yesu alimshinda vipi shetani? Yesu alimshinda shetani kwa njia ya kumtamkia neno la Mungu. Neno la Mungu lililotoka kinywani kwa Yesu ndilo lililomfukuza shetani, na malaika wa Mungu walikuja na kufanya kazi na Yesu. Neno la Mungu lina nguvu, na shetani akilisikia hukimbia kwa kuwa analichukia, anaijua nguvu iliyoko huko.
Neno la Mungu linaitwa upanga kwa kuwa ni kali, linapenya hadi ndani ya moyo wa mwanadamu na kuwajulisha uovu wao na kwamba inabidi wakutane na mwokozi wao. Hakikisha hufumwi ukiwa huna neno la Mungu, na kuwa na neno la Mungu haimaanishi kuwa utembee na bible ukiwa umeishika mkononi, la hasha ulijue neno la Mungu, likae moyoni mwako na ulitumie kila wakati ukiwa unaongea na Mungu na ukiwa vitani pia Ebrania 2:14
1 Yohana 2:14 tunamshinda shetani endapo neno la Mungu lakaa ndani yetu. Tumpende Mungu Baba yetu aliyetupa ahadi nzuri, anayetupenda tuishi maisha safi na ya ushindi. Tuache kuyang’ang’ania ya dunia hii ambayo yaongozwa na shetani. Mshike Mungu ambaye anadumu milele, maana tamaa za dunia na kiburi cha uzima vyote vina mwisho, ila neno linadumu daima.
Mstari wa 18: Kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu kuwaombea watakatifu wote.
Mkristo yeyote lazima akeshe na kudumu ktika maombi kila wakati, la sivyo lazima atarudi nyuma kiroho. Maombi ni mawasiliano halisi kati ya mwanadamu na Mungu wake. Mungu bado akiendelea kuongea nasi kila siku, na tutaisikia sauti yake endapo tutakuwa karibu naye kwa njia hii. Ukifanya hivyo utakuwa ukimsikia kila siku kupitia Neno Lake. Mungu anapenda kushirikiana nasi kwa njia ya maombi huku tukijulishana mawazo yetu, mipango yetu, hata tukimuuliza habari zetu. Tunaweza kusali kimya kimya, kwa sauti au kwa namna yeyote ile, lakini ili mradi tunawasiliana nae kila wakati. Na ukitaka kuwafahamu watu utawafahamu kwa njia ya mawasiliano, ukiwakuta wakiongea. Naye Mungu wetu vivyo hivyo, tutamfahamu pale tutakapokuwa tukiwasiliana naye. Angalia kwenye kitabu cha Yohana 17 jinsi Yesu alivyokuwa akiwasiliana na Baba yake kwa njia ya maombi.
Tusimwendee Mungu pale tunapokuwa na shida tu, tuwasiliane naye hata wakati wa furaha. Utakubaliana nami kwamba, mtu akiwa hana mawasiliano nawe, halafu akawasiliana nawe wakati wa shida yake. Hebu jaribu kufikiria utajisikiaje? Lazima utalalamika kuwa huyu jamaa ananitafuta wakati ana shida tuu, mie simsaidii maana shida yake ikiisha atarudi tena kulekule. Basi na Mungu wetu vile vile huwa hapendezwi na wale wanaomjua wakati wa shida tu, na kumwacha wakiwa hawana shida. Ni furaha iliyoje kwa watu wapendanao na kuwasiliana kila wakati, na kwa Mungu ni vivyo hivyo. Hii ndio inatakiwa iwe na ndivyo inavyomaanisha kwenye maombi.
Anayetuvalisha silaha
Luk 11:20-26
Kidole cha Mungu kinatupa kumshinda shetani, kidole cha Mungu ni Roho Mtakatifu wa Mungu. Twahitaji kidole cha Mungu katika vita. Mara tunaposhinda, ufalme wa Mungu unakuja juu yetu, maana yake, tunafunikwa na ufalme wa Mungu kwa hiyo hakuna atakayetutoa hapo.

No comments:

Post a Comment

NENO NI UZIMA Designed by 5gear Copyright © 2014-2015

Theme images by Jason Morrow. Powered by Blogger.