Vichwa vya Habari

UMEJIANDAA KUSAIDIA WAAMINI WAPYA?, MAISHA YA USHINDI KATIKA KRISTO YESU



Pengine unajiuliza. ‘Nani? Mimi? Sijui la kusema; sijawahi kusoma shule ya Biblia; hakuna mtu amewahi kunifundisha jinsi ya kufanya hivyo’. Kumbuka Yesu aliwatumia watu wa kawaida wasio na elimu ya shuleni. Mdo 4:13 ‘Basi walipoona ujasiri wa Petro na Yohana, na kuwajua ya kuwa ni watu wasio na elimu, wasio na maarifa, wakastaajabu, wakawatambua ya kwamba walikuwa pamoja na Yesu’.

Hatuhitaji kuwa wakamilifu ndipo tuanze kazi hii. Mungu alimuahidi Musa, ‘Nitakuwa pamoja nawe’ (Kut 3:12). Na Yesu aliwaahidi wanafunzi wake, ‘mimi nipo pamoja nanyi sikuzote, hata ukamilifu wa dahari’ (Mt 28:20). Wanafunzi wake hawakuwa shujaa sana ndiyo maana walikimbia Yesu alipokamatwa katika bustani ya Getsemane. Lakini walipojifunza kwamba Yesu yuko pamoja nao, wakawa tayari kufanya lolote alilowataka wafanye.
Mungu ndiye anayetupa uwezo, hekima na ujasiri ili tumalize vyema.1 The 5:24 Yeye ni mwaminifu ambaye awaita, naye atafanya’.

Hata hivyo, kuna mambo kadhaa yanayopaswa kuonekana katika maisha yetu kama tunataka kusaidia wengine wakue katika maisha yao ya Kikristo.

1)   Tuwe na maisha ya ushindi katika majaribu na dhambi (1 Pet 2:12). Tutaishi maisha ya ushindi tukiwa na uhusiano wa upendo na ushirika na Yesu Kristo na tukiwa tumejazwa Roho Mtakatifu.
2)   Tuwe tayari kujitoa kwa ajili ya mwingine anayetaka kukua. Uanafunzi unahitaji muda. Wanafunzi wajue kwamba wanaweza kutujia wakati wowote wanapotaka kutushirikisha mawazo yao na matatizo yao.
3)   Tujue kwamba tunatakiwa kutunza siri za yale wanayotuambia bila kuyasema kwa wengine. Wanahitaji kujua kwamba hata kama watatushirikisha ugumu wowote au dhambi ya siri, hatutawahukumu. Wanahitaji kujua kwamba wana thamani kwetu.
4)   Tuwe tayari kuomba msamaha tunapowakosea. Wanahitaji kujua kwamba hatujafikia ukamilifu lakini tunapitia magumu wanayoyapitia.
5)   Tuwe jasiri kusema ukweli ili kuwakemea na kuwaonya wanafunzi wetu wakiendelea na mwenendo mbaya (Lk 17:3). Lakini wakati wote tujitahidi kuongea katika upendo (Mit 17:17a).
6)   Tuwe tayari kuacha kufanya jambo ambalo tunaona kwamba linamsababisha mwanafunzi ajikwae (Rum 14:1-3, 13-15, 19-21).

Mambo muhimu ya kukumbuka kuhusu uanafunzi:
1)   Ni Mungu anayefanya kazi ya kuwabadilisha wanafunzi. Roho Mtakatifu analitumia Neno la Mungu kuwabadilisha watu. (Fil 2:13; 1 Kor 3:6).
2)   Tusiwe wakubwa sana kwa wanafunzi wetu. Badala yake tuwe watumishi wa kiroho. Wajifunze kufanya analotaka Mungu na sio tunanalotaka sisi wala wanalotaka wao. Kol 1:28.
3)   Tunaweza kutoa mafunzo kwa maneno yetu, lakini mfano wa kuigwa ni muhimu pia.
4)   Kumsaidia mwingine akue kunahitaji uhusiano. Mwalimu asijione kwamba ni muhimu kuliko mwanafunzi wake.
5)   Uanafunzi ni urafiki, kwanza na Mungu na kisha na waamini wengine.

III. MOYO WA ‘MFANYA UANAFUNZI’
1)   Moyo wa maombi
1 The 1:2-3 Paulo aliombea wengine.
Yn 17 Yesu aliombea wanafunzi wake, na sisi tumejumuishwa.
Kol 4:12 Epafra aliwaombea kwa bidii.
Hebu angalia Paulo alivyoombea: Efe 1:15-18; Fil 1:3-11; Kol 1:3-14.
2)   Moyo wa ushujaa
1 The 2:2 Paulo hakusubiri waamini wapya wamjie kwa ajili ya kuomba msaada. Aliwaendea ingawa alipata mateso mengi huko Filipi.
3)   Moyo wa mama
1 The 2:7  Waamini wapya wanahitaji upole na huruma. Yaani, tuwasikilize vizuri kabla ya kuongea na tuonyeshe upendo badala ya hukumu.
4)   Moyo wa baba
1 The 2:11-12 Wakati mwingine tunatakiwa kuwafundisha mambo magumu ili wajifunze kuwa jasiri na kusimama katika imani yao. Tuwafundishe kujitegemea. Wakati mwingine tuweke wazi udhaifu wao na dhambi zao.
5)   Moyo wa kushirikisha nafsi
1 The 2:8  Waamini wapya wanahitaji mambo mengine zaidi ya mafunzo peke yake. Tunatakiwa tushirikishe maisha yetu yote kwao. Mfano:
 a) Kuwa tayari kuwashirikisha magumu tunayopitia bila kusahau ushindi
     tunaoupata.
b) Fanya matembezi nao. Nendeni dukani pamoja, kuchota maji na hata
     kutembelea wagonjwa.
c) Wakaribishe nyumbani kwako. Wanahitaji kuona jinsi tunavyoishi. Wanahitajikuona kwamba si kila kitu ni kamili katika nyumba zetu. Wanahitaji kuona tunavyohusiana na wenzi au watoto wetu. Wanahitaji kuona tunaadibisha vipi watoto wetu.
6)   Moyo usio na lawama.
1 The 2:10 Tukumbuke kwamba tunayotenda yana sauti zaidi kuliko tunayosema. 1 The 2:3-6.

IV.UTEKELEZAJI
1.Jiandae vizuri. Msikilize Roho akuongoze kwamba uanze na somo gani.
2.Uwe na lengo kichwani kwa ajili ya mwanafunzi wako.
3.Uwe na maandiko ya kutumia. Usitumie maandiko mengi sana kwa wakati mmoja.
4.Uwe na mifano hai ya kuelezea unachofundisha.
5.Uwe na andiko la kukumbuka. Likariri pamoja naye ili aone kwamba hata wewe unapenda kuliweka Neno moyoni mwako.


USHAURI
Ndugu msomaji/mwanafunzi, napenda kukutia moyo kwa utayari wako wa kujifunza masomo haya ya kufanyika mwanafunzi wa Yesu. Mpango wa Mungu kwako si kuwa mshirika wa kanisa tu, bali kuwa mwanafunzi wa Yesu (Mt 28:19) Jitahidi kumaliza masomo yote (kozi nzima) ya uanafunzi ili ufae kufundisha na wengine (2 Tim 2:2).



Dr Lawi E. Mshana, Founder & President
Victorious Life Ministries

Box 554 Korogwe, Tanga, Tanzania.

Alhamisi, 26 Juni 2014


UANAFUNZI - Somo linaendelea

3. Mwanafunzi lazima:-
a)   Ajifunze kwa mwalimu wake (head knowledge). Ni muhimu mwanafunzi kuwa na mwalimu wa kumpa mafundisho ya kiroho badala ya kutegemea mafundisho ya kidini.
b)   Apende mafundisho (heart knowledge). Hapa anakubali kwamba haya mafundisho ni kwa ajili yake. Hatafuti kujifunza kwa ajili ya watu wengine.
c)    Atendee kazi (applied knowledge). Hapa mafundisho yanakuwa sehemu ya maisha yake. Anayatumia kuleta mabadiliko maishani mwake.
d)   Ashirikishe (transferred knowledge).  Hapa anayashirikisha kwa wengine
      2 Tim 2:2. Hapa ndipo anafikia hatua ya kuyashirikisha kwa wengine kwa vile
      yamembadilisha yeye mwenyewe tayari.

4. Petro, Barnaba na Paulo

Petro hakuwa na elimu ya kidunia isipokuwa alijifunza kwa Yesu na akawahubiri maelfu wakaokoka. Mdo 2:40, 41 ‘Akawashuhudia kwa maneno mengine mengi sana na kuwaonya, akisema, Jiokoeni na kizazi hiki chenye ukaidi. Nao waliolipokea neno lake wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka watu wapata elfu tatu’.

Ni Barnaba aliyemlea Paulo. Mdo 9:26-27 Na Sauli alipofika Yerusalemu, alijaribu kujiunga na wanafunzi, nao walikuwa wakimwogopa wote, wasisadiki ya kuwa yeye ni mwanafunzi. Lakini Barnaba akamtwaa, akampeleka kwa mitume, akawaeleza jinsi alivyomwona Bwana njiani, na ya kwamba alisema naye, na jinsi alivyohubiri kwa ushujaa katika Dameski kwa jina la Yesu’. Walisafiri pamoja katika huduma (Mdo 11:25-26) mpaka walipopishana kwa ajili ya Yohana Marko aliyewaacha katika safari za kimisheni (Mdo 15:36-40). Barnaba alichagua kumchukua Yohana Marko kwa ajili ya kumfanyia uanafunzi zaidi. Baadaye akafaa zaidi hata kwa Paulo. Kol 4:10 Aristarko, aliyefungwa pamoja nami, awasalimu; na Marko, mjomba wake Barnaba, ambaye mmepokea maagizo kwa habari yake; akifika kwenu mkaribisheni’.
Paulo alimfanyia uanafunzi Timotheo ili aiendeleze huduma pale aliposhindwa kuendelea mwenyewe. 1 Tim 1:2,3 kwa Timotheo, mwanangu hasa katika imani. Neema na iwe kwako, na rehema, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Bwana wetu. Kama vile nilivyokusihi ukae Efeso, nilipokuwa nikisafiri kwenda Makedonia, ili uwakataze wengine wasifundishe elimu nyingine’.

5.Wakristo waliokomaa wanafananaje?

Efe 4:13 ‘ – hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo’. Hili ndilo lengo letu. Lakini kivitendo ina maana gani?

a)   Wako salama katika uhusiano wao na Kristo. 1 Yoh 5:11-13 Wanajua wana uzima wa milele.
b)   Wanatambua mamlaka ya Bwana Yesu maishani mwao. Kol 2:6-7; 1 Kor 8:6.
c)    Wana ushindi katika dhambi maishani mwao. 1 Yoh 5:4-5; 1 Kor 10-13.
d)   Wanayajua maandiko na wanaweza kuyatumia inavyotakiwa katika maisha yao. 2 Tim 3:16-17
e)   Wana maisha ya maombi yenye matokeo. Fil 4:6-7; 1 The 5:16-18.
f)    Tunda la Roho linaonekana maishani mwao. Gal 5:22-23; Yn 15:8.
g)   Wana utii katika kumtumikia Bwana. Yn 14:15,23; 1 Yoh 2:3.
h)   Wanashirikisha kikamilifu imani yao kwa wengine. 1 Pet 3:15.
i)     Wanashiriki kikamilifu katika ushirika wa Kikristo (ibada). Ebr 10:24-25.
j)    Wana huruma ya Kristo kwa ajili ya wengine na wako tayari kuwasaidia wengine. Kol 3:12-14; 2 Kor 9:7; Efe 4: 11-14.
Somo hili litaendelea…


Jumatano, 11 Juni 2014


UANAFUNZI (DISCIPLESHIP)

2 Tim 2:2 “Na mambo yale uliyoyasikia kwangu mbele ya mashahidi wengi, hayo uwakabidhi watu waaminifu watakaofaa kuwafundisha na wengine”.

Ukweli wa andiko hili ni kwamba si mambo yote yanafaa kufundisha watu wote ibadani au mkutanoni. Lazima tutambue hadhira. Somo hili sio kwa ajili ya wabinafsi wanaotaka kujifunza ili tu wapone magonjwa, wabarikiwe, wainuliwe, wajulikane nk. Yaani mimi mimi mimi (me-ism). Kinyume chake ni kwa ajili ya WATU WAAMINIFU WATAKAOFAA KUWAFUNDISHA WENGINE.

I. KANUNI ZA UANAFUNZI

Mt 28:19-20 Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari’.

Maneno haya yanaitwa ‘Agizo Kuu’. Biblia imejaa maagizo mengi lakini hili ni agizo kuu. Kama una shauku kuu ya moyo wa Yesu tambua kwamba agizo hapa ni ‘fanya wanafunzi’ na sio fanya washirika/washarika. Hebu tujiulize kwamba tutalifanyia kazi vipi? Hatua ya kwanza ni kuwaleta kwa Yesu na sio kuwabadilisha tu dini. Kisha lazima tuwasaidie wakue na kuwa wanafunzi wanaomjua Mungu kweli ili nao wawalete wengine kwa Yesu. Kila mkristo anatakiwa ajiwekee utaratibu angalau wa kumleta kwa Yesu mtu mmoja kwa mwaka. Swali ni je tangu umpokee Yesu una miaka mingapi, na wangapi umewaleta kwa Yesu na kuhakikisha wanakua na kuweza pia kuwaleta wengine kwa Yesu?

Tumepewa kazi muhimu ya kuwasaidia waamini wengine wakue Efe 4:11-12 ‘Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe. Tukijua kweli ya Neno la Mungu, tunawekwa huru. Yn 8:32 ‘Tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru’. Yesu ndiye ukweli huo. Yn 14:6 ‘Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi’. Mtoto mchanga haachwi peke yake ajilishe.  Akiachwa peke yake atakufa. Ni kosa kubwa kuzaa watoto hospitalini na kutojali kuwapeleka mahali pa kupata malezi yanayoendana na umri wao.
Kwa nini kukua kiroho ni muhimu? Ebr 5:14 ‘Lakini chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa kupambanua mema na mabaya’. Tunakua ili tuweze kubeba majukumu makubwa. Umebeba majukumu gani makubwa ili tuseme umekua kiroho? Kama bado kuna mtu umeshindwa kumsamehe, hutoi zaka, humleti mtu kwa Yesu, unachelewa ibada kila wakati, hujishughulishi na huduma yoyote kanisani; unastahili mafundisho ya watoto wachanga. 1 Petro 2:2 Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu.

1.Uanafunzi ni nini?

Uanafunzi ni mkristo mmoja kumsaidia mkristo mwingine kukua kiroho na kukua katika uhusiano wake na Yesu Kristo.

Uanafunzi ni sawa na stuli ya miguu mitatu. Miguu hiyo ni maombi, uhusiano namafundisho. Hakuna usalama kama mguu mmoja ni dhaifu.

a)   Maombi. Yesu anasema kwamba pasipo Yeye hatuwezi kufanya lolote. Yn 15:5  ‘Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote’. Lazima tutumie muda wa kutosha katika maombi tukitafuta msaada wa Mungu na kuombea waamini wapya. Tujifunze kuweka tumaini letu kwa Mungu kuliko kwenye dini au kwa wanadamu.

b)  Uhusiano. Waamini wapya wanahitaji upendo na urafiki. Wanahitaji mfano mwema wa kuufuata. Fil 3:17 Ndugu zangu, mnifuate mimi, mkawatazame wao waendao kwa kuufuata mfano tuliowapa ninyi’. Lazima maisha yetu yawaonyeshe kile Mungu anachotarajia. Paulo alimwonyesha Timotheo jinsi ya kuishi. Tunahitaji kujifurahisha pamoja nao, kufanya kazi pamoja, kutembea pamoja, kucheka pamoja na kulia pamoja. 2 Tim 3:10,11 ‘Bali wewe umeyafuata mafundisho yangu, na mwenendo wangu, na makusudi yangu, na imani, na uvumilivu, na upendo, na saburi; tena na adha zangu na mateso, mambo yaliyonipata katika Antiokia, katika Ikonio, na katika Listra, kila namna ya adha niliyoistahimili, naye Bwana aliniokoa katika hayo yote’.


c)   Mafundisho. Waamini wapya wanahitaji mafundisho. Sehemu mojawapo katika ‘Agizo Kuu’ ni mafundisho. Wakristo wapya hawawezi kukua bila mafundisho yenye uzima. Mt 28:20 ‘na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari’.

2.Mwanafunzi ni nani?

Mwanafunzi ni mtu anayejifunza zaidi kwa Bwana wake na anayependa kufuata nyayo za Bwana wake na kubadilika akifanana naye. Mwanafunzi ni mtu anayejifunzaanayefuatana anayekua. Rum 12:2 ‘Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu’. Mwanafunzi wa kweli anatafuta kufanana na Yesu kuliko kufanana na dunia. Hebu jiulize kama uvaaji wako, mahusiano yako, matumizi yako na mapato yako yanaakisi (reflect) tabia ya Yesu Kristo.

Kanisa la kianafunzi ni kanisa ambalo linawaleta watu kwa Yesu Kristo, na kuwajenga katika imani yao na kuwaandaa wawalete wengine kwa Yesu na kuwajenga katika imani yao. Tusijali sana namba ya waumini tu wakati kati yao hakuna wanafunzi. Watumishi wa kipindi cha Biblia walitofautisha kati ya wanafunzi na makutano ya watu.

NENO NI UZIMA Designed by 5gear Copyright © 2014-2015

Theme images by Jason Morrow. Powered by Blogger.